Ndoto ya Madrid ilivyogeuka mtihani kwa Alexander-Arnold

Alexander-Arnold amecheza mechi saba kati ya 13 za Real Madrid msimu huu, akianza kikosini mara nne na kutoa pasi moja ya bao..
Maelezo ya picha, Alexander-Arnold amecheza mechi saba kati ya 13 za Real Madrid msimu huu, akianza kikosini mara nne na kutoa pasi moja ya bao.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Mwanzo wa msimu haujakuwa rahisi kwa Trent Alexander-Arnold.

Beki huyo wa kulia alitua Santiago Bernabeu mwezi Juni 2025 akiwa na matarajio ya kuwa chaguo la kwanza katika nafasi hiyo. Hata hivyo, ushindani mkali ndani ya kikosi umefanya mambo yawe tofauti.

Usajili wa Denzel Dumfries kutoka Inter Milan majira ya kiangazi uliimarisha ushindani upande wa kulia wa ulinzi. Sasa kocha Jose Mourinho anaonekana kumpa nafasi ya kuanza Federico Valverde, ambaye kwa asili ni kiungo, jambo ambalo limemshusha Alexander-Arnold hadi kuwa chaguo la tatu.

Hali hiyo imeibua maswali kuhusu mustakabali wake wa baadaye ndani ya kikosi na namna Mourinho anavyopanga kumtumia nyota huyo wa England.

Msimu huu, Alexander-Arnold amecheza mechi saba kati ya 13 za Real Madrid, lakini ameanza kikosini mara nne pekee. Mchango wake wa moja kwa moja ni pasi moja ya bao aliyoitoa katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Malaga.

Dakika zake uwanjani zimeendelea kupungua katika wiki za karibuni. Hakushiriki dhidi ya Roma, Sevilla na RB Leipzig, huku akicheza kwa muda mfupi tu katika El Clasico baada ya kuingia dakika za mwisho za mchezo.

Alexander-Arnold, 28, aliwasili Madrid kwa matarajio makubwa. Real ililipa euro milioni 10 (£8.33m) ili kumtoa Liverpool mapema kabla ya kumalizika kwa mkataba wake na kumruhusu kushiriki Kombe la Dunia la Klabu.

Lakini licha ya kuwa na mkataba unaoendelea hadi 2031, mustakabali wake sasa umeanza kuzua maswali.

'Ndoto iliyotimia'

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Alexander-Arnold aliingia vizuri katika mioyo ya mashabiki wa Real Madrid mara tu baada ya kuwasili kwake.

Katika hafla yake ya kwanza rasmi, alizungumza kwa Kihispania na kueleza kuwa kujiunga na Real Madrid ilikuwa "ndoto iliyotimia".

"Nina furaha na fahari kubwa kuwa hapa. Nina hamu ya kuwaonyesha klabu na mashabiki kile ninachoweza kufanya."

Wakati huo, usajili wake ulionekana kama sehemu ya mpango wa muda mrefu wa Real Madrid wa kuandaa mrithi wa Dani Carvajal katika nafasi ya beki wa kulia.

Lakini msimu wake wa kwanza haukuenda kama ilivyotarajiwa.

Katika La Liga msimu wa 2025-26, alicheza mechi 21 kati ya 38 zinazowezekana na kuanza michezo 14 pekee. Msururu wa majeraha na kukosekana kwa mwendelezo vilimzuia kujiimarisha ndani ya kikosi.

Kwa mchezaji aliyewasili akiwa na sifa kubwa kutoka Liverpool, huo ulikuwa mwanzo wa kukatisha tamaa.

Hata hivyo, mazingira kadhaa yamechangia hali hiyo.

Kwanza ni majeraha. Jeraha la msuli wa nyuma wa paja mwezi Septemba na la paja mwezi Desemba vilivuruga msimu wake wa kwanza. Kabla ya hapo, pia alipata tatizo la misuli katika maandalizi ya msimu.

Pili, kulikuwa na mabadiliko ya benchi la ufundi. Kuondoka kwa Xabi Alonso na kuwasili kwa Alvaro Arbeloa kulimlazimu kuzoea mifumo na falsafa tofauti katika mwaka wake wa kwanza.

Sasa Mourinho anakabiliwa na jukumu la kupata uwiano sahihi ndani ya kikosi chenye nyota wengi.

Je, anaweza kuondoka Real Januari?

Mourinho amekiri kwamba maamuzi yake ya uteuzi si rahisi, lakini anasisitiza kuwa maslahi ya timu ndiyo yanayokuja kwanza.

"Inaumiza. Sipendi kuona wachezaji wakijisikia vibaya. Nataka wajihisi vizuri.

Lakini kuna mambo muhimu zaidi kuliko hisia hizo. Kwa sasa niliamua kubadilisha safu ya kiungo na kumtumia Fede Valverde.

Nilikuwa naifikiria timu, si mchezaji mmoja mmoja. Trent na Dumfries walielewa kwamba ulikuwa uamuzi kwa ajili ya timu."

Mourinho pia ameisifu uwezo wa Alexander-Arnold kucheza nafasi tofauti na kuelewa maelekezo ya kimkakati.

Mapema msimu huu dhidi ya Inter Milan, alimchezesha kama kiungo wa kati pamoja na Valverde kutokana na upungufu wa viungo waliokuwa wamefungiwa.

Baada ya mchezo huo, Mourinho alisema Alexander-Arnold alitekeleza majukumu yake ya kimkakati kwa kiwango cha juu.

Licha ya ushindani uliopo, Mourinho anasisitiza kuwa kila mchezaji lazima ajisikie sehemu muhimu ya kikosi.

"Tunafanya kazi kuhakikisha kila mchezaji yuko tayari wakati wowote. Kila mmoja anatakiwa kuhisi ana nafasi ya kucheza na ana umuhimu ndani ya timu."

Liverpool Inaweza Kumrudisha?

Beki wa zamani wa Liverpool Jamie Carragher amesema angefurahia kumuona Alexander-Arnold akirejea Anfield.

"Ningemrudisha. Nadhani alifanya kosa kubwa kwenda Madrid.

Kwa hakika tumeukosa ubunifu wake."

Carragher pia aligusia hali yake ya sasa ndani ya kikosi cha Real Madrid.

"Kwa sasa ni chaguo la tatu katika nafasi ya beki wa kulia. Wanamtumia Federico Valverde katika nafasi hiyo na hata Denzel Dumfries, ambaye ndiye chaguo la kwanza, huingia kutoka benchi wakati mwingine.

Ukiwa chaguo la tatu katika klabu kubwa, ni wazi kuna uwezekano wakataka uondoke."

Kwa sasa, Alexander-Arnold atakuwa akitazamia kupata dakika zaidi katika mechi tatu zijazo za Real Madrid kabla ya mapumziko ya michezo ya kimataifa.

Pia atakuwa akipambana kulinda nafasi yake katika kikosi cha England kitakachotangazwa na Thomas Tuchel tarehe 6 Novemba kabla ya mechi za Nations League dhidi ya Croatia na Hispania.

Ingawa alirejeshwa kwenye kikosi cha England mwezi Septemba baada ya kutokuwamo tangu Juni 2025, ukosefu wa muda wa kucheza mara kwa mara katika ngazi ya klabu unaweza kuwa changamoto kwake.

Hivyo basi, Tuchel atapaswa kuamua kama ataendelea kumuamini Alexander-Arnold au kuwapa nafasi wachezaji wengine wanaowania nafasi ya beki wa kulia.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi