Kisiwa ambacho kuku ndio 'mabosi': Jinsi kuku wa mwitu walivyotawala Hawaii

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Fikiria ukitoka nyumbani kwako Nairobi, Dar es Salaam au Mombasa, halafu unakuta mamia ya majogoo yakitembea barabarani, yakitua kwenye magari na kuzurura katika masoko ya mtaani.

Katika jamii nyingi zinazozungumza Kiswahili, si jambo la kawaida kuona kuku wakizurura bila mwenyewe kuwafuatilia. Mara nyingi, kuku anayepatikana akizurura mtaani anaweza kuishia kwenye chungu cha kuku wa kienyeji kabla jua halijazama.

Lakini katika kisiwa cha Kauai, kilichopo Hawaii, Marekani, hali ni tofauti kabisa. Huko, kuku wa porini ndio wanaotawala mitaa. Maelfu yao huzurura kwa uhuru katika fukwe zenye mchanga mweupe, nje ya milango ya benki na kwenye maegesho yenye shughuli nyingi.

Hakuna anayewamiliki, hakuna anayewafungia kwenye mabanda, na cha kushangaza zaidi, ni nadra kuwaona wakifanywa kitoweo.

Lakini ndege ambaye kwa kawaida huishia jikoni amewezaje kutawala kisiwa kizima chenye mandhari ya kuvutia? Jibu linapatikana katika historia ya kisiwa hicho, vimbunga vikali na uwezo wa ndege hao kuishi na kuongezeka kwa kasi.

Lakini kuku hawa walitoka wapi?

Historia ya kuku hao inaanzia zaidi ya miaka 800 iliyopita, wakati mabaharia wa kale wa jamii ya Wapolinesia walipovuka bahari kwa mitumbwi ya mbao na kuleta ndege waliokuwa mababu wa kuku wa porini wa leo.

Kwa karne nyingi, ndege hao waliendelea kuishi katika misitu minene ya milimani, mbali na makazi ya watu.

Hata hivyo, hali ilibadilika mwaka 1992, wakati kimbunga kikali cha Iniki, kilichoainishwa katika daraja la nne, kilipoikumba Kauai. Upepo wake ulifikia kasi ya zaidi ya kilomita 225 kwa saa, ukiharibu mashamba na kubomoa mabanda mengi ya kuku.

Kuku waliokuwa wakifugwa kibiashara walitoroka na kuingia porini, ambako walikutana na kuku wa asili wa kisiwa hicho na kuzaliana nao.

Matokeo yake yakawa kuku wenye uwezo mkubwa wa kuhimili mazingira magumu, waliorithi silika za kuishi porini kutoka kwa mababu zao na uwezo wa kuongezeka kwa kasi kutoka kwa kuku wa kufugwa.

Kisiwa kisichopenda kitoweo cha kuku

Afrika Mashariki, kuku hukabiliwa na hatari kutoka kwa wanyama wanaowawinda, wakiwemo mangusti, paka wa porini, mwewe na nyoka.

Lakini huko Kauai, mangusti hawapo kwa sababu hawakuletwa katika kisiwa hicho, kwa mujibu wa maelezo ya historia ya uhifadhi wa wanyamapori wa eneo hilo. Uamuzi huo ulilenga kulinda ndege wa asili dhidi ya wanyama wanaoweza kuwawinda.

Kwa kukosekana kwa baadhi ya wanyama wanaowinda kuku, pamoja na hali ya hewa ya joto inayodumu mwaka mzima, idadi ya kuku hao imeongezeka kwa kiasi kikubwa.

Leo, kuishi pamoja na ndege hao ni changamoto ya kila siku kwa baadhi ya wakazi.

Kengele ya saa nane usiku? Sahau hilo. Majogoo hao hayasubiri hadi alfajiri ili kuwika. Taa za barabarani au mwanga wa magari yanayopita unaweza kuyachochea kuwika hata kuanzia saa nane usiku, kwa saa za Afrika Mashariki.

Na sio hayo tu wanafanya uharibifu mkubwa wa mali.

Makundi ya kuku huchakura bustani, kuharibu mashamba na wakati mwingine kusababisha msongamano wa magari, madereva wanaposimama ili kuwaacha wavuke barabara.

Kwa nini hawapikwi na kuliwa kama kuku wa kienyeji?

Hili ndilo swali linalowajia watu wengi: kwa nini wakazi hawawakamati kuku hao na kuwapika kwa ugali au pilau?

Sababu mojawapo ni kwamba kuku hao hutembea sana, huruka na kutua kwenye miti mirefu na kujitafutia chakula porini, ikiwemo wadudu. Kwa hiyo, nyama yao huwa kavu, haina mafuta mengi na ni ngumu kutafuna ikilinganishwa na kuku wanaofugwa kwa ajili ya nyama.

Kuna hata utani maarufu wa wenyeji wa Hawaii unaosema:

"Ukitaka kumpika kuku wa porini wa Kauai, mtie kwenye sufuria ya maji yanayochemka pamoja na jiwe la lava. Jiwe hilo likishalainika, basi kuku atakuwa tayari kuliwa!"

Badala ya kuendelea kupambana na kuku hao, baadhi ya wakazi wamewafanya kuwa sehemu ya utambulisho wa kisiwa hicho.

Leo, kuku hao wamekuwa kivutio kwa watalii, huku picha zao zikitumika kwenye fulana, vikombe na zawadi mbalimbali zinazouzwa kwa wageni wanaotembelea Kauai.

Hivyo, katika kisiwa hiki cha Hawaii, kuku ambao sehemu nyingine duniani wangeishia kwenye chungu cha chakula wamegeuka kuwa alama ya eneo hilo na sehemu ya maisha ya kila siku ya wakazi wake.