Moja kwa moja, Iran yatishia kuishambulia Marekani ikijaribu kuingia Mlango wa Hormuz

Hatua hii ni baada ya Marekani kutangaza operesheni iitwayo “Project Freedom”, ambayo itahusisha meli za kivita, ndege zaidi ya 100, mifumo ya droni pamoja na wanajeshi takriban 15,000 kusaidia kulinda usafirishaji katika eneo hilo nyeti la Bahari ya Ghuba.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Nigeria yapanga kuwarejesha raia wake wanaotaka kuondoka Afrika Kusini baada ya mashambulizi

    G

    Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

    Maelezo ya picha, Maandamano ya "March and March" huko Johannesburg mwezi Aprili yalitoa wito kwa wahamiaji haramu wa kigeni kuondoka nchini humo

    Nigeria inapanga kuwarejesha nyumbani raia wake walioko Afrika Kusini watakaokubali kurejea kwa hiari, huku hofu ikiongezeka kwamba mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya raia wa kigeni nchini humo yanaweza kuongezeka.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Bianca Odumegwu Ojukwu, amesema watu 130 tayari wamejiandikisha kwa mchakato huo, na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.

    Amesema Rais Bola Tinubu ana wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi hayo nchini Afrika Kusini, na amelaani vurugu dhidi ya raia wa kigeni pamoja na maandamano yaliyoambatana na kile alichokiita kauli za chuki dhidi ya wageni, hotuba za chuki na matamshi ya uchochezi dhidi ya wahamiaji.

    Nigeria imemuita kaimu Balozi Mkuu wa Afrika Kusini kujieleza kuhusu suala hilo.

    Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria, nchi hiyo itawasilisha rasmi wasiwasi wake mkubwa katika mkutano utakaofanyika baadaye Jumatatu, ikisema matukio hayo yanaweza kuathiri uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili.

    Taarifa hiyo imesema mkutano huo utajikita katika maandamano ya hivi karibuni yaliyoandaliwa na makundi yanayopinga wahamiaji, pamoja na matukio yaliyoripotiwa ya raia wa Nigeria kunyanyaswa na biashara zao kushambuliwa.

    Siku ya Jumapili, waziri wa mambo ya nje wa Nigeria alisema: "Maisha ya Wanigeria na biashara nchini Afrika Kusini lazima zisiendelee kuwekwa hatarini, na tunasalia kujitolea kufanya kazi kutafuta na suluhisho la kumaliza hali hiyo.''

    Ametaja pia kuuawa kwa raia wawili wa Nigeria katika matukio tofauti yaliyowahusisha maafisa wa usalama wa eneo hilo, akisema serikali ya Nigeria inadai haki itendeke.

    Mwezi uliopita, Ghana pia ilimuita balozi mkuu wa Afrika Kusini baada ya kusambaa kwa video iliyomuonyesha raia wa Ghana akihojiwa kuthibitisha uhalali wa nyaraka zake za uhamiaji.

    Hisia za kupinga wahamiaji ziliongezeka mapema mwaka huu baada ya taarifa kwamba kiongozi wa jamii ya Wanigeria katika mji wa bandari wa KuGompo, zamani East London, alitawazwa katika nafasi ya jadi inayoweza kufasiriwa kama mfalme, jambo lililotafsiriwa na baadhi ya raia wa Afrika Kusini kama jaribio la kujipatia ushawishi wa kisiasa.

    Kwa mujibu wa takwimu rasmi, Afrika Kusini ina wahamiaji wapatao milioni 2.4, sawa na chini kidogo ya asilimia nne ya idadi ya watu wake, ingawa inaaminika kuwa wengine wengi wanaishi nchini humo bila vibali rasmi.

    Wengi wao hutoka mataifa jirani kama Lesotho, Zimbabwe na Msumbiji, huku idadi ndogo ikitoka Nigeria.

    Soma zaidi:

  2. Iran yatishia kuishambulia Marekani ikijaribu kuingia Mlango wa Hormuz

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Iran imetangaza kuwa jeshi lake litashambulia majeshi ya Marekani endapo yatajaribu kuingia katika Mlango wa Hormuz, kufuatia tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu operesheni ya kusaidia meli kupita katika eneo hilo.

    Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Iran kupitia kituo cha utangazaji cha taifa IRIB, mkuu wa kamandi ya kijeshi amesema kuwa Iran itashambulia “kikosi chochote cha kijeshi cha kigeni” kitakachokaribia au kuingia katika mlango huo, hasa majeshi ya Marekani ambayo ameyaita ya “uchokozi”.

    Meja Jenerali Ali Abdollahi amesema Iran imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kuwa Mlango wa Hormuz uko chini ya udhibiti wa majeshi yake, na kwamba usafiri salama katika eneo hilo lazima uratibiwe na Tehran chini ya masharti yote.

    Tishio hilo linakuja baada ya Marekani kutangaza operesheni iitwayo “Project Freedom”, ambayo itahusisha meli za kivita, ndege zaidi ya 100, mifumo ya droni pamoja na wanajeshi takriban 15,000 kusaidia kulinda usafirishaji katika eneo hilo nyeti la Bahari ya Ghuba.

    Mvutano kati ya mataifa hayo mawili umeendelea kuongezeka, huku Mlango wa Hormuz ukiwa njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani, na hivyo kufanya hali hiyo kuwa na athari kubwa kimataifa endapo itazidi kushadidi.

  3. Chama cha Modi chakabiliwa na mtihani mkubwa katika uchaguzi muhimu India

    a

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Kura za uchaguzi wa majimbo nchini India unaendelea kuhesabiwa katika majimbo manne ya West Bengal, Tamil Nadu, Kerala na Assam, pamoja na eneo la shirikisho la Puducherry.

    Matokeo ya uchaguzi huu yanaonekana kama kipimo cha awali cha nguvu ya Waziri Mkuu Narendra Modi na chama chake cha Bharatiya Janata Party (BJP) kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2029.

    Chama cha BJP kinalenga kuendelea kushikilia madaraka katika jimbo la Assam, huku kikijaribu kuongeza ushawishi wake kusini mwa India, hususan katika majimbo ya Tamil Nadu na Kerala ambako bado kina changamoto kubwa kisiasa.

    Macho yote sasa yako katika jimbo la West Bengal, ambapo BJP inajaribu kukiondoa madarakani chama cha TMC katika kinyang’anyiro chenye ushindani mkali.

    Kampeni ya West Bengal iligubikwa na utata kufuatia marekebisho ya orodha ya wapiga kura, ambapo mamilioni ya majina yaliondolewa katika daftari la wapiga kura, hali iliyozua mjadala mkali.

    Upigaji kura na hesabu unaendelea kutarajiwa kuchukua muda zaidi, huku matokeo ya awali yakitarajiwa kuanza kutangazwa ndani ya saa chache zijazo.

  4. WHO yathibitisha mlipuko wa Hantavirus duniani, waua watatu kwenye meli ya kitalii

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watu watatu wamefariki dunia kufuatia mlipuko unaoshukiwa kuwa wa virusi vya Hantavirus kwenye meli ya kitalii iliyokuwa safarini kutoka Argentina kuelekea Cape Verde, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

    Mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka 70 alianza kuugua akiwa ndani ya meli ya MV Hondius na kufariki alipowasili katika Kisiwa cha St Helena, huku mwili wake ukisubiri kurejeshwa nchini Uholanzi. Mke wake, mwenye umri wa miaka 69, pia aliugua na kufariki hospitalini mjini Johannesburg, Afrika Kusini. Wawili hao walikuwa raia wa Uholanzi.

    Kisa pekee kilichothibitishwa kuwa ni cha virusi hivyo ni ya raia wa Uingereza mwenye umri wa miaka 69 ambaye kwa sasa yuko hoi katika uangalizi maalum (ICU) jijini Johannesburg. Aidha, wahudumu wawili wa meli hiyo wanahitaji msaada wa haraka wa matibabu.

    Maafisa wa Uholanzi wanapanga kurejesha nchini mwao watu wawili wenye dalili pamoja na mwili wa mtu wa tatu aliyefariki ambao bado uko ndani ya meli hiyo.

    Virusi vya hantavirus huenezwa na panya, hasa kupitia hewa yenye chembechembe kutoka kinyesi au mkojo wa panya. Kwa kawaida, maambukizi kutoka mtu kwenda mtu ni nadra sana.

    Mtaalamu wa magonjwa ya kuambukiza, Profesa Paul Griffin, amesema hali hii ni ya kushangaza kwa sababu meli za kitalii zina mazingira yanayoweza kurahisisha maambukizi kutokana na msongamano wa watu, ingawa ni nadra sana kuona hantavirus ikisambaa katika mazingira kama hayo, hasa baada ya kuboreshwa kwa viwango vya usafi tangu janga la COVID-19.

  5. Iran yathibitisha kupokea jibu la Marekani kuhusu pendekezo lake jipya la amani

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Iran imetangaza kuwa imepokea majibu kutoka Marekani kufuatia pendekezo lake jipya la amani, huku msemaji wa wizara ya mambo ya nje akisema ujumbe huo uliwasilishwa kupitia Pakistan na sasa unafanyiwa tathmini.

    Hata hivyo, Marekani haijathibitisha rasmi kupokea au kujibu pendekezo hilo. Rais Donald Trump amenukuliwa akisema kuwa pendekezo au mpango huo wa iran haukubaliki kwake, akieleza kuwa haukidhi matarajio ya Washington.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, mpango huo wa vipengele 14 pamoja na mengine, unaitaka Marekani kuondoa majeshi karibu na mipaka ya Iran, kusitisha vikwazo kwenye bandari zake na kumaliza mashambulizi yote, ikiwemo yanayohusishwa na Israel nchini Lebanon.

    Pendekezo hilo pia linapendekeza makubaliano yafikiwe ndani ya siku 30, likihimiza pande zote kuzingatia kumaliza vita badala ya kuendeleza usitishaji mapigano wa sasa.

    Wakati huo huo, Trump amesema Marekani itaendelea kulinda usafirishaji wa meli katika Mlango wa Hormuz na kuonya kuwa kuna uwezekano wa kurejea kwa mashambulizi iwapo Iran “itafanya makosa”.

    Mvutano kati ya mataifa hayo unaendelea huku Iran ikikanusha madai ya kutengeneza silaha za nyuklia, wakati Marekani ikisisitiza kuwa haitaruhusu taifa hilo kuwa na silaha hizo.

  6. Marekani kusaidia meli zilizokwama Hormuz - Trump

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa nchi yake itaanza operesheni maalum ya kusaidia meli zilizokwama katika Mlango bahari wa Hormuz, akieleza hatua hiyo ni kama “msaada wa kibinadamu” kwa mataifa yasiyohusika moja kwa moja na vita kati ya Marekani, Israel na Iran.

    Trump amesema operesheni hiyo itaanza rasmi leo Jumatatu, ikilenga kusaidia meli na wafanyakazi wake ambao wamekwama kwa zaidi ya miezi miwili kutokana na vizuizi vya Iran katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

    Katika ujumbe wake, Trump alisema Marekani itaziongoza meli hizo kupita salama ili ziweze kuendelea na shughuli zao, huku akionya kuwa jaribio lolote la kuingilia operesheni hiyo litakabiliwa na nguvu.

    Hatua hiyo inakuja wakati mvutano ukiendelea kuongezeka, ambapo Iran imezuia usafirishaji mafuta na bidhaa zingine kutoka Ghuba ya Uajemi, huku Marekani nayo ikiweka vikwazo kwa meli zinazotoka bandari za Iran.

    Wakati huo huo, Iran imethibitisha kuwa imepokea majibu kutoka Marekani kuhusu pendekezo lake la amani lenye masuala 14, likijumuisha madai ya kuondolewa kwa vikwazo na kusitishwa kwa mapigano, huku Tehran ikisema bado inalichambua jibu hilo.

    Hata hivyo, Trump ameashiria kutoridhishwa na pendekezo hilo la Iran, akisema huenda lisikubalike, wakati Iran ikisisitiza kuwa kwa sasa hakuna mazungumzo ya nyuklia hadi vita vitakapomalizika.

  7. Habari na karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Mei 04, 2026