WHO yathibitisha mlipuko wa Hantavirus duniani, waua watatu kwenye meli ya kitalii
Watu watatu wamefariki dunia kufuatia mlipuko unaoshukiwa kuwa wa virusi vya Hantavirus kwenye meli ya kitalii iliyokuwa safarini kutoka Argentina kuelekea Cape Verde, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 70 alianza kuugua akiwa ndani ya meli ya MV Hondius na kufariki alipowasili katika Kisiwa cha St Helena, huku mwili wake ukisubiri kurejeshwa nchini Uholanzi. Mke wake, mwenye umri wa miaka 69, pia aliugua na kufariki hospitalini mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Wawili hao walikuwa raia wa Uholanzi.
Kisa pekee kilichothibitishwa kuwa ni cha virusi hivyo ni ya raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 69 ambaye kwa sasa yuko hoi katika uangalizi maalum (ICU) jijini Johannesburg. Aidha, wahudumu wawili wa meli hiyo wanahitaji msaada wa haraka wa matibabu.
Maafisa wa Uholanzi wanapanga kurejesha nchini mwao watu wawili wenye dalili pamoja na mwili wa mtu wa tatu aliyefariki ambao bado uko ndani ya meli hiyo.
Virusi vya hantavirus huenezwa na panya, hasa kupitia hewa yenye chembechembe kutoka kinyesi au mkojo wa panya. Kwa kawaida, maambukizi kutoka mtu kwenda mtu ni nadra sana.
Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, Profesa Paul Griffin, amesema hali hii ni ya kushangaza kwa sababu meli za kitalii zina mazingira yanayoweza kurahisisha maambukizi kutokana na msongamano wa watu, ingawa ni nadra sana kuona hantavirus ikisambaa katika mazingira kama hayo, hasa baada ya kuboreshwa kwa viwango vya usafi tangu janga la COVID-19.