Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Devolent Mtui: Mtanzania aliyegundua kipepeo mpya duniani
Alipofika Kihansi Kusini-Kati mwa Tanzania, Dkt. Devolent Mtui hakuwa akitafuta kipepeo mpya.
Alikuwa amepelekwa katika eneo hilo kufanya utafiti kuhusu chura wa Kihansi, lakini muda wa ziada aliokuwa nao ulimpa wazo la kuanza kuchunguza vipepeo.
Alianza kuwakusanya kama jambo la ziada, bila kujua kwamba miongoni mwa sampuli hizo angekutana na kiumbe ambacho hakikuwa katika kumbukumbu za kisayansi.
Alipogundua kipepeo huyo mwaka 2005, alianza kutafuta wataalamu ambao wangeweza kumtambua. Uchunguzi wa kina, uliokuja kujumuisha vipimo vya vinasaba, ulithibitisha kwamba alikuwa amepata aina mpya ya kipepeo.
Miaka baadaye, spishi hiyo ilipewa jina Charaxes mtuiae, likitokana na jina lake la ukoo, Mtui
"Niliona kama kitu hakiko kwenye vitabu"
Kihansi si eneo geni kwa watafiti. Kwa miaka mingi limekuwa kitovu cha tafiti mbalimbali kutokana na utajiri wake wa viumbe na mazingira yake ya kipekee.
Lakini Dkt. Mtui anasema utafiti kuhusu vipepeo haukuwa umefanyika vya kutosha katika eneo hilo dogo la takribani kilomita 20 za mraba.
"Sikuwa nafanya ili nimugundue kipepeo, hii ilikuwa kazi ya ziada katika kazi yangu maalumu iliyonipeleka Kihansi."
Alianza kukusanya vipepeo na kutambua aina mbalimbali. Hatimaye alikuwa amefuatilia zaidi ya aina 200.
Ndipo alipoona mmoja uliomfanya asimame na kujiuliza kama kweli alikuwa tayari anajulikana.
"Katika kuangalia nikaona vipepeo wazuri, nilivyoanza tu kukusanya, hakuna aliyenisimamisha, nikaona ni kama kitu hakiko kwenye vitabu."
Dkt. Mtui aliamua kutafuta msaada wa wataalamu. Kupitia mmoja wa wanazuoni, Charles Msuya, aliunganishwa na watafiti wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi kuhusu misitu ya Afrika Mashariki.
Wataalamu hao walipitia sampuli zake na kugundua kwamba miongoni mwa vipepeo 112 aliokuwa akiwafuatilia kulikuwa na mmoja ambaye hawakuweza kumtambua.
"Walipitia sampuli zote, walisema hatujui ni nani, hayupo kwenye kumbukumbu za kisayansi, wakamchukua wakaenda naye Ulaya."
Vipimo vilivyothibitisha spishi mpya
Mtui anasema, ugunduzi huo haukuwa rahisi, ulichukua karibu miaka mitatu, ikiwemo uchunguzi ambao haukuishia kwenye kumtazama kipepeo huyo kwa macho.
Wataalamu walitafuta pia mazingira yake ya asili na mmea ambao huenda ulikuwa chanzo cha chakula chake. Kipepeo huyo alipatikana katika eneo la takribani mita 950 hadi 1,000 kutoka usawa wa bahari.
Ulinganisho ulifanywa na vipepeo wengine wanaofanana kutoka Malawi, Zimbabwe na Zambia. Wataalamu walichunguza pia maumbile ya viungo vya uzazi na kugundua tofauti kati yake na spishi zilizokuwa tayari zinajulikana.
"Kwenye kuangalia spishi mpya ya kipepeo wanaangalia sehemu zao za siri, uke na ume, halafu wanakuwa wanalinganisha, wakaona zimetofautiana, wakasema huyu lazima atakuwa kipepeo spishi mpya."
Hatua iliyofuata ilikuwa vipimo vya DNA (vinasaba).
"Lakini tukasema lazima twende mbele zaidi, tukafanya vipimo vya DNA na kweli ikaonekana kwamba ni kipepeo spishi mpya."
Wataalamu wakathibitisha kwamba ni kweli spishi mpya wakaamua kumpa jina lake. "Hao wataalamu wakaamua kumuita Charaxes mtuiae, mimi nilitaka aitwe Charaxes Kihansi kuenzi na kuongeza thamani ya lile eneo la Kihansi."
Kipepeo anayehitaji msitu wake
Kwa upande wa Dkt. Mtui, ugunduzi huo haukuwa tu kuhusu kuongeza namba na jina jingine kwenye orodha ya viumbe duniani. Kipepeo huyo ana uhusiano wa karibu na mazingira yake kwa sababu hutegemea aina moja ya chakula.
Hilo linafanya uharibifu wa msitu kuwa tishio kubwa kwake.
"Upekee wa kipepeo huyu anakula chakula cha aina moja tu, ukienda pale Kihansi ukafyeka msitu mzima, ina maana na huyu umempoteza."
Lakini sifa nyingine ya kipepeo huyu ni vigumu kumwona. Katika siku 1,153 za utafiti wa kujua idadi yake kati ya mwaka 2017-2019 chini ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Pori Tanzania (TAWIRI) na Baraza la Mazingira Tanzania (NEMC), Mtui na wenzake walirekodi vipepeo wanne pekee.
Dkt. Mtui anasema spishi hiyo haingii katika mitego inayotumika katika utafiti wa vipepeo na mara nyingi hupatikana juu katika miti mirefu.
Hivyo, bila utafiti maalumu, uwepo wake unaweza kupita bila kutambuliwa. Na hapo ndipo umuhimu wa wadudu kama hawa unapojitokeza.
Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Dkt. Eblate Ernest Mjingo, anasema kila kiumbe kina nafasi katika mfumo wa ikolojia.
"Kila kiumbe katika mfumo ikolojia kina jukumu lake au kazi yake. Kwa mfano kipepeo huyu, unamuona ni mdogo sana lakini katika ikolojia ile ana kitu kikubwa sana cha kufanya, aidha ni chakula cha mnyama mwingine anayeishi pale ama kipepeo huyu anachavusha mimea ambayo iko eneo lile."
Kutoka "kichaa" hadi mwanasayansi anayefundisha wengine
Dr. Mtui mwenye Shahada ya Uzamili (MSc) kutoka Chuo Kikuu cha Witwatersrand (Afrika Kusini) na Shahada ya Uzamifu (PhD) katika Usimamizi wa Mazingira na Maliasili kutoka Chuo Kikuu cha Hawaii (Manoa, Marekani) ni miongoni mwa watafiti wabobezi wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) wanaofanya, kuratibu na kusimamia tafiti za wanyamapori nchini humo.
Mtui anatajwa kama mmoja wa wanawake wanasayansi vinara nchini Tanzania wanaochangia kwa kiasi kikubwa katika uhifadhi wa mazingira na sayansi ya viumbe hai.
Dkt. Mtui mwenye uzoefu wa zaidi ya miongo mwili kwneye utafiti, anasema alipokuwa anaanza kazi yake ya kuchunguza wadudu, si kila mtu alielewa kwa nini alikuwa akitumia muda mwingi kuwafuatilia.
"Nilivyoanza, walikuwa wakisema huyu anahangaika na wadudu, huyu ni kichaa, lakini sasa vijana wengi wanajifunza."
Kwa sasa, kazi yake imepanuka zaidi ya kukusanya vipepeo.
Akiwa mtafiti mwandamizi wa TAWIRI, amehusika katika tafiti kuhusu wadudu na uchavushaji, pamoja na miradi inayolenga kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani katika kutambua na kukusanya taarifa kuhusu wadudu.
TAWIRI pia inasema inaendelea kutoa mafunzo kwa watafiti vijana ili kuongeza uwezo wa Tanzania katika utafiti wa wanyamapori na bioanuwai.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI, Dkt. Mjingo, jina la Charaxes mtuiae lina maana zaidi ya kumuenzi mtafiti mmoja.
"Tuna wadudu wapya tumegundua bado hatujawatoa. Ndiyo maana kipepeo huyu tukampa jina lake. Tayari dunia inajua kuna mtu anaitwa Devolent Mtui, kutoka TAWIRI, Tanzania", anasema Dkt. Mjingo,
Ugunduzi huo pia unaonyesha kwamba bado kuna mengi yasiyojulikana katika mazingira yaliyohifadhiwa Tanzania.
Na kwa shughuli za Dkt. Mtui kupitia TAWIRI hayo ndiyo yanayofanya utafiti wa viumbe wadogo kuwa na thamani kubwa.
Sio bilionea, anajivunia mchango wake kwa dunia
Zaidi ya miaka 20 tangu alipokusanya sampuli ya kwanza ya kipepeo huyo, Dkt. Mtui anaangalia nyuma na kuona safari iliyozaliwa kutokana na muda wa ziada Kihansi.
Anasema vipepeo wanaweza kuwa na taarifa ambazo bado binadamu hajazigundua, huku utafiti wa wadudu ukiwa na manufaa katika uhifadhi na uwezekano wa matumizi mengine ya kisayansi.
"Faida yake anatusaidia katika uhifadhi, pia wamebeba taarifa ambayo bado hatujazifahamu, labda madawa kwa sababu yapo madawa yatokanayo na wadudu."
Anaona pia fursa za kiuchumi kupitia ufugaji wa vipepeo na biashara ya mabuu.
"Kiuchumi, wako wenye mashamba ya vipepeo, kwa wananchi kuna ile biashara ya mabuu wanauza, buu moja ni karibu dola 3-5."
Lakini anapoulizwa ni jambo gani linamfanya ajivunie zaidi baada ya miongo miwili kutokana na ugunduzi wake huo, jibu lake ni fupi.
Anatabasamu na kusema: "Ni ile fahari kwamba... hiki kitu nimekigundua."
Kisha anaongeza kwamba ugunduzi huo ni zaidi ya mafanikio binafsi. Sio kumfanya kuwa bilionea lakini kuchangia kwneye sayansi ya Tanzania na dunia.
Na katika historia hiyo, kuna jambo moja ambalo halikupangwa tangu mwanzo: mtafiti aliyekwenda Kihansi kumtafuta chura, aliondoka akiwa ameisaidia dunia kumtambua kipepeo ambaye haukuwapo kwenye vitabu.