Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, dini zinasemaje kuhusu mwisho wa dunia?
Ikiwa unasoma makala haya, basi bado uko hai na dunia haijaisha.
Watu wengi wamekuwa na wasiwasi kuhusu tarehe 13 Novemba 2026, kufuatia utafiti uliodai kuwa dunia huenda ikafikia mwisho siku hiyo.
Dini kuu mbili duniani, Uislamu na Ukristo, zina mafundisho kuhusu ufufuo wa wafu na mwisho wa dunia. Hata hivyo, zina mitazamo tofauti kuhusu namna matukio hayo yatakavyotokea.
Madai kuhusu tarehe hiyo yanatokana na utafiti ulioandikwa na watafiti watatu na kuchapishwa katika jarida la kisayansi la Marekani la Science tarehe 4 Novemba 1960.
Utafiti huo ulipewa jina la Doomsday: Friday, November 13, yaani Siku ya Mwisho: Ijumaa, Novemba 13.
Watafiti hao walisema kuwa iwapo idadi ya watu duniani ingeendelea kuongezeka kwa kasi iliyojitokeza katika takwimu walizochambua kwa kipindi cha karibu miaka 2,000, basi kwa mujibu wa makadirio yao, kufikia Novemba 2026 idadi hiyo ingefikia kiwango ambacho kingefanya maisha duniani yasiwezekane.
Kwa upande mwingine, Waislamu wanaamini kuwa Siku ya Kiyama itakuwa siku ya Ijumaa, kwa mujibu wa baadhi ya hadithi. Hata hivyo, hakuna uhakika kwamba itakuwa Ijumaa tarehe 13 Novemba 2026.
Lakini dini hizi mbili zinafundisha nini kuhusu Siku ya Kiyama na ufufuo wa wafu?
Mtazamo wa Uislamu kuhusu Siku ya Kiyama
Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, hakuna anayejua wakati kamili wa kutokea kwa Siku ya Kiyama isipokuwa Mwenyezi Mungu.
Wanazuoni wa Kiislamu wanasema kuwa kuna ishara mbalimbali zitakazoonekana kabla ya Siku hiyo. Ingawa baadhi ya hadithi zinaeleza kuwa Kiyama kitatokea siku ya Ijumaa, hazibainishi tarehe wala mwaka.
Katika Suratul A'raf, aya ya 187, Mwenyezi Mungu anasema:
"Wanakuuliza kuhusu Saa hiyo, itatokea lini? Sema: Ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna awezaye kuifunua wakati wake isipokuwa Yeye."
Vilevile, katika Suratu Luqman, aya ya 34, Mwenyezi Mungu anabainisha kuwa ujuzi wa wakati wa Kiyama ni miongoni mwa mambo ambayo hakuna anayeyajua isipokuwa Yeye.
Hii ina maana kwamba hata Mtume Muhammad (SAW) hakujua wakati kamili ambao Siku ya Kiyama itatokea.
Ni ishara zipi zilizotajwa katika Uislamu?
Katika mafundisho ya Kiislamu, ishara za kukaribia kwa Siku ya Kiyama zimegawanywa katika makundi mawili: dalili ndogo na dalili kubwa.
Baadhi ya dalili hizo tayari zimeonekana, nyingine zinaendelea kujitokeza, huku nyingine zikiwa bado hazijatokea.
Miongoni mwa dalili zilizotajwa katika hadithi ni:
- Kuenea kwa ujinga na kupungua kwa elimu.
- Kuongezeka kwa machafuko na migogoro.
- Watu kushindana katika kujenga majengo marefu na makubwa.
- Baadhi ya ishara hizi zimetajwa katika hadithi zinazochukuliwa kuwa sahihi, zikiwemo zilizokusanywa katika vitabu vya Sahih al-Bukhari na Sahih Muslim.
Pia kuna ishara kubwa ambazo zinatarajiwa kutokea wakati Siku ya Kiyama itakapokuwa imekaribia sana.
Katika hadithi iliyopokelewa na Imam Muslim, Mtume Muhammad (SAW) alitaja ishara kumi kubwa za Kiyama. Miongoni mwazo ni:
- Kutokea kwa Dajjal.
- Kushuka kwa Nabii Isa mwana wa Maryam (AS).
- Kutokea kwa Ya'juj na Ma'juj.
- Kutokea kwa moshi.
- Kutokea kwa mnyama kutoka ardhini.
- Jua kuchomoza upande wa magharibi.
- Kutokea kwa maporomoko makubwa ya ardhi mashariki.
- Kutokea kwa maporomoko makubwa ya ardhi magharibi.
- Kutokea kwa maporomoko makubwa ya ardhi katika Rasi ya Uarabuni.
- Kutokea kwa moto kutoka Yemen utakaowasukuma watu kuelekea mahali pao pa kukusanyika.
Uislamu unaonya dhidi ya kujaribu kubashiri wakati kamili wa Siku ya Kiyama au kuhusisha moja kwa moja matukio fulani ya dunia na ishara za mwisho wa dunia.
Ingawa hadithi zinaeleza ishara zitakazotokea, wakati halisi wa Kiyama unajulikana na Mwenyezi Mungu pekee.
Mtazamo wa Ukristo kuhusu ufufuo wa wafu
Ukristo unaamini katika kurejea kwa Yesu Kristo na mwisho wa nyakati. Hata hivyo, Biblia haitaji tarehe maalumu ambayo matukio hayo yatatokea. Badala yake, inaeleza baadhi ya dalili zinazoweza kujitokeza katika kipindi hicho.
Mchungaji Ishaku Ashafa, kiongozi wa dini ya Kikristo katika jimbo la Kaduna, alisema kuwa kutakuwa na mabadiliko makubwa katika namna watu watakavyoishi wakati wa mwisho wa nyakati.
Alisema kuwa kitabu cha Danieli, sura ya 12, aya ya 4, kinaeleza kuwa ujuzi utaongezeka katika kipindi hicho. Pia alieleza kuwa Biblia inazungumzia wakati ambapo watu wataacha kujali na kuwapenda wenzao.
Katika kitabu cha Timotheo wa Pili, sura ya 3, aya ya 1 hadi 5, Biblia inaeleza baadhi ya tabia zitakazojitokeza katika siku za mwisho. Tabia hizo ni pamoja na ubinafsi, kupenda fedha, kutowatii wazazi na kukosa upendo.
Mchungaji Ashafa aliongeza kuwa Yesu Kristo atakaporejea, atawaokoa wale wanaomwamini na kuwapeleka mbinguni.
"Na wale ambao hawatamwamini wataachwa hapa duniani," alisema.
Hata hivyo, Biblia inaeleza kuwa hakuna anayejua siku wala saa ambayo tukio hilo litatokea.
Katika kitabu cha Mathayo, sura ya 24, aya ya 36, Yesu ananukuliwa akisema kuwa hakuna anayejua siku wala saa hiyo, hata malaika wa mbinguni, isipokuwa Mungu pekee.
Mchungaji Ashafa alisema kuwa hilo linaonyesha kuwa licha ya kuwepo kwa ishara mbalimbali, haiwezekani kwa binadamu kujua wakati kamili wa kutokea kwa mwisho wa dunia.
Utafiti huu ulianzia wapi?
Utafiti uliohusishwa na tarehe 13 Novemba 2026 ulianzishwa na mwanafizikia Heinz von Foerster, aliyezaliwa Austria na kuishi Marekani.
Alifanya utafiti huo pamoja na watafiti wengine wawili, Patricia Mora na Lawrence Amiot. Wote watatu walikuwa wanachama wa Idara ya Uhandisi wa Umeme katika Chuo Kikuu cha Illinois nchini Marekani.
Watafiti hao walitumia makadirio ya kihistoria kuhusu idadi ya watu duniani. Takwimu zao zilikuwa na makadirio 24 yaliyokusanywa kuanzia mwanzoni mwa zama za Kikristo hadi mwaka 1958.
Lengo lilikuwa kuchunguza namna idadi ya watu duniani ilivyoongezeka katika vipindi tofauti vya historia.
Watafiti hao hawakutegemea dhana kwamba idadi ya watu duniani inaongezeka kwa kiwango kilekile kila mwaka.
Badala yake, walitumia mfumo wa kihisabati unaoelezea ongezeko la kasi la idadi ya watu, unaojulikana kama Hyperbolic Growth.
Katika mfumo huo, si kwamba idadi ya watu inaongezeka tu, bali pia kasi ya ongezeko hilo inaendelea kuongezeka kadiri muda unavyopita.
Mfumo huo unategemea dhana kwamba uwezo wa binadamu kushirikiana, kusaidiana na kuunda mahusiano na watu wengine humwezesha kukabiliana na baadhi ya changamoto za mazingira.
Kwa mujibu wa nadharia hiyo, uwezo huo huongeza nafasi za binadamu kuishi na kuendelea kuzaliana.
Baada ya kutumia mfumo huo wa kihisabati kuchambua takwimu za kihistoria, watafiti walihitimisha kuwa mfumo wao ungefikia hatua inayojulikana kama singularity mwaka 2026. Walikadiria kuwa hatua hiyo ingefikiwa katikati ya mwezi Novemba.
Hiyo ndiyo sababu tarehe 13 Novemba 2026 ilihusishwa na utafiti huo.
Kwa mujibu wa hesabu zao, idadi ya watu duniani ingefikia kiwango kisicho na kikomo kinadharia siku hiyo, iwapo hali na makadirio waliyotumia yangeendelea bila mabadiliko.
Kwa mtazamo wa kwanza, jina la utafiti huo linaweza kuonekana kama utabiri wa mwisho wa dunia. Hata hivyo, maana yake halisi ni tofauti.
Watafiti hawakutabiri kuwa jiwe kubwa kutoka angani lingeigonga dunia, kwamba jua lingelipuka au kwamba matetemeko ya ardhi na milipuko ya volkano vingesababisha maafa makubwa.
Pia hawakutaja tarehe ambayo binadamu wangetoweka duniani kutokana na janga la kiasili.
Kwa hakika, walitumia neno Doomsday kuelezea hali ya kinadharia ya kihisabati ambapo, kwa mujibu wa mfumo wao, idadi ya watu duniani ingefikia kiwango kisicho na kikomo.
Hali hiyo haiwezekani kutokea katika ulimwengu halisi.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid