Maziwa mabichi yana faida gani kiafya na ni salama kuyanywa?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Ikiwa tutaamini madai yanayotolewa kuhusu faida za maziwa mabichi, yaani maziwa ambayo hayajapitia mchakato wa kupashwa moto au kuchemshwa, yanaonekana kana kwamba ni suluhisho la kila kitu, kuanzia kuimarisha kinga ya mwili, kuzuia mzio wa bidhaa za maziwa hadi kuboresha usagaji wa chakula.

Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, utafutaji wa maziwa haya kwenye Google nchini Uingereza na Marekani umeongezeka kwa kasi kubwa. Aidha, kwenye Instagram kumekuwa na machapisho karibu 260,000 yenye alama ya #rawmilk, huku watu maarufu kwenye mitandao ya kijamii wakiendelea kuyatangaza na kusisitiza manufaa yake.

Ni nini siri ya ongezeko hili kubwa la hamasa na mvuto wa maziwa mabichi?

Maziwa Mabichi: Ni nini na kwa nini watu huyanywa?

Aina nyingi za maziwa zinazouzwa sokoni hupitia mchakato ambapo maziwa huwekwa kwenye joto maalumu ili kuua bakteria hatari na kuongeza muda wa kuhifadhiwa bila kuharibika.

Kwa upande mwingine, maziwa mabichi (raw milk) na krimu mbichi hukamuliwa kutoka kwa ng'ombe, kondoo au mbuzi na kuwekwa moja kwa moja kwenye vyombo vya kuhifadhia bila kufanyiwa usindikaji wowote.

Hivyo, hubaki katika hali yake ya asili, ikiwa na virutubisho vyake pamoja na bakteria wote waliopo ndani yake.

Baadhi ya watu maarufu wanaopendelea kunywa maziwa mabichi, akiwemo mwigizaji Gwyneth Paltrow, wanaamini kuwa yanaweza kuwa rahisi zaidi kumeng'enywa.

Ladha ya maziwa mabichi pia husifiwa mara nyingi kuwa bora na yenye asili zaidi kuliko yaliyochakatwa. Aidha, madai kwamba yana bakteria wenye manufaa kwa mwili na kwamba yanaweza kusaidia kuboresha afya ya utumbo yameenea sana kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanaonya kuwa madai mengi kuhusu faida za maziwa mabichi bado hayajathibitishwa kikamilifu kisayansi, huku wakisisitiza kuwa yanaweza kubeba bakteria hatari ambao husababisha magonjwa.

Je, maziwa mabichi yana afya zaidi kuliko maziwa yaliyochakatwa?

Watu wengi hunywa maziwa kwa sababu yana virutubisho vingi muhimu mwilini, ikiwemo protini, kalsiamu, vitamini na madini mbalimbali.

Watu wengi hunywa maziwa kwa sababu yana virutubisho vingi muhimu, ikiwemo protini, kalsiamu, vitamini na madini.

Kwa kuwa baadhi ya vitamini huathiriwa na joto, baadhi ya watu wana hofu kwamba uchakataji hupunguza kiwango cha vitamini katika maziwa.

Hata hivyo, utafiti mmoja uliofanywa nchini Canada ulibaini kuwa kuchakata kuna athari ndogo sana kwa thamani ya lishe ya maziwa, hasa kutokana na ukweli kwamba maziwa yana kiwango kidogo cha vitamini zinazoharibiwa kwa urahisi na joto.

Pamoja na hayo, huua bakteria waliomo kwenye maziwa, wakiwemo wale wanaoweza kuwa na manufaa pamoja na bakteria hatari wanaoweza kusababisha sumu ya chakula.

Utafiti wa hivi karibuni wa uchunguzi uliofanywa kwa wanafunzi wa Ballymaloe Culinary School uligundua tofauti katika muundo wa bakteria wa utumbo miongoni mwa washiriki waliotumia maziwa mabichi na bidhaa zake, pamoja na tofauti katika viwango vyao vya ustawi walivyoripoti wenyewe.

Hata hivyo, utafiti huo ulihusisha idadi ndogo ya washiriki, hivyo matokeo yake hayawezi kutumika kuthibitisha moja kwa moja kwamba unywaji wa maziwa mabichi ndio uliosababisha tofauti hizo, au kwamba una manufaa ya kiafya yanayoweza kuthibitishwa.

Kwa upande mwingine, hatari zinazohusiana na uwezekano wa maziwa mabichi kuwa na bakteria hatari bado zinaendelea kuwepo.

Je, maziwa mabichi hulinda dhidi ya mzio au pumu?

Baadhi ya tafiti za uchunguzi, hasa zile zilizowahusisha watoto wanaoishi katika jamii za wakulima, zimebaini kuwapo kwa uhusiano kati ya kunywa maziwa mabichi na viwango vya chini vya pumu pamoja na baadhi ya aina za mzio.

Hata hivyo, matokeo hayo hayathibitishi kuwa maziwa mabichi ndiyo sababu ya kupungua kwa matatizo hayo, kwani mambo mengine ya kimazingira na mtindo wa maisha yanaweza pia kuwa na mchango.

Kwa sababu hiyo, watafiti na wataalamu wa afya wanaendelea kuonya dhidi ya matumizi ya maziwa mabichi kutokana na hatari ya kuambukizwa magonjwa yanayosababishwa na bakteria hatari wanaoweza kuwepo kwenye maziwa hayo.

Je, kunywa maziwa mabichi ni salama?

Shirika la Viwango vya Chakula la Uingereza (UK Food Standards Agency) linaainisha maziwa mabichi kutumiwa moja kwa moja kama vyakula vyenye hatari kubwa, likionya kwamba vinaweza kuwa na bakteria hatari wanaosababisha sumu ya chakula.

Shirika hilo pia linasema kwamba watoto wachanga, watoto wadogo, wazee, wanawake wajawazito na watu wenye kinga dhaifu ya mwili hawapaswi kutumia maziwa mabichi kutokana na hatari ya maambukizi makubwa.

"Kwa mtazamo wa usalama wa chakula, kunywa maziwa mabichi si salama," anasema Dkt. Jorge Gutierrez Merino, mhadhiri mwandamizi wa elimu ya vijiumbe vya chakula.

Anaongeza: "Maziwa mabichi yanaweza kuwa na aina mbalimbali za vijiumbe vinavyosababisha magonjwa, vikiwemo baadhi ya bakteria hatari sana ambao wanaweza kusababisha maambukizi makubwa na hata vifo, hasa kwa watoto, wazee na watu wenye kinga dhaifu ya mwili."

Je, ni halali kununua maziwa mabichi?

Tofauti na maziwa yaliyochemshwa yanayouzwa katika maduka makubwa, nchini Uingereza, Wales na Ireland Kaskazini, maziwa mabichi ya ng'ombe yanaweza kuuzwa tu kupitia mashamba yaliyosajiliwa. Mauzo hayo hufanyika moja kwa moja shambani, kupitia mashine za kuuza maziwa, mtandaoni, katika masoko ya wakulima au kupitia magari ya kusambaza maziwa.

Nchini Scotland, uuzaji wa maziwa ya wanyama ambayo hayajapashwa moto umepigwa marufuku kisheria.

Katika nchi kadhaa za Kiarabu, uzalishaji na usambazaji wa maziwa unasimamiwa na sheria na kanuni za afya zinazotofautiana kati ya nchi moja na nyingine.

Nchini Morocco, sheria zinadhibiti uzalishaji, ukusanyaji na usafirishaji wa maziwa mabichi. Nchini Tunisia, wauzaji wa maziwa na bidhaa za maziwa wanatakiwa kuwa na leseni na kuzingatia viwango vya usalama wa chakula.

Nchini Saudi Arabia na Lebanon, mamlaka za afya zimekuwa zikionya kuhusu hatari za matumizi ya maziwa yasiyopashwa moto na kusisitiza umuhimu wa kuyachemsha au kuyafanyia matibabu ya joto ili kuondoa bakteria hatari.