Kwa nini Wasyria wanazidi kuwa maskini tangu kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Mwezi Septemba mwaka huu, maandamano ya kupinga serikali yalishika kasi katika miji mbalimbali nchini Syria.

Waandamanaji walichoma magurudumu katika viwanja na barabarani, wakafunga njia na kupaza sauti kupinga uamuzi wa serikali wa kuongeza tena bei za mafuta.

Yalikuwa maandamano makubwa zaidi ya kuonyesha kutoridhishwa na maamuzi ya serikali tangu Ahmad al-Sharaa aingie madarakani nchini humo miaka miwili iliyopita.

Mmoja wa waandamanaji aliiambia televisheni ya Syria kuwa bado anaiunga mkono serikali, lakini hali yake ya maisha imekuwa mbaya kiasi kwamba hana tena fedha za kununua mkate.

"Kwa kweli, tuna hofu kuhusu uamuzi mpya ambao serikali imetangaza," alisema mwandamanaji mwingine.

Ongezeko jingine la bei za mafuta limekuwa sehemu ya mfululizo wa maamuzi ya serikali ambayo yanaendelea kuifanya hali ya maisha ya wananchi kuwa ngumu zaidi.

Baada ya waasi wakiongozwa na Al-Sharaa kuipindua serikali ya Bashar al-Assad, na kumaliza utawala wa kikatili wa familia ya Assad uliodumu kwa miaka 50 pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 13 na kuharibu nchi hiyo, hali ya maisha ya Wasyria wengi imeendelea kuzorota kwa kiasi kikubwa.

Alipoingia madarakani kama rais, Al-Sharaa alianza juhudi za kujenga upya uchumi ambao ulikuwa umeathiriwa na miaka mingi ya vita na vikwazo vya kiuchumi.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hakuna aliyekuwa na shaka kuwa hilo lilikuwa jukumu gumu sana. Hata hivyo, huenda Wasyria waliokuwa wameshuhudia kuanguka kwa utawala wa Assad walitarajia kuwa maisha yao yangeanza kuboreka ndani ya muda mfupi,wengi wakiwa na matumaini makubwa.

Hata hivyo, hali ya maisha ya wananchi haijaboreka katika kipindi cha miaka miwili tangu serikali mpya iingie madarakani.

Bei za karibu kila kitu, ikiwemo huduma za kijamii na bidhaa muhimu za kila siku, zimepanda. Ongezeko la ghafla la bei za mafuta limechukuliwa na wengi kama ishara kuwa serikali haifahamu hali halisi ya maisha ya wananchi.

"Hatutaki barabara za mzunguko! Kila siku mnajenga makutano mapya ya barabara. Wananchi waliwaunga mkono na bado wako upande wenu," alisema mmoja wa waandamanaji akielekeza ujumbe wake Al-Sharaa.

"Hata hivyo, hatua kama hizi zinaweza kuwavunja wananchi moyo na hatimaye kusababisha hasira zao kulipuka," aliongezea.

Siku chache baadaye, wakati wito wa kuitisha maandamano mapya ulipozidi kushika kasi, serikali ilibatilisha uamuzi wa kuongeza bei hizo.

.

Nilikutana na Fatima Salih Eid katika mojawapo ya maeneo ya pembezoni mwa mji wa Damascus. Alikuwa amefika sokoni kununua chakula cha kutosha kwa familia yake kwa wiki nzima. Fatima ana umri wa miaka 50 na anafanya kazi ya usafi ili kusaidia kuitunza familia yake.

"Tumepitia nyakati ngumu sana," anasema.

Mumewe hivi karibuni alipata kazi katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za kauri. Kabla ya hapo, alikuwa hana ajira kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Hata hivyo, ana bahati kwa sababu watu wengi anaowafahamu wamekuwa bila ajira kwa muda mrefu. Katika baadhi ya mitaa, wanaume hukusanyika wakitarajia kupata kazi ya siku moja, lakini mara nyingi wao husubiri bila mafanikio.

Kama sehemu ya sera za kubana matumizi, serikali ya Al-Sharaa imepunguza kwa kiasi kikubwa ruzuku za serikali zilizokuwa zikitolewa kwa miaka mingi wakati wa utawala wa Assad. Matokeo yake, bei ya mkate, ambao ni chakula kikuu kwa wananchi wengi wa Syria, imeongezeka mara kumi.

Kwa sasa, bei za mafuta nchini Syria zimefikia kiwango cha wastani cha bei katika soko la dunia. Ongezeko kubwa la bei za mafuta limewaathiri pakubwa wakulima. Gharama za aina zote za usafiri pia zimepanda, huku gharama za umeme kwa kampuni nyingi zikiongezeka.

Serikali imejaribu kupunguza hasira na kutoridhika kwa wananchi kwa kuongeza mishahara na marupurupu ya kustaafu za wafanyakazi wa sekta ya umma. Hata hivyo, kutokana na kuendelea kupanda kwa bei ya bidhaa, nyongeza hiyo ya mishahara na malipo ya uzeeni haionekani kuleta tofauti kubwa katika maisha yao.

"Siku hizi tunakula chakula cha kawaida sana. Hatuwezi kumudu kununua kuku au aina nyingine za nyama. Tunakula mboga za majani pekee, lakini hata hizo ni ghali," anasema Fatima. "Mungu akipenda, siku moja bei zitashuka"

"Nina hofu ya malipo ya umeme"

Kulingana na wa Marvan Bashur, mstaafu mwenye umri wa miaka 68, kipato chake cha kila mwezi ni takriban dola 90 za Marekani, kiasi kinacholingana na mshahara wa chini kabisa katika sekta ya umma.

"Fedha hizi hazitoshi kabisa," anasema.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), asilimia 90 ya Wasyria wanaishi kwa umaskini.

Marvan Bashur alituelezea jinsi anavyoweza kumudu maisha kwa kipato cha dola 90 kwa mwezi.

"Wakati mwingine nakopa fedha, wakati mwingine nauza vitu vilivyomo ndani ya nyumba. Kwa mfano, sufuria za zamani, sahani ambazo hatujawahi kutumia au vitu tulivyowahi kupewa kama zawadi. Hata tumelazimika kuuza baadhi ya vifaa vya nyumbani," anasema.

Pia anakabiliwa na changamoto nyingine. Kama ilivyo kwa Wasyria wengi, Marvan alikuwa akitegemea misaada ya kibinadamu ili kukidhi mahitaji yake ya msingi. Hata hivyo, kwa sasa misaada hiyo imekoma.

Kutokana na kupungua kwa ufadhili, mashirika yanayotoa misaada yamelazimika kupunguza kiwango cha msaada wanachowapatia wananchi.

.

Syria pia imekumbwa na athari za mzozo kati ya Marekani na Iran. Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, ongezeko la bei za mafuta lililosababisha maandamano kwa kiasi fulani lilichangiwa na shinikizo katika masoko ya nishati lililotokana na mvutano huo.

Nilikutana na mstaafu mwingine, Nabil al-Remhein, mwenye umri wa miaka 63. Hakuna hata mmoja kati ya watoto wake wanne ambao ni watu wazima aliyefanikiwa kupata ajira.

"Siku hizi tunakula mara moja tu kwa siku. Huu ni msiba mkubwa. Si mimi pekee, bali taifa zima linaishi katika hali hii. Sote tunateseka kwa njaa,kupanda kwa bei kunatukandamiza," alisema.

Dalili za uchovu na kukata tamaa zilionekana wazi usoni mwake.

Nabil alinipeleka nyumbani kwake. Anaishi katika kitongoji maskini chenye mitaa myembamba na nyumba za kawaida. Tulipomtembelea, mkewe alikuwa akiendelea na shughuli za nyumbani. Licha ya nyumba hiyo kuwa na giza, mwanamke huyo hakuwasha taa.

"Nina hofu ya ada ya umeme," anasema Nabil. "Tumeanza kupunguza matumizi ya taa nyumbani. Tunazima jokofu kwa takriban saa tano kila siku."

Hata hivyo, malipo ya mwisho ya umeme ilikuwa karibu sawa na theluthi moja ya kipato cha familia hiyo kwa mwezi, na hadi sasa Nabil bado hajaweza kuilipa

.

Kulingana wa Haid Haid, mchambuzi wa masuala ya Syria na mtaalamu katika kituo cha uchambuzi cha Chatham House jijini London, hali ya maisha ya wengi wa wananchi imekuwa mbaya zaidi ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya kuanguka kwa utawala wa Assad.

Kwa maoni yake, mgogoro wa kiuchumi ni "mojawapo ya changamoto hatari zaidi" zinazoikabili serikali, na serikali yenyewe inachangia kwa kiasi fulani hali hiyo.

"Mgogoro huu unahusiana kwa sehemu na ukosefu wa rasilimali za kifedha pamoja na urithi wa matatizo yaliyoachwa na utawala uliopita," alieleza.

"Lakini pia ni matokeo ya moja kwa moja ya sera mpya inayolenga kuibadilisha Syria na kuwa uchumi wa soko huria. Sera hii haizingatii jinsi mageuzi hayo yatakavyoathiri maisha ya wananchi."

.

Bila shaka, uongozi wa Syria umefanikiwa kupata matokeo muhimu katika baadhi ya maeneo.

Vikwazo vya kimataifa vilivyowekwa wakati wa utawala wa Bashar al-Assad viliondolewa, huku Marekani ikiiondoa Syria katika orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi.

Licha ya hali ya usalama nchini humo kuendelea kuwa tete na yenye kutia wasiwasi, hali kwa ujumla imekuwa tulivu kwa kiasi fulani.

Rais anaendelea kuimarisha mamlaka yake. Hasa, mwanzoni mwa mwaka huu, alifanikiwa kurejesha udhibiti wa maeneo ya kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri wa rasilimali za asili, baada ya kuziondoa vikosi vya wapiganaji wa Kikurdi.

Wakati huohuo, jamii ya Druze bado inadhibiti baadhi ya maeneo kusini mwa nchi hiyo na inajaribu kuanzisha mfumo wa kujitawala katika maeneo hayo. Israel nayo imechukua udhibiti wa baadhi ya maeneo kusini-magharibi mwa Syria.

Hata hivyo, bado ni mapema mno kuzungumzia kufufuka kwa uchumi wa nchi hiyo.

Sehemu kubwa ya Syria bado iko katika magofu kufuatia vita vilivyosababisha vifo vya watu nusu milioni na kuwalazimu nusu ya wakazi wa nchi hiyo kuyakimbia makazi yao.

Familia nyingi zimelazimika kuishi katika majengo yaliyoharibiwa kwa sehemu kwa sababu hazina uwezo wa kulipa kodi ya nyumba.

Benki ya Dunia inakadiria kuwa dola bilioni 216 zinahitajika kwa ajili ya kuijenga upya nchi hiyo. Bila misaada na uwekezaji kutoka nje, Wasyria hawataweza kuijenga upya nchi yao.

Mchumi wa Syria, Samir Aita, ambaye ni mtaalamu katika kituo cha uchambuzi cha Circle of Arab Economists kilichopo Paris, ametathmini mgogoro wa sasa kuwa umetokana na sera za serikali.

Kwa mujibu wake, serikali imeshindwa kujenga matarajio ya wananchi yanayoendana na hali halisi ya nchi, na badala yake imewajengea matumaini ambayo hayawezi kutimizwa.