Jinsi mashambulizi ya 9/11 Marekani yalivyobadilisha masuala ya ujasusi na usalama duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Frank Gardner
- Nafasi, Mwandishi wa BBC
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 11
Jukumu kuu la serikali, kama viongozi wengi sana walivyosisitiza kwa miaka mingi , ni kulinda raia wake.
Marekani ilishindwa waziwazi kutekeleza jukumu hilo mnamo tarehe 11 Septemba 200, taarifa za kijasusi zilikuwepo, lakini kwa masikitiko makubwa, hakuna aliyefanikiwa kuunganisha na kuzielewa kwa wakati mwafaka.
Tukio la 9/11, jina ambalo mashambulizi hayo dhidi ya Marekani yalikuja kujulikana kwalo, pamoja na hatua zilizofuata, viliweka mwelekeo wa sera za kigeni, usalama, na masuala ya kijasusi kwa kizazi kizima katika miongo miwili ya kwanza ya karne hii.
Mnamo tarehe 11 Septemba 2001, wakati marubani wa kujitoa mhanga wa kundi la Al-Qaeda walipokuwa wakirusha ndege walizoziteka nyara na kuzigongesha kwenye majengo ya World Trade Center, nilikuwa nikihitimisha kazi katika ofisi ya ujumbe wetu wa kidiplomasia Mashariki ya Kati.
Dereva wa teksi raia wa palestina alikuwa akinisafirisha kupitia vilima vilivyofunikwa na miti ya misonobari magharibi mwa Jerusalem kuelekea Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion jijini Tel Aviv, wakati ghafla alipoongeza sauti ya redio.
"Kuna jambo zito limetokea Marekani," alisema.
Hakuwa akitia chumvi, watu 2,977 walipoteza maisha siku hiyo.
Mashambulizi hayo hayakutokea ghafla bila sababu, kwa miaka mingi,kabla ya mwaka 2001, Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) lilikuwa likifahamu kuhusu mtandao wa Al-Qaeda na kiongozi wake raia wa Saudi Arabia aliyeishi uhamishoni, Osama bin Laden, na hata lilikuwa na kikosi maalum kilichopewa jukumu la kumtafuta na kumkamata.
Siku tisa baada ya mashambulizi ya tarehe 11 Septemba, Rais wa Marekani wakati huo, George W. Bush, alitangaza "Vita dhidi ya Ugaidi."

Chanzo cha picha, Getty Images
George W. Bush alikuwa katika shule moja katika jimbo la Florida wakati mashambulizi hayo yalipotokea.
Katika kipindi cha miaka 25 iliyofuata, kumekuwa na mafanikio na pia mapungufu mengi katika nyanja ya ujasusi pande zote mbili za Bahari ya Atlantiki.
Mafanikio hayo yanajumuisha njama zilizozuiwa pamoja na washukiwa waliokamatwa, kufikishwa mahakamani, kupatikana na hatia, na kufungwa gerezani.
Lakini taswira pana ya mambo ni ipi?
Je, ukusanyaji wa taarifa za kijasusi, hatua za kukabiliana na ugaidi, na mipango ya kimkakati vimebadilikaje katika miaka 25 tangu kutokea kwa shambulio baya zaidi la kigaidi katika historia ya Marekani?
Kufeli kwa idara ya ujasusi
Hakuna anayeweza kupinga kwamba tukio la tarehe 11 Septemba lilikuwa ni kufeli kukubwa kwa idara za ujasusi au, kwa usahihi zaidi, "kushindwa kutumia mawazo mapana na ubunifu" kwa upande wa jumuiya ya ujasusi ya Marekani.
Wakati huo, mashirika ya CIA na FBI yalikuwa na taarifa ambazo, kama zingeshirikishwa ipasavyo, zingeweza kuzuia matukio yaliyotokea.
Ripoti iliyofuata ya Tume ya 9/11 iliweka lawama kwa serikali ya Marekani, ikitaja "mapungufu katika nyanja zao na ubunifu, sera, uwezo, na usimamizi."
Ripoti hiyo ilihitimisha kuwa CIA na FBI zilishindwa kutathmini taarifa za kijasusi kwa usahihi, hazikushirikishana taarifa, na zilishindwa kuchukua hatua za kutosha kuzuia njama hiyo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tangu wakati huo, walichijifunza kutokana na hili ni muhimu kimeeleweka kwa kiasi kikubwa,ingawa si kikamilifu na ushirikishwaji wa taarifa kati ya mashirika ya kijasusi ya nchi za Magharibi ni bora zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 2001.
Uhasama wa zamani kati ya, kwa mfano, MI5 na vitengo vya polisi vya kupambana na ugaidi umetoweka, kwanza kupitia uundaji wa "vituo vya kuunganisha" katika maeneo mbalimbali ya Uingereza, na hivi karibuni zaidi kupitia kuanzishwa kwa Kituo cha Operesheni za Kupambana na Ugaidi chenye ulinzi mkali jijini London.
Huko, maafisa wa kijasusi wa MI5 wanaweza kukaa bega kwa bega na maafisa wa polisi ambao jukumu lao ni kutekeleza hatua zinazohitajika kuzuia njama za kigaidi.
Wanaweza pia kufanya kazi katika eneo moja na wakala wa FBI ya Marekani au mtaalamu wa lugha aliyetoka GCHQ, shirika la Uingereza linaloshughulikia ujasusi wa mawimbi ya mawasiliano na usalama wa mtandao.
Tangu tukio la 9/11, mashirika ya kijasusi ya Marekani pia yamefanyiwa marekebisho makubwa ya kimfumo, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi (NCTC) karibu na Washington, D.C., na kuanzishwa kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Kitaifa wa Ujasusi, mwenye jukumu la kuhakikisha kuwa taarifa zinafikishwa mahali zinapohitajika miongoni mwa mashirika 18 ya kijasusi ya Marekani.
Uhusiano kati ya CIA na shirika la Uingereza, Secret Intelligence Service, linalojulikana zaidi kama MI6,labda ndio wa karibu zaidi duniani.
Ushirikiano huu unaimarishwa zaidi na muungano wa "Five Eyes," unaounganisha rasilimali za kijasusi za Marekani, Uingereza, Kanada, Australia, na New Zealand.
Hata hivyo, tangu ndege zilipogonga Majengo Pacha (Twin Towers), kumekuwa na makosa makubwa yanayoendelea kutokea kuhusiana na masuala ya kijasusi, tathmini, na mipango ya kimkakati.
Katika kipindi cha maandalizi ya uvamizi wa Iraq ulioongozwa na Marekani mwaka 2003, MI6 iliruhusu taarifa zake za kijasusi kutumiwa kisiasa bila busara, jambo lililosababisha shirika hilo kupata pigo kubwa zaidi kwa sifa yake tangu enzi za usaliti uliofanywa na wakala maradufu Kim Philby pamoja na wapelelezi wengine waliokuwa wakifanyia kazi Umoja wa Kisovieti katika miaka ya 1950 na 1960.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katikati ya shinikizo kubwa la kisiasa kutoka Washington la kutaka ushahidi kwamba Iraq, chini ya Saddam Hussein, bado ilikuwa na "silaha za maangamizi makubwa," shirika la MI6 liliipatia serikali ya Waziri Mkuu Tony Blair taarifa za kijasusi ambazo baadaye zilibainika kuwa na kasoro.
Ingawa ni kweli kwamba Iraq ilikuwa na silaha za maangamizi makubwa hapo awali, ghala lake lote la silaha hizo lilikuwa limeondolewa kufuatia Vita vya Ghuba vya mwaka 1991.
Baada ya uvamizi wa Iraq mwaka 2003, MI6 ilifanyia marekebisho makubwa mfumo wake wa kutathmini taarifa ghafi za kijasusi,zinazojulikana kama "CX", zilizopokelewa kutoka kwa mawakala waliokuwa kazini.
Leo hii, kuna mgawanyo wa wazi kati ya wasimamizi wa mawakala, ambao kazi yao ni kukusanya taarifa hizo kutoka kwa vyanzo katika maeneo kama Iran au Korea Kaskazini, au kutoka ndani ya makundi ya kigaidi kama Al-Qaeda, na timu ya uchambuzi inayohusika na kuhakiki na kuhoji taarifa hizo, mara nyingi ikizirudisha nyuma ili kudai uthibitisho zaidi.
Licha ya mabadiliko haya, hawakujifunza baadhi ya vitu hadi miaka kadhaa baada ya tukio la 9/11.
"Vita vya Iraq vya mwaka 2003 vilijengwa juu ya taarifa za kijasusi zenye kasoro kubwa," anasema Jenerali Richard Shirreff, ambaye aliwahi kuhudumu nchini Iraq kama kamanda wa kitengo.
Anaongeza: "Je, tumejifunza kutokana na hilo? Hapana, nadhani tunapata shida kujifunza... Kama kamanda, ilikuwa dhahiri kwamba tulikuwa tunaelekea kwenye kufeli kimkakati."
Kufuatia uvamizi wa Iraq, uchunguzi mpya ulianzishwa, ambao ulihitimishwa kwa Ripoti ya Butler.
Ripoti hiyo ilihitimisha kuwa taarifa za kijasusi za Uingereza kuhusu mpango unaodaiwa wa Iraq wa silaha za maangamizi makubwa "zilikuwa na kasoro kubwa na zilitegemea sana vyanzo visivyothibitishwa."
Shirika la Usalama (MI5) nalo limepitia changamoto na kufeli kwake, sambamba na mafanikio mengi yasiyopingika, katika kuzuia mipango ya kigaidi.
Kufuatia tukio la 9/11, Jonathan Evans mkurugenzi wa MI5 kuanzia mwaka 2007 hadi 2013 anabainisha kuwa "tathmini ilionyesha kuwa, kwa kiasi kikubwa, tishio kubwa zaidi kwa usalama wa Uingereza lilikuwa tishio la kigaidi kutoka kwa Al-Qaeda na watu binafsi au makundi yanayohusiana nayo."

Chanzo cha picha, Getty Images
Hata hivyo, kutokana na kuwa na hifadhidata iliyokuwa na zaidi ya "watu wanaofuatiliwa" 20,000 wakati huo, pamoja na idadi kubwa ya uchunguzi unaoendelea kwa wakati mmoja, MI5 ilikabiliwa na inaendelea kukabiliwa na changamoto ya kila siku ya kuamua ni vidokezo vipi vipewe kipaumbele.
Na haikufanya uamuzi sahihi kila wakati.
Mwaka 2005, ilishindwa kuzuia mashambulizi ya kujitoa mhanga ya tarehe 7 Julai jijini London, ambayo yalisababisha vifo vya watu 52.
Shirika la Usalama lilikuwa likimfahamu Mohammed Sidique Khan ambaye alikuja kubainika kuwa ndiye kiongozi wa kundi hilo lakini halikujua kuhusu mipango aliyokuwa karibu kuitekeleza.
Shambulio la bomu katika ukumbi wa Manchester Arena mwaka 2017 linachukuliwa kuwa kisa kingine cha kushindwa, na cha hivi karibuni zaidi.
Leo hii, tishio la ugaidi halijatoweka, lakini Evans anabainisha kuwa "hali halisi imebadilika."
"Ugaidi unaofanywa na makundi yasiyo ya kiserikali bado ni suala linalotia wasiwasi mkubwa, lakini vitisho vinavyotoka kwa mataifa vimezidi kuwa hatari na vinahatarisha usalama wa taifa kwa kiwango ambacho ni kikubwa sawa na au zaidi ya ugaidi wa makundi yasiyo ya kiserikali. Vitisho hivi vinatokana na Urusi, Iran, vibaraka wao, na China, na vinajitokeza katika namna mbalimbali," anasema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Inaweza pia kusemwa kuwa uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kuungana na Israel katika kuishambulia Iran mwaka huu ulikuwa ni ishara ya kushindwa kwa idara za ujasusi kutabiri au kufikiria ipasavyo hatua zinazoweza kuchukuliwa na adui.
Washirika wote wa Marekani katika eneo la Ghuba walikuwa wakifahamu vyema hatari kubwa ya Iran kulipiza kisasi kwa kufunga mlango Bahari la Hormuz.
Tahadhari ilikuwepo, lakini Trump alionekana kukosa mkakati mbadala wakati Iran ilipochukua hatua hiyo hasa ambayo ilikuwa imetishia kuifanya, jambo lililosababisha vurugu kubwa katika masoko ya nishati duniani.
Hesabu za kimaadili
Kufuatia mashambulizi ya tarehe 11 Septemba, kulikuwa na hofu kubwa kwamba wimbi la pili la mashambulizi lingetokea. Kwa hakika, kundi la Al-Qaeda lenyewe lilitangaza "wimbi la ndege" ambazo zingeshambulia majengo zaidi.
Katika jitihada za kuzuia shambulio kama hilo, Marekani na washirika wake walifanya ukiukwaji mwingi wa haki za binadamu.
Washukiwa walizuiliwa nchini Afghanistan au Pakistan,mara nyingi kwa kuzingatia taarifa za kijasusi zisizoaminika na mamia ya watu walisafirishwa (wakiwa wamefungwa, wamefumbwa macho, na kuvalishwa nepi) hadi upande wa pili wa dunia, kwenye gereza la muda katika kambi ya jeshi la wanamaji la Marekani huko Guantanamo Bay, Cuba, ambapo walibaki kizuizini bila kufikishwa mahakamani.
Mashirika ya haki za binadamu yalilaani hali hii kama doa katika dhamiri ya kimaadili ya Marekani.
Visa vya unyanyasaji wa wafungwa waliokuwa mikononi mwa Marekani nchini Iraq na Afghanistan vilifichuka, na baadhi ya waliohusika waliwajibishwa, ingawa wakosoaji wanabainisha kuwa maafisa wa ngazi za juu waliepuka adhabu.
Hata hivyo, Marekani inaendelea na utaratibu wa kuweka watu kizuizini bila kesi huko Guantanamo Bay, na mwaka 2025, ilihamisha zaidi ya wanaume 200 kutoka eneo la Marekani hadi Kituo cha Kuzuia Magaidi cha El Salvador, kituo ambacho kimezua utata.
Kipindi kilichofuata mara moja baada ya tukio la 9/11 pia kiliacha doa katika rekodi ya Uingereza ya haki za binadamu.
Mwaka 2004, shirika la kijasusi la MI6 lilishiriki katika utekaji nyara na uhamishaji wa siri wa mwanaharakati wa Kiislamu kutoka Libya, Abdelhakim Belhaj, na mkewe kutoka Thailand hadi Libya.
Akiwa huko, alikaa gerezani kwa miaka mingi na kuteswa na utawala wa Kanali Muammar Gaddafi.
Hatimaye suala hilo lilifichuka na kusababisha Mwanasheria Mkuu kutoa ombi rasmi la msamaha kwa umma bungeni mwaka 2018.
Leo hii, idara ya sheria ya ndani inatajwa kuwa kitengo kinachokua kwa kasi zaidi ndani ya mashirika haya.
Kuimarika kwa Urusi na Uchina

Chanzo cha picha, Reuters
"Tulitumia miaka 20 ya kwanza ya karne hii tukijikita karibu kabisa katika kupambana na ugaidi na uasi," alisema Alex Younger, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa Shirika la Ujasusi la Uingereza (MI6) kuanzia mwaka 2014 hadi 2020.
Aliyekuwa mkuu wa MI6 alitoa kauli hizo katika tamasha la fasihi muda mfupi baada ya kuondoka katika wadhifa wake, akiongeza kuwa "Tulishindwa kuona kuibuka kwa China kama nguvu ya kijeshi na changamoto ya kimkakati."
Katika muktadha huohuo, Jenerali Shirreff aliandika kitabu cha kusisimua chenye maudhui ya kisiasa kilichoitwa *War With Russia* (Vita na Urusi) mwaka 2016, ambamo alitabiri uvamizi mkubwa wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Kufuatia mashambulizi ya Septemba 11 na "Vita dhidi ya Ugaidi" vilivyofuata,wakati mataifa ya Magharibi yakishughulika kupambana na Taliban na kundi linalojiita Islamic State, au kujaribu kudhibiti hali ya vurugu iliyotokana na uvamizi wa Iraq,Urusi na China zilianza mipango mikubwa ya kujihami na kuimarisha jeshi.
Mipango hiyo ilijumuisha uvumbuzi kama vile makombora ya kasi ya juu sana, ambayo yamepunguza kwa kiasi kikubwa faida ya kijeshi ambayo NATO ilikuwa nayo hapo awali.
"Makosa ya nchi za Magharibi hayakuwa tu kupoteza mwelekeo kutokana na mapambano dhidi ya ugaidi baada ya tukio la Septemba 11," anabainisha Sam Olsen, mchambuzi mkuu katika kampuni ya ujasusi wa kiusalama ya Sibylline.
"Pia zilikosea kutafsiri asili ya kuibuka kwa China, zikidhani kuwa ushirikiano wa kiuchumi ungesababisha kuoana kwa mifumo ya kisiasa."
China, kama ilivyo kwa Iran, Urusi, na Korea Kaskazini, inachukuliwa kuwa "msingi thabiti" kwa ajili ya ukusanyaji wa taarifa za kijasusi.
Mwaka 2001, teknolojia ya bayometriki ilikuwa bado katika hatua za awali, lakini matumizi yaliyofuata ya mifumo ya kutambua sura, mboni, na namna ya kutembea yamechangia katika changamoto kubwa ya kuingiza na kutoa mawakala na wasimamizi wao mipakani bila kugundulika leo.
Leo hii, China pamoja na Urusi ni nchi muhimu katika ujasusi kwa MI6. "Mashirika ya ujasusi ya Magharibi yanaelewa mambo mengi kuhusu China," anabainisha Sam Olsen wa kampuni ya ushauri ya Sibylline.
Anasisitiza kuwa "hatari kubwa zaidi iko katika kuangalia vipengele binafsi bila kuelewa kikamilifu picha nzima inayoundwa na vipengele hivyo."
"Nguvu ya China haiko tena kwenye meli, makombora, na askari pekee, inazidi kujikita katika sekta ya,vipengele vya kielektroniki, madini muhimu, betri, bandari, mawasiliano, na uwezo wa viwanda."
Anaongeza kuwa "Kwa hivyo, tatizo mara nyingi ni suala la kutafsiri vibaya mikakati badala ya kushindwa kukusanya taarifa za kijasusi."

Chanzo cha picha, Getty Images
Miaka ishirini na mitano iliyopita, katika siku ya mashambulizi ya tarehe 11 Septemba, maafisa wa ujasusi wa Marekani walikuwa na vipande vya fumbo hilo,mfano ambao mara nyingi hutumiwa na wapelelezi,lakini walishindwa kuvikusanya pamoja ili kuona wazi kilichokuwa kikija.
Ukusanyaji bora wa taarifa za kijasusi hauna faida yoyote ikiwa hautageuzwa kuwa faida ya kimkakati.
Dunia isiyotambulika
Ni dhahiri kwamba mazingira ya ujasusi na kupambana na ugaidi yamebadilika, hadi kufikia hali ya kutotambulika,katika muda wa robo karne tangu asubuhi hiyo ya Septemba huko New York.
Kwa ujio wa ujasusi unde au mnemba AI na kompyuta ya kwanta, mabadiliko haya yataendelea, yakiendelea kwa kasi kubwa katika sekta mbali mbali.
Hata hivyo, katika ulimwengu uliojaa simulizi zinazokinzana na maslahi yanayoshindana, mataifa ya Magharibi hayana ukiritimba wa kushindwa kwa ujasusi, uangalizi, au hesabu potofu za kimkakati.
Mifano mingine muhimu ni pamoja na uvamizi mbaya wa Urusi dhidi ya Ukraine mwaka wa 2022 na kile ambacho baadhi wamekiita "9/11 ya Israeli", uvamizi ulioongozwa na Hamas kutoka Gaza mnamo Oktoba 7, 2023.
Hatimaye, maswali yanaendelea kuhusu maamuzi makubwa ya kimkakati ya kitaifa.
Je, ilikuwa hatua sahihi kwa Uingereza kujiunga na uvamizi wa Iraq uliokuwa ukiungwa mkono na Rais Bush?
Je, ilikuwa sahihi kushiriki katika Operesheni Enduring Freedom inayoongozwa na Marekani nchini Afghanistan, na kisha kuiacha nchi hiyo kwa Taliban miongo miwili baadaye baada ya kujiondoa kwa haraka?
Maswali haya na mengine mengi yanaendelea kujitokeza leo
Imetafsiriwa na Sarafina Robi na kuhaririwa na Ambia Hirsi












