Mashindano ya 'uzembe' yanavyoenea duniani

.

Chanzo cha picha, Shutterstock

Maelezo ya picha, .
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Kukaa bila kufanya chochote kwa dakika 90 kunaweza kuonekana kuwa jambo rahisi. Lakini kwa baadhi ya watu, hilo limegeuka kuwa changamoto inayohitaji nidhamu kubwa.

Nchini Korea Kusini, mashindano ya Space-out yamekuwa yakifanyika kila mwaka, ambapo washiriki hutakiwa kutofanya chochote kwa dakika 90; Hawatakiwa kulala, kutumia simu au kuzungumza.

Lengo la mashindano ni kuangalia nani hajishughulishi au nani anayeweza kutulia zaidi.

Washiriki hufuatiliwa pia mapigo yao ya moyo, huku watazamaji wakipiga kura kuwachagua washiriki 10 wanaowapenda zaidi. Mshindi huchaguliwa miongoni mwao kwa kuangalia nani aliyekuwa na mapigo ya moyo yaliyotulia zaidi.

Mashindano hayo yalianzishwa Seoul mwaka 2014 na msanii wa maonyesho anayejulikana kwa jina la Woopsyang, baada ya yeye mwenyewe kukumbwa na uchovu mkubwa wa akili na mwili.

Kwa mujibu wa Woopsyang, alijiuliza kwa nini alihisi wasiwasi kila alipokuwa ametulia na hafanyi chochote. Baadaye aligundua kuwa wasiwasi huo ulihusishwa na kujilinganisha na watu wengine waliokuwa na shughuli nyingi.

Ndipo akapata wazo la kugeuza hali hiyo ya kutofanya chochote ambao wengine wanaita 'uzembe' kuwa mashindano.

Zaidi ya watu 4,000 waliomba kushiriki katika mashindano ya mwaka 2024 mjini Seoul, huku washiriki 117 wakichaguliwa. Walitoka katika makundi mbalimbali ya umri, kuanzia mtoto wa darasa la pili hadi watu wenye umri wa zaidi ya miaka 60.

Kwa baadhi yao, mashindano hayo ni fursa ya kupumzika kutokana na msongo wa mawazo na uchovu wa kazi.

Miongoni mwa washiriki alikuwa mwanariadha wa kuteleza kwenye barafu Kwak Yoon-gy, mshindi wa medali mbili za fedha za Olimpiki. Alisema katika miaka 30 ya mazoezi aliyokuwa anafanya hakuwahi kupata mapumziko ya kweli.

Mchezo huo umeanza kuenea

.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Kila baada ya robo saa mshiriki hupimwa mapigo ya moyo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini wazo la shindano hilo la kutofanya chochote halijaishia Korea Kusini.

Tangu lilipoanzishwa Seoul, mashindano hayo yameenea katika miji mingine duniani, ikiwemo Beijing, Rotterdam, Taipei, Hong Kong na Tokyo.

Umaarufu wake unaibua swali: Kwa nini jambo linaloonekana kuwa rahisi sana- yaani unakaa tu hufanyi chochote, lakini mbona limekuwa jambo gumu kiasi hicho?

Utafiti wa wanasaikolojia katika Chuo Kikuu cha Virginia nchini Marekani mwaka 2014 ulionyesha jinsi watu wanavyoweza kupata ugumu wanapoachwa peke yao na mawazo yao.

Katika jaribio hilo, washiriki waliombwa kukaa peke yao kwa dakika 15 wakifikiria, bila na kitu kingine chochote cha kuwaburudhisha isipokuwa kitufe ambacho wangeweza kubonyeza na kujipa mshtuko mdogo wa umeme ambao haukuwa na madhara lakini ulikuwa wa kuudhi.

Takriban nusu ya washiriki walishindwa kujizuia na kubonyeza kitufe hicho.

Kwa waandaaji wa mashindano ya Space-out, kutulia si kupoteza muda.

Wanayaona mashindano hayo kama njia ya kuhoji utamaduni unaothamini kuwa na shughuli kila wakati na kuonyesha kwamba wakati mwingine, kutofanya chochote kunaweza kuwa jambo muhimu.

Na hivyo, katika dunia inayozidi kuwa na shughuli nyingi, huenda changamoto mpya isiwe kufanya zaidi, bali kujua namna ya kutulia na kufanya kitu chochote.