Kwa nini wanasayansi wanataka kuleta sampuli kutoka sayari ya Mars duniani?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Safari moja ya anga inatarajiwa kuanza kwa lengo la kukusanya sampuli kutoka Phobos, mojawapo ya miezi ya sayari ya Mirihi, na kuirejesha duniani.

Ikiwa safari hiyo itafanikiwa, itakuwa mara ya kwanza kwa sampuli kutoka Mirihi au miezi yake kuletwa duniani kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi katika maabara.

Chombo hicho cha anga kitarushwa kutoka nchini Japan na kinatarajiwa kuwasili Phobos mwezi Agosti 2027.

Safari hiyo, inayojulikana kama Mars Moon Exploration (MMX), inaongozwa na Shirika la Japan la Uchunguzi wa Anga za Juu (JAXA) na inatarajiwa kutatua jibu la jinsi miezi ya Mirihi ilivyoundwa.

"Hakujawahi kuwa na safari iliyofanikiwa ya kwenda Phobos na kurejesha sampuli yake duniani," alisema Profesa Sarah Russell wa Makumbusho ya Historia ya Asili, ambaye ni naibu mkurugenzi wa uchambuzi wa sampuli katika mradi wa MMX.

"Nadhani hii ni safari yenye malengo makubwa sana na ya kusisimua," aliongeza.

Kuna miezi mitatu pekee katika sehemu ya ndani ya mfumo wa jua; mwezi wa Dunia na miezi miwili ya Mirihi, ambayo ni Phobos na Deimos.

Miezi hiyo yote miwili ni midogo sana. Phobos ina kipenyo cha takriban kilomita 20, huku Deimos ikiwa na kipenyo cha takriban kilomita 10. Pia, haina umbo la duara kama miezi mingi, bali ina maumbo yasiyo ya kawaida yanayofanana na viazi.

Chombo cha anga cha safari ya MMX kitachunguza Deimos kitakapowasili katika obiti ya Mirihi na kuchunguza mazingira ya sayari hiyo, kabla ya kuichunguza Phobos.

Safari hiyo inalenga kutua kwa chombo kidogo cha uchunguzi kinachotembea, maarufu kama rover, ili kuchunguza uso wa mwezi huo, ingawa kutua huko hakutakuwa rahisi.

Profesa Sarah Russell anasema hakuna mtu aliyewahi kufanikiwa kutua na rover kwenye mwezi mdogo kiasi hicho.

"Mwezi huo wenyewe hauna nguvu kubwa ya uvutano," alieleza, akiongeza kuwa, "Lakini uko karibu na sayari kubwa yenye nguvu kubwa zaidi ya uvutano, jambo linalofanya kutua kwa rover kwenye uso wake kuwa kugumu zaidi."

Rover hiyo itabaini eneo linalofaa kwa kutua, ili chombo cha anga cha MMX kiweze kutua kwenye Phobos katika hatua inayofuata.

Baada ya kutua, chombo hicho kitatumia mkono wa roboti na vifaa viwili vya kukusanyia sampuli ili kukusanya vumbi kutoka kwenye uso wa mwezi huo.

Sampuli hizo zitawekwa katika kapsuli ndogo itakayorejea duniani mwaka wa 2031 na kutua katika Jangwa la Woomera, kusini mwa Australia.

Kiasi cha sampuli kitakachorejeshwa duniani kitakuwa kidogo sana, gramu 10 pekee.

"Kwa kweli, hicho ni kiasi kidogo sana," alisema Dkt. Chrissa Everledo wa Chuo Kikuu cha Leicester, ambaye anashirikiana na timu ya safari hiyo ya Japan.

"Hata hivyo, tunaweza kufanya tafiti mbalimbali hata kwa kutumia chembe moja moja.Huhitaji kuleta kilogramu kadhaa za sampuli kutoka kwenye uso wa mwezi hadi duniani ili kufanya utafiti wa kisayansi. Kwa hiyo, kila gramu ina thamani kubwa."

Wanasayansi wanaamini kuwa sampuli itakayoletwa duniani kutoka Phobos inaweza hatimaye kutoa majibu kuhusu fumbo la asili ya miezi ya sayari ya Mirihi.

Kwa sasa, kuna nadharia mbili zinazoshindana kueleza jinsi miezi hizo zilivyotokea.

Katika nadharia ya kwanza, katika hatua za awali za historia ya Mirihi, jiwe kubwa kutoka angani liligongana na sayari hiyo, na Phobos pamoja na Deimos viliundwa kutokana na mabaki ya mgongano huo.

Nadharia ya pili inaeleza kuwa miezi hiyo miwili awali ilikuwa asteroidi zilizokuwa zikizunguka katika maeneo ya nje ya mfumo wa jua, kabla ya kunaswa na nguvu ya uvutano ya sayari nyekundu ya Mirihi.

"Sampuli hiyo itakaporejeshwa duniani, tutaweza kuchunguza kwa kina muundo wake wa kikemia na madini yaliyomo, na nadharia hizo mbili zinatabiri matokeo tofauti kabisa," alisema Profesa Sarah Russell.

Timu ya wataalamu wanaoendesha safari hiyo pia inatumai kuwa sampuli zitakazorejeshwa duniani zitatoa mafanikio mengine zaidi ya lengo kuu la mradi huo.

"Moja ya mambo yanayosisimua sana ni kwamba Phobos iko karibu sana na uso wa Mirihi kiasi kwamba kila kitu kinapogonga uso wa Mirihi, chembe ndogo zinaweza kung'oka na kutua kwenye Phobos," alisema Russell.

"Hii ina maana kwamba sampuli itakaporejeshwa duniani, huenda ikawa na chembe zilizotoka kwenye Mirihi yenyewe. Kwa hiyo, inaweza kutupatia taarifa za moja kwa moja kuhusu muundo na historia ya Mirihi," aliongeza.

Kurejesha sampuli kutoka Mirihi hadi duniani kumekuwa kwa muda mrefu ndoto ya wanasayansi wengi wanaochunguza anga za juu.

Rover ya NASA, Perseverance, ambayo imekuwa ikichunguza Mirihi tangu mwaka 2021, imekusanya kwa uangalifu sampuli na kuzihifadhi katika makontena maalumu.

Hata hivyo, mradi wa pili wa NASA kwa ushirikiano na Shirika la Anga za Juu la Ulaya (ESA), unaojulikana kama Mars Sample Return, uliokuwa na lengo la kukusanya makontena hayo na kuyarejesha duniani, umesitishwa baada ya Bunge la Marekani kusimamisha ufadhili wake.

China pia inapanga kufanya safari yake ya kukusanya sampuli kutoka Mirihi, inayotarajiwa kurushwa angani mwaka 2028. Mradi huo unalenga kurejesha sampuli hizo duniani mwaka wa 2031.

Wanasayansi wanatamani sana kupata sampuli za moja kwa moja kutoka Mirihi na miezi yake ambazo wanaweza kuzichunguza katika maabara, kwa sababu sampuli hizo zitakuwa katika hali yake ya asili, bila kuchafuliwa na mazingira ya duniani.