Mikutano mitano mikubwa zaidi ya kidini duniani

H

Chanzo cha picha, IWM/Getty Images

    • Author, Usman MINJIBIR
    • Nafasi, BBC Hausa
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Dini na tamaduni mbalimbali duniani huwa na sherehe na mikusanyiko inayowakutanisha mamilioni ya waumini katika eneo moja kwa ajili ya ibada, kumbukumbu au maadhimisho ya kidini.

Mikusanyiko mingi hufanyika kila mwaka, jambo linalowawezesha waumini kupanga safari zao mapema na kujiandaa kifedha kwa gharama za usafiri na malazi.

Kwa sasa, miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kidini duniani, mitatu ni ya Waislamu, mmoja ni wa Wahindu na mmoja ni wa Wayahudi. Ingawa orodha hii haijawasilishwa kama rekodi rasmi ya Guinness World Records, matukio haya yanajitokeza kutokana na idadi kubwa ya washiriki wanaohudhuria.

1. Maha Kumbh Mela, India

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Maha Kumbh Mela ndiyo mkusanyiko mkubwa zaidi wa kidini duniani. Kwa mujibu wa mamlaka za jimbo la Uttar Pradesh, idadi ya washiriki hubadilika katika kila maadhimisho.

Kwa mfano, mwaka 2013 mkusanyiko huo ulihudhuriwa na takribani watu milioni 120, huku maadhimisho ya mwaka 2025 yakikadiriwa kuvutia zaidi ya watu milioni 670, na hivyo kuwa miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya binadamu.

Maha Kumbh Mela hufanyika mara moja kila baada ya miaka 12 kwa kuzingatia kalenda ya unajimu ya dini ya Kihindu. Maadhimisho hayo huzunguka vituo vinne muhimu vya ibada vya Wahindu ambavyo ni Prayagraj, Haridwar, Nashik na Ujjain.

Maarufu zaidi ni Prayagraj, ambako waumini huoga katika makutano ya mito Ganges, Yamuna na Saraswati, wakiamini kuwa ibada hiyo huwasafisha dhambi na kuwasaidia kufikia ukombozi wa kiroho.

2. Arbaeen, Karbala, Iraq

H

Chanzo cha picha, Getty Images

Arbaeen ni mkusanyiko mkubwa wa pili wa kidini duniani, unaowakutanisha mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji wa Karbala, Iraq.

Maadhimisho hayo hufanyika siku 40 baada ya Ashura, ikiwa ni kumbukumbu ya kuuawa shahidi kwa Imam Hussein bin Ali, mjukuu wa Mtume Muhammad.

Kwa mujibu wa takwimu za Karbala, kati ya watu milioni 20 na milioni 30 hushiriki kila mwaka katika kilele cha maadhimisho hayo kinachofanyika tarehe 20 Safar.

Mwaka 2022, takribani watu milioni 21 walihudhuria, huku mwaka 2017 idadi ikifikia karibu milioni 30, kwa mujibu wa wasimamizi wa Haram ya Al Abbas na Haram ya Imam Hussein.

Mahujaji wengi husafiri kwa miguu kutoka miji na mataifa mbalimbali kuelekea Karbala.

3. Bishwa Ijtema, Bangladesh

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Bishwa Ijtema ni mkusanyiko wa kila mwaka wa Kiislamu unaofanyika Tongi, karibu na mji wa Dhaka nchini Bangladesh, na huvutia zaidi ya Waislamu milioni tano kutoka zaidi ya nchi 150.

Lengo kuu la mkusanyiko huo ni kuimarisha maadili, ibada na umoja wa Waislamu, badala ya kujadili masuala ya kisiasa.

Ratiba ya mkutano hujumuisha mafundisho ya dini ya Kiislamu, vikao vya dua na dhikri, mijadala kuhusu kuimarisha maisha ya Kiislamu na kueneza dini kwa njia ya amani, pamoja na dua ya mwisho inayojulikana kama Akheri Munajat, ambayo ndiyo sehemu inayovutia waumini wengi zaidi.

4. Hija, Makka

G

Chanzo cha picha, Getty Images

Hija ni ibada inayotekelezwa katika mwezi wa Dhul Hijja, mwezi wa 12 wa kalenda ya Kiislamu.

Ibada kuu hufanyika kati ya tarehe 8 na 13 Dhul Hijja kila mwaka.

Hija ni nguzo mojawapo ya Uislamu na ni wajibu kwa kila Muislamu mwenye uwezo wa kimwili na kifedha kuitekeleza angalau mara moja katika maisha yake.

Katika miaka ya karibuni, Hija imekuwa ikiwavutia kati ya watu milioni mbili na milioni tatu kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Takwimu ya Saudi Arabia, mwaka 2010 mahujaji walikuwa takribani milioni 2.8, huku mwaka 2012 wakifikia watu 3,161,573.

5. Ukuta wa Magharibi, Jerusalem

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Ukuta wa Magharibi uliopo Jerusalem ni moja ya maeneo matakatifu zaidi kwa Wayahudi na hutembelewa na takribani watu milioni tano kila mwaka.

Ukuta huo upo katika Mji wa Kale wa Jerusalem na unaaminika kuwa sehemu pekee iliyosalia ya ukuta uliokuwa umeizunguka Hekalu la Pili la Wayahudi, lililoharibiwa na Waroma mwaka 70 BK.

Kwa sababu hiyo, Wayahudi kutoka sehemu mbalimbali za dunia hufika katika eneo hilo kwa ajili ya kusali na kufanya ibada.