Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, kuvaa hijabu au kofia ya kujikinga kunaweza kusababisha nywele kupukutika?
- Author, Sajal Das Role
- Akiripoti kutoka, BBC Bangla
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Je, kuvaa kofia ya kujikinga kwa muda mrefu kunaweza kusababisha nywele kupukutika? Vipi kuhusu hijabu? Je, kufunika kichwa kwa muda mrefu kunazuia hewa kufika kwenye ngozi ya kichwa na hivyo kudhoofisha mizizi ya nywele? Na je, kubadilisha shampoo au kupaka mafuta kila siku kunaweza kuzuia nywele kupukutika?
Hizi ni baadhi ya imani zinazotawala mazungumzo kuhusu afya ya nywele. Lakini ni zipi zina ukweli, na zipi ni dhana tu?
Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha nywele kupukutika, na vilevile njia mbalimbali zinazopendekezwa kuzuia au kutibu tatizo hilo. Hata hivyo, si kila ushauri unaosambaa kuhusu afya ya nywele una msingi wa kisayansi.
Wataalamu wanasema nini kuhusu suala hili?
Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Uingereza, NHS, ni kawaida kwa mtu kupoteza nywele kati ya 50 na 100 kwa siku. Hata hivyo, iwapo utagundua kuwa nywele zinapukutika kwa wingi kuliko kawaida, unashauriwa kumwona daktari bingwa mapema.
Kitaalamu, hali ya kupoteza nywele kwa kiwango kikubwa kuliko kawaida, bila nywele mpya kuota kwa kasi inayolingana, huitwa alopecia.
Kwa mujibu wa takwimu za NHS, zaidi ya watu milioni 140 duniani wana tatizo la alopecia, linaloweza kusababisha upotevu wa nywele kwa sehemu au kichwa kizima.
Wataalamu wanaeleza kuwa kupukutika kwa nywele ni sehemu ya mchakato wa kawaida wa mwili. Hata hivyo, wakati mwingine kunaweza kusababishwa na magonjwa, mabadiliko ya homoni, lishe duni au msongo wa mawazo.
Kwa hiyo, ni muhimu kuelewa kiwango cha kawaida cha kupoteza nywele, wakati hali hiyo inapokuwa tatizo na kutambua kuwa baadhi ya imani maarufu kuhusu nywele hazina ukweli.
Kwa nini nywele hupukutika?
Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha nywele kupukutika, na hutofautiana kati ya mtu na mtu. Baadhi ya watu hupoteza nywele kutokana na urithi wa vinasaba, wengine kutokana na kutotunza vizuri nywele na ngozi ya kichwa, huku kwa wengine tatizo hilo likihusiana na umri.
Pia, namna nywele zinavyopukutika hutofautiana kati ya wanaume na wanawake.
Kwa wanaume, aina inayojulikana zaidi ya upara huitwa androgenetic alopecia. Hali hii husababisha nywele kuanza kupukutika katika pande zote mbili za paji la uso, huku upara ukionekana pia katikati ya kichwa.
Kwa wanawake, mara nyingi nywele hupungua katika eneo la katikati ya kichwa, na mstari unaotenganisha nywele unaweza kuonekana kupanuka. Hali hii inaweza kusababishwa na urithi wa vinasaba au mabadiliko ya homoni mwilini. Tatizo hilo linaweza kuongezeka kadiri mwanamke anavyozeeka.
Kwa wanawake, tatizo la uvimbe kwenye vifuko vya mayai linalojulikana kama polycystic ovary syndrome (PCOS), pamoja na mabadiliko ya homoni wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua, linaweza pia kusababisha nywele kupukutika.
Vilevile, kiwango cha homoni za tezi ya shingo kuwa juu au chini kuliko kawaida kinaweza kuchangia tatizo hilo.
Daktari bingwa wa ngozi na upasuaji wa urembo, Dkt Shaila Haq, anasema kupukutika kwa nywele kunaweza kusababishwa na urithi wa vinasaba au kutokuwiana kwa homoni mwilini.
Akizungumza na BBC, alisema watu wenye lishe duni, hasa upungufu wa madini ya chuma, vitamini D na zinki, wanaweza kukumbwa na tatizo la kupukutika kwa nywele. Msongo mkubwa wa mawazo na wasiwasi pia vinaweza kuchangia hali hiyo.
Kwa mujibu wa Dkt Haq, namna nywele zinavyopukutika kwa wanaume hutofautiana na kwa wanawake.
Anasema wanawake wengi hupoteza nywele kutokana na kutokuwiana kwa homoni na upungufu wa vitamini D.
Nywele kwa kiasi kikubwa huundwa na protini iitwayo keratini. Upungufu wa protini, madini ya chuma, zinki, vitamini D, vitamini B12 na biotini mwilini unaweza kuzifanya nywele kuwa dhaifu.
Wanawake wengi nchini Bangladesh wanakabiliwa na upungufu wa damu unaosababishwa na ukosefu wa madini ya chuma. Hali hiyo ni miongoni mwa sababu zinazochangia kupukutika kwa nywele.
Vilevile, kupungua kwa uzito ghafla kutokana na kujinyima chakula, kufunga kula kwa muda mrefu au matatizo ya ulaji kunaweza kusababisha nywele kupukutika kwa wingi.
Baadhi ya watu pia hupata tatizo la nywele kupukutika ghafla miezi miwili hadi mitatu baada ya kupitia msongo wa mawazo, homa kali, magonjwa kama surua, homa ya matumbo na COVID 19, kufanyiwa upasuaji au kujifungua.
Magonjwa ya ngozi kama fangasi, ugonjwa wa seborrheic dermatitis na maambukizi mengine ya fangasi yanaweza kuathiri ngozi ya kichwa na kusababisha nywele kupukutika kwa wingi.
Pia, ugonjwa wa kingamwili unaojulikana kama alopecia areata unaweza kusababisha upotevu wa nywele.
Baadhi ya dawa, zikiwemo dawa za chemotherapy zinazotumika kutibu saratani, pamoja na dawa za shinikizo la damu, sonona na maumivu ya viungo, zinaweza pia kusababisha nywele kupukutika.
Kwa mujibu wa Dkt Haq, matumizi ya kupita kiasi ya mbinu mbalimbali za urembo wa nywele, kama vile dawa za kemikali na kunyoosha nywele kwa njia ya rebonding, yanaweza pia kuchangia tatizo hilo.
Je, kuvaa hijabu au kofia ya kujikinga kunasababisha nywele kupukutika?
Je, kuvaa kofia ngumu za kujikinga na hijabu husababisha nywele kupukutika?
Kuvaa kofia ngumu za kujikinga kwa muda mrefu, hasa katika maeneo yenye joto na unyevunyevu mwingi kama baadhi ya nchi za Afrika na Asia, kunaweza kusababisha jasho kujikusanya kwenye ngozi ya kichwa.
Mchanganyiko wa jasho, vumbi na mafuta unaweza kuchochea maambukizi ya fangasi, mba au uvimbe kwenye vinyweleo.
Maambukizi yakidumu kwa muda mrefu kwenye ngozi ya kichwa, yanaweza kusababisha nywele kupukutika kwa wingi. Hata hivyo, wataalamu wanasema kuwa si kuvaa hijabu au kofia yenyewe kunakosababisha nywele kupukutika.
Daktari bingwa wa ngozi, Dkt Tohida Rahman Eren, anasema kufunika nywele kwa muda mrefu kunaweza kusababisha joto, unyevunyevu na jasho kujikusanya, hali inayoweza kuathiri vinyweleo vya kichwa.
Anasema kuvaa kofia ngumu za kujikinga, kofia za kawaida au hijabu kwa muda mrefu katika mazingira ya joto na unyevunyevu kunaweza kuchochea maambukizi ya fangasi au bakteria kwenye vinyweleo.
Iwapo ukingo wa hijabu au kofia utavaliwa kwa kubana sana kiasi cha kuvuta nywele katika eneo moja kila siku, unaweza kusababisha aina fulani ya upara.
Kitaalamu, hali hiyo huitwa traction alopecia.
Hata hivyo, tatizo hilo mara nyingi halisababishwi na kuvaa hijabu au kofia yenyewe, bali na kufunga nywele kwa kubana sana au kuzivuta mara kwa mara kwa namna ileile.
Imani potofu kuhusu kupukutika kwa nywele
Kuna imani nyingi zisizo sahihi kuhusu sababu za nywele kupukutika na namna ya kutibu tatizo hilo. Baadhi ya watu hutumia muda na fedha nyingi kujaribu dawa mbalimbali badala ya kutafuta ushauri wa daktari.
Kubadilisha shampoo kunaweza kuzuia nywele kupukutika
Watu wengi wanaamini kuwa kubadilisha shampoo kunaweza kuzuia nywele kupukutika. Hata hivyo, kazi kuu ya shampoo ni kusafisha nywele na ngozi ya kichwa, si kuchochea nywele kuota.
Shampoo bora inaweza kusaidia kuweka ngozi ya kichwa katika hali ya usafi na kupunguza kukatika kwa nywele. Lakini haiwezi kutibu matatizo ya ndani ya mwili kama mabadiliko ya homoni au lishe duni.
Kutopaka nywele mafuta kila siku husababisha kupukutika
Mafuta husaidia kulainisha nywele na kupunguza ukavu wa ngozi ya kichwa, lakini hayalishi mizizi ya nywele.
Kwa upande mwingine, kupaka mafuta mengi kwenye ngozi ya kichwa kunaweza kuongeza tatizo la mba na maambukizi ya fangasi kwa baadhi ya watu.
Juisi ya kitunguu, tangawizi na kitunguu saumu hutibu upara
Hakuna ushahidi wa kutosha wa kisayansi unaothibitisha kuwa bidhaa hizi zinaweza kutibu upara.
Badala yake, matumizi yake yanaweza kusababisha muwasho na mzio kwenye ngozi ya kichwa kwa baadhi ya watu.
Akizungumza na BBC Bangla, Dkt Shaila Haq alisema imani hizo si sahihi.
Anashauri kutumia shampoo zisizo na kemikali kali, zikiwemo shampoo zisizo na salfeti au zenye viambato laini, ili kutunza ngozi ya kichwa. Pia anapendekeza matumizi ya mafuta ili kusaidia kuhifadhi unyevunyevu kwenye nywele.
Aidha, watu wengi wanaamini kuwa kupukutika kwa nywele ni dalili ya saratani au ugonjwa mwingine hatari. Wengine hudhani kuwa mtu akishapata upara, nywele haziwezi kuota tena.
Wataalamu wanasema kuwa katika hali nyingi, sababu za kupukutika kwa nywele si za kutisha. Hata hivyo, iwapo nywele zitaanza kupukutika ghafla kwa mafungu au utaona vidonda na muwasho kwenye ngozi ya kichwa, ni muhimu kumwona daktari mara moja.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid