Moja kwa moja, 'Ni mwanzo tu,' Iran yaionya Marekani baada ya mashambulizi katika Mlango wa Hormuz

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Iran “itafutwa kabisa duniani” ikiwa itashambulia meli zake.

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Mariam Mjahid

  1. Jumuiya ya Kiarabu yasema Iran inahatarisha 'makubaliano tete ya kusitisha mapigano'

    f

    Chanzo cha picha, EPA

    Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiarabu, Hossam Zaki, amesema shambulio la Iran dhidi ya bandari ya mafuta nchini Umoja wa Falme za Kiarabu ni jambo la kusikitisha.

    Akizungumza na BBC Radio 4, Zaki amesema hatua za Iran zinahatarisha “makubaliano tete ya kusitisha mapigano.”

    Ameongeza kuwa Jumuiya ya Kiarabu si sehemu ya mazungumzo yanayoongozwa na Pakistan, lakini inaunga mkono suluhisho lolote litakalohakikisha meli zinaendelea kupita kwa usalama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

  2. Korea Kusini yatathmini pendekezo la Trump kuhusu Mlango wa Hormuz - wizara

    Korea Kusini imesema “inatathmini pendekezo la Marekani kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz,” kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo.

    Taarifa hiyo imeongeza kuwa Seoul “inafuatilia kwa karibu” kauli za Rais Donald Trump kuhusu njia hiyo muhimu ya baharini.

    Jumatatu, Korea Kusini ilisema imeanzisha uchunguzi baada ya kile ilichokitaja kuwa “shambulio linaloshukiwa” dhidi ya meli ya mizigo katika mlango huo, kufuatia mlipuko ulioripotiwa katika chumba cha injini cha meli hiyo.

    Baadaye Trump alisema, “Huenda sasa ni wakati wa Korea Kusini kuja na kujiunga na operesheni hiyo.”

    Ikumbukwe kuwa Trump alitangaza kile alichokiita “Freedom Project” siku ya Jumapili, akisema unalenga “kuongoza” meli zilizokwama kutoka katika mlango huo.

    Kuhusu “Freedom Project,” wizara hiyo imeongeza kuwa Korea Kusini na Marekani zimekuwa zikidumisha mawasiliano ya karibu na endelevu kuhusu matumizi salama ya njia muhimu za baharini, ikiwemo Mlango wa Hormuz.

    Soma pia:

  3. Kwa nini Fujairah ni muhimu sana kwa Umoja wa Falme za Kiarabu?

    f

    Kama tulivyoripoti, Umoja wa Falme za Kiarabu umeituhumu Iran kwa kulenga eneo la sekta ya mafuta la Fujairah.

    Swali linalojitokeza sasa ni hili: Eneo la Viwanda vya Mafuta la Fujairah, linalojulikana kama FOIZ, ni nini hasa, na kwa nini lina umuhimu mkubwa kwa UAE?

    Fujairah iko katika pwani ya mashariki ya United Arab Emirates, kusini mwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, jambo linaloipa njia ya moja kwa moja kuelekea Bahari ya Arabia na Bahari ya Hindi.

    Eneo la Viwanda vya Mafuta la Fujairah ni miongoni mwa vituo vikubwa zaidi vya kuhifadhi mafuta katika Mashariki ya Kati, likiwa na uwezo wa kuhifadhi takriban mapipa milioni 70 ya mafuta.

    Kwa kulinganisha, matumizi ya mafuta duniani huzidi mapipa milioni 100 kwa siku.

    Bomba la mafuta limejengwa kutoka vituo vya mafuta vya Abu Dhabi hadi Fujairah, likiruhusu kiasi fulani cha mafuta ghafi kupakiwa kwenye meli za mafuta na kusafirishwa kwenda masoko ya kimataifa hata katika hali ambayo Mlango wa Bahari wa Hormuz umefungwa au usafirishaji wake umetatizwa.

    Kwa sababu hiyo, Fujairah ni kitovu muhimu cha kimkakati kwa usalama wa nishati wa UAE na njia mbadala ya usafirishaji wa mafuta wakati wa mivutano ya kikanda.

    Soma pia:

  4. Viongozi mbalimbali wakemea vikali shambulizi la Iran dhidi ya UAE

    Waziri mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer

    Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, amelaani mashambulizi ya makombora na droni dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kuilaumu Iran kwa matukio hayo.

    “Tunaiunga mkono UAE na tutaendelea kusaidia ulinzi wa washirika wetu katika Ghuba ya Uajemi. Mvutano huu lazima ukome. Iran lazima ijihusishe kwa dhati katika mazungumzo ili kulinda makubaliano ya kusitisha mapigano Mashariki ya Kati na kufanikisha suluhisho la kidiplomasia la muda mrefu,” amesema.

    Kwa upande wake, kwa mujibu wa shirika la habari la Saudi (SPA), Mwanamfalme wa Saudi Arabia na Waziri Mkuu Mohammed bin Salman amelaani vikali mashambulizi ya Iran dhidi ya UAE katika mazungumzo ya simu na Mohammed bin Zayed Al Nahyan, akiyataja kuwa “yasiyo na msingi.”

    SPA imesema pia Mwanamfalme huyo alisisitiza uungaji mkono wa Saudi Arabia kwa UAE katika kulinda usalama na utulivu wake.

    Vile vile, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesema katika taarifa yake kuwa analaani mashambulizi hayo, akibainisha kuwa raia watatu wa India wamejeruhiwa, na kusisitiza kuwa kulenga raia na miundombinu “hakukubaliki kabisa.”

    Ameongeza kuwa kuhakikisha usafiri salama wa baharini katika Mlango wa Hormuz ni muhimu kwa amani ya kudumu na usalama wa nishati duniani.

    Naye, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia amelaani mashambulizi ya Iran dhidi ya UAE, akiyataja kuwa yasiyo ya haki na yasiyokubalika.

    Macron amesema mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia hayawezi kukubalika kwa namna yoyote, akisisitiza uungaji mkono wa Ufaransa kwa UAE na washirika wake katika kulinda mipaka yao.

    Pia amesisitiza umuhimu wa kufunguliwa tena kwa Mlango wa Hormuz, akisema uhuru wa usafiri wa baharini ni muhimu katika kupunguza mvutano na kurejesha utulivu katika eneo hilo.

    Soma pia:

  5. Jeshi la Israel laamuru wakazi wa miji miwili kusini mwa Lebanon kuhama

    F

    Chanzo cha picha, EPA

    Jeshi la Israel limetangaza asubuhi ya Jumanne kuwa wakazi wa miji miwili iliyoko kusini mwa Lebanon wanapaswa kuondoka makwao na kuhamia maeneo salama zaidi.

    IDF imesema katika taarifa yake kuwa imelazimika kuchukua “hatua kali” dhidi ya kile inachodai kuwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano unaofanywa na Hezbollah.

    Jeshi hilo la Israel linaituhumu Hezbollah kwa kushambulia vikosi vyake kwa makombora ya milimita (mortar) mara mbili kusini mwa Lebanon, ingawa hadi sasa Hezbollah haijatoa majibu yoyote kuhusu tuhuma hizo.

    Kwa upande mwingine, Wizara ya Afya ya Lebanon imesema watu 17 wameuawa katika mashambulizi ya Israel siku ya Jumatatu, na hivyo kufikisha idadi ya vifo 110 tangu Alhamisi iliyopita.

    Israel inasema wanajeshi wake 17 wameuawa katika mapigano na Hezbollah nchini Lebanon tangu Machi, huku pia ikiishutumu kundi hilo kwa kufanya mashambulizi mamia ya roketi na droni.

    Ikumbukwe kuwa Hezbollah haikuwa sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya Israel na Lebanon mwezi uliopita, ingawa kundi hilo limesema liko tayari kuyakubali iwapo Israel itazingatia masharti ya makubaliano hayo.

    Hata hivyo, jeshi la Israel linasema makubaliano hayo yanairuhusu kuchukua hatua dhidi ya “mashambulizi,” wakati mamlaka za Lebanon zikiyapinga na kuishutumu Israel kwa kukiuka mara kwa mara makubaliano ya kusitisha mapigano.

    Soma zaidi:

  6. Obama: Netanyahu alitumia hoja zile zile kuhusu Iran katika tawala zote mbili za Marekani

    h

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, amesema katika mahojiano na jarida la The New Yorker kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitumia hoja zile zile alizotumia kumshawishi kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Iran, baadaye kumshawishi Donald Trump.

    Obama amesema kuwa wakati wa uongozi wake, Netanyahu mara kwa mara alihimiza msimamo mkali zaidi dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya kijeshi, lakini yeye alichagua njia ya diplomasia badala yake.

    Pia amehoji iwapo hatua za kijeshi zinazoendelea sasa zitawanufaisha Marekani au Israel kwa namna yoyote ya muda mrefu.

    Soma pia:

  7. Wabunge Mauritania wahukumiwa miaka minne kwa kumtukana rais kuhusu ubaguzi wa rangi

    Wabunge wawili wa upinzani wanawake nchini Mauritania wamehukumiwa kifungo cha miaka minne jela baada ya kumkashifu rais na kutoa madai ya ubaguzi wa rangi, mawakili wao waliiambia shirika la habari la Associated Press siku ya Jumatatu.

    Hatua hiyo imekuja katika taifa hilo la Afrika Magharibi ambalo kwa muda mrefu limekuwa likikosolewa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa ukiukaji wa haki za binadamu pamoja na kuendelea kwa utumwa.

    Mwezi uliopita, wabunge hao, Marieme Cheikh Dieng na Ghamou Achour, walifikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya “kushambulia mihimili za dola” na “kuitisha mikusanyiko kwa lengo la kuhatarisha usalama wa umma” baada ya kuchapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii uliomkosoa Rais Mohamed Ould Ghazouani.

    Katika machapisho kadhaa kwenye mitandao ya kijamii, wabunge hao walitaka Ghazouani aondolewe madarakani na kuutuhumu mfumo wa sheria unaotawaliwa na Waarabu kwa kuwachukulia raia Weusi pamoja na vizazi vya watumwa kama raia wa daraja la pili.

    Mawakili wa wabunge hao, Mohamed Ould Ahmed Miske, Yaghoub Ould Sèïf na Moctar Ould Ely, walithibitisha hukumu hiyo iliyotolewa na mahakama ya jinai katika mji mkuu wa Nouakchott kwa shirika la AP.

    Serikali haijatoa kauli yoyote kuhusu hukumu hiyo.

    Mauritania imekuwa ikilaumiwa kwa muda mrefu kwa ukiukaji wa haki za binadamu, huku kuendelea kuwepo kwa utumwa kukiendelea kuwa doa kubwa katika historia yake.

    Kwa karne nyingi, tabaka la kisiasa na kiuchumi la Waarabu na Amazigh nchini humo liliwafanya watu Weusi kutoka kaskazini magharibi mwa Sahara kuwa watumwa.

    Mauritania ilipiga marufuku utumwa mwaka 1981, ikiwa nchi ya mwisho duniani kufanya hivyo. Hata hivyo, makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema utumwa bado unaendelea.

    Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2023 ya Global Slavery Index, takriban watu 149,000 wanaishi katika utumwa wa kisasa nchini humo, taifa lenye idadi ya watu wasiofikia milioni tano.

    Soma zaidi:

  8. Marekani imeweka usambazaji wa nishati hatarini - Qalibaf

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mohammad Baqer Qalibaf, mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa katika uongozi wa Iran na Spika wa Bunge la nchi hiyo, amesema katika taarifa ya hivi karibuni kuwa “mkakati mpya unaendelea kuimarishwa kuhusu Mlango wa Bahari wa Hormuz.”

    Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa X, amesema kuwa “ukiukaji wa usitishaji mapigano pamoja na mzingiro uliowekwa na Marekani na washirika wake umeleta tishio kubwa kwa usalama wa usafirishaji wa baharini na usambazaji wa nishati.”

    Qalibaf amesema zaidi kuwa kile alichokitaja kama “uadui” wa utawala wa Marekani hatimaye utadhoofika.

    “Tunafahamu vyema hali hii na tunajua kuwa mazingira ya sasa hayawezi kuvumilika kwa Marekani kuendelea nayo, lakini hadi sasa hatujaanzisha rasmi hatua yoyote kwa upande wetu,” amesema kupitia ujumbe wake kwenye X.

    Qalibaf amekuwa mmoja wa viongozi wakuu waliokuwa mstari wa mbele katika duru ya mazungumzo kati ya Marekani na Iran iliyofanyika Islamabad.

    Soma pia:

  9. Waziri Mkuu wa Pakistan alaani mashambulizi ya makombora na droni dhidi ya miundombinu ya kiraia nchini UAE

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, amelaani vikali mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyolenga miundombinu ya kiraia nchini United Arab Emirates usiku wa kuamkia leo.

    Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wa X, Sharif ameeleza mshikamano kamili na Rais wa UAE, Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, akisema Pakistan inalaani kwa nguvu zote mashambulizi ya makombora na droni yaliyolenga miundombinu ya kiraia nchini humo.

    Katika taarifa hiyo, Sharif amesema kuwa Pakistan iko pamoja na ndugu zao wa Imarati pamoja na serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu katika kipindi hiki kigumu.

    Sharif amesema pia kuwa Pakistan inaona ni muhimu kwa usitishaji mapigano kuheshimiwa katika hali zote na kutekelezwa kikamilifu, ili kufungua njia ya kufikiwa kwa amani ya kudumu na utulivu katika eneo hilo kupitia mazungumzo na diplomasia.

    Soma pia:

  10. Katika Picha:Mavazi yaliyozua gumzo zaidi katika Met Gala ya mwaka huu

    Hufafanuliwa kuwa usiku mkubwa zaidi katika ulimwengu wa mitindo.

    Mastaa walifika kwenye tamasha la Met Gala la mwaka 2026 wakiwa na tafsiri zao za mada ya mwaka huu ya sanaa ya mavazi, ambapo waandalizi waliwataka wageni kujaribu mitindo ya mavazi ya kifahari, ya ubunifu na yenye mvuto wa kipekee.

    Heidi Klum

    f

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Ndiyo, huyo ni Heidi Klum. Mwanamitindo huyo maarufu alileta hulka yake ya kupenda mavazi ya kupitiliza, ambayo amezoeleka nayo hasa wakati wa Halloween, hadi kwenye Met Gala, ambapo alivaa kama moja ya sanamu nyingi za marumaru zinazopamba kumbi za makumbusho hayo.

    Katy Perry

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Katy Perry naye alionekana kuakisi taswira ya fumbo. Mwimbaji huyo wa muziki wa pop alivaa barakoa ya kipekee ya vioo iliyofunika uso wake, na kumpa mwonekano wa kutisha kiasi. Hata hivyo, barakoa hiyo iliweza kufunguka.

    Lisa

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Lisa, mwanachama wa kundi la K Pop la Blackpink, alivaa gauni jeupe la Robert Wun lenye udanganyifu wa kuvutia wa kimtazamo. Mikono ya mfano wa sanamu ilionekana kushikilia shela jeupe, huku mikono yake halisi ikibaki huru kupiga mitindo ya picha.

    Mwigizaji Sarah Paulson

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwigizaji Sarah Paulson alivaa gauni la kijivu la tulle pamoja na barakoa iliyoundwa kwa mfano wa noti ya dola, iliyofunika sehemu ya uso wake.

    Alipoulizwa na BBC barakoa hiyo iliashiria nini, alijibu kwa kifupi, “Asilimia moja.”

    Mwimbaji Sam Smith

    g

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Mwimbaji Sam Smith aliwasili akiwa amevalia joho la kuvutia la kifahari, lililoambatana na pambo kubwa la manyoya kichwani lililoufanya mwonekano wake kujitokeza zaidi.

    Tukio hilo la kila mwaka ni hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Taasisi ya Mavazi ya Metropolitan Museum of Art, na pia huwa jukwaa la watu mashuhuri pamoja na wabunifu wa mitindo kuonesha ubunifu wao wa hali ya juu kupitia mavazi ya kuvutia na ya kushangaza.

    Soma zaidi:

  11. Rais Samia ataka Kenya na Tanzania kushirikiana kukabili uanaharakati wa 'kuvuka mipaka'

    G

    Chanzo cha picha, IKULU

    Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Kenya na Tanzania kushirikiana kwa karibu kukabiliana na kile alichokitaja kuwa ni uanaharakati unaovuruga utulivu, akihimiza hatua madhubuti dhidi ya watu aliowatuhumu kutumia demokrasia kuchochea machafuko.

    Akizungumza wakati wa ziara ya kiserikali ya Rais William Ruto nchini Tanzania, Suluhu amesema suala la uanaharakati wa kuvuka mipaka pamoja na maandamano yanayoongozwa na vijana imejitokeza kwa uzito katika mazungumzo yake na kiongozi huyo wa Kenya.

    Amesema viongozi hao wamejadili namna ya kushughulikia kile alichokitaja kuwa tabia ya vijana wanaojiita Gen Z ambao, kwa mujibu wake, huzunguka wakidai kutetea demokrasia huku wakisababisha vurugu, kuchoma mali na kuvuruga utulivu wa serikali zao.

    “Tunapaswa kusimama kidete dhidi ya watu hawa. Wakija kwangu nitashughulika nao, wakija kwako washughulikie ili wajifunze kuwa na nidhamu,” amesema, akiongeza kuwa demokrasia haipaswi kutumiwa kama kisingizio cha kuvuruga serikali au kuharibu mali.

    Aidha, Suluhu alisema mifumo ya kidemokrasia inapaswa kuakisi mila, desturi na mazingira ya jamii husika badala ya kuiga mifumo kutoka nje.

    “Demokrasia isiharibu nchi zetu, mila zetu wala desturi zetu. Demokrasia haina mfumo mmoja wa wote,” alisema.

    Kauli zake zinakuja wakati serikali za Afrika Mashariki zinaendelea kuangaliwa kwa karibu kuhusu namna zinavyoshughulikia maandamano ya vijana na sauti za upinzani.

    Hivi karibuni, Kenya na Tanzania zimekumbwa na ukosoaji kutoka kwa makundi ya kutetea haki za binadamu kuhusu hatua kali dhidi ya wanaharakati.

    Nchini Kenya, maandamano dhidi ya muswada wa fedha wa mwaka 2024 yaliyoongozwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa Gen Z, yalikumbana na nguvu kubwa ya polisi, hatua iliyolaaniwa na asasi za kiraia pamoja na waangalizi wa kimataifa.

    Ripoti ya karibuni ya Freedom House imezidisha mjadala huo baada ya kuitaja Kenya na Tanzania miongoni mwa nchi zinazotuhumiwa kutumia ukandamizaji wa kuvuka mipaka, ikiwemo kuwafuatilia wapinzani wa kisiasa nje ya mipaka yao.

    Wanasiasa wa upinzani nchini Kenya walikuwa wa kwanza kujibu kauli hizo. Katibu Mkuu wa Orange Democratic Movement, Edwin Sifuna, alitetea uanaharakati akisema ni nguzo muhimu ya demokrasia. “Kama wanasema tupigwe, basi iwe hivyo. Tutaendelea kuitetea demokrasia, hata kama wanatuona kuwa ni vijana wasio na nidhamu,” Sifuna aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.

    Ruto, ambaye yuko katika ziara ya siku mbili ya kiserikali inayolenga kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika biashara, miundombinu na ushirikiano wa kikanda, hakugusia moja kwa moja matamshi ya Suluhu kuhusu wanaharakati wakati wa kuonekana kwao pamoja hadharani.

    Soma zaidi:

  12. Rais wa Marekani Donald Trump asema Iran “itafutwa kabisa duniani” ikiwa itashambulia meli zake

    Trump

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Rais wa Marekani, Donald Trump, alisema katika mahojiano na Fox News siku ya Jumatatu kwamba Iran “itafutwa kabisa duniani” ikiwa itashambulia meli za Marekani wakati wa operesheni iitwayo “Project Freedom”.

    Pia alisema Iran imekuwa “rahisi zaidi kushawishika” katika mazungumzo ya amani, huku akisisitiza kuwa Marekani ina uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi kuliko Iran.

    Kauli za Trump zilikuja baada ya kuandika kwenye Truth Social kwamba majeshi ya Marekani yalishambulia boti saba ndogo za Iran kama sehemu ya operesheni ya kufungua njia ya mlango bahari wa Hormuz. Marekani pia ilisema ilidungua droni na makombora ya Iran.

    Rais huyo alitangaza operesheni ya “Project Freedom” Jumatatu, akidai kuwa Marekani iliombwa na nchi mbalimbali duniani kusaidia kuachilia meli za kibiashara zilizokuwa zimekwama katika mlango bahari.

    Unaweza kusoma;

  13. Seneti kujadili hoja ya kumnyang'anya Uhuru Kenyatta stahiki zake

    Uhuru Kenyatta

    Chanzo cha picha, gett

    Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, amewasilisha hoja inayolenga kumnyang’anya aliyekuwa Rais mstaafu, Uhuru Kenyatta, marupurupu na stahili zake za kustaafu, akidai kuwa bado anajihusisha na siasa kikamilifu, Citizen imeripoti.

    Hoja hiyo iliwasilishwa katika Seneti siku ya Jumatatu, siku chache baada ya Kenyatta kuhutubia wajumbe wa Jubilee huko Narok kwa njia ya simu, ambapo alimshutumu Rais William Ruto kwa kujaribu kumziba mdomo.

    Cherargei alidai kuwa rais huyo wa zamani hawezi kuendelea kupokea mafao ya kustaafu huku akiwa bado kiongozi wa chama cha Jubilee zaidi ya miaka mitatu baada ya kuondoka madarakani.

    “Bado yeye ni kiongozi wa chama cha Jubilee… Katika simu hiyo alisema anataka kuendelea kuwa hai kisiasa,” alisema Samson Cherargei.

    Seneta huyo alisema kuwa hoja hiyo inatarajiwa kujadiliwa Jumanne mchana.

    “Adhabu pekee unayoweza kumpa ni kumwondolea fedha hizo na kuzitenga upya kwa mahitaji mengine tuliyo nayo katika nchi hii,” aliongeza.

    Hata hivyo, viongozi na washirika wa chama cha Jubilee walipuuza pendekezo hilo, wakisisitiza kuwa Uhuru Kenyatta ana haki ya kikatiba ya kujieleza.

    Kiongozi wa chama cha Jubilee, Fred Matiang’i, alisema kuwa mwitikio wa serikali kwa kauli za Kenyatta ulikuwa wa kupitiliza.

    “Rais wa zamani akipiga simu moja tu, serikali inapiga kelele wikendi nzima. Hawa ni watu wa aina gani?” alisema Fred Matiang’i.

    Katibu Mkuu wa Jubilee, Moitalel Ole Kenta, alisisitiza kuwa mafao ya wastaafu kwa marais wa zamani si hisani inayoweza kuondolewa wakati wowote.

    “Mafao ya kustaafu kwa Marais si zawadi ya kuondolewa kiholela. Nataka kumpa changamoto Rais William Ruto ajitokeze mwenyewe azungumzie suala hili badala ya kutumia watu wa pembeni,” alisema Kenta.

  14. Rais wa Mali Goïta ajiteua kuwa Waziri wa Ulinzi

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, Assimi Goïta

    Kiongozi wa kijeshi wa Mali, Meja Jenerali Assimi Goïta, amejiteua kushika nafasi ya Waziri wa Ulinzi, akiongeza wadhifa huo kwenye nafasi yake ya sasa ya Rais wa mpito.

    Hatua hiyo inafuatia kuuawa kwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Sadio Camara, katika mashambulizi yaliyoratibiwa na wapiganaji wa JNIM pamoja na waasi wa Tuareg FLA. Camara alikuwa na mchanfgo mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na Urusi, hivyo kifo chake ni pigo kubwa kwa jeshi la Mali.

    Kama Waziri wa Ulinzi, Goïta ambaye alitwaa madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi, sasa ataongoza moja kwa moja vyombo vya usalama akisaidiwa na Mkuu wa Majeshi ya nchi hiyo, Jenerali Oumar Diarra, aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ulinzi.

    Mali kwa sasa inakabiliwa na ongezeko kubwa la mashambulizi na kupoteza maeneo kadhaa kwa makundi ya wapiganaji.

    Goïta aliingia madarakani mwaka 2020 akiwa na cheo cha kanali, kabla ya kupanda hadi kuwa Jenerali ndani ya miaka minne.

    Wachambuzi wanamkosoa wakisema hajafanikiwa kutimiza ahadi yake ya kurejesha usalama licha ya msaada wa kijeshi kutoka Moscow.

  15. Kilichojiri saa 24 zilizopita katika vita ya Iran

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umesema Iran imefanya shambulio la kwanza la makombora na droni dhidi ya taifa hilo tangu kusitishwa kwa mapigano na Marekani kuanza Aprili 8, katika mfululizo wa matukio yanayoashiria kuongezeka tena kwa mvutano wa kijeshi katika Ghuba.

    Kwa mujibu wa taarifa za UAE, Iran ilirusha droni mbili dhidi ya meli iliyokuwa inapita katika Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

    Katika upande mwingine, Jeshi la Marekani limesema limeendesha operesheni kali katika Mlango wa Hormuz, ambapo limeshambulia na kuziharibu boti saba ndogo za kijeshi za Iran zilizodaiwa kujaribu kuingilia usafirishaji wa meli zilizo chini ya ulinzi wa Marekani.

    Rais Donald Trump amesema operesheni hiyo ni sehemu ya mpango unaoitwa “Project Freedom” unaolenga kuhakikisha meli zinapita salama katika eneo hilo.

    Aidha, Marekani imeripoti kuwa meli mbili za kibiashara zilifanikiwa kupita salama katika Mlango wa Hormuz siku ya Jumatatu, zikilindwa na jeshi la Marekani, katika juhudi za kupunguza hatari kwa wafanyakazi wa baharini.

    Iran kwa upande wake imeendelea kusisitiza kuwa inadhibiti usalama wa Mlango wa Hormuz na imetishia kuzuia au kushambulia majeshi ya kigeni yanayojaribu kuingilia eneo hilo.

    Katika upande wa kidiplomasia, Tehran imesema imepokea jibu kutoka Marekani kuhusu pendekezo lake la amani lenye mambo 14, ambalo inalenga kumaliza vita. Hata hivyo, Trump amesema huenda akalikataa pendekezo hilo, akidai Iran “bado haijalipa gharama ya kutosha,” jambo linaloacha mustakabali wa mazungumzo ukiwa na mashaka makubwa.

  16. Iran yaishambulia UAE kwa droni na makombora 15

    X

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Maelezo ya picha, UAE imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya Iran, tangu mwezi Februari, 2026

    Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), imesema imekumbwa na shambulio jipya kutoka Iran lililohusisha makombora 15 pamoja na ndege zisizo na rubani (droni), katika tukio linaloendelea kuongeza mvutano katika eneo la Ghuba.

    Kwa mujibu wa wizara ya ulinzi ya UAE, shambulio hilo lilijumuisha makombora 12 ya balistiki, makombora matatu ya cruise pamoja na droni nne. Watu watatu waliripotiwa kujeruhiwa kufuatia tukio hilo.

    UAE inasema mifumo yake ya ulinzi ilifanikiwa kudhibiti sehemu kubwa ya mashambulizi hayo kutoka Iran

    Taarifa hiyo imeongeza kuwa mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo imekuwa ikikabiliana na mashambulizi hayo tangu kuanza kwa mgogoro wa Marekani na Iran Februari 28, ikidai kuwa imezuia jumla ya makombora 549 ya balistiki, makombora 29 ya cruise na zaidi ya droni 2,260.

  17. Iran yaubeza mpango wa Marekani wa 'Project Freedom' yasema hauna suluhisho

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi ameikosoa vikali operesheni ya Marekani iitwayo “Project Freedom”, akisema haina suluhisho la kijeshi na inaweza kuongeza mkwamo katika mgogoro unaoendelea katika Mlango wa Hormuz.

    Kupitia ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Araghchi amesema matukio yanayoendelea Hormuz yanaonyesha wazi kuwa mgogoro huo ni wa kisiasa na hauwezi kutatuliwa kwa nguvu za kijeshi. Amesisitiza kuwa hatua za kijeshi zinaweza kuendeleza zaidi mzozo badala ya kuutatua.

    Kauli hiyo inakuja wakati mvutano ukiendelea kuongezeka kati ya Iran na Marekani, kufuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya boti za Iran katika eneo hilo muhimu la usafirishaji wa mafuta duniani.

    Araghchi pia ameeleza kuwa mazungumzo ya kidiplomasia yanaanza kupata muelekeo kupitia juhudi za Pakistan, na kuitaka Marekani kutochochea mzozo mkubwa zaidi.

  18. Marekani yashambulia boti saba za kijeshi za Iran huko Hormuz

    s

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema jeshi la nchi yake limeshambulia na kuziharibu boti saba ndogo za kijeshi za Iran katika Mlango bahari wa Hormuz, huku hali ya kijeshi katika njia hiyo muhimu ya usafirishaji duniani ikiendelea kuwa tete.

    Kwa mujibu wa taarifa za jeshi la Marekani, mashambulizi hayo yalitekelezwa kwa kutumia helikopta. Hata hivyo, Iran bado haijathibitisha wala kukanusha madai hayo.

    Operesheni hiyo ni sehemu ya mpango wa Marekani unaoitwa “Project Freedom”, ambao kwa mujibu wa Trump unalenga kusaidia meli zilizokwama na wafanyakazi wa baharini kuondoka salama katika Mlango wa Hormuz.

    Hata hivyo, Iran inaendelea kusisitiza kuwa mlango huo bado umefungwa na imedai kufyatua risasi za onyo dhidi ya manowari za Marekani, madai ambayo Washington imeyakanusha vikali.

    Operesheni hiyo ya kijeshi ya Marekani inahusisha meli za kivita na ndege zaidi ya 100 pamoja na wanajeshi takribani 15,000.

  19. Karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo Mei 05, 2026