Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Alienda Saudi kutafuta Riziki, akahukumiwa viboko 100
Wakati Mahakama Kuu ya Saudi Arabia ilipotangaza mwaka 2020 kufutwa kwa adhabu ya viboko katika makosa ya hiari ya kimahakama na badala yake kuanzisha vifungo, faini au adhabu mbadala, hatua hiyo ilisifiwa duniani kama moja ya mageuzi makubwa katika mfumo wa sheria wa ufalme huo.
Mashirika ya haki za binadamu yalipokea uamuzi huo kama ishara ya utayari wa Saudi Arabia kujibu ukosoaji wa muda mrefu kuhusu matumizi ya adhabu za viboko, ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikitazamwa na jumuiya ya kimataifa kama adhabu ya kikatili na inayodhalilisha utu wa binadamu.
Lakini miaka sita baadaye, simulizi ya mfanyakazi wa ndani kutoka Kenya, Esther Wanga Muthoni, imeibua tena maswali kuhusu mipaka ya mageuzi hayo na ukweli unaowakabili maelfu ya wafanyakazi wa kigeni wanaoishi katika mataifa ya Ghuba.
Mwanamke aliyetaka kurudi kwa watoto wake
Esther Wanga Muthoni ni mama wa watoto watano mwenye umri wa miaka 40 kutoka Kenya. Alisafiri kwenda Saudi Arabia kutafuta ajira kama wafanyakazi wengi wa Afrika Mashariki wanaokwenda Mashariki ya Kati wakitumaini kuboresha maisha ya familia zao.
Badala ya kurejea nyumbani akiwa na akiba na matumaini mapya, leo amejikuta katikati ya mzozo wa kisheria ulioibua mjadala wa kimataifa.
Mahakama ya Saudi ilimhukumu viboko 100 baada ya kumtia hatiani kwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa na kujifungua mtoto nje ya mfumo wa ndoa unaotambuliwa kisheria. Mbali na viboko hivyo, alihukumiwa pia kufukuzwa nchini kwa muda wa mwaka mmoja.
Kwa wengi nje ya Saudi Arabia, hukumu hiyo ilikuja kama mshangao mkubwa. Watu wengi waliamini kwamba adhabu ya viboko ilikuwa imeondolewa kabisa nchini humo baada ya mageuzi yaliyotangazwa mwaka 2020.
Lakini wataalamu wa sheria za Kiislamu na mfumo wa Saudi wanasema hali halisi ni tofauti zaidi.
Kwa nini viboko bado vinatumika?
Sheria ya Saudi Arabia inatofautisha kati ya aina mbili za adhabu za viboko.
Aina ya kwanza ni viboko vya makosa ya hiari ya kimahakama, ambapo jaji huwa na mamlaka ya kuamua aina ya adhabu kwa makosa ambayo hayana adhabu maalum iliyoainishwa wazi kwenye sheria za Kiislamu. Hivi ndivyo viboko vilivyofutwa mwaka 2020.
Aina ya pili ni viboko vinavyohusishwa na adhabu za hudud, ambazo zinatokana na tafsiri ya sheria za Kiislamu kwa makosa maalumu yaliyobainishwa kwenye matini za kidini.
Makosa hayo yanaweza kujumuisha uzushi wa uzinzi, kashfa za uzinifu, matumizi ya vileo katika mazingira fulani na makosa mengine yanayoangukia katika kundi la hudud. Katika aina hii ya kesi, viboko bado ni sehemu ya mfumo wa sheria wa Saudi Arabia.
Kwa sababu hiyo, kesi ya Esther haikuangukia katika makosa ya hiari yaliyofanyiwa mageuzi mwaka 2020, bali katika eneo ambalo bado linaongozwa na kanuni za kimapokeo za kisheria.
Hofu inayowazuia wanawake kutafuta huduma za afya
Kulingana na Ekaterina Buras-Sevolopova, mwanzilishi wa shirika la Do Bold linalotetea haki za wafanyakazi wahamiaji katika nchi za Ghuba, mamlaka za Saudi zilifahamu kuhusu hali ya Esther alipokwenda hospitalini kujifungua.
Mara baada ya kufikishwa hospitalini, taarifa ziliripotiwa kwa mamlaka husika, jambo lililoanzisha mchakato wa kisheria dhidi yake.
Kwa mujibu wa Sevolopova, tukio hilo si la kipekee.
Anasema wanawake wengi wanaofanya kazi katika mataifa ya Ghuba huishi kwa hofu kubwa kiasi kwamba baadhi yao huchagua kujifungulia majumbani badala ya kwenda hospitalini.
"Hofu ya kushitakiwa au kukabiliwa na matatizo ya kisheria huwafanya baadhi ya wanawake wajifiche hata wanapohitaji huduma muhimu za afya," anasema.
Jambo hilo linaibua swali kubwa kuhusu afya ya uzazi na upatikanaji wa huduma za afya kwa wafanyakazi wa kigeni wanaoishi katika mazingira yenye masharti magumu ya kisheria.
Je, alipata haki ya kujitetea?
Kulingana na ushahidi wa Esther na nyaraka za mahakama zilizoripotiwa na gazeti la New York Times, hakupata wakili wa kumwakilisha katika vikao vya kesi yake.
Msaada pekee aliopewa ulikuwa mkalimani aliyeteuliwa na mahakama.
Aidha, hakukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo kwa sababu aliamini kuwa kukubali uamuzi wa mahakama kungemwezesha kurejeshwa Kenya haraka zaidi na kuungana tena na watoto wake.
Hata hivyo, matarajio hayo hayakutimia.
Kwa nini bado hajarejea Kenya?
Licha ya hukumu kutolewa, Esther na mwanawe bado wako Saudi Arabia.
Sababu kubwa ni kwamba mtoto huyo hana cheti cha kuzaliwa, hati muhimu inayohitajika ili kupata nyaraka za kusafiria na kuruhusu safari ya kuondoka nchini.
Shirika la Do Bold linasema liliwasiliana na Wizara ya Serikali ya Kenya inayoshughulikia Wakenya walio nje ya nchi mnamo Oktoba 27, lakini halikupata majibu.
Kwa mujibu wa shirika hilo, mamlaka za Kenya hapo awali zilitoa nyaraka za dharura za usafiri kwa Esther na mtoto wake, lakini nyaraka hizo zilikwisha muda wake kabla ya kutumika.
Matokeo yake ni kwamba mama huyo amebaki katika hali ya sintofahamu, akiwa mbali na watoto wake wengine walioko Kenya na bila uhakika wa lini ataweza kurudi nyumbani.
Takriban akina mama 70 wakenya wako katika hali kama hiyo
Wanatetea haki za wafanyakazi wahamiaji wanasema tatizo hilo ni kubwa kuliko kesi ya Esther pekee.
Kwa mujibu wa Do Bold, kuna takriban akina mama 70 kutoka Kenya waliopo Saudi Arabia ambao wanakabiliwa na changamoto kama hizo kwa sababu watoto wao hawana vyeti vya kuzaliwa au nyaraka za kisheria zinazokubalika.
Bila nyaraka hizo, ni vigumu kwa watoto kupata pasi za kusafiria au vibali vya kuondoka nchini.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanataka kuwepo kwa utaratibu wa wazi kati ya serikali za Saudi Arabia na Kenya utakaorahisisha usajili wa watoto hao na kutoa suluhu za haraka kwa familia zilizonaswa katika hali kama hiyo.
Mageuzi ya Saudi Arabia yanapimwa kwa namna gani?
Kesi hii imeibuka wakati Saudi Arabia ikijaribu kujijengea taswira mpya chini ya mpango wa Vision 2030.
Katika miaka ya hivi karibuni, ufalme huo umeanzisha mabadiliko kadhaa ya kijamii na kisheria, ikiwemo kuongeza ushiriki wa wanawake katika soko la ajira, kurekebisha baadhi ya sheria za familia na ajira pamoja na kufanya marekebisho katika mfumo wake wa mahakama.
Lakini wakosoaji wanasema mafanikio ya mageuzi hayo hayajaonekana kwa kiwango sawa kwa watu wote.
Maryam Al-Dosari, msomi wa Saudi na kaimu mkurugenzi wa shirika la ALQST for Human Rights, anaamini kuwa kisa cha Esther kinaonyesha pengo kati ya mageuzi yanayotangazwa rasmi na hali halisi inayowakabili wafanyakazi wengi wa kigeni wanapoingia kwenye mfumo wa haki jinai.
Kwa maoni yake, changamoto ya kupata uwakilishi wa kisheria na haki ya kujitetea bado ni kubwa kwa wafanyakazi wengi wa kigeni, hasa wale wenye kipato cha chini.
Sevolopova naye anasema mageuzi yoyote yanapaswa kupimwa kwa kuangalia athari zake kwa maisha ya kila siku ya wafanyakazi na uwezo wao wa kulinda haki zao wanapokabiliwa na mashtaka ya kisheria.
Kenya yajibu kwa tahadhari
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Korir Sing'oei, alielezea masikitiko yake kuhusu hukumu hiyo akisema kuwa kwa mujibu wa viwango vya sheria vya Kenya, adhabu hiyo ni ya kikatili na isiyo ya kibinadamu.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa Kenya inaheshimu mamlaka na mfumo wa kisheria wa Saudi Arabia.
Aidha alisema Nairobi itaendelea kushirikiana na mamlaka za Saudi Arabia kuhusu suala hilo pamoja na masuala mengine yanayohusu utekelezaji wa maamuzi ya mahakama.
Kwa upande wake, mamlaka za Saudi Arabia hazijatoa tamko rasmi kuhusu kesi hiyo.
Hata hivyo, mchambuzi wa masuala ya Saudi, Ali Shihabi, ambaye anaonekana kuwa karibu na duru za maamuzi za ufalme huo, amesema kuwa Saudi Arabia imepiga hatua kubwa za mageuzi lakini bado kuna mifumo ya zamani ambayo haiwezi kubadilishwa mara moja.
"Rehema katika sheria ya Kiislamu si kauli mbiu tu. Haki na rehema si vitu vinavyopingana," amesema.
Kisa Kinachozua Maswali Makubwa
Zaidi ya mjadala wa sheria na dini, simulizi ya Esther Wanga Muthoni imegeuka kuwa hadithi ya ubinadamu.
Ni hadithi ya mama anayetamani jambo moja tu: kurejea nyumbani na kuwaona watoto wake.
Lakini pia ni hadithi inayofichua changamoto zinazowakabili maelfu ya wafanyakazi wa Afrika Mashariki katika nchi za Ghuba, kuanzia upatikanaji wa haki, uwakilishi wa kisheria, huduma za afya, hadi hatima ya watoto wanaozaliwa mbali na nchi zao za asili.
Kadiri ulimwengu unavyoendelea kufuatilia mageuzi ya Saudi Arabia, kesi ya Esther inabaki kuwa kipimo muhimu cha iwapo mabadiliko hayo yanawafikia pia wale walio katika pembezoni mwa jamii, hasa wafanyakazi wa kigeni ambao mara nyingi hawana sauti wala nguvu ya kujitetea.
Imefasiriwa na Asha Juma