Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Tufaha moja kwa siku: Je, kweli lina faida kwa afya?
Tunaambiwa kula tunda la tufaha kila siku, huzuia kumuona daktari mara kwa mara, lakini swali ni, je tunda hili linauwezo huo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika afya yetu?
Watu wengi wanapenda matunda ya tufaha. Kila mwaka karibu tani millioni moja za tufaha huzalishwa kote duniani. Tunda hili huja katika rangi tofauti, ladha tofauti, na ina sifa ya kutukinga kutokana na magonjwa.
Kuna msemo maarufu kwa lugha ya kiingereza usemao, kula tufaha moja kila siku huzuia kumwona daktari.
Je tunda hili la tufaha ni bora kuliko matunda mengine?
Tunda hili lina madini ya phytochemicals na Flavanols, ambazo zinajulikana kuboresha afya, haswa uzani wa mwili na kupunguza hatari ya kupata mshtuko wa moyo.
Mbona tufaha zina afya?
Tufaha pia zina madini aina ya polyphenols na anthocyanins, ambazo huipa maganda ya tufaha rangi yake nyekundu, ambayo husaidia kuimarisha afya ya moyo. Madini mengine ambayo hupatikana kwenye tufaha ni phloridzin, ambayo husaidia kudhibiti viwango vya sukari mwilini.
Tufaha pia zina ufumwele aina ya pectin ambayo hupunguza mafuta mabaya mwilini. Madini ya pectin husaidia kupunguza sukari mwilini na pia kufyonza mafuta kutoka kwa chakula tunachokila na kusaidia mwili kusawazisha viwango vya sukari mwilini.
Katika uhakiki wa mwaka wa 2017 wa tafiti tano zilizofanywa kuhusu kula matunda ya tufaha, matokeo yalionyesha kuwa ulaji wa matunda hayo hupunguza kwa asilimia kumi na nane uwezekano wa mtu kupata aina ya pili ya ugonjwa wa kisukari.
Uhakiki mwingine uliofanywa mwaka wa 2022, baada ya kupitia ripoti kumi na nane za utafiti zilionyesha kuwa kula vyakula ambavyo vimetengenezwa na tufaha au sharubati ya tufaha, hupunguza mafuta mwilini, iwapo utayatumia matunda hayo kwa zaidi ya wiki moja.
Kuwa na mfumo mzuri wa kula chakula, kijumla husaidia kupunguza uwezekano wa mtu kupata ugonjwa wa saratani kwa 45% kutokana na madini yanayopatikana kwa matunda ya tufaha.
Lakini matunda haya ya tufaha, yana uwezo wa kukuzuia kumuona daktari ikilinganishwa na matunda na mimea mingine?
“Tufaha hazina vitamini C kwa wingi, wala madini ya chuma au Calcium, ila zina virutubishi vingine ambavyo hukuza afya ya mtu,'' anasemaJanet Colson, Professa wa lishe na sayansi ya chakula katika Chuo Kikuu cha Middle Tennessee State, nchini Marekani
Watafiti wengine wanasema tufaha ina kiwango cha juu cha antioxidants kushinda matunda mengine.
Tufaha zina madini ambayo hupatikana katika matunda mengine na mboga kama vile polyphenols, anasema Flavia Guzzi, profesa mwandamizi wa mimea katika chuo kikuu cha Verona nchini Italia.
Utafiti unasema kuwa madini ya kemikali Phenolic ambayo yaliyoko kwenye tufaha, yanahusishwa na kupunguza hatari ya kupata maradhi ya moyo, saratani, pumu, kisukari na kudhibiti unene kupita kiasi.
Watafiti wanashauri ulaji wa tufaha kila mara, kutokana na upatikanaji wake katika maeneo mengi.
Mwaka wa 2015, watafiti walifanya uchunguzi kwa zaidi ya watu elfu tisa, ambapo watu hao ambao walisema walikuwa wanakula angalau tufaha moja kila siku.
Watafiti waligundua kuwa waliokuwa wanakula tufaha, hawakuwa wanamtembelea daktari ikilinganishwa na wale ambao hawakuwa wanakula tufaha. Utafiti wao pia uligundua kuwa waliokuwa wanakula tufaha wengi wao ni wasomi na hawakuwa wavutaji sigara.
“Kikubwa kilichogunduliwa, hakuna uhusiano kati ya watu wanaokula tufaha kila siku na uwezekano wa kumtembelea daktari' anasema mtafiti mkuu Mathew Davis katika chuo kikuu cha udaktari cha Geisel School, jimbo la Hampshire nchini Marekani.
Kulingana na Davis, ni bora kusema kuwa tufaha inazuia mtu kutotembelea duka la kuuza dawa, ila akasisitiza kuwa wale wanaokula tufaha huwa na afya njema kwa ujumla na hawatumii dawa za kununua dukani mara kwa mara.
Tufaha huchangia kupunguza unene
Utafiti mwingine wa tufaha ulionyesha kwamba kula matunda hayo matatu kwa siku kunasaidia kupunguza unene wa mwili.
Katika utafiti uliochapishwa mwaka wa 2020, watafiti waliwashirikisha watu arubaini ambao walikuwa na kiwango cha juu cha mafuta mwilini na kuwaweka katika vikundi viwili. Kundi moja lilikuwa linakula tufaha mbili kwa siku, ila wengine walikuwa wanakunywa sharubati ya tufaha. Jaribio hilo lilidumu kwa wiki nane, huku watu walioshirikishwa wakiendelea kula vyakula vyao vya kawaida.
Watafiti waligundua kuwa, wale waliokuwa wanakula tufaha, kiwango chao cha mafuta mwilini kilipungua. Changamoto ya utafiti huu ni kiwango kidogo cha watu walioshiriki na haiwezi thibitisha kwa uhakika iwapo matokeo yatakuwa sawia kwa kundi la watu wengi.
utafiti mwingine unaashiria kuwa kula tufaha tatu kila siku husaidia kupunguza unene na kuimarisha viwango vya sukari mwilini.
Guzzo anashauri kuwa, njia bora ya kula tufaha ni usitoe maganda yake kwanza kabla ya kula.
Ikija katika rangi ya tufaha, Guzzo anasema haina utofauti mkubwa. Madini ya polyphenols, yanapatikana katika tufaha zenye maganda ya rangi nyekundu na ya kijani.
Hatimaye kula tufaha kila siku haimaanishi kuwa hutamtembelea daktari, ila itaimarisha afya yako, na kupunguza kutegemea dawa mara kwa mara.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula