Laika: Mbwa wa mitaani aliyemtangulia binadamu kufika anga za juu

Chanzo cha picha, Alamy
Mwezi Novemba mwaka wa1957, wanasayansi wa Umoja wa Kisovieti walimtuma mbwa jike aliyeitwa Laika, katika safari ya anga yenye uwezekano wa kutorejea duniani, na kumfanya kuwa shujaa wa taifa aliyekumbukwa ila taarifa yake ilikuwa ya kusikitisha.
Takribani miaka 60 baadaye, mtoto wa mmoja wa wanasayansi hao aliiambia BBC kuhusu jinsi alivyokuwa akicheza na Laika alipokuwa mtoto.
Sehemu isiyofahamika sana ya mashindano ya anga za juu wakati wa Vita Baridi ilihusisha wanasayansi wa Kisovieti waliokuwa wakizunguka mitaa ya Moscow kutafuta mbwa waliokuwa wakizurura bila wenyewe.
Kabla ya safari za kwanza za binadamu kwenda angani, mbwa wa kike walifundishwa kukabiliana na safari hizo zilizokuwa na hatari kubwa.
Tarehe 3 Novemba 1957, mbwa mmoja aliyeitwa Laika alipelekwa angani kutoka kituo cha Baikonur Cosmodrome, na kuwa kiumbe hai wa kwanza kabisa kuzunguka sayari ya Dunia.
Hata hivyo, kwa bahati mbaya, Laika hakunusurika katika safari hiyo.
Sehemu ya kusikitisha zaidi ya simulizi yake ni kwamba wanasayansi wa Kisovieti walijua tangu mwanzo kuwa Laika hangeweza kurejea duniani akiwa hai.
"Wakati huo, wanasayansi hawakujua jinsi ya kuwarejesha viumbe hai kutoka kwenye mzunguko wa anga za juu hadi duniani," Profesa Viktor Yazdovsky aliiambia BBC katika kipindi cha Witness History mwaka 2017.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Kila mtu alikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu Laika. Walijua kwamba hangerejea baada ya safari hiyo."
Baba yake Yazdovsky, Vladimir, alikuwa akisimamia masuala ya kitabibu katika mpango wa Umoja wa Kisovieti wa safari za anga za juu. Viktor anakumbuka jinsi alivyokuwa akicheza na Laika akiwa na umri wa miaka tisa, muda mfupi kabla ya mbwa huyo kurushwa angani.
"Alikuwa mbwa mwenye subira sana na mwenye upendo. Ilikuwa rahisi kumfundisha. Alionekana kuwa mwerevu sana. Alikuwa na macho meusi yaliyokuwa yakionyesha hisia zake kwa uwazi."
"Baba yangu alimleta katika nyumba ya bibi yangu, iliyokuwa karibu na Moscow, na mimi pamoja na dada zangu tulicheza naye. Baba aliamini kwamba kabla ya safari yake ya anga, Laika alihitaji kupata uzoefu wa kuishi katika mazingira ya nyumbani."
Baada ya mafanikio ya kurushwa angani kwa Sputnik 1 tarehe 4 Oktoba 1957, iliyokuwa satelaiti ya kwanza kutengenezwa na binadamu kuzunguka Dunia, Waziri Mkuu wa Umoja wa Kisovieti, Nikita Khrushchev, aliamuru maandalizi ya safari nyingine mpya.
"Mara baada ya mafanikio hayo, alisema: 'Hatukuamini kwamba mngeweza kurusha satelaiti angani kabla ya Wamarekani, lakini mmefanikiwa,' alisema mhandisi Georgi Grechko, aliyeshiriki katika timu ya urushaji wa Sputnik 1 na Sputnik 2, katika mahojiano na BBC mwaka 2019.
'Katika kuadhimisha miaka ya mapinduzi ya tarehe 7 Novemba, nataka muwe mmefanikiwa kurusha kitu kingine kipya angani, 'alisema Khrushchev.
Katika kuadhimisha miaka 40 tangu Mapinduzi ya Urusi ya mwaka 1917, Khrushchev alikuwa amewapa wanasayansi wake, wakiongozwa na mbunifu mkuu Sergei Korolev, wiki chache tu kuandaa safari nyingine ya anga za juu baada ya mafanikio ya Sputnik 1.
Kwa bahati nzuri, jukumu hilo liliendana pia na malengo binafsi ya Korolev. Akifahamika kama mwanzilishi wa mpango wa Umoja wa Kisovieti wa safari za anga za juu, baada ya Vita vya Pili vya Dunia, alitumia teknolojia ya kubuniwa upya kutoka kwenye makombora ya V2 ya Wanazi, ili kutengeneza toleo la Kisovieti lililoweza kurusha mabomu yao ya nyuklia, ambayo yalikuwa na uzito mkubwa zaidi kuliko yale ya Marekani.
Roketi yake ya R7 Semyorka ilifanikiwa kurushwa angani mnamo Agosti 1957, na kuwa kombora la kwanza duniani la masafa marefu linaloweza kuvuka mabara (intercontinental ballistic missile).
Hata hivyo, Korolev alikuwa na ndoto za muda mrefu zilizozidi matumizi ya makombora hayo ya kijeshi.
Tangu alipoanza kutengeneza roketi katika miaka ya 1930, alikuwa akitamani kuzitumia katika safari za kwenda angani, kama binti yake alivyoieleza BBC mwaka 2019.
"Tangu utotoni, baba yangu alitamani kutawala anga. Aliota kuwa rubani. Alitengeneza vitelezaji vya angani au gliders na hata ndege. Baadaye alianza kubuni roketi," alisema Profesa Natalya Koroleva.
"Katika maisha yake yote, alikuwa na shauku kubwa ya kubuni roketi na kuzirusha angani. Aliwahi kuandika: 'Kuanzia sasa, lengo langu moja pekee maishani ni kufika kwenye nyota.'
Kwa nini mbwa huyo alichaguliwa?
Wakati roketi ya R7 iligunduliwa kuwa na uwezo wa kurusha silaha za nyuklia za Kisovieti kuelekea maeneo ya maadui wao, kwa Korolev roketi hiyo ilikuwa na matumizi mengine pia.
Kwa kurusha Sputnik 1 ,katika mzunguko wa anga kuizunguka Dunia, Korolev aliweza kuthibitisha kuwa safari za anga za juu zinawezekana.
Ndani ya mwezi mmoja, alitarajiwa kurusha satelaiti nyingine, ambayo ingebeba kiumbe hai.
"Hata leo, pamoja na maendeleo yote tuliyopiga na uwepo wa kompyuta kila mahali, sidhani kama kuna mtu angeweza kurusha satelaiti mpya ndani ya mwezi mmoja. Lakini chini ya uongozi wa Korolev, hilo ndilo tulilofanikiwa kufanya," alisema Grechko.
Kwa kuwachagua mbwa kwa ajili ya safari hizo za anga, Wasovieti walitofautiana na wanasayansi wa Marekani, ambao awali walikuwa wametuma nzi wa matunda na baadaye nyani angani.
"Ilionekana wazi kuwa kila nyani waliporushwa angani kwa kutumia roketi, mara nyingi majaribio hayo yalishindwa. Baadhi yao walipata mshtuko wa moyo. Ikiwa wangerushwa wakiwa wamepewa dawa za kuwafanya walale, taarifa zilizotumwa duniani zingekuwa pungufu na zisizo sahihi," alisema Yazdovsky.
"Na kama wangetuma wanyama wadogo zaidi, kama panya, ingewezekanaje kutumia matokeo ya majaribio hayo kuelewa athari kwa binadamu na maandalizi ya safari za baadaye za binadamu kwenda angani?"
Alikumbuka kuwa kulikuwa na sababu nyingine iliyowafanya Wasovieti kupendelea mbwa.
"Fiziolojia ya mbwa ilikuwa inafahamika vizuri sana na wanasayansi wa Kisovieti. Mwanasayansi mashuhuri wa Urusi, Pavlov, alifanya utafiti kuhusu mfumo wa mzunguko wa damu, mfumo wa usagaji chakula na shughuli za juu za mfumo wa neva kwa mbwa. Alitunukiwa Tuzo ya Nobel kwa utafiti huo," alisema.
Aidha, wanasayansi wa Kisovieti walichagua kwa makusudi mbwa waliokuwa wakizurura mitaani badala ya mbwa wa jamii maalumu.
"Waliamua kuwafundisha mbwa wa mitaani, badala ya mbwa wa jamii maalumu, kwa ajili ya mpango wa safari za anga. Mbwa hao hawakuwa na makazi.
Kwa nini walichaguliwa? Kwa sababu walikuwa na uwezo wa kustahimili hali ngumu na hawakuhitaji matunzo mengi. Maisha yao ya mitaani yalikuwa yamewafanya kuwa imara kwa njia ya asili," alisema.
Mbwa wa kike walichaguliwa kwa sababu walikuwa rahisi zaidi kufundishwa na kutii maelekezo. Pia, ili waweze kutoshea ndani ya chombo cha anga, uzito wao ulitakiwa usizidi kilo sita hadi saba.
Katika maandalizi ya safari hizo, mbwa hao waliwekwa kwa siku na hata wiki kadhaa ndani ya vyumba vidogo vilivyodhibitiwa shinikizo la hewa kabla ya kurushwa angani. Madaktari walifuatilia jinsi walivyoitikia sauti mbalimbali, mabadiliko ya shinikizo la hewa na hali ya kutokuwa na uzito.
Hasira na ukosoaji kutoka kimataifa
Baada ya mbwa mtulivu aliyeitwa Kudryavka Mwenye manyoya madogo yaliyopinda kutambulishwa kwa umma kupitia redio, alibweka na kuanza kujulikana kwa jina la Laika, ambalo kwa Kirusi linamaanisha "mbwa anayebweka".
"Kila mtu alimtazama kama shujaa," alisema Yazdovsky.
Hata hivyo, wanasayansi walikuwa katika harakati za kuharakisha maandalizi, wakifanya mabadiliko ya ghafla katika mipango ya Sputnik I ili kujumuisha sehemu maalumu yenye shinikizo la hewa kwa ajili ya mbwa huyo.
"Mfumo wa kudhibiti joto katika kifaa kilichombeba Laika haukuwa umeandaliwa ipasavyo," alikumbuka Yazdovsky. "Alifariki kutokana na joto kali sana ndani ya kifaa hicho."

Chanzo cha picha, Getty Images
Taarifa kuhusu hatima ya Laika zilitofautiana wakati huo. Kwa mfano, taarifa moja ya BBC ilidai, "Inaaminika kuwa Warusi wanapanga kumrejesha mbwa huyo duniani kwa kutumia kifaa maalumu cha kumrusha, ingawa hakuna tangazo rasmi lililothibitisha mpango huo."
Kwa miaka mingi, Warusi walidai kuwa Laika aliendelea kuishi angani kwa siku kadhaa. Hata hivyo, mwaka 2002, walikiri kuwa mifumo ya kudhibiti hali ya hewa ndani ya chombo hicho ilifeli, na Laika alifariki kutokana na joto kali na msongo wa mawazo kati ya saa tano na saba tu baada ya safari kuanza.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za vipimo vya mwili wa Laika wakati wa safari hiyo, ambazo ziliondolewa kwenye siri na kuhifadhiwa katika Makumbusho ya Kitaifa ya Anga na Anga za Juu ya Marekani (National Air and Space Museum), Laika alifanikiwa kufika katika mzunguko wa Dunia akiwa hai. Alikuwa akiizunguka Dunia, huku kila mzunguko ukichukua takribani dakika 103.
Uamuzi wa kumtuma Laika katika safari ambayo abgefariki, ulizua hasira na ukosoaji mkubwa kimataifa wakati huo.
Mashirika ya kutetea haki za wanyama nchini Uingereza yaliandamana nje ya ubalozi wa Sovieti, yakitoa wito kwa wamiliki wa mbwa kote nchini kuadhimisha dakika moja ya ukimya kwa heshima yake.
Nchini Marekani, wapenzi wa mbwa waliandamana wakiwa na wanyama wao nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. Aidha, Shirika la Marekani la Kuzuia Ukatili dhidi ya Wanyama (ASPCA) lilituma barua ya kupinga hatua hiyo kwa serikali ya Sovieti kupitia Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani.
Mwitikio huo mkali ulichangia kubadili namna programu za safari za anga zilivyowashughulikia wanyama. Safari zilizofuata zilibuniwa kwa kutumia mifumo ya kuwawezesha wanyama kurejeshwa duniani salama.
Takribani miaka mitatu baada ya safari ya Laika iliyosababisha kifo chake, Wasovieti walituma mbwa wengine wawili angani, nao walinusurika. Tarehe 19 Agosti 1960, Belka na Strelka walikamilisha mizunguko 17 kuizunguka Dunia kabla ya kutua salama siku iliyofuata.
Hata hivyo, akiwa mbwa wa kwanza kuzunguka Dunia, Laika alikuja kuwa alama muhimu ya mwanzo wa uchunguzi wa anga za juu wa Kisovieti. Stempu na bahasha za kumbukumbu zilitengenezwa zikiwa na picha yake. Pia, kulikuwa na sigara na viberiti vilivyopewa jina la Laika nchini Sovieti.
Mnara wa ukumbusho wenye urefu wa mita mbili, uliozinduliwa mjini Moscow mwaka 2008, unaonyesha roketi inayogeuka na kuwa mkono, huku mbwa akiwa amesimama kwenye kiganja chake.
Kama alivyosema Yazdovsky, kujitolea kwa Laika kulitangaza mwanzo wa enzi mpya.
"Safari ya Laika ilionyesha kuwa kiumbe hai kinaweza kuendelea kuishi katika mazingira ya kutokuwa na uzito. Hilo lilifungua njia kwa binadamu kusafiri kwenda angani."
Hata hivyo, si kila mtu aliyekubaliana na mtazamo huo. Mwaka 1998, Oleg Gazenko, aliyeongoza mpango wa Sovieti wa kuwafundisha mbwa kwa ajili ya safari za anga na ndiye aliyemchagua na kumfundisha Laika, alisema katika mkutano na wanahabari:
"Kufanya majaribio kwa kutumia wanyama ni jambo linalotusababishia sote maumivu. Kadiri muda unavyopita, ndivyo ninavyozidi kujutia… Hatukujifunza vya kutosha kutokana na safari hii kiasi cha kuhalalisha kifo cha mbwa huyo."



































