Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Msichana mwenye umri wa miaka 16 alivyokuwa sehemu ya majaribio ya siri ya CIA
Kitu cha kwanza ambacho Lana Ponting anakumbuka kuhusu Taasisi ya Allen Memorial huko Montreal, hospitali ya zamani ya magonjwa ya akili, ni harufu yake; ilikuwa kama harufu ya dawa.
"Sikupenda jinsi ilivyoonekana; haikuonekana kama hospitali kwangu," alisema akiwa nyumbani kwake Manitoba, Canada.
Hospitali hiyo, ambayo zamani ilikuwa makazi ya tajiri Mskoti wa biashara ya usafirishaji wa meli, ilikuja kuwa makazi ya msichana huyo mwenye umri wa miaka 16 kwa mwezi mmoja mnamo Aprili 1958 baada ya jaji kuagiza apatiwe matibabu kwa tabia iliyotajwa kuwa "isiyotii maadili."
Bi. Ponting alikuwa mmoja wa maelfu ya watu waliokuwa huko ambao walifanyiwa majaribio kama sehemu ya utafiti wa siri wa CIA kuhusu udhibiti wa akili.
Kulingana na rekodi zake za matibabu, ambazo alizipata baadaye, Bi. Ponting alikimbia nyumbani baada ya familia yake kuhama kwa shida kutoka Ottawa kwenda Montreal na akaanza kuandamana na marafiki ambao wazazi wake hawakuwapenda.
"Nilikuwa kijana wa kawaida," alisema. Hata hivyo, jaji alimpeleka katika Taasisi ya Allen.
Alipowasili huko, bila kujua aligeuka kuwa mshiriki wa majaribio ya siri ya CIA yaliyojulikana kama MK-Ultra. Mradi huo, wakati wa Vita Baridi, ulijaribu athari za dawa za kulevya za kisaikolojia kama LSD, mshtuko wa umeme, na mbinu zakuupumbaza ubongo kwa binadamu bila ridhaa yao.
Zaidi ya taasisi 100, zikiwemo hospitali kadhaa, magereza, na shule nchini Marekani na Canada, zilihusika katika mpango huo.
Katika Taasisi ya Allen, Dkt. Evan Cameron, mtafiti wa Chuo Kikuu cha McGill University, alikuwa akiwapa wagonjwa dawa za kulevya na kuwafanya wasikilize sauti zilizorekodiwa zikijirudia tena na tena, wakati mwingine mara elfu, mchakato aliouita "uchunguzi"
Taasisi ya Allen Memorial huko Montreal ilikuwa mahali ambapo majaribio yaliyofadhiliwa na CIA yalifanyika nchini Canada.
Dkt. Cameron alikuwa akimfanya Bi. Ponting asikilize sauti yenye ujumbe unaojirudia tena na tena, hata mara mia.
"Sauti ilikuwa ikiendelea kurudia; wewe ni msichana mzuri, wewe ni msichana mbaya," anasema Bi. Ponting.
Kulingana na Jordan Torby, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu aliyefanya utafiti kuhusu majaribio haya na athari zake za kimaadili, mbinu hiyo ilikuwa aina ya mwongozo wa kisaikolojia na kuvunja mfumo wa mawazo wa mtu.
"Akili za wagonjwa zilikuwa zikidhibitiwa kwa kutumia maelekezo ya maneno," alisema. Anaongeza kuwa Dkt. Cameron pia alichunguza athari za dawa za usingizi, kunyimwa hisia kwa lazima, na kuingizwa katika hali ya kutokuwa na fahamu.
Rekodi za matibabu zinaonesha kuwa Bi. Ponting alipewa LSD pamoja na dawa nyingine kama sodium amytal, aina ya barbiturate, kichocheo kinachoitwa deoxycholate, na nitrous oxide inayojulikana pia kama gesi.
Dkt. Cameron aliandika katika moja ya rekodi zake za matibabu: "Kufikia Aprili 30 mgonjwa alikuwa ameingia katika hatua ya exploration… Baada ya kupewa nitrous oxide, alikua mwenye msongo mkubwa na mwenye vurugu, akaruka kutoka kitandani na kupiga mayowe."
Ukweli wa kutisha kuhusu majaribio ya MK-Ultra ulifichuliwa katika miaka ya 1970. Tangu wakati huo, baadhi ya waathirika walijaribu kushtaki serikali za Marekani na Canada.
Nchini Marekani, kesi nyingi hazikufanikiwa, lakini mwaka 1988 mahakama ya Canada iliiamuru serikali ya Marekani kulipa kila mmoja wa waathirika tisa dola 67,000.
Mwaka 1992, serikali ya Canada, bila kukubali kuwajibika, ilimlipa kila mmoja wa waathirika 77 dola 100,000 za Canada, ambazo wakati huo zilikuwa karibu dola 80,000 za Marekani.
Bi. Ponting anasema jina lake halikuwemo miongoni mwa waliopokea fidia kwa sababu wakati huo alikuwa bado hajajua kuwa alikuwa mwathirika wa majaribio hayo.
Anasema kwa miaka mingi alihisi kuna kitu hakikuwa sawa, lakini ni katika miaka ya hivi karibuni ndipo alipojifunza kwa undani kuhusu ushiriki wake bila ridhaa katika majaribio hayo.
Bi. Ponting anasema hakumbuki mengi kuhusu yaliyomtokea Allen wala miaka iliyofuata.
Baadaye aliolewa na kuhamia Manitoba, ambako watoto wake wawili walizaliwa na bado ana uhusiano wa karibu nao. Sasa ana wajukuu wanne, lakini anasema athari zimeendelea kuwa sehemu ya maisha yake yote.
"Hisia hii imekuwa nami maisha yangu yote; nimekuwa nikijiuliza kwa nini nafikiri hivi na nini kilinitokea," alisema.
Anasema amelazimika kutumia mchanganyiko wa dawa maisha yake yote ili kudhibiti matatizo ya afya ya akili na ndoto za kutisha zinazojirudia.
"Wakati mwingine naamka usiku wa manane nikipiga kelele kwa hofu ya yale yaliyotokea kwangu," alisema.
Hospitali ya Royal Victoria na Chuo Kikuu cha McGill zilikataa kutoa maoni kwa sababu kesi hiyo bado ilikuwa mahakamani. Serikali ya Canada iliambia BBC kuwa mwaka 1992 ilifikia makubaliano ya "kiubinadamu" bila kukubali kuwajibika kisheria.
Kwa Bi. Ponting, kesi hiyo ilikuwa nafasi ya kupata angalau utulivu baada ya miaka mingi. "Wakati mwingine ninakaa sebuleni kwangu na akili yangu hurudi nyuma; ninaishi tena yale yaliyotokea. Kila ninapoona picha ya Dkt. Cameron, ninajawa na hasira," alisema.
Ingawa jina la Dkt. Cameron sasa linahusishwa na mradi wa MK-Ultra, Bi. Torby anasema utafiti wake unaonyesha kuwa wakati huo hakuwa akijua kuwa mradi huo ulifadhiliwa na CIA. Kazi yake na shirika la ujasusi la Marekani iliisha mwaka 1964 na alifariki miaka michache baadaye, mwaka 1967, kutokana na mshtuko wa moyo.
Lakini Bi. Ponting alisema kuwa bila kujali kama Dkt. Cameron alijua chanzo cha ufadhili huo au la, alipaswa kujua kuwa majaribio aliyokuwa akifanya hayakuwa ya kimaadili. Alisema ana matumaini kuwa uchunguzi utaendelea na kwamba waathirika watahisi angalau haki fulani imetendeka.
"Lengo si kufidia kile wagonjwa walichopoteza, kwa sababu hilo haliwezekani; kilicho muhimu ni kwamba mateso yao yasiwe bure na kwamba somo lifunzwe," alisema Bi. Ponting.