Heche aitaka Kenya kuhakikisha Twaha Mwaipaya anapatikana salama
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, amesema wamejitahidi usiku kucha kuwasiliana na vyombo husika nchini Kenya ili kupata taarifa kuhusu aliko Twaha Mwaipaya.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Heche amesema haamini kuwa serikali ya Kenya ina sababu ya kumteka Mwaipaya, lakini amehoji jinsi watekaji wanavyoweza kuingia katika nchi nyingine na kumchukua mtu bila msaada wa watu wenye mamlaka.
“Ni vipi mtu anaweza kuingia katika nchi nyingine na kumchukua mtu bila msaada wa watu walioko ndani ya serikali hiyo?” amehoji Heche.
Amemwomba Rais wa Kenya, William Ruto, na serikali yake kusaidia kuhakikisha Mwaipaya anapatikana akiwa hai na salama.
Heche ameonya kuwa tukio hilo, iwapo litathibitishwa, linaweza kulitia doa jina la Kenya kama taifa la kidemokrasia, akisema mtu aliyekimbilia nchini humo kutafuta hifadhi hapaswi kutekwa akiwa ndani ya mipaka yake.
Aidha, amedai kuwa makundi machache nchini Tanzania yamekuwa yakitumia vitendo vya mauaji, utekaji na vitisho kuwanyamazisha wanaokosoa uovu. Amewataka Watanzania kutokubali hali hiyo kuendelea na kusisitiza kuwa wanamtaka Mwaipaya apatikane akiwa salama.
Kwa upande wake, serikali ya Tanzania imekuwa ikikanusha madai ya kuhusika na vitendo visivyo halali dhidi ya wapinzani wa kisiasa.
Hadi kufikia sasa, hakuna taarifa rasmi au tamko lolote lililotolewa na mamlaka za usalama nchini Kenya kuhusiana na tukio hilo la kutekwa kwa Mwaipaya.
BBC Swahili inafuatilia na serikali ya Kenya kujua msimamo wao.