Mambo 7 yaliyotikisa mjadala wa siasa Tanzania

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Tanzania imekuwa katika kipindi cha mijadala mikali kuhusu uelekeo wa siasa za nchi, hasa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 na matukio yaliyofuatia.

Maswali kuhusu mustakabali wa taifa, namna ya kujenga maridhiano na hatua zinazohitajika kurejesha imani miongoni mwa Watanzania yameendelea kujadiliwa katika nyanja mbalimbali.

Ni katika mazingira hayo ambapo wadau kutoka vyama tofauti vya siasa, taasisi za serikali, wanasheria, wasomi, vijana na makundi mengine walikutana Dar es Salaam kujadili hali ya kisiasa nchini.

Mjadala huo uliibua mitazamo tofauti kuhusu namna Tanzania inavyoweza kutoka katika changamoto za sasa, huku baadhi ya washiriki wakitaka hatua za haraka na wengine wakisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu na kujenga maridhiano kwanza.

Katika kongamano hilo la siku mbili lilifanyika wiki hii na lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), hoja mbalimbali ziliibuka kuhusu Tanzania ya sasa na aina ya taifa ambalo wadau wanataka kuliona katika siku zijazo.

1. Muungano

Mustakabali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulikuwa miongoni mwa hoja zilizojadiliwa kwa kina. Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, alionya kuwa mwenendo wa sasa unaweza siku moja kusababisha Muungano kuvunjika, akisisitiza kuwa Muungano ndio "gundi ya umoja" wa Watanzania.

"Mnayo yaona haya yanaelekea siku moja tutavunja Muungano. Lakini Muungano ndiyo gundi ya umoja wetu. Tukivunja Muungano tumesambaratika."

Warioba alisema anakatishwa tamaa na kile alichokiita kutokuwepo kwa jitihada za kutosha za kuimarisha Muungano.

Kwa upande mwingine, Makamu wa kwanza wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Othman Masoud alisema mjadala unapaswa kuangalia misingi ya Katiba, akisema tishio kubwa kwa Muungano linaweza kuwa Katiba yenyewe.

Alisema baadhi ya mambo yanaendeshwa kwa mazoea na kujuana badala ya kufuata Katiba, hali ambayo, kwa maoni yake, inaweza kuleta vurugu iwapo mtu ataamua kudai utekelezaji wa Katiba kikamilifu.

Sheikh Issa Ponda, kiongozi wa Shura ya Maimamu, alisema kizazi cha sasa kinataka kuona Tanganyika ikiwa na nafasi yake ndani ya Muungano, akirejea hoja ya serikali tatu iliyowahi kujadiliwa na Tume ya Jaji Warioba. Huku, Waziri wa zamani, Profesa Anna Tibaijuka akisema utambulisho wa Tanganyika hauwezi kuondolewa kwa kuimarisha utambulisho wa Zanzibar.

"Huwezi kuua Utanganyika ukalea Uzanzibari, huwezi, kwa sababu Watanganyika nao watasema na sisi tupo." Hata hivyo, Tibaijuka alisema yeye binafsi angependa kuona serikali moja, akisisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa.

Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira, kwa upande wake alihoji sera ya ACT Wazalendo ya "Zanzibar yenye mamlaka kamili", akitaka kufafanuliwa kama mamlaka hayo yanamaanisha Zanzibar kuwa dola yenye mamlaka kamili au bado kuwa sehemu ya Muungano.

2. Tundu Lissu: "Mandela wa Tanzania?

Kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ilikuwa nyingine ya hoja zilizogawanya mjadala.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alisema kumuachia Lissu ni miongoni mwa hatua muhimu zinazoweza kujenga mazingira ya maridhiano.

Akimlinganisha na rais wa zamani Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Shaibu alisema:

"Mandela wetu katika muktadha ninaouzungumza ni Tundu Lissu."

Lissu anakabiliwa na mashtaka ya uhaini katika Mahakama Kuu, huku kesi ikiwa katika hatua ya utetezi.

Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Boniface Mwabukusi, alitoa wito kwa CCM kusimamia hatua ya kufutwa kwa kesi zenye viashiria vya kisiasa, akisema hilo linaweza kuwa sehemu ya mchakato wa uponyaji wa taifa.

Lakini hoja hiyo ilipingwa na Wasira, aliyesema haelewi ni kesi zipi zinazotajwa kama "kesi za kisiasa".

"Kesi ambayo iko Mahakamani huwezi kuiita ya kisiasa, maana Mahakama hizi hazikusomea siasa, mahakama wamesomea sheria", anasema Wassira

Wasira alisema Tanzania ina mfumo wa sheria na kwamba CCM haiwezi kugeuka kuwa Mahakama na kuamua kufuta kesi.

"tuseme leo tusimame tuseme kesi zote zimefutwa utakuw aunafanya CCM igeuka kuwa Mahakama", anaongeza

Kwa mantiki hiyo, alisema masuala ya kesi yanapaswa kushughulikiwa kwa kufuata taratibu za kisheria na si kwa chama cha siasa kuingilia mamlaka ya Mahakama.

3. Maridhiano: Ukweli, haki na uwajibikaji vianzie wapi?

Neno maridhiano lilijirudia katika mijadala ya siku zote mbili.

Ado Shaibu wa ACT Wazalendo alisema ni dhahiri kuna sauti kubwa inayotaka Tanzania ifikie maridhiano, lakini akaonya kuwa maridhiano ya kweli yana masharti na misingi yake.

Alitaja mambo matatu muhimu: kumuachia Lissu, kushughulikia kesi anazodai kuwa na mwelekeo wa kisiasa, na kuweka ukweli, haki na uwajibikaji mbele katika kushughulikia vifo vilivyotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 29.

"Damu ya watu, uhai wa watu, sio kama uhai wa kuku. Ni lazima tuwe na ukweli, haki na uwajibikaji."

Kwa upande wake, Dkt Avemaria Emilius Semakafu wa Taasisi ya Ulingo alisema Tanzania inahitaji kujenga mazingira ya kuheshimu uongozi na kupunguza hali ya mvutano iliyopo.

Mwabukusi alionya dhidi ya kukimbilia mchakato wa Katiba Mpya bila kwanza kujenga mazingira ya maelewano. Alisema haoni uwezekano wa kuandika Katiba Mpya kwa utulivu ikiwa taifa bado halijaweza kukubaliana kuhusu yaliyotokea.

"Hakuna uponyaji wa taifa. Kilichosababisha vurugu za uchaguzi ni ibara kama kumi kwenye Katiba, unataka ukajadili ibara mia moja na ishirini na kitu, si tutang'ofoana macho?"

4. Katiba Mpya: Ahadi iko, utekelezaji lini?

Katiba Mpya ilikuwa mojawapo ya hoja zilizozua mjadala mkali, ikiwamo ndani ya CCM.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanataaluma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), Profesa Elgidius Ichumbaki, alihoji utekelezaji wa ahadi ya CCM ya kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya.

Alisema ilani ya uchaguzi ya CCM iliahidi kuanzisha mchakato huo ndani ya siku 100, na akauliza kwa nini wanachama wa chama hicho wanaozungumzia suala hilo wanaonekana kukumbana na matatizo.

Ichumbaki alimtaja Emmanuel Nchimbi kama mfano wa mwanasiasa ambaye msimamo wake wa hadharani kuhusu Katiba Mpya umehusishwa na hatua zilizochukuliwa dhidi yake ndani ya CCM.

Wasira alipinga hoja hiyo. Alisema si kweli kwamba mwanachama anayezungumzia mambo yanayotakiwa na wananchi anashughulikiwa kwa sababu hiyo, akisisitiza kuwa CCM yenyewe imeahidi Katiba Mpya.

Kwa upande wa ACT Wazalendo, Mwenyekiti wake, Isihaka Mchinjita, alitaka kuwe na kalenda ya utekelezaji wa mchakato huo.

Alisema Bunge lililopo linaweza kuanza mchakato wa kisheria kwa kuwasilisha na kujadili muswada unaoweza kukubaliwa na wadau.

Kuhusu mchakato huo wa katiba Wassira alisema CCM na serikali yake itaanzisha mchakato wa katiba mpya hivi karibuni.

5. Tanzania kwanza, vyama baadaye

Nafasi ya vyama vya siasa katika kujenga taifa pia ilijadiliwa, huku baadhi ya washiriki wakitaka maslahi ya taifa yawekwe mbele ya vyama.

Mwanasiasa mkongwe Ally Mzee aliwataka vijana kuwa wazalendo na kuipenda Tanzania, akisema vyama vya siasa ni taasisi zilizokuja baadaye.

"Muipende nchi yenu, vyama vya siasa ni vitu vilivyokuja tu."

Lakini Joseph Mrindoko, mmoja wa wanaounda kundi la Wachokonozi, alisema tatizo ni kwamba vijana hawasemi wenyewe bali "wanasemewa na wanaseshwa".

Alisema wazee wanashindwa kutafsiri ndoto za kizazi kipya, hali aliyohusisha na mvutano uliojitokeza wakati wa matukio ya Oktoba 29.

Mwabukusi aligusa pia suala la uwakilishi wa wananchi, akisema:

"Wabunge wanamilikiwa na vyama zaidi kuliko kuwa wawakilishi wa wananchi."

Hoja hiyo inaibua swali pana kuhusu uwajibikaji wa wawakilishi wa wananchi kwa wapiga kura wao na kwa vyama vyao.

6. Oktoba 29: Nani anawajibika kwa yaliyotokea?

Matukio ya Oktoba 29, 2025 yalikuwa miongoni mwa mambo mazito zaidi katika kongamano hilo.

Warioba kwa mfano alisema matumizi ya nguvu yanaweza kuleta utulivu lakini hayawezi kujenga amani ya kudumu.

"Kwa sasa tunafikiri bunduki ndiyo inaweza kulinda amani. Inaweza kuleta utulivu lakini hailindi amani."

Kwa mujibu wa ripoti rasmi watu 518 walifariki katika vurugu zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 29.

Warioba alisema Tanzania inahitaji kurejea katika misingi ya usawa, uadilifu, uwajibikaji na uzalendo, huku akizitaka taasisi na vyama vya siasa kutafuta njia za kuwaunganisha wananchi.

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Juma Ali Khatib, alisema yaliyotokea hayapaswi kujirudia.

"Ni wakati wa kukaa pamoja kama Watanzania kujadili namna bora ili yaliyotokea yasitokee tena."

Huku Mwabukusi akisisitiza kuwa kabla ya kuangalia mbele, taifa linahitaji ukweli, haki na uwajibikaji kuhusu yaliyotokea.

7. Utekaji: "Mtu mzima kama Polepole anaweza akayeyuka?"

Suala la utekaji na kupotezwa kwa wakosoaji lilikuwa pia sehemu ya mjadala mkali.

Mwabukusi alisema ni vigumu kujenga mazingira ya uhuru wa kujadili mustakabali wa nchi ikiwa watu wanaweza kupotea bila maelezo.

Akirejea suala la kupotea kwa Balozi na kiongizi wa zamani wa CCM, Humphrey Polepole, alisema:

"Leo kuna watu wa ngazi za juu kabisa wamepotea kama Polepole. Utaniambia niwe huru kujadili na kukosoa kwenye taifa ambalo mtu mzima kama yule anaweza akayeyuka?"

Alisema kinachohitajika si kisasi bali ukweli kuhusu kilichotokea.

"Ukweli sio kwa sababu ya kisasi, ni ili tuweze kujua tulikosea wapi."