Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , UN: Kufichwa kwa ripoti ya ghasia Tanzania kunawanyima waathiriwa haki

UN imetaka Tanzania kuchapisha ripoti ya uchunguzi wa ghasia za Oktoba 29 na kufanya uchunguzi huru ili waathiriwa wapate ukweli, haki na fidia.

Moja kwa moja

Na MariamMjahid

  1. Mwili wa mwanamke waopolewa kwenye vifusi vya jengo Eastleigh

    Waokoaji wamefanikiwa kuutoa mwili wa mwanamke mmoja kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka eneo la Eastleigh, jijini Nairobi, huku msako wa kuwatafuta watu wanaohofiwa kunasa chini ya vifusi ukiingia siku ya nane.

    Mwili huo umepatikana huku operesheni ya uokoaji ikiendelea tangu Ijumaa, Oktoba 23, jengo hilo la ghorofa 16 lilipoporomoka katika Barabara ya 9.

    Juhudi za uokoaji zimekabiliwa na changamoto kadhaa, huku timu za dharura zikiendelea kuondoa vifusi na kujaribu kufikia sehemu za chini za jengo hilo, ambako watu wengine wanahofiwa kuwa bado wamenasa.

    Hatua hiyo mpya inajiri baada ya timu za uokoaji kuripoti kuwa zimeondoa takribani asilimia 80 ya vifusi, huku juhudi za sasa zikielekezwa katika kufikia sehemu ya chini ya jengo, ikiwemo eneo la chini ya ardhi.

    Siku ya Alhamisi, mamlaka zilisema watu 16 walikuwa bado hawajulikani walipo baada ya zoezi la kuhakiki taarifa lililofanywa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI).

    Kamishna wa Kaunti ya Nairobi Kaskazini, Simon Osumba, alisema taarifa za simu za mkononi zilionyesha kuwa watu tisa kati ya waliotajwa kutoweka walikuwa katika eneo la jengo hilo muda mfupi kabla halijaporomoka. Aliongeza kuwa mamlaka zilikuwa bado zikifuatilia taarifa kuhusu watu wengine wanne, huku familia tatu zikiwa hazijawasilisha nambari za simu zinazohitajika kusaidia katika ufuatiliaji.

    Awali, matumaini ya kuwapata manusura zaidi yaliongezeka baada ya vifaa maalumu vilivyoletwa kusaidia operesheni hiyo kubaini ishara zinazoweza kuashiria kuwepo kwa watu hai chini ya vifusi.

  2. UN yaonya kufichwa kwa ripoti ya uchunguzi wa ghasia Tanzania kunanyima waathiriwa haki

    Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu wameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kucheleweshwa kuchapishwa kwa matokeo ya Tume ya Uchunguzi kuhusu ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 2025.

    Aidha, wameeleza kuwa mwaka mmoja baada ya ghasia hizo, waathiriwa na familia zao bado hawajapata haki wala uwajibikaji kwa watu waliotekeleza uhalifu unaodaiwa, ikiwemo utekaji na upotezaji wa watu kwa lazima, mauaji ya kiholela, kukamatwa bila kufuata sheria.

    “Bado hakuna haki wala uwajibikaji kwa mamia ya waathiriwa wa utekaji na upotezaji wa watu kwa lazima, mauaji ya kiholela, kukamatwa kiholela na wale walioteswa au kufanyiwa vitendo vingine vya kikatili, visivyo vya kibinadamu na kudhalilisha utu. Majibu wanayoyatafuta bado yamefichwa katika ripoti ambazo hazijawekwa wazi,” walisema wataalamu hao.

    Ghasia zilizofuatia uchaguzi wa Oktoba 2025 ziliripotiwa kuhusisha matumizi ya nguvu kupita kiasi na nguvu za kuua na vyombo vya usalama, kukatika kwa huduma za intaneti pamoja na vitisho na unyanyasaji dhidi ya waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu nchini Tanzania.

    Hata hivyo, wataalamu hao wanasema hakuna kiongozi yeyote wa serikali aliyefunguliwa mashtaka kuhusiana na ghasia hizo katika kipindi cha mwaka mmoja.

    Umoja wa Mataifa pia umesisitiza umuhimu wa uchunguzi huru, wa haraka, wa kina na usioegemea upande wowote ili kuhakikisha waathiriwa wanapata haki ya kujua ukweli, kupata haki na kufidiwa kwa madhara waliyopata.

    Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa na Ofisi ya Rais mwezi Novemba 2025 iliwasilisha ripoti yake ya mwisho mwezi Aprili 2026. Hata hivyo, wataalamu hao wanasema muhtasari wa matokeo ya tume hiyo haujabainisha waliohusika na ukiukaji huo, haujapendekeza watu wafunguliwe mashtaka wala kuweka mapendekezo kuhusu uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja.

    Vile vile wametoa wito kwa serikali ya Tanzania kuchapisha ripoti hiyo yote bila kuchelewa zaidi, wakisema kuificha kunakiuka haki ya waathiriwa kupata ukweli na haki.

    Mwezi Agosti 2026, tume ya pili ya uchunguzi ilianzishwa na bado inaendelea na kazi yake. Hata hivyo, wataalamu hao wanasema hakuna maelezo ya kina kuhusu mamlaka na wigo wa kazi ya tume hiyo, huku ushirikishwaji wa waathiriwa ukiripotiwa kuwa mdogo.

    Vile vile, UN imependekeza serikali ya Tanzania iweke wazi malengo na majukumu ya tume ya uchunguzi wa matukio ya ghasia, na kuhakikisha matokeo yanachapishwa baada ya kukamilika.

    Wataalamu hao pia wameibua wasiwasi kuhusu madai ya kuendelea kushikiliwa kiholela kwa mamia ya watu ambao wamekaa gerezani kwa muda mrefu wakisubiri kesi zao kusikilizwa, huku wakikabiliwa na mashtaka ya uhaini na makosa yanayohusiana na ugaidi.

    Aidha, wamesema wamepokea taarifa kuhusu madai ya kuwepo kwa makaburi ya halaiki, kuendelea kwa visa vya watu kkupotezwa kwa lazima, miili kuondolewa katika vyumba vya kuhifadhia maiti na polisi kutumia video za maandamano kuwatambua waandamanaji.

    “Waathiriwa wanaendelea kukabiliwa na hali mbaya na inayozidi kuzorota ya haki za binadamu, huku nafasi ya wananchi kushiriki katika shughuli za kiraia ikiendelea kubanwa. Familia za waathiriwa, mashirika ya kiraia, waandishi wa habari na watetezi wa haki za binadamu wanaripotiwa kukabiliwa na vitisho, vitisho vya kutishwa na ufuatiliaji,” walisema.

    Wataalam hao pia wameongeza kuwa ukandamizaji dhidi ya wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari na wafuasi wa vyama vya upinzani unawafanya wengi kuogopa kujieleza na kushiriki katika shughuli za kiraia. Wamesema hata baadhi ya waliokimbilia nchi jirani wanaendelea kukabiliwa na vitendo vya ukandamizaji vinavyovuka mipaka ya nchi.

    Wataalamu hao wamesema wamewasilisha rasmi wasiwasi wao kwa serikali ya Tanzania.

    Soma pia:

  3. Mahakama ya Kenya yaamuru usajili wa wakimbizi urejeshwe

    Mahakama ya Juu nchini Kenya imeiamuru serikali kurejesha mara moja mchakato wa kuwasajili raia wa Eritrea na Ethiopia wanaotafuta hifadhi nchini humo. Mahakama hiyo imeamua kuwa kucheleweshwa kwa usajili huo kwa kipindi cha mwaka mmoja ni kinyume cha sheria, ni ubaguzi na kunakiuka wajibu wa Kenya wa kuwalinda wakimbizi.

    Katika uamuzi unaotajwa kuwa hatua muhimu katika kulinda haki za wakimbizi katika eneo la Pembe ya Afrika, mahakama imebatilisha agizo la serikali lililowazuia raia wa Eritrea na Ethiopia kujisajili katika mfumo wa hifadhi ya wakimbizi nchini Kenya tangu Julai mwaka jana.

    Uamuzi huo unafungua njia kwa maelfu ya watu wanaotafuta hifadhi kusikilizwa kwa maombi yao, baada ya miezi kadhaa ya mapambano ya kisheria.

    Katika hukumu iliyotolewa Oktoba 19, Jaji Gregory Mutai alisema kusitishwa kwa usajili huo hakukuwa halali, kulikuwa na ubaguzi na kulikiuka Katiba ya Kenya pamoja na wajibu wa nchi hiyo chini ya sheria za kimataifa kuhusu ulinzi wa wakimbizi.

    Kesi hiyo iliwasilishwa na muungano wa mashirika yanayotetea haki za wakimbizi na haki za binadamu, yakiwemo Refugee Legal Networks, Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini Kenya, Kenya Refugee Consortium, Kituo Cha Sheria na Sanctuary Foundation.

    Mashirika hayo yalipinga tangazo la Idara ya Huduma za Wakimbizi la Julai 31, 2025, lililositisha usajili wa raia wa Eritrea na Ethiopia wanaotafuta hifadhi nchini Kenya hadi itakapotangazwa vinginevyo.

    Serikali ilikuwa imetetea hatua hiyo, ikisema ililenga kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu, changamoto za uadilifu wa takwimu na vitisho kwa usalama wa taifa.

    Pia Unaweza Kusoma:

  4. AFCON kuandaliwa kila baada ya miaka miwili - CAF

    Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) litarejea kufanyika kila baada ya miaka miwili, baada ya Kamati Tendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kubatilisha kwa kauli moja uamuzi wake wa awali wa kuandaa mashindano hayo kila baada ya miaka minne.

    Rais wa CAF, Dkt Patrice Motsepe, alikuwa ametangaza wakati wa mkutano wa mkakati wa shirikisho hilo uliofanyika Cabo Verde kuanzia tarehe 7 hadi 9 Oktoba 2026, kuwa kamati hiyo itapitia upya uamuzi uliofikiwa mwaka jana.

    Motsepe amesema kurejea kwa mfumo wa miaka miwili ni kwa manufaa ya soka la Afrika, vyama 54 wanachama wa CAF pamoja na wachezaji wa Afrika wanaocheza katika klabu nje ya bara hilo.

    Ameeleza kuwa mpango wa kuanzisha Ligi ya Mataifa ya Afrika, ambayo ilipendekezwa kuchukua nafasi ya AFCON kama mashindano ya kila baada ya miaka miwili, ungehitaji miaka kadhaa kuzalisha mapato makubwa yanayohitajika kuendeleza soka la Afrika na kuongeza ushindani wake kimataifa.

    Toleo lijalo la AFCON litafanyika mwaka 2027, likiwa limeandaliwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania na Uganda.

    Mashindano yatakayofuata yamepangwa kufanyika mwaka 2028, 2031 na 2033, huku toleo la mwaka 2030 likiachwa ili kutoa nafasi kwa Kombe la Dunia la FIFA.

    Motsepe amesema AFCON si mashindano ya soka pekee, bali pia ni jukwaa muhimu la kuadhimisha utajiri wa tamaduni, mila na watu wa Afrika.

    Soma Pia:

  5. Kiongozi wa upinzani Venezuela ataka uchaguzi baada ya kurejea nchini

    Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela, María Corina Machado, ametaka uchaguzi mkuu ufanyike mwaka ujao, akisema juhudi za kurejesha demokrasia nchini humo haziwezi tena kusitishwa.

    Akizungumza na wanahabari mjini Caracas Alhamisi, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel alisema mchakato wa kuelekea demokrasia nchini humo ni “usioweza kutenguliwa”.

    Machado pia ameishukuru serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump kwa kile alichokiita kufungua “milango ya uhuru”, baada ya Marekani kumkamata mpinzani wake, aliyekuwa rais Nicolás Maduro.

    Siku hiyo hiyo, rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodríguez, alisema uchaguzi utafanyika na kwamba serikali yake inapaswa kusimamia mchakato huo wa mpito. Hata hivyo, hakutaja tarehe ya uchaguzi.

    Machado alipinga wazo la serikali ya Rodríguez kusimamia mchakato huo, akilitaja kuwa lisilo na mantiki. Alisema uchaguzi utafanyika mwaka 2027, lakini hakubainisha tarehe kamili.

    Alieleza kuwa mabadiliko ya kisiasa nchini Venezuela yatakuwa ya kudumu, yenye mpangilio na ya amani.

    Machado amerejea nchini humo baada ya juhudi kadhaa za awali za kuingia Venezuela kushindikana. Mwaka jana, aliondoka nchini humo kwa boti ya mwendo kasi usiku na kusafiri hadi Norway kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel. Muda mfupi baadaye, mwezi Januari, Marekani ilimkamata Maduro.

    Utawala wa Trump ulimuunga mkono Rodríguez, aliyekuwa makamu wa rais wa Maduro, kuwa kiongozi wa mpito. Baadaye aliapishwa rasmi na kutia saini mkataba wa mafuta ulioipa Marekani masharti yenye manufaa.

    Bado haijafahamika Machado anapanga kufanya nini baada ya kurejea. Hata hivyo, awali alisema angewania tena urais iwapo uchaguzi ungefanyika. Kurejea kwake nchini kulitegemea idhini ya serikali ya Trump.

    Akizungumzia kurejea kwake, Machado alisema ujumbe aliokuwa akiupokea kutoka kwa maelfu ya wafuasi waliokusanyika kando ya njia yake kuelekea mji mkuu ulikuwa mmoja: uhuru.

    “Nimekuja kutekeleza jukumu na kukamilisha dhamana niliyopewa,” alisema.

    Kiongozi huyo wa upinzani pia amesema hajapokea ujumbe wala mwaliko wa kukutana na Rodríguez. Ameongeza kuwa hatashiriki binafsi katika mazungumzo kuhusu uchaguzi kati ya wawakilishi wa upinzani na serikali.

    Soma Pia:

  6. Tetesi za soka Ijumaa: Chelsea yamuwinda Alexander-Arnold wa Madrid

    Chelsea huenda ikaingia kwenye kinyang’anyiro cha kumsajili beki wa kulia wa Real Madrid na timu ya taifa ya England, Trent Alexander-Arnold, mwenye umri wa miaka 28, iwapo atapatikana sokoni.(Football Insider)

    Manchester United inafikiria kumsajili mshambuliaji wa Leeds United, Dominic Calvert-Lewin, mwenye umri wa miaka 29, katika dirisha la usajili la Januari. (Athletic - subscription)

    Manchester City inaongoza katika mbio za kumsajili winga wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Marekani chini ya miaka 18, Mathis Albert, mwenye umri wa miaka 17. Chelsea pia inamuwania.(Teamtalk)

    Chelsea inakaribia kufikia makubaliano ya kumsajili kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, mwenye umri wa miaka 23, kwa ada inayokadiriwa kufikia pauni milioni 90 kabla ya dirisha la Januari. (Mail - subscription required), external

    Arsenal, Manchester United, Tottenham na Chelsea zinafuatilia kwa karibu maendeleo ya mshambuliaji wa Club Brugge, Nicolo Tresoldi, mwenye umri wa miaka 22. Hata hivyo, klabu hiyo ya Ubelgiji haina mpango wa kumuuza katika dirisha la Januari.(Football Insider)

    Chelsea inamfuatilia beki wa Como, Jacobo Ramon, mwenye umri wa miaka 21. Arsenal na Manchester United pia zimehusishwa na mchezaji huyo wa Hispania. (Mail - subscription required)

    Paris Saint-Germain na Barcelona zinaweza kuishinda Liverpool na Arsenal katika mbio za kumsajili kiungo wa Galatasaray kutoka Urusi, Aleksey Batrakov, mwenye umri wa miaka 21, ambaye yuko tayari kujiunga na klabu kubwa barani Ulaya.(Teamtalk)

    Tottenham haitapata malipo ya ziada kutokana na Harry Kane kushinda tuzo ya Ballon d’Or, kwa kuwa mkataba wa uhamisho wake kwenda Bayern Munich mwaka 2023 haukuwa na kipengele kinachohusiana na tuzo hiyo. (Goal)

    Rais wa Barcelona, Joan Laporta, anataka kumsajili beki wa pembeni wa Tottenham na timu ya taifa ya Hispania, Pedro Porro, mwenye umri wa miaka 27. (3Cat, in Catalan)

    Soma pia:

  7. Ndege za kijeshi za Marekani zatua Israel huku hofu ya mashambulizi dhidi ya Iran ikiongezeka

    Ndege kumi za kijeshi za Marekani zinazotumika kusafirisha vifaa na zana za kijeshi zimeripotiwa kutua katika kambi mbili za kijeshi nchini Israel, wakati vikosi vya usalama vya nchi hiyo vikijiandaa kwa uwezekano wa mashambulizi dhidi ya Iran.

    Shirika la utangazaji la Israel, KAN, limeripoti kuwa ndege hizo zilitua katika kambi za Ovda na Nevatim ndani ya saa 24 zilizopita.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ndege hizo zilitoka katika kambi ya kijeshi ya Fort Bliss, jimboni Texas, Marekani, ambayo huhifadhi akiba kubwa ya mifumo ya ulinzi wa anga ya jeshi la Marekani.

    KAN inasema huenda ndege hizo zilisafirisha makombora ya kuzuia mashambulizi ya angani, yakiwemo yanayotumika katika mifumo ya THAAD na Patriot, ili kuimarisha ulinzi wa Israel na mali za kijeshi za Marekani katika eneo hilo.

    Taarifa hiyo inajiri huku kukiwa na ripoti kwamba Marekani imeonya kuhusu uwezekano wa vita vifupi na vilivyolengwa dhidi ya Iran, iwapo Rais Donald Trump ataamua kuchukua hatua za kijeshi.

    Ndege nyingine zilizokuwa katika msafara huo ziliripotiwa kutua Jordan, Qatar na Saudi Arabia.

    Hata hivyo, taarifa ya KAN haikubainisha aina ya ndege zilizotua Israel. Hata hivyo, inaaminika kuwa huenda ni C-5M Super Galaxy au C-17 Globemaster III, ambazo zina uwezo wa kusafirisha mizigo mizito ya kijeshi.

    Marekani pia imeripotiwa kupeleka mfumo mwingine wa makombora ya Patriot katika eneo hilo, huku mvutano na Iran ukiendelea kuibua wasiwasi wa kuongezeka kwa mapigano.

    Hadi sasa, hakuna uthibitisho rasmi wa Marekani au Israel kuhusu aina ya vifaa vilivyosafirishwa na ndege hizo au kama hatua hiyo inahusishwa moja kwa moja na maandalizi ya mashambulizi dhidi ya Iran.

    Soma Pia:

  8. Wahouthi watangaza kushambulia viwanja vya ndege na viwanda vya mafuta Saudi Arabia

    Kundi la waasi wa Houthi, Ansar Allah, limetangaza Alhamisi kuwa limefanya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta na viwanja vya ndege nchini Saudi Arabia, ikiwemo viwanda vya kusafisha mafuta vya Ras Tanura na Rabigh, pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Khalid mjini Riyadh. Hata hivyo, mamlaka za Saudi Arabia hazikuwa zimethibitisha madai hayo mara moja.

    Wakati huo huo, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umetangaza kuzuia na kuangamiza makombora mawili ya balestiki yaliyokuwa yakielekezwa katika mji mkuu, Riyadh.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, kundi hilo lilidai pia kulenga kituo cha kampuni ya mafuta ya Aramco mjini Abqaiq na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Fahd, mjini Dammam, mashariki mwa Saudi Arabia.

    Shirika la habari la AFP limeripoti kusikia milipuko isiyopungua minane mjini Riyadh, wakati wakazi wakipokea tahadhari kwenye simu zao kuhusu tishio la mashambulizi ya angani.

    Mamlaka ya Ulinzi wa Raia ya Saudi Arabia ilitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa hatari katika maeneo ya Riyadh, Al-Kharj na Najran, kabla ya kuiondoa muda mfupi baadaye.

    Mapema Alhamisi, muungano huo ulitangaza pia kuzuia kombora jingine la balestiki lililorushwa na Wahouthi kuelekea eneo la mashariki mwa nchi hiyo. Msemaji wa muungano huo, Turki al-Maliki, alithibitisha tukio hilo.

    Maendeleo hayo yanajiri siku moja baada ya Wahouthi kutangaza kulenga Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia, kiwanda cha kusafisha mafuta cha Ras Tanura na Uwanja wa Ndege wa Abha, katika kile kinachoonekana kuwa ongezeko la mashambulizi na mvutano kati ya pande hizo mbili.

    Soma Pia:

  9. Natumai umzima na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 30/10/2026.