Moja kwa moja , Trump ataka makubaliano ya kudumu na Iran

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House Ijumaa, Trump alisema Marekani inataka makubaliano ya kweli na Iran, akidai kuwa licha ya Tehran kutaka kufanya mazungumzo, masharti inayotaka hayawezi kukubalika kwake.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Chanzo cha moto ulioteketeza hoteli 6 Zanzibar bado chachunguzwa

    .

    Mamlaka za usalama Zanzibar zinaendelea kuchunguza chanzo cha moto ulioteketeza hoteli sita katika eneo la Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja, huku baadhi ya taarifa zikielekeza uwezekano wa hitilafu ya umeme au jenereta.

    Moto huo ulizuka mchana wa Ijumaa, Novemba 21, 2026, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali katika hoteli kadhaa pamoja na maduka ya wafanyabiashara wadogo waliokuwa wakiuza vinyago.

    Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Omary Abdallah, amenukuliwa na vyombo vya habari vya ndani akisema chanzo cha moto huo bado kinachunguzwa.

    Akizungumza na AyoTV kwa njia ya simu, Katibu wa Sheha wa Nungwi, Khamis Kibata, alisema baadhi ya majengo ya hoteli hizo yalikuwa yamejengwa kwa makuti, hali iliyochangia moto kusambaa kwa kasi.

    Aidha, njia finyu katika eneo hilo ziliripotiwa kuwa changamoto kwa magari ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kufika eneo la tukio kwa urahisi.

    Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lilifanikiwa kuudhibiti moto huo, huku hakuna vifo wala majeruhi vilivyoripotiwa.

    Kwa upande mwingine, Kamisheni ya Utalii Zanzibar pamoja na uongozi wa wilaya waliandaa malazi mbadala kwa wageni walioathirika na tukio hilo.

    Hii si mara ya kwanza kwa hotel nyingi Zanzibar kuungua kwa wakati mmoja. Hili ni tukio la tatu kwa miaka 5 iliyopita, ambapo kwa miaka hiii karibu hotel 13 ziliteketea.

    Ukiacha 6 za sasa, mwaka 2023, hoteli tano zenye wastani wa vyumba sita hadi 16 na nyumba ya kulala wageni huko Paje Wilaya ya Kusini Unguja, Mkoa wa Kusini Unguja ziliungua kwa moto. Hotel hizo ni Cristal Resort, Merak, Maisha Matamu, Drifters na The Next Boutique Resort.

    Tukio lingine lilitokea mwaka 2021 ambapo hotel mbili zingine za Toptube Hotel na Oceanic Paradise ziliteketea katika matukio ambayo yote hata hivyo hayakusababisha vifo.

  2. Mexico yamkamata kinara wa dawa za kulevya aliyekuwa akisakwa na FBI

    .

    Mmoja wa vinara wa biashara ya dawa za kulevya nchini Mexico, aliyekuwa kwenye orodha ya watu 10 wanaosakwa zaidi na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), amekamatwa baada ya majibizano ya risasi kati ya vikosi vya usalama na washukiwa wa uhalifu nchini humo.

    Fausto Isidro Meza Flores, anayefahamika kwa jina la utani la "Chapo Isidro", alikamatwa Ijumaa pamoja na watu wengine saba na vikosi maalumu vya jeshi la Mexico katika eneo la Guasave, jimbo la Sinaloa.

    Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Mexico, washukiwa wengine saba waliuawa katika operesheni hiyo, pamoja na wanajeshi wanne waliokuwa safarini kwenda kuongeza ulinzi katika eneo la Guasave.

    Meza Flores alikuwa akitafutwa nchini Mexico kwa tuhuma za kujihusisha na uhalifu wa kupangwa, huku FBI ikimtuhumu kusafirisha kwa wingi dawa za kulevya aina ya fentanyl, cocaine, heroini na nyingine hatari kwenda Marekani. Marekani inataka akabidhiwe ili akabiliwe na mashtaka.

    Mexico imeongeza juhudi za kupambana na biashara ya dawa za kulevya kufuatia shinikizo kutoka kwa Rais wa Marekani Donald Trump tangu arejee madarakani.

    Meza Flores, anayeongoza kundi la Meza Flores Organisation, linalojulikana pia kama Guasave Cartel, anadaiwa kujihusisha na biashara ya usafirishaji wa dawa za kulevya tangu miaka ya 1990. Hata hivyo, aliweza kukwepa vyombo vya usalama kwa muda mrefu kwa kutojiweka sana hadharani.

  3. Indonesia yasaka watu 36 baada ya moto kiwandani kuua watatu

    .

    Waokoaji nchini Indonesia wanaendelea na juhudi za kuwatafuta wafanyakazi 36 ambao hawajulikani walipo, kufuatia moto mkubwa uliotokea katika kiwanda cha kutengeneza pipi na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine wanne kujeruhiwa.

    Moto huo ulizuka Jumamosi jioni katika kiwanda kilichopo Cikande, wilayani Serang, mkoani Banten, magharibi mwa kisiwa cha Java.

    Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka, watu 15 waliweza kunusurika katika tukio hilo, huku wanne kati yao wakipelekwa katika vituo vya matibabu kwa ajili ya kupata huduma.

    Timu za uokoaji zinaendelea kukagua maeneo mbalimbali ya jengo lililoharibiwa na moto, wakiamini huenda baadhi ya wafanyakazi waliokuwa ndani wamenasa kwenye vifusi.

    Hadi mapema leo Jumapili, wazima moto walikuwa bado wakifanya kazi ya kupoza maeneo ya kiwanda hicho baada ya kubaini kuwa baadhi ya sehemu bado zilikuwa na mabaki ya moto na joto kali.

    Mamlaka bado hazijatoa taarifa kuhusu chanzo cha moto huo.

  4. Trump ataka makubaliano ya kudumu na Iran

    .

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema nchi yake inataka kufikia makubaliano ya kudumu na Iran, akisisitiza kuwa hataki makubaliano yasiyo na uhakika, huku akidokeza kuwa anaweza kusubiri hadi mwaka 2027 kabla ya kuamua hatua nyingine kuhusu vita kati ya nchi hizo.

    Akizungumza na waandishi wa habari huko Ikulu ya White House Ijumaa, Trump alisema Marekani inataka makubaliano ya kweli na Iran, akidai kuwa licha ya Tehran kutaka kufanya mazungumzo, masharti inayotaka hayawezi kukubalika kwake.

    " Wanataka kufanya makubaliano, lakini hawataki makubaliano ambayo mimi nitayakubali," alisema Trump.

    Aliongeza kuwa Iran imekuwa ikiidanganya Marekani kwa miaka 51.

    Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Israel siku ya Alhamisi, Trump alisema hana haraka ya kufanya uamuzi kuhusu hatua inayofuata katika vita dhidi ya Iran, na anaweza kusubiri hadi mwaka 2027.

    Hata hivyo, katika mahojiano na kituo cha Fox News Jumamosi, alisisitiza kuwa anataka makubaliano ya kudumu na utawala wa Iran.

    Wakati huo huo, taarifa zilizotolewa na vyanzo vinavyofahamu mazungumzo hayo zinaeleza kuwa Marekani na Israel zinafikiria uwezekano wa kuanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran katika kipindi cha hivi karibuni.

    Kwa mujibu wa CBS, serikali ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ina wasiwasi kuhusu kasi ambayo Iran inarejesha uwezo wake wa kuzalisha silaha.

    Kwa upande wake, Iran Alhamisi ilikanusha tuhuma za Trump kwamba huenda inatafuta kutengeneza silaha za kemikali au kibayolojia.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisema madai ya Marekani kuhusu suala hilo yamekuwa yakibadilika mara kwa mara, na kuyafananisha na madai yaliyotumiwa na Marekani kuhalalisha uvamizi wa Iraq mwaka 2003.

    Tehran ilisema madai hayo yanafuata kile ilichokiita simulizi ya udanganyifu lililotumiwa na Washington wakati huo kuhalalisha vita dhidi ya Iraq.