Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Harry Kane mshindi tuzo ya Ballon d'Or
"Wow wow wow!" alisema Harry Kane alipopanda jukwaani kupokea tuzo yake.
"Karibu niishiwe maneno. Kuwa hapa London kumefanya usiku huu kuwa wa kipekee zaidi kwangu. Imekuwa bahati nzuri usiku wa leo. Asanteni wote mlionipigia kura. Ninaweza kufikiria haikuwa rahisi kufanya uamuzi mwaka huu.
Kuna wachezaji wengi wa kiwango cha dunia waliopo hapa usiku wa leo. Hongereni washindi wote na walioteuliwa.
Mmeonesha kwa namna ya kuvutia kwamba dhamira, kujituma na jitihada vinaweza kuleta mafanikio makubwa."
Nahodha wa England, Harry Kane, alifunga mabao 73 katika mashindano ya klabu na timu ya taifa msimu wa 2025-26.
Ingawa wapiga kura wa tuzo hii huagizwa kuzingatia msimu mmoja wa hivi karibuni pekee wanapowapanga wachezaji, rekodi ya Kane ya kufunga mabao 156 katika mechi 158 akiwa na Bayern Munich tangu mwaka 2023 imemwezesha kupanda hadi nafasi ya saba katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo.
Kane ameongoza chati ya wafungaji wa Bundesliga kwa misimu mitatu mfululizo, na pia alikuwa mfungaji bora zaidi wa klabu barani Ulaya kwa jumla katika msimu wa 2025-26.
Aidha, aliiongoza timu ya taifa ya England kufikia mafanikio yao makubwa zaidi katika Kombe la Dunia tangu walipotwaa ubingwa mwaka 1966. England ilishinda mechi ya kuwania nafasi ya tatu na kutwaa medali ya shaba, huku Kane akimaliza mashindano hayo akiwa miongoni mwa wafungaji watano bora wa mashindano.
Harry Kane amewashukuru wote waliokuwa sehemu ya safari yake ya soka, kuanzia wachezaji wenzake, makocha hadi familia yake.
Akiwa mwenye hisia na kuanza kutokwa na machozi anapowashukuru wazazi wake.
"Ni heshima kubwa kuwa nahodha wa England"
"Kwa wachezaji wenzangu wa timu ya England, ninasema tena jambo lilelile. Tulikuwa na mwaka wa kipekee. Haukuwa mwaka mkamilifu, lakini tulipata nyakati nyingi nzuri sana. Tumejenga uhusiano na mshikamano mkubwa kati yetu.
Umoja tuliokuwa nao kambini wakati wa Kombe la Dunia ulikuwa wa pekee. Ni heshima kubwa kuwa nahodha wenu na kuwaongoza. Hilo linanifanya nijivunie sana.
Tuzo hii ni yetu sote, bila shaka. Pia kwa Thomas Tuchel na benchi lote la ufundi la England, uongozi wenu, namna mnavyotuongoza na kutusukuma kufikia viwango vya juu zaidi ni jambo la kupongezwa na kuheshimiwa."
"Shukrani kwa Tottenham"
"Naishukuru pia Tottenham Hotspur. Nisingekuwa hapa nilipo leo bila Tottenham. Kwa mwongozo wote na makocha wote walionisaidia kunifanya niishi ndoto yangu ya soka. Matukio yote, mema na mabaya, niliyopitia katika safari hii yamenifikisha kwenye wakati huu muhimu leo.
Kwa mashabiki wote wa Bayern, England, Spurs na mashabiki wangu kote duniani, ninawapenda sana. Msaada na sapoti mnayonipa ninaithamini kwa moyo wangu wote. Nakumbuka si muda mrefu uliopita nilikuwa shabiki kama nyinyi, na ninaelewa maana ya kuucheza mchezo huu. Ilikuwa ndoto yangu. Kila ninapopata nafasi ya kuwarudishia upendo na furaha mnayonipa, huwa ni heshima na fursa kubwa kwangu kufanya hivyo."
Mfungaji Bora wa Mwaka kwa Wanaume, Harry Kane
Mshambuliaji wa England na Bayern Munich, Harry Kane, ametwaa tuzo hii baada ya kuwa na mwaka wa kipekee wenye mafanikio makubwa ya kufunga mabao.
"Asanteni nyote. Kwanza kabisa, ningependa kuishukuru tuzo ya Ballon d'Or na jarida la France Football.
Mwaka uliopita ulikuwa wa kipekee sana kwangu, jambo ambalo najivunia mno. Bila shaka huo ndio ulikuwa msimu bora zaidi katika maisha yangu ya soka.
Kufunga idadi hii kubwa ya mabao ni matokeo ya juhudi za timu nzima. Nina timu bora inayonizunguka, ambayo inanisaidia kubaki mnyenyekevu.
Mke wangu Kate, tumekuwa pamoja katika safari hii. Najua mafanikio haya yasingewezekana bila msaada wako."
Mshindi wa Ballon d'Or kwa Wanawake - Alexia Putellas
Linapokuja suala la mafanikio katika ngazi ya klabu, ni vigumu kutarajia zaidi kutoka kwa Alexia Putellas baada ya kuiongoza Barcelona kama nahodha kutwaa mataji manne makubwa ya ndani na Ulaya katika msimu wa 2025/26: Liga F, Copa de la Reina, Super Cup ya Hispania na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa Wanawake.
Mwezi Mei, Putellas alifikia rekodi ya kuwa mfungaji wa pili kwa idadi ya mabao katika historia ya Barcelona kwa pamoja, baada ya kufunga mabao mawili katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa. Aidha, alitunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano kutokana na kiwango chake cha juu.
Mshindi huyo wa mara mbili wa tuzo hiyo amesawazisha rekodi ya mwenzake, Aitana Bonmatí, ya kushinda tuzo hizo mara tatu. Pia alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Hispania kilichotwaa ubingwa wa UEFA Nations League.
"Asante sana. Ni furaha kubwa kuwa hapa tena. Asante, France Football.
Asante kwa wote mlioamini kuwa nilistahili tuzo hii. Kwa kweli sijui niseme nini, nina mengi sana moyoni! Hongereni kwa wote walioteuliwa, na hongereni pia kwa washindi wote.
Ningependa kuanza kwa kuwashukuru wachezaji wenzangu.
Ninaamini kwamba yeyote kati yetu ambaye yuko hapa angeweza kushinda tuzo hii kwa haki kabisa na kusimama hapa hivi sasa kutoa hotuba hii.
Ni heshima na furaha kubwa kucheza pamoja na kila mmoja wenu.
Tumepitia nyakati za kipekee kama timu, tukashinda changamoto mbalimbali, majeraha, na vipindi ambavyo hatukuvitegemea. Kama nahodha wa timu, ninajivunia sana yale tuliyoyafanikisha pamoja."
Kwa wavulana na wasichana wote duniani, ikiwa unaipenda soka na unatamani kucheza soka, basi cheza soka. Haijalishi kama wewe ni mvulana au msichana.
Pia haijalishi unatoka wapi. Usisikilize mtu yeyote anayekwambia huwezi kufanya hivyo. Jiamini na uamini uwezo wako."Alisema Putellas.
Lamine Yamal atwaa tuzo ya kipaji bora cha mwaka kwa wanaume
Lamine Yamal pia ni miongoni mwa waliokuwa wakiwania tuzo ya Ballon d'Or, lakini amekuwa mshindi wa tuzo hii kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Ni heshima kubwa kuwa hapa na kupokea tuzo hii.
Nilitamani mwenzangu katika timu, Cubarsí, awe hapa, kwa sababu ninaamini tuzo hii ilipaswa kuwa yake. Amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu sana kwa muda mrefu.
Huu ni mwaka wangu wa tatu kupanda jukwaani kupokea tuzo hii. Ningependa kuishukuru klabu yangu na timu yangu ya taifa.
Kuhusu tuzo hii hasa, naamini ilipaswa kwenda kwa Cubarsí."