Ni nini hasa kinachoiunganisha China na Urusi?

H
    • Author, Ankur Shah
    • Nafasi, Mhariri Mkuu, Kitengo cha China cha Kimataifa cha BBC
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Walipokuwa wakitembea katika Uwanja wa Tiananmen mjini Beijing Septemba mwaka jana, Rais wa China, Xi Jinping, na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, walionekana kujadili uwezekano wa upandikizaji wa viungo vya binadamu kuongeza kwa kiasi kikubwa maisha ya mwanadamu.

"Mwanadamu anaweza kuendelea kupandikizwa viungo. Kadiri mtu anavyoishi kwa muda mrefu, ndivyo anavyozidi kuwa kijana, na huenda hata akaweza kuishi milele," mkalimani wa Putin alisikika akisema.

"Wapo wanaotabiri kuwa katika karne hii, binadamu wanaweza kuishi hadi miaka 150," mkalimani wa Xi alijibu.

Mazungumzo hayo yalionekana kufaa kwa viongozi hao wawili wenye ushawishi mkubwa ambao hujitaja kuwa marafiki wa karibu. Baada ya miongo kadhaa madarakani, hakuna dalili kwamba wanapanga kuachia uongozi hivi karibuni.

Mazungumzo hayo ya kawaida yalitoa mwanga wa nadra kuhusu uhusiano ambao mara nyingi hueleweka vibaya. Ni miongoni mwa fursa chache ambazo umma umeweza kuona kwa karibu mahusiano ya viongozi hao wawili ambao kwa kawaida huwa wa siri sana.

Mara tu maikrofoni ilipowashwa ilitoa mtazamo wa kuvutia katika uhusiano

Chanzo cha picha, Kremlin Press Office/Anadolu via Getty Images)

Maelezo ya picha, Mara tu maikrofoni ilipowashwa ilitoa mtazamo wa kuvutia katika uhusiano wa viongozi hao wawili

Putin anatarajiwa kurejea Beijing wiki hii kuadhimisha miaka 25 ya Mkataba wa Ujirani Mwema na Ushirikiano wa Kirafiki kati ya China na Urusi.

Tofauti na ziara ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kwa Xi wiki iliyopita iliyohusisha hafla za kifahari, ziara ya Putin imeandaliwa kwa unyenyekevu zaidi na taarifa chache zimetolewa kabla ya kuanza kwake.

Baadhi ya watu mjini Washington walitarajia Trump angeweza kuishawishi Beijing ijitenge na Moscow, lakini matumaini hayo yanaonekana kuwa mbali na uhalisia.

Katika miaka ya karibuni, China na Urusi zimeeleza uhusiano wao kama "urafiki usio na mipaka". Hata hivyo, urafiki huo umejengwa juu ya nini, na unaweza kudumu kwa muda gani?

Uhusiano wenye masharti ya China

E

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa mujibu wa Alexander Gabuev, uhusiano kati ya nchi hizo mbili hauna usawa, na makubaliano mengi yanafanyika kwa masharti yanayoinufaisha China.

"Urusi imewekwa mfukoni na China, na Beijing inaweza kuwapangia masharti."

Anasema kuwa Urusi sasa inategemea sana China kiasi kwamba Beijing inaweza kuwa na uwezo mkubwa wa kuathiri mwelekeo wa mahusiano hayo.

Hali hiyo inaonekana zaidi katika sekta ya uchumi.

China ndiyo mshirika mkuu wa biashara wa Urusi, lakini Urusi inachangia takriban asilimia nne pekee ya biashara ya kimataifa ya China.

Uchumi wa China pia ni mkubwa zaidi kwa kiwango kikubwa ukilinganishwa na wa Urusi.

Miaka ya vikwazo vya Magharibi imeifanya Moscow kuimarisha zaidi biashara yake na Beijing.

Kampuni ya teknolojia ya Huawei imefaidika kutokana na kuondoka kwa kampuni nyingi za Magharibi nchini Urusi na sasa ni miongoni mwa nguzo muhimu za sekta ya mawasiliano ya nchi hiyo.

Tangu uvamizi mkubwa wa Urusi nchini Ukraine mwaka 2022, Moscow imezidi kutegemea vipuri, teknolojia na bidhaa kutoka China kwa ajili ya sekta yake ya kijeshi.

Huku uhusiano na nchi za Magharibi ukizidi kugawanyika, China imekuwa mahali pa msingi kwa utaalamu, iwe wa kiteknolojia, kisayansi au kiviwanda.

Urusi haitaki kuwa mshirika mdogo

Moscow imezidi kutegemea vifaa vya Wachina kwa mashine yake ya vita.

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

Maelezo ya picha, Moscow imezidi kutegemea vifaa vya Wachina kwa mashine yake ya vita.

Ripoti ya hivi karibuni ya Bloomberg imebaini kuwa zaidi ya asilimia 90 ya teknolojia zinazokabiliwa na vikwazo ambazo Urusi huagiza kutoka nje sasa zinatoka China, ongezeko la asilimia 10 ikilinganishwa na mwaka uliotangulia.

Urusi inafahamu vyema hatari zinazotokana na utegemezi huo.

Katika makala ya hivi karibuni iliyoandikwa na Dmitry Trenin yenye kichwa "Hatumpigii mtu magoti", alisisitiza kuwa Urusi haitaki kuwa taifa tegemezi kwa nchi nyingine.

Akizungumzia China, alisema:

"Ni muhimu sana kwetu kudumisha usawa katika mahusiano yetu na kukumbuka kwamba Urusi ni dola kubwa ambayo haiwezi kuwa mshirika wa daraja la pili."

Hata hivyo, Moscow ina chaguo chache mbadala kwa Beijing.

China ndiyo mnunuzi mkubwa anayetoa mahitaji na ukubwa wa soko unaohitajika kuiwezesha Urusi kuendelea kustahimili athari za kutengana kwake na nchi za Magharibi.

Iwapo China ingepunguza kiwango cha biashara yake na Urusi, hali hiyo ingeathiri kwa kiasi kikubwa malengo ya sera ya mambo ya nje ya Moscow.

Pamoja na hayo, nguvu kubwa ya Urusi katika kukabiliana na shinikizo la Beijing iko katika uwezo wake wa kusimama kidete na kutetea maslahi yake ya kitaifa.

China inajizuia kuisukuma Urusi

Putin na Xi walijielezea kuwa marafiki wakubwa.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Putin na Xi walijielezea kuwa marafiki wakubwa.

Kwa mujibu wa Marcin Kaczmarski, China inafahamu tofauti hiyo ya nguvu lakini haiko tayari kuisukuma Urusi kupita kiasi.

Anasema sera ya China kuelekea Urusi imejengwa juu ya tahadhari na kujizuia.

Hata kama Beijing ina nguvu kubwa zaidi kiuchumi, inafahamu kuwa Urusi ni taifa lenye fahari kubwa ya kitaifa na si rahisi kulazimishwa.

Mfano mmoja uliotajwa ni ziara ya Xi mjini Moscow mwaka 2023, ambapo inadaiwa alimhimiza Putin kutotumia silaha za nyuklia nchini Ukraine.

Siku chache baadaye, Urusi ilitangaza kupeleka silaha za nyuklia nchini Belarus, hatua iliyotafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kama ishara ya kujitegemea na kutokubali kushinikizwa.

Ingawa vita vya Urusi nchini Ukraine vimekuwa mzigo mkubwa kwa Moscow katika nyanja nyingi, pia vinaipa China manufaa fulani ya kimkakati inapozingatia chaguo zake kuhusu Taiwan.

Kwa mujibu wa Alexander Gabuev, Urusi bado ina mchango mkubwa katika teknolojia ya kijeshi.

"Urusi ina mengi ya kutoa katika eneo la teknolojia ya kijeshi, ikiwemo vifaa maalumu ambavyo bado inaweza kuuza na pia kutoa mazingira ya kufanyia majaribio baadhi ya vifaa au vipuri vya kijeshi vya China," alisema.

Nishati na usalama wa kimkakati

Urusi ni muuzaji mkubwa wa mafuta nje

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

Maelezo ya picha, Urusi ni muuzaji mkubwa wa mafuta nje

Aidha, Urusi inamiliki rasilimali kubwa za nishati ambazo zina umuhimu wa kimkakati kwa China.

Katika mkutano na waandishi wa habari mwezi Mei, Vladimir Putin alisema kuwa pande hizo mbili zilikuwa karibu kuchukua "hatua muhimu sana katika ushirikiano wa mafuta na gesi."

Kauli hiyo huenda ilihusu mradi wa bomba la gesi la Power of Siberia 2, ambalo linatarajiwa kusafirisha mita za ujazo bilioni 50 za gesi ya Urusi kwenda China kupitia Mongolia.

Kwa China, ushirikiano huo ni muhimu hasa wakati kuna wasiwasi kuhusu usalama wa usambazaji wa nishati kupitia mlango bahari wa Hormuz.

Washirika, lakini si marafiki

Kila mara China na Urusi zinapoonesha tofauti za msimamo, ukweli mmoja hubainika wazi: uhusiano wao si muungano rasmi unaoibana nchi moja kuifuata nyingine. Hivyo, kila upande unaendelea kuhifadhi uhuru wake wa kufanya maamuzi kulingana na maslahi yake ya kitaifa.

Licha ya ukaribu wao, China na Urusi si washirika wa kijeshi kwa maana rasmi.

Bobo Lo anasema nguvu ya mahusiano yao iko katika kubaki na uhuru wa kufanya maamuzi badala ya kufungwa na masharti ya muungano rasmi wa kijeshi.

Anauita uhusiano huo "ushirikiano wa kimkakati wenye kubadilika", jambo ambalo limeusaidia kudumu licha ya utabiri wa mara kwa mara kwamba ungeporomoka.

Wachambuzi wa Magharibi kwa muda mrefu wameuelezea ushirikiano kati ya China na Urusi kwa namna mbili tofauti: ama kama "mhimili wa tawala za kiimla" unaounganishwa na lengo la pamoja la kuipinga Magharibi, au kama uhusiano dhaifu unaokaribia kuvunjika wakati wowote.

Hata hivyo, mitazamo hiyo miwili haielezi kikamilifu kwa nini uhusiano huo umeendelea kuwa sehemu muhimu ya maslahi ya nchi hizo mbili jirani na kwa nini unazidi kuwa mgumu kubadilishwa, licha ya tofauti zao za kiuchumi, kisiasa na kimkakati.

Kwa mujibu wa Bobo Lo, hata kama mahusiano ya China na Urusi na nchi za Magharibi yangeimarika, bado mataifa hayo mawili yana sababu nyingi za kuendelea kushirikiana na kudumisha uhusiano wao wa karibu.

Kinachowakutanisha zaidi

Urusi na Uchina zinashiriki mpaka wa kilomita 4,300

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

Maelezo ya picha, Urusi na Uchina zinashiriki mpaka wa kilomita 4,300

Sababu kuu zinazoiunganisha China na Urusi ni pamoja na:

  • Mpaka wa pamoja wenye urefu wa kilomita 4,300.
  • Uchumi unaokamilishana, ambapo Urusi huuza nishati na malighafi huku China ikiwa soko kubwa la bidhaa hizo.
  • Upinzani wao wa pamoja dhidi ya mfumo wa dunia unaoongozwa na Marekani.
  • Kutokosoana hadharani kuhusu masuala ya ndani kama haki za binadamu.

Kwa mujibu wa Gabuev, nchi hizo mbili mara nyingi huunga mkono misimamo inayofanana katika majukwaa ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa, jambo linaloimarisha ushirikiano wao.

Je, uhusiano huu utadumu?

Miaka ya vikwazo vya nchi za Magharibi hatua kwa hatua imeisukuma Moscow kuimarisha ushirikiano wake wa kibiashara na Beijing

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Miaka ya vikwazo vya nchi za Magharibi hatua kwa hatua imeisukuma Moscow kuimarisha ushirikiano wake wa kibiashara na Beijing

Lo anaongeza kuwa pia kuna historia ndefu ya kuimarika kwa mahusiano kati ya China na Urusi.

"Mwelekeo huu wa kujenga uhusiano wa kimatendo zaidi ulianza tangu enzi za viongozi wa Umoja wa Kisovieti kama Andropov, Chernenko, Gorbachev na Yeltsin," alisema. "Nadhani China nayo imefuata mkondo huo."

Wachambuzi wengi wanaamini kuwa licha ya tofauti zilizopo, uwezekano wa kuvunjika kwa uhusiano huo katika siku za karibu ni mdogo.

Kwa hakika, alisema, taswira hiyo ni nyenzo muhimu ya kisiasa inayosaidia kuficha au kupunguza athari za tofauti za mara kwa mara za maslahi kati ya pande hizo mbili.

China bado inataka kudumisha mawasiliano na Marekani na huepuka hatua za haraka zinazoweza kuongeza mvutano wa kimataifa.

Urusi, kwa upande mwingine, mara nyingi huwa tayari kuchukua msimamo mkali zaidi.

Uhusiano wa raia wa Urusi na China

Ingawa kuna urafiki wa karibu kati ya viongozi wa juu wa China na Urusi, Charles Parton ana mashaka kuhusu kiwango cha ukaribu wa kitamaduni kati ya wananchi wa kawaida wa mataifa hayo mawili.

Anahoji iwapo Wachina wengi wangependa kwenda kusoma, kuishi au kununua nyumba mjini Moscow.

"Je, Wachina wanataka kusoma Moscow, kuhamia huko na kununua nyumba? Hapana," alisema.

Parton anaamini kwamba iwapo wangekuwa na uchaguzi mpana zaidi, Warusi wengi wangependelea kuwekeza katika nchi za Magharibi na kununua nyumba katika miji kama Paris, London au nchini Cyprus badala ya kufanya hivyo mjini Beijing.

Hii inaashiria kwamba, licha ya ushirikiano wa karibu wa kisiasa kati ya Beijing na Moscow, mvuto wa kijamii na kitamaduni kati ya wananchi wa kawaida unaweza usiwe mkubwa kwa kiwango kinachoonekana katika ngazi ya viongozi wao.

Hata hivyo, Warusi wanazidi kutumia simu za China na kuendesha magari ya Kichina, hasa kutokana na vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya Moscow.

Alexander Gabuev anaeleza kuwa:

"Muunganiko wa mifumo, misamaha ya viza, pamoja na urahisi wa malipo na usafiri vimeifanya China kuwa karibu zaidi kuliko ilivyokuwa awali."

Anaongeza kuwa programu za kubadilishana wanafunzi, ufadhili wa masomo na miradi ya pamoja ya utafiti pia zimechangia kuleta jamii za nchi hizo mbili karibu zaidi kuliko hapo awali.

f

Chanzo cha picha, Sputnik/ Kremlin/ PA/Shutterstock

Hata hivyo, maslahi yao ya pamoja katika biashara, nishati, usalama na siasa za kimataifa yanaendelea kuwaunganisha.

Kama anavyosema Bobo Lo:

"Ushirikiano kati ya China na Urusi unaendelea kuwa imara. Pande zote mbili zinafahamu kuwa ni muhimu mno kuuruhusu ushindwe, hasa kwa kuwa hakuna mbadala wa kweli wa kuendeleza ushirikiano huo."