Mkenya akamatwa kwa matamshi ya chuki dhidi ya Warundi
Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kutoka Buru Buru wamemkamata Mkenya mwenye umri wa miaka 32 kwa tuhuma za kutoa matamshi ya chuki dhidi ya Warundi wanaoishi na kufanya kazi nchini Kenya.
DCI imesema Kevin Odiwuor Otieno, maarufu kama Engineer Kevin, alitoa matamshi hayo katika mkutano wa Bunge la Mwananchi uliofanyika Jacaranda Grounds, Kayole. Matamshi hayo yalirekodiwa na kusambazwa mitandaoni, na kusababisha uchunguzi kuanzishwa.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa matamshi hayo yalilenga raia wa Burundi wanaoishi Kenya na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatano, Septemba 9, akikabiliwa na shtaka la matamshi ya chuki chini ya Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, pamoja na mashtaka mengine yatakayoibuka kutokana na uchunguzi.
DCI imesema uhuru wa kujieleza haulindi matamshi ya chuki, uchochezi wa kikabila au wito wa vurugu, na kwamba kulenga watu kwa misingi ya utaifa au kabila hakutavumiliwa.
“DCI inawakumbusha wananchi kwamba, ingawa uhuru wa kujieleza unalindwa na Katiba, hauhusishi matamshi ya chuki, uchochezi wa kikabila au kuhimiza vurugu. Kenya ni taifa lenye watu wa jamii na mataifa mbalimbali, wakiwemo raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini,” DCI ilisema.
“Kuwalenga watu binafsi au jamii kwa misingi ya utaifa au kabila, hasa pale ambapo vitendo hivyo vinalenga kuchochea chuki, uhasama au vurugu, hakutavumiliwa.”
DCI pia imewaonya wananchi dhidi ya kujichukulia sheria mkononi au kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa umma.