Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini Umoja wa Mataifa ulibadilisha ramani ya dunia?
Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulitoa wito wa kubadilishwa kwa ramani ya dunia inayotumika kwa sasa na ramani nyingine inayoonesha kwa usahihi zaidi ukubwa halisi wa mabara, ikiwemo Afrika.
Azimio la "Marekebisho ya Ramani", lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, linalenga kushughulikia kasoro za ramani ya Mercator, ambayo huifanya Afrika ionekane kuwa na ukubwa unaokaribiana na Greenland, licha ya ukweli kwamba Afrika ni kubwa kwa takriban mara 14 zaidi.
Azimio hilo limependekeza matumizi ya ramani mpya inayojulikana kama Equal Land Projection, ambayo inaonesha kwa usahihi zaidi ukubwa halisi wa maeneo ya nchi na mabara, ingawa ramani hiyo pia ina baadhi ya mapungufu.
Katika miaka michache iliyopita, kumekuwa na jitihada kadhaa za kutafuta suluhisho la changamoto ya kuwakilisha kwa usahihi uso wa dunia, ambao una umbo la duara, kwenye ramani bapa yenye umbo la mstatili. Kila ramani ina faida na hasara zake.
Ramani ya Mercator
Mchoraji ramani kutoka Flanders, Gerardus Mercator, alitengeneza ramani hiyo iliyopewa jina lake mwaka 1569, na hadi leo bado inatumika kwa kiasi kikubwa.
Lengo lake kuu lilikuwa kuwasaidia mabaharia wa Ulaya kusafiri na kuelekeza meli zao baharini, kama alivyoeleza James Cheshire, profesa wa masuala ya uchoraji ramani katika Chuo Kikuu cha London.
Cheshire aliiambia BBC: "Alitaka mstari ulionyooka uliochorwa kwenye ramani uonekane kuwa umenyooka pia wakati mtu anapofuata mwelekeo fulani wa dira. Hilo ndilo lilikuwa kusudi la ramani hiyo, na ilitimiza kazi hiyo kwa ustadi mkubwa."
Ili kudumisha usahihi wa pembe hizo kwenye ramani bapa, Mercator alilazimika kuongeza nafasi kati ya mistari ya gridi kadiri ilivyokuwa ikisogea kutoka Ikweta kuelekea kwenye ncha za dunia.
Ramani yake hushughulikia mviringo wa Dunia kwa namna inayofanya nchi zilizo karibu na Ikweta zionekane kuwa ndogo zaidi kuliko ukubwa wao halisi, huku nchi zilizo karibu na ncha za dunia zikionekana kurefuka na kuwa kubwa zaidi.
Upotoshaji huu unatokana na ukweli kwamba haiwezekani kuwakilisha uso wa Dunia kwa usahihi kwenye ramani yenye vipimo viwili.
Zaidi ya miaka 450 baadaye, uvumbuzi wa Mercator bado ndio msingi wa ramani nyingi tunazoziona madarasani, kwenye televisheni na mtandaoni, zikiwemo za Google.
Hata hivyo, wakosoaji wa ramani ya Mercator wanasema kwamba kuona baadhi ya maeneo yakiwa madogo kuliko ukubwa wao halisi na mengine yakiwa makubwa kuliko yalivyo, kunaweza kuwa na athari za kisaikolojia, kwa sababu kwa asili huwa tunahusisha vitu vikubwa na umuhimu zaidi.
Mtaalamu wa jiografia kutoka Kenya, Kyoko Mwendo, anasema kwamba namna Afrika inavyooneshwa kwenye ramani hizi hupunguza kwa njia isiyo ya moja kwa moja ukubwa wa rasilimali zake, idadi ya watu na fursa za uwekezaji.
Aliliambia BBC: "Ramani si miongozo tu kwa wasafiri, bali pia huchangia katika kuunda mtazamo wetu kuhusu maeneo mbalimbali kisiasa na kiuchumi."
Ramani ya Equal Earth
Ramani ya Equal Earth inalenga kushughulikia tatizo la upotoshaji unaotokana na makadirio ya Mercator.
Ilibuniwa mwaka 2018 na timu ya wataalamu wa uchoraji ramani kwa lengo la kuonesha kwa usahihi zaidi ukubwa na maumbo ya maeneo ya nchi na mabara. Ilihamasishwa na makadirio ya Robinson ya mwaka 1963, ambayo ni aina ya ramani inayoonesha uso mzima wa Dunia katika picha moja.
Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zilipitisha Ramani ya Equal Earth mwezi Februari.
Hata hivyo, ramani hiyo inaacha matumizi ya mistari iliyonyooka ambayo yaliifanya ramani ya Mercator kuwa bora kwa urambazaji. Pia, Equal Earth haifai kwa kupima umbali halisi kati ya maeneo mbalimbali.
Cheshire alisema kuwa ramani bapa haiwezi kuonesha ukubwa, umbo, umbali na mwelekeo kwa usahihi kwa wakati mmoja. Ili kuonesha mambo hayo yote kwa usahihi, ramani inahitaji kubaki katika umbo la duara kama dunia.
Ramani ya Peters
Ramani ya dunia iliyopewa jina lake iliundwa na mwanahistoria Mjerumani Arno Peters mwanzoni mwa miaka ya 1970. Ramani hii yenye umbo la mstatili inatumia makadirio yaliyoelezwa kwa mara ya kwanza na mchoraji ramani kutoka Scotland, James Gall, mwaka 1855.
Makadirio haya yanatoa usahihi wa ukubwa wa maeneo badala ya usahihi wa maumbo. Kwa hiyo, maeneo ya karibu na ncha za dunia huonekana yakiwa yamebanwa, huku maeneo yaliyo karibu na Ikweta yakionekana yameinuliwa au kurefuka.
Hii husaidia kutatua tatizo la tofauti kubwa ya ukubwa kati ya Greenland na Afrika, na huwapa watumiaji picha iliyo wazi zaidi ya ukubwa halisi wa maeneo mbalimbali ya nchi na mabara, huku mistari ya longitudo na latitudo ikiendelea kuwa iliyonyooka.
Hata hivyo, ramani hii hupotosha kwa kiasi kikubwa maumbo ya maeneo, na kuyafanya yaonekane tofauti na jinsi yalivyozoeleka. Kwa mfano, Urusi huonekana kuwa ndogo zaidi.
Aidha, mistari iliyonyooka kwenye ramani ya Peters haiwakilishi mwelekeo sahihi wa dira, na hivyo ramani hii haifai kwa matumizi ya urambazaji.
Njia nyingine za kuchora ramani ya dunia
Kuna njia nyingine za kuchora ramani ya dunia.
Kwa mfano, makadirio ya azimuth ya isometriki (isometric azimuth projection) huonesha maeneo mbalimbali ya dunia kwa uwiano sahihi na umbali sahihi kutoka kwenye sehemu moja ya kati iliyochaguliwa.
Bendera ya Umoja wa Mataifa ni mfano mzuri wa ramani ya aina hii, kwa sababu ramani ya dunia iliyo kwenye bendera hiyo imejikita kwenye Ncha ya Kaskazini.
Katika aina hii ya ramani, maeneo yote huwekwa katika "azimuth" sahihi, yaani mwelekeo sahihi wa ulalo kutoka kwenye sehemu ya kati.
Pia kuna ramani zinazoelekeza kusini juu, au ramani zilizogeuzwa, ambapo nusu ya dunia ya kusini huonekana upande wa juu wa ramani.
Kwa ufupi, ni ramani ya kawaida ambayo kaskazini huwa juu, lakini imezungushwa kwa nyuzi 180.