Vikosi vya kijeshi vinafanya nini katika shule za Iran?

JAMARAN
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Picha za wanafunzi wakipatiwa mafunzo ya matumizi ya silaha mashuleni, taarifa za wanafunzi kutakiwa kuvaa vitambulisho maalumu, pamoja na kuanzishwa kwa programu kama"Fighting Youth" na"New+Meydan", zimeibua upya mjadala kuhusu kuongezeka kwa ushawishi wa taasisi za kijeshi na vyombo vya usalama katika mfumo wa elimu wa Iran.

Mamlaka za Iran zinaeleza kuwa programu hizo ni sehemu ya mafunzo ya uzalendo, ulinzi wa taifa na malezi ya kizazi kinachoendana na misingi ya mapinduzi ya nchi hiyo. Hata hivyo, wakosoaji wanasema hatua hizo zinaashiria kuendelea kuingizwa kwa shughuli za kijeshi katika mazingira ya shule.

Uchunguzi wa makubaliano na mipango iliyotekelezwa katika miaka ya hivi karibuni unaonyesha kuwa uwepo wa taasisi za kijeshi na usalama katika shule za Iran hauishii kwenye shirika la wanafunzi la Basij pekee. Hata chini ya serikali ya Masoud Pezeshkian, programu mpya zimeendelea kutekelezwa, jambo ambalo limezua ukosoaji kuhusu kuongezeka kwa nafasi ya vyombo hivyo katika sekta ya elimu.

Tangu mwishoni mwa miaka ya 1980 na mwanzoni mwa miaka ya 1990, mradi unaojulikana kama "Circles of the Righteous" ulianza kuingizwa mashuleni kupitia shirika la Basij. Awali, mradi huo ulilenga kutoa mafunzo ya kidini kwa vijana katika misikiti na vituo vya Basij, lakini baadaye ukapanuliwa hadi mashuleni. Miongoni mwa malengo yake ilikuwa kuwahamasisha wanafunzi kushiriki katika shughuli za Basij.

Mwaka jana, Wizara ya Elimu ya Iran ilisaini makubaliano ya ushirikiano na Jeshi la Polisi la Iran. Chini ya makubaliano hayo, wizara ilitakiwa kushirikiana katika utekelezaji wa programu za vitengo mbalimbali vya polisi, ikiwemo polisi wa mtandao (FATA), kitengo cha kupambana na dawa za kulevya, polisi wa usalama barabarani, polisi wa kuzuia uhalifu pamoja na taasisi za kiintelijensia. Programu hizo zinawahusu wanafunzi, walimu na wazazi.

Wakosoaji wanaonya kuwa makubaliano hayo yanaweza kufungua njia ya kuongezeka kwa ushiriki wa vyombo vya usalama na utekelezaji wa sheria katika shughuli za shule, hatua ambayo kwao inaibua maswali kuhusu mipaka kati ya elimu na shughuli za kijeshi au kiusalama.

Mwezi uliopita, Siavash Moslemmi alielezea kile alichodai kuwa mafanikio ya mpango wa"Fighting Youth" wakati wa vita, na kutangaza kuanzishwa kwa mradi mwingine unaoitwa"New+Meydan Student League", alioueleza kuwa ni"operesheni ya pili ya pamoja."

Mradi huo ulianzishwa kwa ushirikiano wa Shirika la Uhamasishaji wa Wanafunzi (Basij), kitengo cha elimu na utamaduni cha Wizara ya Elimu ya Iran, pamoja na taasisi nyingine kadhaa. Kwa mujibu wa waandaaji wake, lengo ni kutambua, kuendeleza na kutumia uwezo wa wanafunzi katika shughuli za kijamii, utoaji wa taarifa, mawasiliano, uhamasishaji na vyombo vya habari. Programu hiyo inawahusisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari ya chini na sekondari ya juu.

Aidha, sehemu ya mradi wa"New+Meydan" inahusisha mafunzo ya kijeshi kwa wanafunzi. Katika siku za karibuni, vyombo mbalimbali vya habari vya Iran, ikiwemo wakala wa habari wa wanafunzi, vimechapisha picha zinazoonyesha wanafunzi wakipewa mafunzo ya matumizi ya silaha za moto. Hatua hiyo imechochea mjadala kuhusu kuongezeka kwa ushiriki wa taasisi za kijeshi na usalama katika mfumo wa elimu wa nchi hiyo.

Mnamo Novemba 1, msemaji wa Wizara ya Elimu ya Iran alikanusha vikali madai kuwa wanafunzi wanapewa beji za kijeshi.
Maelezo ya picha, Mnamo Novemba 1, msemaji wa Wizara ya Elimu ya Iran alikanusha vikali madai kuwa wanafunzi wanapewa beji za kijeshi.

Mbali na mipango na makubaliano mapya, elimu ya ulinzi imekuwa sehemu ya mfumo wa elimu wa Iran kwa miongo kadhaa. Tangu mwaka 1986, somo la elimu ya ulinzi limekuwa sehemu rasmi ya mtaala wa shule za sekondari. Somo hilo linajumuisha alama 12 za nadharia na alama 8 za vitendo, huku sehemu ya mafunzo ya vitendo ikitekelezwa kwa ushirikiano na vituo vya mafunzo vya Basij na vitengo vya wanafunzi wa Basij.

Katika utangulizi wa kitabu cha Maandalizi ya Ulinzi, somo hilo linaelezwa kuwa ni miongoni mwa masomo ya lazima. Mbali na mada kama ulinzi wa kiraia na ulinzi usio wa moja kwa moja, maudhui yake yanahusisha mfumo wa pamoja, mbinu za mapambano ya mtu mmoja mmoja na namna ya kukabiliana na kile kinachoitwa "vita laini".

Hata hivyo, si maudhui ya vitabu vya kiada pekee yaliyoibua mjadala katika miezi ya karibuni. Kusambaa kwa picha na taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa vikosi vya kijeshi katika baadhi ya shule, hasa za ngazi za chini, kumezua wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa mafunzo ya kijeshi katika mazingira ya elimu.

Baada ya kuchapishwa kwa picha za watoto wakijifunza kufungua na kuunganisha silaha za moto mashuleni na katika maeneo ya umma, taarifa ziliibuka kuwa baadhi ya shule zilikuwa zikiwataka wazazi kuwapatia watoto wao beji za utambulisho, jambo lililozua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii.

Katika miji ya Bandar Abbas, Kermanshah, Mashhad, Urmia na Karaj, baadhi ya wazazi walidai kuwa shule ziliwataka kuwapatia watoto wao beji za utambulisho au kwamba shule zenyewe zilikuwa zimeanza kuzitengeneza.

Suala hilo lilipata uzito zaidi baada ya kusambaa kwa video ya ukaguzi wa usalama katika shule ya wasichana. Katika video hiyo, mzima moto mmoja alimnukuu afisa wa shule akisema kuwa wanafunzi walitakiwa kuvaa beji za utambulisho. Alipoulizwa kuhusu kufanana kwa beji hizo na za kijeshi, afisa huyo alijibu:"Agizo limetoka juu."

Hata hivyo, haijabainika ni mamlaka gani iliyokusudiwa na kauli hiyo, wala kama maagizo hayo yalitolewa rasmi kwa shule.

Mnamo Novemba 1, msemaji wa Wizara ya Elimu ya Iran alikanusha vikali madai kwamba wanafunzi wanapewa beji za utambulisho wa kivita. Alisema:"Wakuu wa shule hawana mamlaka ya kutangaza masuala yanayoweza kuzua hofu miongoni mwa familia." Awali, Idara Kuu ya Elimu ya Hormozgan nayo ilikuwa imekanusha taarifa kwamba wanafunzi katika jimbo hilo walitakiwa kuvaa beji za utambulisho.

Kuibuka kwa taarifa hizi, pamoja na kuongezeka kwa mvutano wa kikanda na uvumi kuhusu uwezekano wa kuzuka kwa migogoro mipya, kumeibua maswali na wasiwasi kuhusu madhumuni ya hatua hizo na matumizi ya alama pamoja na vifaa vinavyofanana na vile vya mazingira ya vita katika shule

.

Tuhuma za Kutumia Watoto Katika Shughuli za Kijeshi: Mjadala wa Muda Mrefu

Mjadala kuhusu ushiriki wa watoto na vijana katika shughuli za kijeshi nchini Iran si mpya. Kwa miongo kadhaa, viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kurithisha maadili ya vita na mapinduzi kwa vizazi vipya, wakimtumia Fahmideh kama mmoja wa mifano ya kujitolea mhanga.

Mjadala huo uliibuka upya wakati wa maandamano ya mwaka 2009, 2022 na 2025, baada ya watoto na vijana kuonekana wakishirikiana na vikosi vya usalama.

Katika kipindi cha hivi karibuni, programu kama"Fighting Youth","New+Meydan" na kampeni ya"Sacrifice for Iran" zimefufua tena mjadala kuhusu nafasi ya watoto na vijana katika shughuli zinazohusisha taasisi za kijeshi na usalama nchini humo.

Kupewa nafasi kwa watoto na vijana katika simulizi rasmi za vita na utamaduni wa kujitolea mhanga nchini Iran ni jambo lenye historia ndefu, karibu sawa na historia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yenyewe. Mfano maarufu zaidi ni wa Mohammad Hossein Fahmideh, kijana mwenye umri wa miaka 13 ambaye Ruhollah Khomeini alimwita "kiongozi wetu."

Katika muktadha huo, viongozi wa Iran wameendelea kusisitiza umuhimu wa kurithisha maadili ya vita na mapinduzi kwa vizazi vipya. Mwaka 2020, akizungumza na kundi la wanafunzi, Ali Khamenei alisema:"Yaangazeni masuala haya ili wanafunzi wa leo wafahamu mambo makubwa yaliyofanywa na kizazi kilichopita katika umri kama wao."

Baada ya Vita vya Iran na Iraq kumalizika, suala la ushiriki wa watoto na vijana katika shughuli za kijeshi halikupewa uzito mkubwa katika vyombo vya habari kwa miaka mingi. Hata hivyo, mjadala huo ulifufuka baada ya kuonekana kwa watu wenye umri wa chini ya miaka 18 wakishiriki pamoja na vikosi vya usalama wakati wa maandamano ya Green Movement mwaka 2009, harakati za Woman, Life, Freedom mwaka 2022, na maandamano ya Januari 2025.

Katika matukio hayo, picha zilionyesha watoto na vijana waliovaa sare za Basij wakifanya kazi pamoja na vikosi vya usalama vilivyokuwa vikikabiliana na waandamanaji. Kila mara picha hizo zilipoibuka, zilizua mjadala mkali, lakini kadiri maandamano yalivyopungua, ndivyo mjadala huo ulivyofifia.

Hata hivyo, baada ya vita viwili vya hivi karibuni, mjadala kuhusu ushiriki wa watoto na vijana katika shughuli zinazohusisha taasisi za kijeshi na usalama umeibuka tena kupitia miradi kama"Fighting Youth","New+Meydan" na kampeni ya"Sacrifice for Iran".