Viongozi wa Uingereza na Ukraine wakutana huku mvutano na Iran ukiongezeka

Chanzo cha picha, x/Zelensky
Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, Andy Burnham, amemkaribisha Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, katika kambi ya jeshi la wanamaji ya Uingereza katika mkutano wake wa kwanza na kiongozi wa kigeni tangu aingie madarakani.
Mkutano huo umefanyika wakati uhusiano wa usalama na kisiasa kati ya Iran, Uingereza na Ukraine ukiendelea kuwa na mvutano. Kwa upande wa Uingereza, ziara hiyo imeelezwa kuwa ishara ya kuendelea kuiunga mkono Ukraine.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alizionya Uingereza na Ukraine kuhusu kile alichosema ni matokeo ya hatua zao dhidi ya Iran.
Mvutano kati ya Iran na Uingereza umeongezeka baada ya taarifa kwamba ndege ya kivita ya Marekani aina ya B-1 iliondoka katika kituo cha anga cha RAF Fairford nchini Uingereza na kufanya mashambulizi dhidi ya Iran siku moja baada ya Andy Burnham kuapishwa kuwa Waziri Mkuu. Safari ya ndege hiyo ilionekana kupitia mifumo ya kufuatilia ndege.
Baghaei alisema matumizi ya vituo vya kijeshi vya Uingereza na Marekani, pamoja na kile alichokiita "kukiri" kwa Burnham, ni ushiriki katika kitendo kinachokiuka sheria za kimataifa, na kwamba London inapaswa kuwajibishwa.
Aliongeza:
"Tulitarajia serikali mpya ya Uingereza ichukue hatua za busara zaidi kuliko serikali iliyopita, lakini kwa bahati mbaya tumeona imefuata njia ileile, na huenda hata kwa kiwango kikubwa zaidi."


































