Jinsi jumba la kifahari lilivyogeuka kuwa 'nyumba ya kutisha'

    • Author, Mengchen Zhang
    • Nafasi, Global China Unit, BBC World Service
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Mwezi Mei 2025, mtoto wa miezi miwili aitwaye Walter alipelekwa hospitalini katika kitongoji cha kifahari cha Arcadia, California, akiwa na jeraha la kichwa.

Mwanamke aliyejitambulisha kuwa mama yake alisema mtoto huyo alikuwa ameanguka kutoka kitandani kwa bahati mbaya, kwa mujibu wa ripoti ya polisi.

Hata hivyo, daktari alishuku kuwa huenda kulikuwa na jambo lisilo la kawaida. Alisema hali ya Walter ilifanana zaidi na majeraha yanayotokana na ajali ya gari au kutikiswa kwa nguvu.

Kwa kushuku uwezekano wa unyanyasaji wa mtoto, polisi walipekua jumba la kifahari alimoishi Walter na kuwazuilia kwa muda wazazi wake, Guojun Xuan, mwenye umri wa miaka 66, na Silvia Zhang, mwenye umri wa miaka 39.

Waendesha mashtaka walisema walichokikuta ndani ya nyumba hiyo "kingeweza tu kuelezewa kama nyumba ya kutisha" — jumba lenye kamera nyingi na vyumba vilivyounganishwa kwa njia tata, ambako kulikuwa na watoto 14 waliozaliwa kupitia huduma ya kumbebea mtu mimba, wenye umri wa kati ya miezi sita na miaka mitatu. Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, watoto hao walikuwa wakipigwa kila siku.

Baadaye, mamlaka ziligundua kuwa anwani ya jumba hilo pia ilikuwa imesajiliwa kama makao ya wakala wa huduma za uzazi wa kupangwa ulioendeshwa na wanandoa hao na kutumiwa kuwapata wanawake wa kubeba mimba zao.

Mwezi Oktoba mwaka huu, wanandoa hao walikamatwa tena na kushtakiwa kwa kula njama ya kuwadhulumu watoto. Wanakanusha mashtaka hayo na wanaendelea kuzuiliwa. Dhamana yao imewekwa kuwa dola milioni 20 za Marekani (takriban pauni milioni 15) kwa kila mmoja.

Iwapo watapatikana na hatia, Xuan anaweza kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka 17 na miezi minne jela, huku Zhang akikabiliwa na kifungo cha hadi miaka 11 na miezi minane.

"Nyumba ya kutisha"

Wanandoa hao walihamia katika jumba hilo la Arcadia mwezi Aprili 2021. Matangazo ya mauzo ya nyumba mtandaoni yanaonyesha kuwa jumba hilo lenye ukubwa wa futi za mraba 10,000 (takriban mita za mraba 929) liliuzwa kwa dola milioni 3.3 (pauni milioni 2.48) mwaka huohuo.

Jumba hilo lina vyumba tisa vya kulala, bafu 11 na bwawa la kuogelea lenye mfumo wa kupasha maji joto.

Arcadia, kitongoji tajiri kilicho upande wa mashariki wa Los Angeles, kimepewa jina la utani la "Beverly Hills ya Wachina" na vyombo vya habari vya eneo hilo.

Takwimu za hivi karibuni za sensa ya Marekani zinaonyesha kuwa karibu asilimia 60 ya wakazi wake ni Waasia, wengi wao wakiwa na asili ya China. Mapato ya kaya katika eneo hilo ni ya juu zaidi kuliko ya familia nyingi nchini Marekani.

Waendesha mashtaka wanasema kuwa jumba la Xuan na Zhang lilikuwa na kamera zinazowashwa zinapotambua mwendo, zilizowekwa katika maeneo mbalimbali ya nyumba hiyo yenye ukubwa wa futi za mraba 10,000.

"Nyumba hii inaweza tu kuelezewa kama nyumba ya kutisha kwa watoto hawa wadogo sana walioletwa hapa kupitia utaratibu wa uzazi wa kupangwa," alisema Nathan Hochman, Mwendesha Mashtaka wa Wilaya ya Los Angeles, katika mkutano na waandishi wa habari mwezi Oktoba baada ya wanandoa hao kushtakiwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kamera 32 zilikuwa zimewekwa ndani ya jumba hilo.

Video zilionyesha kuwa watoto wadogo walitumia saa nyingi wakiwa wameketi karibu na madawati. Katika chumba kimoja hakukuwa na kamera, lakini kamera zilizokuwa katika vyumba vingine zilirekodi walezi wakiwabeba watoto na kuwaingiza humo. Baadaye, watoto walisikika wakipiga mayowe kutoka ndani ya chumba hicho.

Waendesha mashtaka wanadai kuwa majeraha ya Walter yalisababishwa na mmoja wa walezi, Chunmei Li. Li ameshtakiwa kwa kumdhulumu mtoto katika mazingira yanayoweza kusababisha majeraha makubwa ya mwili au kifo. Hadi sasa, hajakamatwa na anaendelea kutafutwa.

Wakili wa wanandoa hao, Mitchell Krems, alisema madai hayo yalikuwa "upotoshaji" wa ushahidi aliokuwa ameupitia, kwa mujibu wa CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani.

Krems alisema mteja wake Xuan hana hatia.

"Analengwa kwa kutumia haki yake ya kikatiba ya kuwa na familia kubwa," CBS News ilimnukuu wakili huyo akisema.

Walipataje watoto wote hao?

Marekani imekuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika huduma za uzazi wa kupangwa, ambapo mwanamke hubeba mimba na kujifungua mtoto kwa niaba ya mtu au wanandoa wengine.

Utafiti wa mwaka 2024 kuhusu takwimu za huduma hizo nchini Marekani uligundua kuwa karibu theluthi moja ya watu waliokusudia kupata watoto kupitia utaratibu huo kati ya mwaka 2014 na 2020 walitoka nje ya Marekani.

China, ambako uzazi wa kupangiwa umepigwa marufuku, ilikuwa chanzo kikubwa zaidi cha wateja wa kimataifa, ikiwa na takriban asilimia 42 ya watu waliotoka nje ya Marekani kutafuta huduma hizo.

Marekani inatoa huduma za kiteknolojia za uzazi ambazo watu wengi nchini China hawawezi kuzipata kwa urahisi katika nchi yao. Wanawake wasio na wenza na watu wa jumuiya ya LGBTQ mara nyingi hukabiliwa na vikwazo vya kupata huduma za urutubishaji wa mayai nje ya mwili (IVF) na kugandisha mayai.

Pia, baadhi ya wanandoa waliathiriwa na sera ya China ya mtoto mmoja iliyodumu kwa miongo kadhaa. Sera hiyo ilipokoma mwaka 2016, baadhi yao walikuwa wamefikia umri ambao kufanya ujauzito wenyewe kulikuwa kugumu, hali iliyowasukuma baadhi yao kutafuta huduma za uzazi wa kupangiwa nje ya nchi.

Kwa baadhi ya wanawake waliobeba mimba kwa niaba ya Xuan na Zhang, ombi la wanandoa hao la kupata mtoto kupitia uzazi wa kupangwa halikuonekana kuwa na shaka mwanzoni, kwa mujibu wa nyaraka za mahakama.

Wanawake kadhaa waliajiriwa kupitia wakala ulioitwa "Mark Surrogacy". Kwa kawaida, wakala wa aina hiyo huonekana kama taasisi huru inayowaunganisha wazazi wanaotaka watoto na wanawake wanaokubali kubeba mimba kwa niaba yao.

Hata hivyo, ilibainika kuwa kampuni ya Mark Surrogacy ilikuwa ikiendeshwa na wanandoa hao wenyewe — jambo ambalo, kwa mujibu wa kesi mbili zilizofunguliwa na baadhi ya wanawake hao, halikuelezwa wazi kila wakati.

Katika rekodi za usajili wa kampuni, Silvia Zhang alitajwa kuwa meneja wa Mark Surrogacy, huku anwani ya jumba lao la Arcadia ikionyeshwa kuwa makao ya kampuni hiyo.

Katika kikao cha mahakama cha tarehe 16 Oktoba, Naibu Mwendesha Mashtaka wa Wilaya, MacKenzie Cameron Teymouri, pia aliiambia mahakama kuwa hakuna mzazi mwingine aliyewahi kuunganishwa na mwanamke wa kubeba mimba kupitia wakala huo ulioendeshwa nyumbani kwa Xuan na Zhang.

Mmoja wa wanawake hao, Tronderrica James, aliwafungulia wanandoa hao kesi mwaka 2025 akidai fidia kwa madai ya udanganyifu na kutoa taarifa za kupotosha kwa makusudi.

James alidai kuwa Zhang hakumweleza uhusiano wake na kampuni ya Mark Surrogacy katika hatua za mwanzo. Alisema asingekubali kuendelea na utaratibu huo kama angejua ukweli kuhusu mpangilio huo.

James hakujibu ombi la BBC la kufanya mahojiano naye.

Baadaye, wanandoa hao waliwasilisha ombi la kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali, wakisema kuwa mwanamke huyo hakuwa na msingi wa kutosha wa kufungua kesi. Kesi hiyo bado inaendelea.

Wanawake wengine watano — Stacy Raelyn King, Evelyn Senolos Areja, Kayla Elliott, Hallie Hernandez na Vanity McGoveran — walitoa madai yanayofanana katika kesi nyingine iliyowasilishwa mwezi Agosti dhidi ya Xuan na Zhang.

Kesi hiyo ilidai kuwa Zhang hakufichua uhusiano wake na Xuan na wakala huo, wala idadi halisi ya watoto ambao wanandoa hao walikuwa nao.

"Kila mlalamikaji aliongozwa kuamini kuwa ndiye mwanamke pekee aliyekuwa amebeba mimba kwa ajili ya wanandoa hao, na kwamba alikuwa akiisaidia familia kupata mtoto mmoja wa pekee na anayethaminiwa," ilisema hati ya madai.

Wanandoa hao pia walikuwa wametumia huduma za wakala mwingine huru wa uzazi wa kupangiwa, Babytree Surrogacy, wenye makao yake California.

Patrick Yu, mwanzilishi wa Babytree, aliiambia BBC kuwa Xuan aliwasiliana nao mwaka 2018.

Yu alisema Xuan alimweleza kuwa alitaka kuwa na familia kubwa. Wakala huo uliwasaidia kumtafutia Xuan wanawake kadhaa waliobeba mimba na kujifungua angalau watoto wanne.

"Tulipoona taarifa za habari kwamba alikuwa akichunguzwa, ndipo nilipotambua kwa mara ya kwanza kuwa alikuwa na watoto wengi hivyo. Tuliacha mara moja kufanya kazi naye," alisema Yu.

Hata hivyo, mmoja wa wanawake aliyeunganishwa na Xuan kupitia wakala huo mwaka 2024 alikuwa tayari mjamzito wakati taarifa kuhusu majeraha ya Walter zilipoibuka mwezi Mei mwaka uliofuata.

Mamlaka zilikuwa zimewaweka watoto 21 chini ya ulinzi wa serikali wakati polisi wakichunguza madai ya unyanyasaji.

Yu alisema alipanga mkutano kati ya wanandoa hao na mwanamke huyo, ambaye wakati huo alikuwa tayari mjamzito. Alisema wanandoa hao walionekana kuwa na uhakika mkubwa walipomhakikishia mwanamke huyo kuwa wanawatunza watoto wao vizuri.

Mwanamke huyo aliamua kuendelea na mpango huo na akajifungua mtoto mapema mwaka 2026.

Kwa mujibu wa Dkt Liang Yu, Makamu Mwenyekiti wa Kikundi cha China cha Jumuiya ya Marekani ya Tiba ya Uzazi na Mkurugenzi wa Mpango wa Sayansi ya Kliniki ya Uzazi katika Chuo Kikuu cha Old Dominion, hakuna kikomo cha kisheria kuhusu idadi ya mimba za uzazi wa kupangiwa ambazo mzazi anayetarajia kupata mtoto anaweza kuomba. Pia, hakuna sharti la kisheria linalomtaka kutoa taarifa hizo.

Liang alisema baadhi ya mawakala wanaweza kuwa na masharti yao wenyewe, lakini si jambo linalotakiwa kisheria.

Aliongeza kuwa wanandoa wanaweza pia kufanya kazi na mawakala kadhaa kwa wakati mmoja bila kufichua kikamilifu taarifa zao kwa kila mmoja.

"Hali hii inazua utata katika sheria na kanuni zinazosimamia sekta hii," alisema.

Liang aliongeza kuwa katika utata huu ameshuhudia mifano mingi inayohusisha wateja matajiri, wakiwemo wasiokuwa Wachina. Hata hivyo, kutokana na ulinzi wa faragha na makubaliano ya usiri yanayosainiwa na madaktari na kliniki za uzazi, visa vingi havijulikani kwa umma.

"Kwa maneno mengine, tabia ya aina hii, kama ile inayodaiwa kuhusishwa na Xuan, si jambo ambalo halijawahi kutokea," alisema.

BBC iliwasiliana na mawakili wanaowawakilisha Xuan na Zhang kuhusu madai hayo. Mitchell Krems, anayewawakilisha wote wawili, hakujibu.

Matt Koohanim, anayemwakilisha Zhang, alisema suala hilo litashughulikiwa kupitia njia zinazofaa za kisheria.

Wazazi ni kina nani?

Katika kikao cha mahakama cha tarehe 16 Oktoba, Teymouri aliiambia mahakama kuwa thamani ya mali za wanandoa hao kwa pamoja ilikuwa zaidi ya dola milioni 100 (pauni milioni 75) mwaka 2025.

Teymouri aliongeza kuwa mamlaka zilipata pasipoti tatu za Xuan — ya Mexico, China na Marekani.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya China, Xuan alizaliwa katika jimbo la Zhejiang, mashariki mwa China, mwaka 1959.

Alipokuwa na umri wa miaka 18, alianza kufanya kazi kama mhasibu katika kampuni ya serikali ya kuuza bidhaa za madukani mjini Urumqi.

Mwaka 1997, alikua mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Wananchi mjini Urumqi. Baadaye, mwaka 2008, akawa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Mkoa wa Xinjiang, chombo cha kutunga sheria katika ngazi ya mkoa kinachofanana na baraza la wawakilishi wa jimbo nchini Marekani.

Kuhusika kwake katika maisha ya umma kuliendelea hata baada ya kuhamia Marekani.

Alikuwa rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Xinjiang nchini Marekani (US Xinjiang Chamber of Commerce) na makamu wa rais wa China America Federation. Alionekana katika hafla mbalimbali za umma tangu mwaka 2019.

Katika picha moja iliyoonekana na BBC, Xuan alikuwa ameshikana mikono na Eileen Wang, aliyekuwa meya wa zamani wa Arcadia, katika hafla ya mwaka 2022.

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa umeya wa Wang mwaka huo, Xuan alichangia dola 4,900 kupitia kampuni iliyokuwa chini ya jina lake.

Wang alijiuzulu wadhifa wa umeya mwezi Mei mwaka huu baada ya Wizara ya Sheria ya Marekani kumshtaki kwa kutenda kama wakala haramu wa China. Alikiri kosa la jinai alilokuwa akikabiliwa nalo.

Kuna taarifa chache kuhusu Zhang, ambaye alifanya kazi kama wakala wa mali isiyohamishika.

Xuan na Zhang hawakuwa wameoana. Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Zhang alikuwa ameolewa na mwanamume mwingine, ambaye aliachana naye mwaka 2022.

Nini kitatokea kwa watoto hao?

Katika kikao cha mahakama kilichofanyika mapema mwezi huu, Teymouri aliiambia mahakama kuwa kuna watoto 26 wanaohusishwa na familia hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Zhang alikuwa ametunza jedwali la kielektroniki lililoonyesha jumla ya watoto 21 kufikia Mei 2025. Watoto hao waliondolewa nyumbani na kuwekwa chini ya uangalizi wa serikali.

Watoto wengine watano walizaliwa baada ya hapo, kwa mujibu wa CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, katika taarifa iliyochapishwa Januari 2026.

Mtoto mmoja aliyezaliwa kupitia uzazi wa kupangwa bado anaishi na mwanamke aliyembeba tumboni katika jimbo la Virginia.

Melissa Epps, mmoja wa wanawake walioajiriwa na wanandoa hao kubeba mimba, alikuwa mjamzito alipopata habari kuhusu uchunguzi huo mwaka jana. Aliamua kumlea mtoto huyo mwenyewe.

Wanandoa hao walimfungulia Epps kesi wakimtuhumu kwa kukiuka mkataba wa uzazi wa kupangiwa. Walitaka mtoto huyo wa kike arejeshwe kwao, pamoja na kulipwa dola milioni moja na Epps.

Mwanzoni, Epps hakuwa na wakili na alilazimika kujitetea mwenyewe mahakamani, hadi Pamela DeCamp, wakili wa Shirika la Msaada wa Kisheria la Virginia, alipoamua kumwakilisha.

Epps alikataa kufanya mahojiano na BBC.

Katika taarifa aliyotoa kwa BBC, DeCamp alisema walikuwa "na shukrani kubwa kwa juhudi za Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Wilaya ya Los Angeles, California, za kutafuta haki kwa watoto hao wadogo".

Kesi yao itaendelea hadi Machi mwakani.

Mtoto huyo wa kike yuko chini ya uangalizi wa huduma za kijamii lakini kwa sasa anaishi na Epps. Hivi karibuni aliadhimisha siku yake ya kwanza ya kuzaliwa.

"Bado yuko salama na ana furaha huko Virginia. Tuna imani kuwa hali hiyo itaendelea," alisema DeCamp.