Jinsi papa wanavyojenga urafiki wa karibu baharini

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Papa mara nyingi huonekana kama viumbe wapweke, lakini utafiti mpya unaonyesha kuwa baadhi yao wana maisha ya kijamii yaliyo tata kuliko ilivyodhaniwa.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Exeter, Chuo Kikuu cha Lancaster, Fiji Shark Lab na Beqa Adventure Divers umebaini kuwa papa wa aina ya bull shark huunda mahusiano mbalimbali ya kijamii, kuanzia urafiki wa kawaida hadi urafiki wa karibu. Pia huonekana kuchagua papa wa kushirikiana nao na hata kuwaepuka wengine.

Katika uchunguzi wa miaka sita uliowahusisha papa 184 wa aina ya bull shark, watafiti waliwachunguza katika makundi matatu ya umri: wale ambao hawajakomaa kijinsia, waliokomaa kijinsia, na waliopita hatua ya uzazi.

Watafiti walifuatilia aina mbalimbali za maingiliano, ikiwemo papa waliokuwa ndani ya umbali wa urefu mmoja wa mwili wao, pamoja na wale walioogelea sambamba au kufuatana.

Matokeo yalionyesha kuwa papa wa jinsia zote walipendelea kushirikiana na majike. Hata hivyo, papa dume walikuwa na mahusiano mengi zaidi ya kijamii kuliko majike. Kwa kuwa madume ni wadogo kwa ukubwa, watafiti wanaamini kuwa uwepo wa majike unaweza kusaidia kupunguza migogoro au tabia za uchokozi miongoni mwao.

"Tunaanza tu kuelewa maisha ya kijamii ya spishi nyingi za papa. Kama ilivyo kwa wanyama wengine, huenda uhusiano wa kijamii unawasaidia kujifunza ujuzi mpya, kupata chakula, kutafuta wenzi wa kuzaliana na kuepuka migogoro," alisema Profesa Darren Croft wa Kituo cha Utafiti wa Tabia za Wanyama cha Exeter.

Watafiti pia waligundua kuwa papa waliokomaa kijinsia walikuwa kitovu cha mitandao ya kijamii, huku wale wadogo zaidi wakiwa na mahusiano machache.

Hatari ya kushambuliwa na madume wakubwa huwafanya papa wadogo kujitenga na makundi ya kijamii, ingawa baadhi yao hujenga mahusiano na kujifunza kutoka kwa papa wenye uzoefu mkubwa zaidi.

"Papa hawa wakubwa wana uzoefu wa miaka mingi wa kuwinda na kuzaliana, hivyo huenda maingiliano ya kijamii yasiwe muhimu kwao kama ilivyo kwa papa vijana," alisema Natasha Marosi, mwandishi mkuu wa utafiti huo.

Marosi alisema uelewa wa tabia za kijamii za papa unaweza kusaidia kuboresha sera za usimamizi na uhifadhi wa viumbe hao wa baharini.

Papa wana marafiki wa karibu

Papa si wawindaji wapweke pekee kama wanavyoonyeshwa mara nyingi.

Papa wa mwamba wa kijivu (grey reef shark) wanajulikana kubaki katika makundi yale yale ya kijamii kwa muda wa hadi miaka minne. Makundi hayo hugawanyika katika vikundi vidogo, kufuata njia tofauti na baadaye kuungana tena kulingana na misimu.

Vilevile, papa wachanga wa aina ya limau (lemon shark) huishi kwa makundi na kujifunza kutoka kwa wenzao. Kupitia maingiliano ya kijamii, hujifunza namna ya kupata chakula na kuepuka wanyama wanaowawinda. Mara nyingi hupendelea kukaa na papa wa ukubwa sawa na wale waliowahi kukutana nao awali.

Hata papa wakubwa weupe (great white sharks), ambao kwa kawaida huonekana kuwa wapweke, wanaweza kuwa na urafiki wa kudumu. Papa wawili maarufu waliopewa majina Simon na Jekyll walionekana kusafiri pamoja kwa zaidi ya kilomita 6,000 bila kutengana.

Watoto wa papa hula wenzao wakiwa tumboni mwa mama yao

Mojawapo ya mambo ya kushangaza zaidi kuhusu papa ni kwamba baadhi yao huanza mapambano ya kuishi kabla hata ya kuzaliwa.

Kwa papa wa aina ya sand tiger, watoto walioko tumboni mwa mama yao huwashambulia na kuwala ndugu zao. Papa jike wa aina hii huwa na mifuko miwili ya uzazi, na kila mmoja unaweza kubeba hadi viinitete vitano.

Hata hivyo, viinitete hivyo hupigania rasilimali zilizopo hadi kubaki mtoto mmoja mwenye nguvu zaidi katika kila mfuko wa uzazi.

Hali hii inajulikana kama adelphophagy, neno la kisayansi linalomaanisha "kumla ndugu yako". Baada ya kuwala wenzao, watoto hao huendelea kukua kwa kula mayai yasiyorutubishwa yanayozalishwa na mama yao.

Papa ni wakongwe zaidi kuliko miti na dinosauri

Papa ni miongoni mwa viumbe wa kale zaidi duniani.

Visukuku vya awali vya viumbe wanaohusishwa na papa vinakadiriwa kuwa vya miaka milioni 450 iliyopita. Hiyo ni takriban miaka milioni 60 kabla ya miti ya kwanza kuonekana duniani na zaidi ya miaka milioni 200 kabla ya dinosauri.

Meno ya kwanza yanayofanana na ya papa yalionekana karibu miaka milioni 410 iliyopita, huku makundi ya kwanza yaliyofanana na papa wa sasa yakitokea karibu miaka milioni 380 iliyopita.

Leo kuna takriban spishi 500 za papa duniani. Ingawa idadi hiyo ni ndogo kuliko ilivyokuwa katika baadhi ya vipindi vya kale vya kihistoria, spishi mpya bado zinaendelea kugunduliwa.

Papa pia ni miongoni mwa viumbe wachache walionusurika matukio yote matano makubwa ya kutoweka kwa viumbe duniani, yakiwemo Maafa Makubwa ya Permian-Triassic ambayo yaliangamiza takribani asilimia 90 ya viumbe wa baharini.

Baada ya mamia ya mamilioni ya miaka ya mageuzi, papa wameendelea kustawi katika karibu kila eneo la bahari duniani.

Papa wa Greenland huishi kwa mamia ya miaka

Miongoni mwa wanyama wote wenye uti wa mgongo, papa wa Greenland (Somniosus microcephalus) ndio wanaojulikana kwa kuishi maisha marefu zaidi.

Wanaoishi katika maji baridi ya Atlantiki Kaskazini, papa hawa hukua polepole sana, mara nyingi chini ya sentimita moja kwa mwaka.

Watafiti wamegundua kuwa hawafikii ukomavu wa kijinsia hadi wanapofikisha umri wa karibu miaka 150. Papa mzee zaidi aliyewahi kukadiriwa umri wake alifikiriwa kuwa na takribani miaka 392.

Ingawa mara nyingi huchukuliwa kuwa viumbe wa upweke, ushahidi unaongezeka kuonyesha kuwa baadhi ya spishi za papa huunda urafiki na mitandao ya kijamii inayoweza kudumu kwa miaka mingi, jambo linalobadilisha kwa kiasi kikubwa mtazamo wa muda mrefu kuhusu viumbe hao wa baharini.