Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon yaongezwa kwa wiki tatu

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon yamesogezwa mbele kwa muda wa wiki tatu, lakini akasisitiza kuwa hatakimbilia kufikia makubaliano yoyote na Iran.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Martha Saranga

  1. Hezbollah na Israel zalaumiana kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano

    Jeshi la Israel na kundi la Hezbollah wameshutumiana kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Awali, Israel ilisema ilifanikiwa kuzuia makombora kadhaa yaliyofyatuliwa kutoka Lebanon, huku ving’ora vya tahadhari vikisikika katika eneo la Shtula.

    Kwa upande wake, Hezbollah ilithibitisha kupitia Telegram kwamba ililenga eneo hilo kwa shambulio la makombora.

    Katika taarifa yake kupitia mtandao wa X, IDF ilisema pia imewaua watu watatu inaowataja kama “wanamgambo wa Hezbollah” baada ya kushindwa kufyatua kombora kuelekea ndege ya Jeshi la Israel.

    IDF pia ilidai kuwa katika matukio mawili tofauti, Hezbollah ilifyatua makombora dhidi ya wanajeshi wake walioko kusini mwa Lebanon, ikisema kuwa hatua hizo ni “uvunjaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano.”

    Hata hivyo, Hezbollah ilijibu Alhamisi jioni ikisema ilifyatua makombora kuelekea kaskazini mwa Israel kama kujibu kile ilichokiita “uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano” uliofanywa na Israel.

    Wakati huohuo, Shirika la Habari la Taifa la Lebanon linaripoti kuwa Israel imefanya mashambulizi katika mji wa Tyre ulioko kusini mwa nchi hiyo asubuhi ya leo.

    Unaweza kusoma pia:

  2. Mataifa ya Afrika Mashariki kuanzisha mradi wa pamoja wa kiwanda cha mafuta

    Nchi za Afrika Mashariki zinaendelea kujadili mpango wa kujenga kiwanda cha pamoja cha kusafishia mafuta katika bandari ya Tanga, Tanzania, kwa mfano wa kiwanda cha Dangote cha Nigeria, amesema rais wa Kenya William Ruto siku ya Alhamisi.

    Kwa sasa, Afrika Mashariki huagiza mafuta yote yaliyosafishwa, hasa kutoka Mashariki ya Kati, hali inayofanya eneo hilo kuwa katika hatari ya kupanda kwa bei na usumbufu wa upatikanaji wa mafuta, kama ilivyoshuhudiwa wakati wa mzozo wa Iran.

    “Tutakuwa na kiwanda cha pamoja cha kusafishia mafuta Tanga ambacho kitawanufaisha wote, kwani kitachakata mafuta kutoka Jamhuri ya demokrasia ya Congo, Kenya, Sudan Kusini na Uganda,” alisema Ruto katika mkutano wa ufadhili wa miundombinu uliofanyika Nairobi.

    Mfanyabishara tajiri zaidi barani Afrika, Aliko Dangote, ambaye pia alihudhuria mkutano huo, alisema anaweza kuanzisha mradi Afrika Mashariki kama wa kiwanda chake cha Nigeria kinachozalisha mapipa 650,000 ya mafuta kwa siku, endapo serikali za eneo hilo zitaunga mkono mpango huo.

  3. Mwanajeshi wa Marekani aliyeshiriki operesheni ya Maduro akamatwa baada ya kushinda kamari

    Serikali ya Marekani inamshikilia wanajeshi mmoja aliyeshiriki katika operesheni ya kumkamata aliyekuwa rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, kwa tuhuma za kutumia taarifa za siri kufanya biashara katika kamari za kidijitali maarufu kama Polymarket.

    Mamlaka nchini Marekani imemfungulia mashitaka Gannon Ken Van Dyke, mwanajeshi wa kikosi maalum, kwa kutumia taarifa za siri kufanya biashara kwenye masoko yanayohusiana na mpango wa kumwondoa Maduro madarakani.

    Serikali imesema kitendo hicho kinahesabika kama biashara kwa kutumia taarifa za siri chini ya sheria za shirikisho ni kosa la jinai.

    Van Dyke, aliyekuwa akifanya kazi katika kambi ya Fort Bragg, North Carolina, anadaiwa kupata zaidi ya dola 409,000 kutokana na mchezo huo.

    Unaweza kusoma pia:

  4. Muda wa ziada wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon haujashusha bei ya mafuta

    Bei ya mafuta ilipanda Ijumaa barani Asia licha ya kutangazwa kwa kuongezwa kwa muda wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon.

    Brent, kiwango cha kimataifa cha mafuta ghafi, iliongezeka kwa 0.7% hadi dola 105.80 (£78.60) kwa pipa, huku mafuta ya Marekani yakipanda kwa 0.6% hadi dola 96.50 kwa pipa.

    Hata hivyo, mapigano kati ya Israel na Lebanon yanatishia kudhoofisha usitishaji huo dhaifu wa mapigano unaohusisha Marekani na Iran, baada ya Tehran kusema masharti ya makubaliano hayo yamekiukwa.

    Bei ya mafuta imekuwa ikipanda tangu Donald Trump alipotangaza kuwa Marekani itasitisha mashambulizi hadi Iran itakapowasilisha “pendekezo la pamoja.”

    Wakati huohuo, usafirishaji katika Mlango wa Bahari wa Hormuz bado unasuasua kwa kiasi kikubwa, hali inayovuruga usafirishaji wa mafuta duniani.

    Unaweza kusoma pia:

  5. Usitishaji mapigano Lebanon si wa uhakika kwa 100% - Israel

    Balozi wa Israel katika umoja wa mataifa anasema hana uhakika kuhusu hatua ya kusogezwa mbele usitishaji mapigano kama itakomesha mzozo kati ya Israel na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon.

    "Serikali ya Lebanon haidhibiti Hezbollah," Danny Dannon anasema katika mahojiano na CNN.

    "Hezbollah inatuma makombora kujaribu kuhujumu usitishaji mapigano, na Israel - tunapaswa kulipiza kisasi. Kila wakati tunapoona tishio, tunachukua hatua."

    Maoni yake yanakuja baada ya mabalozi wa Israeli na Lebanon nchini Marekani kukutana katika Ikulu ya White House ambapo Trump alitangaza kuongeza wiki tatu za usitishaji mapigano baada ya siku 10 za sasa.

    "Hayana uhakika wa 100%," anasema akimaanisha makubaliano mapya.

    "Natumai ... kuona kwamba jeshi la Lebanon linaweza kutekeleza usitishaji huu wa mapigano."

    Unaweza kusoma pia:

  6. Papa alaani mauaji ya waandamanaji nchini Iran, asisitiza msimamo wake dhidi ya vita

    Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Leo siku ya Alhamisi alilaani vikali mauaji ya waandamanaji nchini Iran, kufuatia ukosoaji kutoka kwa rais wa Marekani Donald Trump wiki iliyopita kwa madai kuwa hakuchukua msimamo huo wazi alipokuwa akizungumzia vita vinavyohusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Akiwa papa wa kwanza kutoka Marekani, Leo pia alilaani vifo vya raia wengi katika mzozo huo na kueleza masikitiko yake kuhusu kuvunjika kwa mazungumzo ya amani kati ya Marekani na Iran.

    Alitoa kauli hizo akiwa ndani ya ndege akirejea Roma baada ya ziara yake barani Afrika.

    “Ninalaani vitendo vyote visivyo vya haki. Ninalaani kuuawa kwa watu,” alisema papa alipokuwa akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu ripoti za kuuawa kwa waandamanaji nchini Iran.

    Aliongeza kusema kuwa pale ambapo serikali au taifa linachukua maamuzi yanayosababisha vifo vya watu bila haki, hatua hiyo inapaswa kulaaniwa wazi.

    Hapo awali, Aprili 12, Trump alimshambulia Papa Leo kupitia mitandao ya kijamii akimuita “asiyefaa,” baada ya kiongozi huyo wa kanisa Katoliki kuonekana kukosoa vikali vita vya Iran pamoja na sera za kupinga uhamiaji za rais huyo.

    Katika chapisho lingine siku mbili baadaye, Trump alihoji ikiwa kuna mtu angemfahamisha Papa Leo kuhusu vifo vya waandamanaji nchini Iran.

    Unaweza kusoma pia:

  7. Iran haijazuiwa kushiriki Kombe la Dunia - Marekani

    Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema hakuna mamlaka yoyote ya Marekani iliyowaambia wanamichezo wa Iran kuwa hawaruhusiwi kushiriki mashindano ya kombe la dunia FIFA yatakayofanyika nchini humo msimu huu wa joto.

    Amesema kumekuwa na uvumi kuwa Iran huenda isishiriki na kwamba Italia inaweza kuchukua nafasi yao, lakini akaongeza kuwa ikiwa Iran haitashiriki, huo utakuwa uamuzi wao wenyewe.

    Rubio alieleza kuwa tatizo si wanamichezo wa Iran, bali ni baadhi ya watu wanaoweza kuandamana nao.

    “Wasichoweza kufanya ni kuingiza magaidi wa IRGC nchini kwetu na kujifanya waandishi wa habari au wakufunzi wa michezo,” alisema.

    Unaweza pia kusoma:

  8. Makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon yaongezwa kwa wiki tatu

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon yamesogezwa mbele kwa muda wa wiki tatu, lakini akasisitiza kuwa hatakimbilia kufikia makubaliano yoyote na Iran.

    Katika tangazo lake, Trump amesema kuwa mkutano huo ulihudhuriwa pia na Makamu wa Rais JD Vance pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, na ulifanyika kwa mafanikio makubwa. “Marekani itashirikiana na Lebanon ili kuisaidia kujilinda dhidi ya Hezbollah,” aliandika Trump.

    Amesema ilikuwa “heshima kubwa” kushiriki katika mkutano huo wa kihistoria, na akaongeza kuwa anatarajia kuwapokea waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu pamoja na rais wa Lebanon Joseph Aoun katika siku zijazo.

    Trump alizungumza na vyombo vya habari akiwa katika Ofisi yake kwa mara ya pili siku hiyo, akiwa ameambatana na Vance, Rubio, pamoja na mabalozi wa Marekani nchini Lebanon na Israel, na pia mabalozi wa mataifa hayo mawili nchini Marekani.

  9. Habari karibu na katika matangazo yetu ya habari za moja kwa moja