Maafisa wa Iran watoa majibu yanayofanana kwa Trump

Muda wa kusoma: Dakika 3

Saa moja tu baada ya Donald Trump kudhihaki hali ya uongozi wa kisiasa nchini Iran kuwa ya kuchanganya, na kusema haijulikani kiongozi wa taifa hilo ni nani, na kwamba kuna mvutano kati ya watu wenye misimamo mikali, wale wenye misimamo ya kadri pamoja na viongozi wa idara tofauti nchini Iran, sasa amejibiwa.

Viongozi wa matawi matatu ya uongozi wa Iran walitoa taarifa na kusema "hakuna watu wenye misimamo mikali au ya kadri, wote ni raia wa Iran, na wote wako chini ya jeshi na kiongozi wa Iran"

Kamanda wa jeshi la IRGC na Quds amesisitiza uwepo wa mshikamano katika idara za serikali ya Iran.

Madai ya Trump kwamba kumekuwa na mvutano miongoni mwa viongozi wa Iran baada ya kufanya mazungumzo nao inaonekana kuambulia patupu, baada ya idadi kubwa ya ujumbe wa Iran kushiriki katika mazungumzo hayo.

Watu wenye msimamo mkali nchini Iran, wameilaumu timu ya wapatanishi "kwa kutoheshimu" damu ya Wairan.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, Mohammad Bagher Ghalibaf, na Gholamhossein Mohseni Ejei viongozi wa matawi matatu ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamepinga semi za mgawanyiko ndani ya serikali ya Iran.

Kulingana na tovuti ya habari ya serikali ya Iran, viongozi hao watatu walisisitiza katika ujumbe wa pamoja kwamba,

"Nchini Iran hakuna mtu aliye na misimamo mikali au ya wastan"

Trump: Hakuna mtu nchini Iran anayejua nani ndiye kiongozi

Tarehe 23 mwezi Aprili, Trump kwa mara ya kwanza alichapisha ujumbe kwenye mtandao wake wa Truth Social, akirejelea mgawanyiko katika serikali ya Iran, na kudai kuwa hakuna anayejua kiongozi wa Iran kwa sasa.

"Iran inapitia wakati mgumu sana kujaribu kubaini kiongozi wake ni nani! Hawajui kabisa."aliandika Trump.

Trump, ambaye amekuwa akizungumzia mara kwa mara suala la mabadiliko ya utawala nchini Iran, aliandika kuwa "kuna mgogoro wa ndani kwa ndani kati ya wale walio na misimamo mikali ambao wameshindwa katika vita hivi na watu wenye msimamo wa wastani ambao si wa wastani kabisa lakini wanapata kukubalika, ni hali yenye vurugu sana."

Saa chache baada ya ujumbe huo kuchapishwa, akijibu swali la mwandishi wa habari kuhusu muda ambao atasubiri majibu kutoka kwa maafisa wa Iran, alirejelea vita vya zamani vya Marekani na kusema: "Msiharakishe, nimekuwa nikifanya haya kwa wiki sita tu."

Aliendelea kusema kuwa "tumefanya kazi nzuri sana. Lakini uongozi wao uko katika matatizo. Siwezi kujibu swali lako kwa uhakika. Wana uongozi mpya kabisa na wanagombana. Haijulikani ni nani atachukua mamlaka, kwa sababu tumewaingiza katika fujo kubwa, na wao pia wameleta fujo ulimwenguni katika miaka 47 iliyopita."

Makamanda wa IRGC: Mikono iko kwenye "kitufe"

Uongozi wa Kikosi cha Anga na Jeshi la Wanamaji la IRGC pia ulichapisha tena kile kilichoitwa "ujumbe wa umoja" na kuandika,"Kwa malengo maalum, mikono ikiwa kwenye "kitufe" msaada wetu ni kudumisha umoja mitaani na mshikamano wa wanaohusika."

Ali Akbar Ahmadian, mwakilishi wa Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu katika Baraza la Ulinzi, pia aliandika katika ujumbe wa pamoja "ulinzi wa nchi yetu hii leo ni umoja na mamlaka ya wananchi"