Moja kwa moja , Marekani yapiga kura leo kuamua udhibiti wa bunge la Congress

Matokeo ya uchaguzi huo yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa Rais Trump kutekeleza ajenda yake ya kisiasa katika miaka miwili iliyosalia ya muhula wake wa urais.

Muhtasari

Marekani yapiga kura leo kuamua udhibiti wa bunge la Congress

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Wang Yi: China yaunga mkono juhudi za Iran kulinda mamlaka na usalama wake

    M

    Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, amesema nchi yake inaiunga mkono Iran katika juhudi za kulinda mamlaka yake ya kujitawala na usalama wake.

    Akizungumza katika mkutano na Ali Bagherikani, Naibu Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Wang amesema China inazitaka pande zote zinazohusika katika mzozo wa Mashariki ya Kati kuelekeza nguvu zao katika kutafuta suluhisho la kisiasa.

    Rais wa China, Xi Jinping, pia alisema Jumatatu alipokutana na Sultan wa Oman, Haitham bin Tariq Al Said, kuwa Mashariki ya Kati na eneo la Ghuba havipaswi kuwa uwanja wa mashindano ya mataifa yenye nguvu duniani.

    Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa baada ya mkutano huo, Oman iliunga mkono mapendekezo ya China kuhusu amani Mashariki ya Kati, huku ikieleza matumaini kuwa Beijing itachukua nafasi kubwa zaidi na inayoonekana katika juhudi za kuhakikisha utulivu wa kudumu katika eneo hilo.

    China ndiyo mnunuzi mkubwa zaidi wa mafuta kutoka Iran na ni miongoni mwa washirika wake muhimu wa kiuchumi.

    Beijing imelaani mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, pamoja na vikwazo ilivyowekewa na Washington. Pia imekuwa ikitoa wito wa kusitishwa kwa vita, ikisisitiza umuhimu wa kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kupitia diplomasia.

    Soma pia:

  2. Trump kuiondoa Rwanda na Afrika Kusini katika mpango wa biashara wa Marekani

    x

    Rais wa Marekani, Donald Trump, ameiarifu Bunge la nchi hiyo kuhusu mpango wake wa kuiondoa Rwanda na Afrika Kusini katika mpango wa upendeleo wa kibiashara, kuanzia Januari Mosi mwaka 2027.

    Mpango wa Sheria ya Ukuaji na Fursa za Afrika (AGOA) unaziwezesha nchi za Afrika zinazokidhi vigezo kuuza maelfu ya bidhaa nchini Marekani bila kutozwa ushuru wa forodha.

    Katika taarifa yake, Mwakilishi wa Biashara wa Marekani, Jamieson Greer, amesema tathmini ya kila mwaka imebaini kuwa nchi hizo mbili zinajihusisha na vitendo vinavyokwenda kinyume na masharti ya mpango huo.

    Ameongeza kuwa utawala wa Trump tayari umeziarifu Rwanda na Afrika Kusini kuhusu uamuzi huo.

    Utawala wa Marekani umetaja vikwazo katika biashara na uwekezaji wa Marekani, pamoja na wasiwasi kuhusu masuala ya usalama wa taifa na maslahi ya sera za kigeni katika eneo hilo.

    Kwa upande wa Rwanda, Washington pia imeibua wasiwasi kuhusu hali ya haki za binadamu, uwepo wa vyama na mitazamo mbalimbali ya kisiasa, utawala wa sheria na haki za wafanyakazi.

    Hatua hiyo inakuja takribani wiki moja baada ya Wizara ya Ulinzi ya Rwanda kuwekewa vikwazo na Wizara ya Fedha ya Marekani kutokana na madai ya kuhusika kwake katika uasi wa makundi yenye silaha mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

    Wizara ya Fedha ya Marekani ilisema Wizara ya Ulinzi ya Rwanda ilielekeza maelfu ya wanajeshi kushirikiana na waasi wa M23 katika mapigano mashariki mwa DRC, huku ikiwapatia silaha, vifaa, msaada wa usafirishaji na mahitaji ya kijeshi pamoja na mafunzo.

    Soma Pia:

  3. Tetesi za soka Jumanne: Arsenal wamnyatia Kroupi katika dirisha la usajili la Januari

    n

    Mabingwa wa Ligi Kuu ya England, Arsenal, wanataka kuimarisha safu yao ya ushambuliaji kwa kumsajili mshambuliaji wa Bournemouth, Eli Junior Kroupi katika dirisha la usajili la Januari.

    Hata hivyio, wanakabiliwa na ushindani kutoka kwa Bayern Munich na Paris Saint-Germain katika kinyang'anyiro cha kumwania mshambuliaji huyo Mfaransa mwenye umri wa miaka 20. (Mirror)

    Kiungo mshambuliaji wa Juventus, Kenan Yildiz, mwenye umri wa miaka 21, pia anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaovutia Arsenal. Hata hivyo, kocha Mikel Arteta kwa sasa ameweka mkazo katika kuimarisha safu ya ushambuliaji. (Mirror)

    Manchester United imekuwa ikifuatilia kwa karibu wachezaji wanne wa Borussia Dortmund. Wachezaji hao ni mshambuliaji wa Guinea Serhou Guirassy, mwenye umri wa miaka 30, kiungo Mwingereza Jobe Bellingham, 21, kiungo Mjerumani Felix Nmecha, 26, na beki wa Sweden Daniel Svensson, 24. (Teamtalk)

    Kipa wa Brighton na timu ya taifa ya Uholanzi, Bart Verbruggen, mwenye umri wa miaka 24, yuko tayari kujiunga na Real Madrid endapo klabu hiyo itatoa nafasi ya kumsajili. (Football Insider)

    Brighton pia inamfuatilia beki chipukizi wa Estoril, Jordan Arnolin, mwenye umri wa miaka 18. Hata hivyo, klabu hiyo ya England inakabiliwa na ushindani kutoka Barcelona, ambayo pia inavutiwa na huduma ya beki huyo Mreno. (Record kupitia Sport Witness)

    Sunderland inatarajiwa kumpa kocha Regis Le Bris fedha za kufanya usajili katika dirisha la Januari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha matokeo ya klabu hiyo. (The i)

    Kocha wa Nottingham Forest, Oliver Glasner, ambaye amekuwa akikabiliwa na presha kutokana na matokeo ya timu hiyo, amepata uungwaji mkono kutoka kwa wachezaji wake baada ya kufanya nao kikao katika uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo. (Telegraph)

    Klabu kadhaa za Ligi Kuu ya England zinafuatilia maendeleo ya beki wa Celta Vigo, Javi Rodriguez, mwenye umri wa miaka 23. (Teamtalk)

    Atletico Madrid nayo inataka kumsajili kiungo chipukizi wa Almeria, Stefan Dzodic, mwenye umri wa miaka 21, raia wa Serbia, ili kuimarisha kikosi chake kwa msimu ujao. (Marca)

    Soma pia:

  4. Watu 26 wauawa katika shambulio la Urusi nchini Ukraine

    d

    Takribani watu 26 wameuawa baada ya mabomu ya Urusi kulenga kituo cha usambazaji wa misaada ya kibinadamu nchini Ukraine, katika shambulizi ambalo Rais Volodymyr Zelensky amelielezea kuwa la kutisha mno.

    Watu wengine watano wamejeruhiwa, huku 27 wakiripotiwa kutoweka awali baada ya angalau mabomu tisa ya angani, kila moja likiwa na uzito wa tani tatu, kuliporomoka katika kijiji cha Komyshuvakha, katika eneo la Zaporizhzhia kusini mwa Ukraine.

    Mkuu wa eneo hilo, Mykhailo Semikin, amesema mashambulizi hayo yalitokea Jumatatu.

    Rais Zelensky amesema shambulizi la kwanza lililenga shule ya eneo hilo iliyokuwa ikitumika kwa shughuli za kibinadamu. Ameongeza kuwa shambulizi la pili lilifuata, likilenga eneo ambalo watu walikuwa wamejisitiri.

    Katika video aliyochapisha, Zelensky alionyesha shimo kubwa lililoachwa na mlipuko huo pamoja na waokoaji wakifanya shughuli za kutafuta manusura na miili ya watu kwenye vifusi.

    Jeshi la Urusi halijatoa tamko lolote hadharani kuhusu shambulizi hilo.

    Soma pia:

  5. Marekani yapiga kura leo kuamua udhibiti wa bunge la Congress

    d

    Wagombea wa vyama vya Republican na Democratic nchini Marekani wamehitimisha kampeni zao za mwisho kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula, huku udhibiti wa Bunge la Congress ukiwa hatarini kwa chama cha Rais Donald Trump.

    Wamarekani wanatarajiwa kupiga kura leo Jumanne, Novemba 3, katika uchaguzi utakaohusisha viti vyote 435 vya Baraza la Wawakilishi na viti 35 kati ya 100 vya Seneti.

    Chama cha Democratic kinaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kurejesha udhibiti wa Baraza la Wawakilishi, lakini kinakabiliwa na ushindani mkali zaidi katika kinyang’anyiro cha Seneti.

    Matokeo ya uchaguzi huo yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa Rais Trump kutekeleza ajenda yake ya kisiasa katika miaka miwili iliyosalia ya muhula wake wa urais.

    Iwapo chama cha Republican kitapoteza udhibiti wa chumba chochote cha bunge la Marekani yaani Congress, uwezo wa Trump kupitisha sheria unaweza kudhoofika, huku Democrats wakipata nafasi ya kuchunguza utendaji wa utawala wake.

    Kudhibiti Seneti pia kungewawezesha Democrats kuzuia au kuchelewesha uteuzi wa Trump wa majaji katika mahakama za shirikisho, wakiwemo majaji wa Mahakama ya Juu.

    Mvutano umeonekana pia katika jimbo la Michigan, ambako mgombea Abdul El-Sayed anawania kuwa Mwislamu wa kwanza kuchaguliwa katika Seneti ya Marekani.

    Wakati huohuo, huko California, Mahakama ya Juu imekataa ombi la Wizara ya Sheria ya Marekani la kuingilia mchakato unaohusiana na uchaguzi huo.

    Katika siku yake ya mwisho ya kampeni, Trump alitumia hotuba yake kuu kuzungumzia ukarabati wa bwawa la maji katika eneo la Lincoln Memorial Reflecting Pool mjini Washington, mojawapo ya miradi ya miundombinu ambayo ameipa kipaumbele tangu kurejea kwake Ikulu ya White House.

    Uchunguzi wa maoni uliofanywa na Reuters kwa ushirikiano na Ipsos unaonyesha kuwa wagombea wa Democratic wanaongoza kwa tofauti ya asilimia nane dhidi ya Republican, ishara ya changamoto inayokikabili chama cha Trump katika uchaguzi huo.

  6. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 03/11/2026.