Kujifunza kuendesha baiskeli kulivyowasaidia wanawake kujifunza kusoma na kuandika

Muda wa kusoma: Dakika 4

"India ilijipatia uhuru wake mwaka wa 1947, lakini mimi nilipata uhuru wangu mwaka wa 1992" alisema Jayachithra mwenye umri wa miaka 55, ambaye sasa ni mwalimu mkuu katika shule moja ya umma kusini mwa India.

Maisha yake yalibadilika miaka 33 iliyopita baada ya viongozi wa wilaya yake kusisitiza wanawake wajifunze kuendesha baiskeli.

Jayachithra, ni miongoni mwa wanawake laki moja kutoka maeneo ya mashinani, ambao walikuwa hawajahi kutoka nyumbani kwao, walijipatia uhuru wa kusafiri kupitia baiskeli.

Baadhi ya wanawake ambao walijifunza kuendesha baiskeli miaka ya 1990, walipata nafasi nzuri za kazi, wakabadilisha maisha yao, pamoja na ya wanao, na wajukuu wao.

Waanzilishi

Mwaka wa 1988, mradi wa kitaifa wa Elimu ya Kusoma na Kuandika (National Literacy Mission) ulianzishwa nchini India ili kuboresha viwango vya masomo na kuongeza uelewa kuhusu haki za msingi.

Katika wilaya ya Pudukkottai iliyopo kusini mwa India, takriban kilomita 380 kusini mwa jiji la Chennai mradi huu ulipewa jina la "the awakening movement".

Kulingana na sensa ya mwaka wa 1990, chini ya nusu ya wanawake katika wilaya hiyo walikuwa wanaweza kusoma na kuandika. Takribani wanawake 270,000 walikuwa hawajui kusoma wala kuandika.

"Katika utafiti uliofanywa kuhusu uwezo wa kusoma na kuandika, ilibainika wazi kwamba wanawake wangenufaika na mradi huo," anasema Kannammal, mratibu wa mpango huo.

Kampeni ya elimu ya kusoma na kuandika ilikadiria kuwa watu 30,000 wangejitolea kuwafundisha wanawake hao kusoma na kuandika, ila kulikuwepo na changamoto ya usafiri, ndipo mradi wa baiskeli ukuaanzishwa.

Tatizo lilikuwa kwamba familia za wanawake hao wasiojua kusoma na kuandika zilitarajia mwalimu wao awe mwanamke, lakini ni wanawake wachache sana waliokuwa na mbinu za usafiri.

"Wakati huo, wanawake hawakuwa na baiskeli au pikipiki. Hawakuweza kusafiri peke yao. Niliona ni muhimu kuwapa fursa hiyo," alisema Sheela Rani Chunkath, ambaye wakati huo alikuwa afisa mwandamizi wa wilaya.

"Kuendesha baiskeli kumewafanya wanawake kujihisi huru na kujiamini," anaeleza Bi. Chunkath.

"Kulikuwa na baadhi ya maafisa waliokataa kuwaajiri wanawake waliojitolea kutoa mafunzo, wakidai kwamba wanawake hawawezi kwenda katika vijiji vya mbali, lakini mkuu wa wilaya Bi. Chunkath alikataa hoja zao," anasema Kannammal.

"Wanawake walipoanza kuendesha shughuli zao bila kusita, waligundua kwamba wanaweza kufanya chochote," anaongeza Kannammal. "Hii ilifungua njia kwao kuvunja vikwazo vingine vyote vilivyowekwa na wanaume."

Mafanikio

Mradi huu baadaye ulisaidia idadi kubwa ya wanawake kutoka tabaka mbalimbali za kijamii, iwe walikuwa walimu au wanafunzi.

"Wakati huo, niliishi kama mtumwa," anakumbuka Jayachithra, ambaye alikuwa amepata elimu nzuri .

"Baba yangu hakuruhusu hata nifungue madirisha ili nione nje."

Wakati huo, wanawake wasio na waume mara nyingi walikuwa wakifichwa wasionekane na wanaume.

"Baada ya kumaliza darasa la kumi, familia yangu iliniambia nijifunze kushona, taaluma hizi zilionekana kuwa salama na zinazowafaa wanawake."

Jayachithra alikuwa amepata asilimia 99 katika hesabu, na mapendekezo haya yakujifunza kushona yalimuumiza sana.

Kama sehemu ya kampeni ya elimu ya kusoma na kuandika, alichaguliwa kufundisha wanawake waislamu katika kijiji jirani.

Jayachithra aligundua kuwa hangeweza kufika huko kwa kutembea na alitumia fursa hiyo kujifunza kuendesha baiskeli.

"Nilivaa sketi ndefu.Wakati huo hakukuwa na baiskeli za wanawake, hivyo nilijifunza kwa kutumia baiskeli ya wanaume."

"Maisha yangu yalibadilika kabisa. Nilihisi kama kipepeo. Nilikuwa nikisubiri kwa hamu jioni ifike ili niendeshe baiskeli kwenda kwenye madarasa yangu kufunza."

"Mwanzoni baba yangu hakukubali, lakini baadaye alibadili nia na kuninunulia baiskeli." anasema Jayachithra.

Vasantha, ambaye sasa ana zaidi ya miaka 50, alikuwa hajui kusoma wala kuandika na alitoka katika familia maskini ya Dalit, tabaka ambalo limekumbwa na ubaguzi wa kijamii kwa karne nyingi. Aliolewa akiwa mdogo sana, na mume wake pia hakuwa na elimu.

Wawakilishi wa harakati hiyo walimfikia akiwa anafanya kazi kwenye machimbo ya mawe, ambako alikuwa akivunja mawe kwa kutumia zana za mikono.

Wakati huo, kuendesha baiskeli ilikuwa sehemu muhimu ya mradi huo wa kusoma na kuandika.

"Maafisa wa mpango wa elimu ya kusoma na kuandika walituambia tunaweza kupata baiskeli na kujifunza kuziendesha," Vasantha aliambia BBC.

Baada ya kujifunza kusoma, kuandika, na kufanya hesabu za msingi, alishirikiana na wanafunzi wengine watatu kama yeye, akakodi machimbo ya mawe na kuanzisha biashara yake mwenyewe.

Vasantha anasema mpango wa kuendesha baiskeli ulimfanya aweze kujiamini na kumpa uhuru pamoja na heshima. Sasa anamsaidia mjukuu wake, ambaye anatamani kuwa daktari.

Urithi wa kudumu

Leo hii wanawake kama Vasantha wanapatikana katika kijiji cha Pudukkottai. Baadhi yao wameanzisha biashara zao ndogo, na wengi wameachana na kazi za msimu na kupata kazi za ofisini.

Mradi wa kusoma na kuandika uliwasaidia wanawake hawa kutambua kwamba mara nyingi walikuwa wakipewa malipo madogo kupita kiasi, na wakadai nyongeza za mishahara.

Baiskeli iliwawezesha wanawake wasitegemee tena ndugu zao wa kiume kwa ajili ya kusafiri nje ya nyumba zao, wakati ambapo vijiji vingi havikuwa na barabara nzuri na usafiri wa umma ulikuwa bado haujaendelezwa vizuri.

Mwezi Agosti mwaka wa 1992, Pudukkottai ilitangazwa kuwa wilaya iliyojua kusoma na kuandika kwa 100%.

Hivi leo ni jambo la kawaida kuwaona wanawake wakiendesha baiskeli eneo la Pudukkottai, lakini Jayachithra si mmoja wao.

Sasa yeye anatumia skuta, na binti yake amenunua gari.