Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran yailaumu Marekani kwa kuvunjika mazungumzo ya kusaka amani

Iran yasema kuwepo kwa matakwa mengi ya Marekani ndio yamesababisha mazungumzo ya amani kushindwa huko Islamabad

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Maharamia wateka meli nyingine karibu na pwani ya Somalia

    Mamlaka za baharini zinaonya kuhusu tishio kwa meli zinazopita katika pwani ya Somalia baada ya meli ya mizigo kukamatwa katika kitendo kinachoshukiwa kuwa cha uharamia.

    Kituo cha Biashara za Baharini cha Uingereza (UKMTO) kimeongeza kiwango cha tishio katika eneo hilo baada ya watu kuiteka meli na kuilekeza iende kwenye maji ya eneo la Somalia siku ya Jumapili.

    Meli nne zimetekwa katika matukio yanayoshukiwa kuwa ya uharamia katika wiki iliyopita ikiwemo meli ya uvuvi na meli ya mafuta.

    Miaka mitatu iliyopita uharamia ulikuwa umetoweka katika eneo hili la Bahari ya Hindi ambalo hapo awali lilikuwa maarufu kwa utekaji nyara.

    "Kutokana na tishio la uharamia meli zinashauriwa kusafiri kwa tahadhari," UKMTO ambayo inahusika na masuala ya usalama baharini imesema katika taarifa yake.

    UKMTO ilisema katika taarifa kwamba utekaji nyara huo wa siku ya Jumapili ulitokea maili sita kutoka Garacad, Somalia. Hakuna maelezo zaidi yaliyoripotiwa.

    UKMTO pia ilitoa onyo kuhusu utekaji nyara mwingine kando ya pwani ya Mareeyo, kaskazini mwa Somalia uliotokea tarehe 21 Aprili.

    Maharamia pia waliteka nyara meli ya mafuta, Honour 25, ikiwa na wafanyakazi 17 iliyokuwa ikisafiri karibu na pwani ya Somalia Aprili 22, kulingana na maafisa kadhaa wa usalama waliozungumza na BBC .

    UKMTO pia iliripoti kwamba meli ya uvuvi yenye bendera ya Somalia ilitekwa Alhamisi.

    Watu wawili wenye silaha pia walijaribu kupanda meli ya mizigo kutoka kwenye boti ndogo siku ya Alhamisi, UKMTO iliripoti, ingawa walishuka baada ya wafanyakazi wa meli hiyo kufyatua risasi za onyo.

    Kati ya mwaka 2005 na 2012, maharamia kutoka Pembe ya Afrika walipata kati ya dola milioni 339 (£266m) na dola milioni 413 (£325) kwa kuwashikilia mateka wafanyakazi na kudai malipo ya fidia, kwa mujibu wa makadirio ya Benki ya Dunia.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Watu 42 wauawa Chad katika mzozo kuhusu kisima cha maji

    Maafisa wanasema watu wasiopungua 42 wameuawa na 10 kujeruhiwa katika mapigano kati ya makabila hasimu mashariki mwa Chad katika mzozo ulioanza kuhusu kisima cha maji.

    Mgogoro katika jimbo la Wadi Fira, ambao mwanzoni ulikuwa kati ya familia mbili, uliongezeka na kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi yaliyoenea katika eneo kubwa, huku vijiji vikiteketezwa.

    Serikali ya Chad ilisema siku nya Jumapili kwamba ujumbe ulioongozwa na naibu Waziri Mkuu Limane Mahamat umetumwa katika eneo hilo na hali imedhibitiwa.

    Mapigano makali ya kijamii ni ya kawaida katika taifa hilo la Afrika ya Kati, huku kukiwa na mzozo wa muda mrefu kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na mivutano ya kikabila.

    Mapigano hayo mara nyingi husababishwa maji na ardhi ya malisho.

    Kuwasili kwa wakimbizi waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi jirani ya Sudan katika miezi ya hivi karibuni kumeongeza mvutano zaidi kuhusu rasilimali na usalama.

    Siku ya Jumapili, naibu waziri mkuu alisema serikali inachukua hatua zote muhimu kuzuia mzozo nchini Sudan usivuruge eneo la mpaka.

    Mapigano ya kijamii nchini Chad yamesababisha vifo vya mamia ya watu katika miaka ya hivi karibuni, wakiwemo 33 waliouawa mwezi Novemba kutokana na kisima kilichokuwa kinagombaniwa huko Dibebe, kusini-magharibi.

    Kulingana na shirika la kimataifa la kukabiliana na mizozo, watu 1,000 waliuawa na wengine 2,000 kujeruhiwa katika mapigano takriban 100 kati ya mwaka 2021 na 2024.

    Kundi la Haki za Binadamu la Amnesty International mwaka jana lilisema limerekodi matukio saba ya vurugu kati ya wafugaji na wakulima kati ya 2022 na 2024, na kusababisha vifo 98.

    Mapigano hayo yalisababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na masuala mengine, na licha ya vurugu zinazojirudia, serikali imeshindwa kuwalinda watu.

    Amnesty inasema mara nyingi majibu ya vikosi vya usalama huchelewa na wahusika hawawajibishwi.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Mashambulizi ya Israel yaua 14 Lebanon wakiwemo watoto wawili

    Wizara ya afya ya Lebanon inasema mashambulizi ya Israeli siku ya Jumapili yamewaua watu 14 , wakiwemo watoto wawili na wanawake wawili.

    Jeshi la Israeli (IDF) lilifanya mashambulizi ya angani kwenye maeneo ambayo lilidai yalitumika "kuendeleza mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa IDF".

    Katika taarifa tofauti, jeshi la Israeli linasema mwanajeshi wa IDF mwenye umri wa miaka 19 ameuawa na wengine sita kujeruhiwa na shambulio la ndege zisizo na rubani za Hezbollah nchini Lebanon.

    Mapigano kati ya Hezbollah na Israel nchini Lebanon yameendelea huku kukiwa na usitishaji mapigano.

    Mkataba wa kusitisha mapigano ulianza kutekelezwa tarehe 16 Aprili, na tangu wakati huo umeongezwa kwa wiki tatu.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Iran yailaumu Marekani kwa kuvunjika mazungumzo ya kusaka amani

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi anasema wingi wa matakwa ya Marekani kumesababisha mazungumzo ya amani kushindwa huko Islamabad, Pakistan, amewaambia waandishi wa habari baada ya kuwasili Urusi.

    Akiwasili St Petersburg, Araghchi anasema atashauriana na washirika wake wa Urusi kuhusu vita vya Mashariki ya Kati, katika mahojiano kwa lugha ya Kiajemi na kuchapishwa kwenye chaneli yake ya Telegram.

    Kuwasili kwa Araghchi nchini Urusi kunakuja baada ya mazungumzo na wapatanishi wa Pakistan huko Islamabad. Aliwaambia waandishi wa habari majadiliano hayo yalishughulikia masharti ambayo yanaweza kubeba mazungumzo ya kusaka amani.

    Waziri wa mambo ya nje pia alitaja kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz akisema suala hilo bado ni suala la kimataifa na anatoa wito kwa majirani ikiwemo Oman kufanya kazi na Iran kwa maslahi yao ya pamoja kwa ajili ya mlango huo.

    Kauli ya Araghchi inakuja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuvunja safari iliyopangwa ya maafisa wa Marekani kwenda Pakistani mwishoni mwa wiki kwa ajili ya mazungumzo kuhusu vita vya Mashariki ya Kati, akidai itakuwa ni kupoteza "muda."

    Pia unaweza kusoma:

  5. Gachagua afika mahakamani katika kesi ya kupinga kuondolewa madarakani

    Vikao vya kusikiliza mashauri ya kesi iliyowasilishwa na aliyekuwa Niabu wa Rais wa Kenya Rigathi Gachagua Rigathi Gachagua kutaka uamuzi wa kumuondoa madarkani ubatilishwa vimeanza leo Jumatatu jijini Nairobi.

    Mawakili wake wameiambia Mahakama Kuu kuwa mchakato wa kumuondoa madarakani ulikuwa na mapungufu mengi.

    Kiongozi wa Chama cha Demokrasia kwa Wananchi (DCP) aliwasili mahakamani Jumatatu, akifuatana na mkewe Dorcas Rigathi, wanawe wawili na timu yake ya mawakili.

    Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu.

    Gachagua aliwasilisha kesi mahakamani kupinga uhalali na uhalali wa kikatiba wa mchakato wa kumshtaki uliosababisha kuondolewa kwake madarakani kama Naibu Rais.

    Anasema mchakato huo ulikiuka taratibu, ukiukwaji wa ulinzi wa kikatiba, na kunyimwa haki yake ya kusikilizwa.

    Kesi hiyo pia inatilia shaka maamuzi na hatua zilizochukuliwa wakati na baada ya uongozi wake, huku timu yake ya wanasheria ikisisitiza baadhi ya hatua zilizochukuliwa dhidi yake zilichochewa kisiasa na hazikuwa na msingi wa kisheria.

    Kesi hiyo inatarajiwa kushughulikia maswali muhimu ya kikatiba kuhusu kuondolewa kwa Naibu Rais, mgawanyo wa madaraka, na maamuzi ya mahakama katika shughuli za bunge.

    Gachagua, alipokuwa akizungumza Mombasa siku ya Jumapili, alisema amejenga kesi ngumu kuthibitisha kwamba alifukuzwa kazi kwa misingi isiyo ya kikatiba, akionyesha imani kwa Mahakama kumpa haki.

    Gachagua aliondolewa madarakani Oktoba 2024, na kuwa naibu rais wa kwanza wa Kenya kushtakiwa, na tangu wakati huo amedai kwamba hongo zilitumika katika Bunge la Kitaifa na Seneti ili kuunga mkono kuondolewa kwake madarakani.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Kipa wa Real Zaragoza apoteza udhibiti, na kumpiga mpinzani uwanjani

    Kipa wa Real Zaragoza, Esteban Andrada, anakabiliwa na adhabu kali baada ya kumpiga mpinzani wake katika mechi ya mchuano mkali wa daraja la pili nchini Hispania dhidi ya Huesca, licha ya kuwa tayari alikuwa amefukuzwa uwanjani.

    Mchezaji huyo raia wa Argentina alipokea kadi ya pili ya njano baada ya kumdondosha mchezaji wa Huesca katika dakika za nyongeza za mchezo uliokuwa mkali wa kuamua kuepuka kushuka daraja.

    Baada ya hapo alikimbia moja kwa moja kuelekea kwa nahodha wa Huesca, Jorge Pulido, na kumpiga ngumi usoni.

    Tukio hilo lilisababisha vurugu kubwa uwanjani, na kupelekea pia kipa wa Huesca Dani Jiménez na mchezaji wa Zaragoza Dani Tasende kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

    Baadaye Andrada aliomba radhi akisema “alipoteza umakini” na yuko tayari kupokea adhabu yoyote itakayotolewa.

    Klabu ya Zaragoza pia ilitoa taarifa ikilaani vikali tukio hilo na kusema itachukua hatua za kinidhamu.

    “Tulishuhudia matukio yasiyofaa katika mchezo huu na ambayo hayakupaswa kutokea,” ilisema klabu hiyo.

    “Imeongeza kuwa matukio hayo hayaakisi maadili ya Real Zaragoza wala mashabiki wake, ambao kihistoria wamejulikana kwa nidhamu, ujasiri na heshima kwa wapinzani.”

    Kocha mkuu wa Huesca José Luis alisema baada ya mchezo kuwa tukio hilo ni “kupoteza udhibiti kabisa” na kwamba licha ya hali ya mchezo kuwa ya presha kubwa, halikubaliki.

    Huesca ilishinda mchezo huo kwa bao 1-0 kupitia Oscar Sielva, huku timu zote mbili zikiendelea kubaki katika eneo la kushuka daraja zikiwa na mechi tano zilizobaki msimu huu.

    Soma zaidi:

  7. DRC yaanzisha kikosi cha kijeshi kulinda migodi ya madini

    Mamlaka ya madini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo leo imezindua kikosi cha wanamgambo kitakachohusika na kulinda migodi, kutekeleza sheria zake na kufuatilia kwa ukaribu uzalishaji wa madini.

    Rafael Kabengele, mkuu wa shirika la madini, amesema kikosi hicho ni wazo la Rais Félix Tshisekedi kama sehemu ya mageuzi ya sekta hiyo na mapambano dhidi ya usimamizi mbovu wa madini ya thamani.

    Awamu ya kwanza ya kikosi hicho cha kijeshi itakuwa na wanajeshi kati ya 2,500 na 3,000 ambao wanatarajiwa kuanza kazi Desemba 2026 baada ya mafunzo.

    Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni nchi yenye utajiri mkubwa wa rasilimali za asili, lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa za kuhakikisha wananchi wananufaika nazo.

    Kufikia mwaka 2028, inatarajiwa kuwa watu 20,000 watakuwa wameajiriwa katika kikosi hicho kusimamia hadi migodi 22 katika maeneo mbalimbali ya nchi.

    Baadhi ya migodi, kama Rubaya mojawapo ya migodi mikubwa zaidi ya koltani duniani kwa sasa iko chini ya udhibiti wa muungano wa AFC M23.

    Kikosi hicho kipya cha dola milioni 100, kinachoitwa Walinzi wa Migodi, kitachukua nafasi ya wanajeshi wa kawaida waliokuwa wakilinda migodi, na kimefadhiliwa na Marekani na Umoja wa Falme za Kiarabu.

    Wanachama wake watasimamia uchimbaji na usafirishaji wa madini ya thamani hadi yanapotoka nchini.

    Inakadiriwa kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina utajiri wa madini usiotumika wenye thamani ya dola trilioni 25, lakini sehemu kubwa ya wananchi wake bado wanaishi katika umaskini mkubwa na vita vinavyoendelea mashariki mwa nchi.

    Soma zaidi:

  8. Ziara ya Mfalme Charles Marekani kuendelea kama ilivyopangwa

    Kasri la Buckingham linasema ziara ya kiserikali ya Mfalme Charles III nchini Marekani - ambayo inaanza baadaye leo - "itaendelea kama ilivyopangwa", japo kuna marekebisho madogo.

    Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya majadiliano kufanywa pande zote mbili za Atlantiki na ushauri kutoka kwa serikali, kulingana na taarifa ya Jumapili.

    Ikulu ilisema Mfalme "amefarijika sana" kusikia rais wa Marekani, Melania Trump na wageni wengine hawakujeruhiwa katika tukio la Wanshington.

    Mfalme Charles anatarajiwa kuhutubia mabunge yote mawili ya Congress, kutembelea ukumbusho wa 9/11 huko New York na kuhudhuria uwekaji wa shada la maua kuwaenzi wanajeshi waliokufa wa Marekani na Uingereza huko Virginia.

    Bado haijabainika ni marekebisho gani yamefanywa kwenye safari hiyo.

    Inatarajiwa kufanyika siku chache baada ya ripoti kuibuka kwamba Marekani inaweza kuktathmini msimamo wake juu ya uhuru wa Uingereza juu ya Visiwa vya Falklands.

  9. 'Tunaishi katika ulimwengu wa ajabu' - asema Trump baada ya jaribio la mauaji dhidi yake

    Tukio la shambulio la risasi kwenye dhdifa ya Waandishi wa White House linaonekana kuwa jaribio la tatu la mauaji dhidi ya Donald Trump, kufuatia matukio ya Butler, Pennsylvania mnamo Julai 2024, na katika klabu yake ya gofu huko Florida mnamo Septemba mwaka huo.

    Lakini katika mahojiano na 60 Minutes jana, Trump alisema: "Sikuwa na wasiwasi. Ninaelewa maisha. Tunaishi katika ulimwengu wa ajabu."

    Alipoulizwa kuhusu kilichojiri - ambapo JD Vance aliondolewa wa kwanza ukumbini - Trump alisema "haikuwa rahisi" kwa maafisa wa usalama kumuondoa kwenye chumba hicho.

    "Nilitaka kuona kinachofanyika.. nilitaka kuona kinachoendelea. Na kufikia wakati huo ndipo tulibaini, labda kuna kitu kibaya kimetokea."

    Alipoulizwa kuhusu "kushuka" alipokuwa akiongozwa kutoka ukumbini, Trump alijibu: "Nilianza kutembea nao [maafisa wa usalama]. Niligeuka, nikaanza kutembea, wakasema, 'Tafadhali shuka. Tafadhali shuka chini.'

    "Kwa hiyo nilishuka na yule mwanamke wa kwanza akashuka pia."

    CBS, mshirika wa habari wa BBC imeona hati iliyoandikwa inayoaminika kuhusishwa na mshukiwa, Cole Allen, ikisema alitaka kuwalenga wanachama wa utawala wa Trump "kutoka ngazi ya juu hadi chini".

    Wakati wa mahojiano ya Dakika 60, Trump alikasirishwa na mwandishi wa habari Norah O'Donnell baada ya kuuliza juu ya yaliyomo kwenye dondoo, ambayo ni yalijumuisha maneno kama vile "mnyanyasaji, mbakaji na msaliti".

    Alimsuta O'Donnell kwa kumuuliza juu ya dondoo hizo, na kuongeza kuwa "unapaswa kuona aibu kusema hivyo, kwa sababu mimi sihusiki na mambo hayo".

    Maelezo zaidi:

  10. Bei ya mafuta yapanda baada ya mazungumzo ya amani ya Marekani na Iran kukwama

    Bei ya mafuta imepanda baada ya duru ya pili ya mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Iran kukwama tena.

    Mafuta ya Brent ilipanda hadi dola 107.26 kwa pipa, wakati mafuta yasiyosafishwa ya Marekani yalipanda kwa 1% kwa dola 95.40.

    Haya yanajiri baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kusema Jumamosi kwamba Washington iliahirisha mpango wa kutuma ujumbe wake nchini Pakistan kwa mazungumzo na wenzao wa Iran.

    Ugavi wa nishati duniani umekuwa chini ya shinikizo kubwa tangu kuanza kwa vita vya Iran kwani njia kuu ya baharini ya Hormuz imefungwa.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi alisema Jumapili kwamba "majadiliano muhimu juu ya masuala ya nchi mbili na maendeleo ya kikanda" yanaendelea na Oman.

    Alichapisha kwenye mtandao wa kijamii: "Lengo letu lilijumuisha njia za kuhakikisha usafiri salama ambao ni wa kufaidisha majirani wote wapendwa na ulimwengu.

    Majirani zetu ndio kipaumbele chetu." Araghchi amewasili St Petersburg, Urusi leo Jumatatu "kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin", shirika la habari la serikali ya Iran Irna liliripoti.

    Takriban thuluthi moja ya mafuta ghafi na gesi asilia (LNG) hupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Maelzo zaidi:

  11. Vita vya Iran: Araqchi awasili Urusi kwa mazungumzo na Putin

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araqchi amewasili St. Petersburg, Urusi ambapo anatarajiwa kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow, shirika la habari la Iran, limeripoti likimnukuu balozi wa Iran nchini Urusi, Kazem Jalali.

    Bwana Araghchi alisafiri kwa ndege ya "Minab Flight 168" kuwakumbuka watoto waliouawa katika shule ya Minab, Mkoa wa Hormozgan, waliouawa katika shambulio la Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Madhumuni ya ziara ya Bw. Araqchi inaelezwa kuwa "kukutana na kujadiliana na Rais wa Urusi Vladimir Putin."

    Siku ya Jumapili, baada ya kusafiri hadi Muscat na kukutana na maafisa wa Oman, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alielekea Islamabad kwa mara ya pili katika siku tatu zilizopita, na kukutana na maafisa wa Pakistan kabla ya kuondoka kwenda Moscow.

    Maelezo ya ziara hizi na sababu ya kurejea kwake Oman na Pakistan bado haijafichuliwa.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Watu 14 wauawa Lebanon licha ya mpango wa usitishaji mapigano kufikiwa

    Wizara ya Afya ya Lebanon inasema kuwa watu 14 wakiwemo watoto wawili waliuawa Jumapili katika mashambulizi ya Israel.

    Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) hapo awali alitoa ilani ya kuhama kwa wakaazi kutoka vijiji kadhaa kusini mwa Lebanon, na kuonya kuwa wa kupuuza ilani hiyo "kungelihatarisha maisha yao".

    IDF baadaye ilisema ilifanya "mashambulizi ya angani" kuwalenga wanamgambo wa Hezbollah katika maeneo ya kusini mwa Lebanon ambayo inadai yanatumiwa "kuendeleza mashambulizi dhidi ya wanajeshiwa Israel".

    Pia imesema mwanajeshi wa IDF mwenye umri wa miaka 19 ameuawa na wengine sita kujeruhiwa na shambulio la ndege isiyo na rubani ya Hezbollah nchini Lebanon.

    Hezbollah ilirusha ndege tatu zisizo na rubani kuelekea Israeli, IDF iliripoti, huku ikiongeza kuwa ziliangushwa na jeshi la anga la Israeli kabla ya kuvuka mpaka.

    Nchi hizo mbili zilifikia mpango wa usitishaji mapigano, ambao ulianza kutekelezwa tarehe 16 Aprili na kuongezwa muda kwa wiki tatu Alhamisi wiki iliyopita.

    Chini ya makubaliano hayo, Israel inasalia na "haki yake ya kuchukua hatua zote za kujilinda, wakati wowote, dhidi ya mashambulizi yaliyopangwa, yanayokaribia, au yanayoendelea".

    Akizungumza katika mkutano wa serikali, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema IDF "inaendelea, na inafanya kazi kwa nguvu" nchini Lebanon, akisema hatua za Hezbollah "zinasambaratisha usitishaji mapigano".

    Soma zaidi:

  13. Traoré alaani mashambulizi ya Mali na kuyataja kuwa 'ya kinyama'

    Kapteni Ibrahim Traoré, rais wa muungano wa Mataifa ya Sahel (AES), amelaani mashambulizi ya kupangwa nchi ya Mali, takribani saa 48 baada ya matukio hayo.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumapili usiku, alitaja mashambulizi hayo kama "ya kinyama " na kusema "yanaungwa mkono na maadui wa mapambano ya ukombozi wa Sahel".

    Traoré aliongeza kuwa mashambulizi hayawezi "kuyumbisha nia ya watu mashujaa wa Sahel kuishi kwa uhuru, amani na heshima". Pia alitoa salamu za rambirambi kwa walioathirika.

    Alisema mashambulizi hayo yaliyoratibiwa yalipangwa kwa muda mrefu kwa madhumuni ya kuathiri vikosi vya usalama vya Mali na kuwatia hofu raia.

    Kapteni Traoré alichukua urais wa zamu wa AES mwezi Desemba, akichukua nafasi ya kiongozi wa kijeshi wa Mali, Jenerali Assimi Goïta.

    AES inayaleta pamoja mataifa ya Mali, Niger na Burkina Faso, ambayo yanaongozwa na serikali za kijeshi zilizoingia madarakani kufuatia mapinduzi katika miaka ya hivi karibuni.

    Nchi hizo tatu zilijiondoa katika Jumuiya ya kikanda ya Ecowas na tangu wakati huo zimeimarisha ushirikiano chini ya muungano huo.

    Ubia huo unalenga kuimarisha uratibu wa usalama, kuunganisha rasilimali na kukuza utangamano wa kiuchumi, ikijumuisha mipango ya miundomsingi ya pamoja, usafiri huria wa watu, na, kwa muda mrefu, soko la pamoja na sarafu.

    Soam pia:

  14. Trump na maafisa wake 'huenda' ndio walengwa wa shambulio la risasi Washington - Mamlaka

    Rais wa Marekani Donald Trump na maafisa wake ndio "huenda" walengwa wa mtu anayeshukiwa kuwa na bunduki ambaye alijaribu kuvamia dhifa ya Waandishi wa White House, kaimu Mwanasheria Mkuu wa Marekani Todd Blanche amesema.

    Mshukiwa huyo, aliyetambuliwa na vyombo vya habari vya Marekani kama Cole Tomas Allen mwenye umri wa miaka 31, alikamatwa baada ya polisi kusema alifyatua risasi karibu na kituo cha ukaguzi wakati wa tukio katika hoteli ya Washington DC siku ya Jumamosi.

    Blanche, akizungumza na NBC News, alisema nia ya mtu anayedaiwa kuwa na bunduki bado inachunguzwa, lakini matokeo ya "awali" yanaonyesha kuwa alikuwa akiwalenga maafisa wa utawala.

    Kikosi kazi cha FBI cha kitengo cha uhalifu na ugaidi kinachunguza tukio hilo.

    Baada ya kuondolewa jukwaani na kupelekwa mahali salama, Trump baadaye aliwaambia waandishi wa habari katika kikao fupi siku ya Jumamosi: "Nadhani hakuna taaluma ambayo ni hatari zaidi".

    Katika taarifa ya Jumapili, Ikulu ya White House ilisema Trump "yuko imara" baada ya kunusurika, pamoja na wajumbe wa baraza la mawaziri, "jaribio la mauaji wakati risasi zilifyatuliwa".

    Rais wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Ikulu ya White House, Weijia Jiang, alitaja shambulio hilo kuwa "la kutisha".

    Maelezo zaidi:

  15. Natumai hujambo. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja leo Jumatatu 27.04.2026