Wataalamu: Tishio jipya la fangasi sugu kwa dawa lazua wasiwasi

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 8

Aina mpya ya fangasi hatari ambaye hustahimili kila aina ya dawa za kuua fangasi zilizopo kwa sasa imegunduliwa, huku wataalamu wakionya huenda zipo aina nyingine kama hizo ambazo bado hazijatambuliwa.

Aina hii yenye usugu mkubwa ya fangasi Candidozyma auris (C. auris) ilibainika kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 28 nchini Kenya, ambaye alipata maambukizi kwenye jeraha baada ya kufanyiwa upasuaji.

Licha ya kupewa takriban dawa 13 tofauti za kupambana na vijidudu, maambukizi yake yaliendelea kuwepo, jambo lililowashangaza madaktari wakikosa tiba iliyothibitishwa ya kumsaidia.

Hadi kufikia sasa, matokeo ya mwisho ya hali yake hayajawekwa wazi kwa umma.

Inaelezwa kwamba fangasi huyu si mpya. C. auris alitambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2009 kwenye sikio la mgonjwa mmoja nchini Japan.

Tangu wakati huo, amebainika katika zaidi ya nchi 40 kwenye mabara sita duniani, huku baadhi ya aina zake zikiendelea kupata uwezo wa kustahimili hata dawa zenye nguvu zaidi za kuua fangasi.

Kisa cha kwanza kinachojulikana cha C. auris mwenye usugu mkubwa dhidi ya dawa kiliripotiwa mwaka 2022 kwa mwanamke mwenye umri wa miaka 29 huko New Jersey, Marekani.

Mwanamke huyo aligundulika kuwa na maambukizi hayo baada ya kufanyiwa upandikizaji wa viungo kadhaa vya mwili.

Hata hivyo, bado haijulikani ikiwa visa hivi viwili vilitokea kwa kujitegemea au kama maambukizi yaliyogunduliwa nchini Kenya yanahusiana na yale ya awali na yaliingia nchini humo bila kutambuliwa.

Dawa za kuua fangasi ni miongoni mwa dawa ngumu zaidi kutengenezwa kutokana na ukweli kwamba seli za fangasi zinafanana kwa kiasi kikubwa na seli za binadamu. Hali hiyo ina maana kwamba dawa zinazolenga kuharibu fangasi mara nyingi zinaweza pia kuathiri seli za mwili wa binadamu na kusababisha madhara.

Matokeo ya utafiti kuhusu aina hii mpya ya fangasi yalichapishwa mwezi uliopita katika jarida la kisayansi Scientific Reports.

Waandishi wa utafiti huo walisema ugunduzi huo unaashiria "ongezeko la tishio la maambukizi ya fangasi ambayo hayawezi kutibika."

Watafiti hao walisisitiza kuwa kuna haja ya haraka ya kuimarisha mifumo ya kugundua, kufuatilia na kutibu maambukizi ya fangasi ili kuzuia hatari ya kuenea kwa vijidudu hivi sugu katika siku zijazo.

Profesa Matthew Fisher, mtaalamu wa magonjwa ya fangasi katika Chuo cha Imperial College London, amesema kuna uwezekano mkubwa kwamba kisa kilichogunduliwa nchini Kenya si cha pekee.

Akizungumza na BBC Science Focus, alisema idadi halisi ya maambukizi ya aina hiyo huenda ni kubwa zaidi kuliko inavyoonekana kwa sasa.

"Kwa hakika idadi halisi ni kubwa zaidi, na tunachokiona ni visa ambavyo tuna uwezo wa kuvitafuta na kuvigundua," alisema.

Hali hiyo imeibua maswali kuhusu iwapo kuibuka kwa fangasi huyu mpya mwenye usugu mkubwa dhidi ya dawa ni dalili ya milipuko mikubwa zaidi inayoweza kutokea siku zijazo.

Pia wataalamu wanajiuliza ni kwa namna gani dunia inaweza kukabiliana na fangasi wanaoendelea kubadilika na kustahimili hata dawa zenye nguvu zaidi zinazopatikana kwa sasa.

Nani yupo hatarini?

Kwa sasa, maambukizi ya fangasi sugu kwa dawa yanaonekana kupatikana zaidi katika mazingira ya hospitali, anasema Dkt Neil Stone, mshauri wa magonjwa ya kuambukiza na profesa wa maambukizi na kinga katika Chuo Kikuu cha University College London.

Ingawa amesema maambukizi hayo ni sababu ya kutia wasiwasi, alieleza kuwa kuna uwezekano mdogo wa kuathiri watu wanaoendelea na shughuli zao za kawaida za kila siku.

Profesa Fisher alikubaliana na mtazamo huo, akisema kwamba watu wenye afya njema hawapo katika hatari kubwa, lakini baadhi ya wagonjwa waliolazwa hospitalini wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa.

Hii ni kwa sababu fangasi C. auris huhitaji njia ya kuingia mwilini, kama vile kupitia jeraha, upasuaji au vifaa vya tiba vinavyoingizwa mwilini, kabla ya kuanza kusababisha madhara.

"C. auris huishi kwenye ngozi, na ngozi isiyokuwa na jeraha ni kinga nzuri sana," alisema Profesa Fisher. "Fangasi huyu anaweza kubaki kwenye ngozi kwa miezi kadhaa bila kusababisha madhara yoyote."

Hata hivyo, katika mazingira ya hospitali hali huwa tofauti. Kwa mujibu wa Fisher, vifaa vya tiba kama mirija ya kuingiza dawa moja kwa moja kwenye mshipa na mirija ya kutolea mkojo vinaweza kuupa fangasi huyo "njia ya moja kwa moja" ya kuingia kwenye mfumo wa damu au kibofu cha mkojo, na hivyo kusababisha maambukizi makubwa zaidi.

Vifaa vya tiba kama mirija ya kutolea mkojo vinaweza kutoa njia ya moja kwa moja kwa fangasi waliopo kwenye ngozi ya mgonjwa au katika mazingira yanayomzunguka kuingia ndani ya mwili.

Tofauti na ukungu mweusi au uyoga unaoonekana kwa macho, C. auris ni aina ya chachu, yaani fangasi mdogo sana mwenye seli moja ambaye haonekani kwa macho bila kutumia hadubini. Mtu anaweza kubeba fangasi huyu kwenye ngozi kwa wiki au hata miezi bila kuonyesha dalili zozote, huku akiweza kuusambaza kwenye sehemu mbalimbali kama vitanda vya hospitali, vipini vya milango na vifaa vya matibabu.

Kwa mujibu wa Profesa Fisher, C. auris ana uwezo wa kipekee wa kutengeneza safu za vijiumbe vinavyoshikamana kwenye nyuso za plastiki. Hali hii hufanya iwe vigumu kwa mfumo wa kinga wa mwili au dawa kufika na kuuangamiza fangasi huyo baada ya kujikita.

Aidha, matumizi ya antibiotiki za wigo mpana yanaweza kuua bakteria wanaosaidia kudhibiti ukuaji wa fangasi, na hivyo kutoa nafasi kwa C. auris kuenea kwa urahisi zaidi.

Kutokana na hali hiyo, wagonjwa waliolazwa katika vyumba vya uangalizi maalumu (ICU), ambao mara nyingi kinga zao za mwili zimepungua na hutegemea vifaa vya plastiki kwa ajili ya dawa na majimaji, wako katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa.

"Iwapo fangasi huyu ataingia ndani ya mwili na kuenea, kwa mfano kupitia mfumo wa damu, hali hiyo inaweza kuhatarisha maisha na huhitaji matibabu ya haraka," alisema Dkt Stone.

Je, fangasi sugu kwa dawa huambukiza zaidi?

Hapana. Kwa mujibu wa Profesa Fisher, uwezo wa fangasi kustahimili dawa hauumaanishi kwamba ana uwezo mkubwa zaidi wa kuenea kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

"Usugu wa dawa na uwezo wa kusambaa ni sifa mbili tofauti," alisema.

Hata hivyo, usugu huo unaweza kusaidia fangasi kuenea kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Profesa Fisher alieleza kwamba aina ya fangasi inayostahimili matibabu ndiyo inayobaki mwilini baada ya tiba kutolewa, hivyo humwezesha mgonjwa kuendelea kubeba maambukizi kwa muda mrefu zaidi na kuongeza nafasi za kuyaeneza kwa wengine.

Kwa maneno mengine, fangasi mwenye usugu mkubwa dhidi ya dawa hana uwezo wa ziada wa kuambukiza watu, bali ana faida ya kuishi kwa muda mrefu zaidi bila kuathiriwa na matibabu.

Uwezo huo wa kuendelea kuwepo hauishii kwa wagonjwa pekee. Mara fangasi C. auris anapoanza kusambaa ndani ya hospitali, huwa vigumu sana kumwangamiza kabisa.

Profesa Fisher alisema fangasi huyo anaweza kuishi kwa wiki kadhaa kwenye ukavu na pia ana uwezo wa kustahimili baadhi ya viuatilifu vya kawaida vinavyotumika kusafisha mazingira.

Jinsi ya kukabiliana naye

Hata kama hakuna dawa madhubuti za kutosha dhidi ya baadhi ya aina zake, bado kuna njia za kujikinga na kudhibiti maambukizi ya C. auris.

Kwa mujibu wa Profesa Fisher, fangasi huyu amewahi kudhibitiwa kwa mafanikio kupitia hatua za kuzuia maambukizi kama kuwachunguza watu waliokaribiana na wagonjwa, kuwatenga wenye maambukizi na kutumia viuatilifu sahihi kwa usafi wa mazingira.

Aidha, wataalamu wanaeleza kuwa hata kama fangasi huyu ni sugu kwa dawa, hatua hizi za kudhibiti maambukizi zinaweza kuendelea kuwa na ufanisi katika kuzuia kuenea kwake.

"Kimsingi, mbinu za usafi zinazopendekezwa kwa sasa zinapaswa kuwa na ufanisi bila kujali kama [fangasi hao] wana usugu dhidi ya dawa moja au dawa nne, kwa kuwa hatua hizo za usafi hazitegemei kiwango cha usugu," alisema Dkt. Johanna Rhodes, profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Birmingham ambaye anafanya utafiti kuhusu usugu wa fangasi dhidi ya dawa.

Kinadharia, hatua za usafi kama kutumia viuatilifu sahihi na kuwatenga watu walioambukizwa zinapaswa kuwa na uwezo wa kudhibiti hata aina za fangasi ambazo hazisikii dawa.

Hata hivyo, alionya kuwa tafiti zaidi zinahitajika kuthibitisha hilo kwa vitendo.

"Kinachotia wasiwasi ni kwamba ikiwa kimelea kimebadilika na kuwa sugu kwa dawa zote, basi kuna uwezekano pia wa kuwepo kwa mabadiliko mengine ya kijenetiki yanayokipa uwezo wa kukwepa hatua za usafi na udhibiti," alisema.

Hata bila kuwepo kwa dawa zinazofanya kazi dhidi ya fangasi hao, madaktari bado wana njia nyingine za kupambana nao, alieleza Stone. Mbinu hizo ni pamoja na kuondoa vifaa vya tiba vilivyochafuliwa, kama mirija ya kuingiza dawa kupitia mshipa, kuondoa kwa upasuaji tishu zilizoambukizwa, pamoja na kujaribu mchanganyiko wa dawa za kuua fangasi ambazo zinaweza kufanya kazi kwa pamoja.

Hata hivyo, mbinu hizo husaidia tu ikiwa madaktari wanaweza kugundua mapema lini na wapi Candida auris ipo.

"Changamoto kubwa zaidi ni ugunduzi wa fangasi huyu," alisema Fisher.

"Candida auris mara nyingi hutambuliwa kimakosa na mifumo ya zamani ya maabara inayotegemea uchunguzi wa kemikali za kibiolojia. Zaidi ya hayo, maabara nyingi duniani bado hazina uwezo wa kutambua aina mahususi za chachu na fangasi hao kwa usahihi."

Hali hiyo ina maana kwamba maambukizi ya Candida auris yanaweza kuendelea kuenea bila kugunduliwa kwa wakati, jambo linalofanya juhudi za kuyadhibiti kuwa ngumu zaidi.

Hata pale ambapo fangasi huyu husababisha maambukizi, dalili zake mara nyingi zinaweza kufanana na magonjwa mengine mengi. Kwa kawaida mgonjwa hupata homa ambayo haiitiki matibabu ya antibiotiki, jambo linalofanya iwe vigumu kutambua chanzo halisi cha tatizo.

Ili kuthibitisha kuwa mgonjwa ameambukizwa Candida auris, wahudumu wa afya hulazimika kuchukua sampuli kutoka kwa mgonjwa na kufanya vipimo vya maabara. Hata hivyo, si hospitali zote zilizo na uwezo wa kufanya vipimo hivyo, na wakati mwingine matokeo yanaweza kuchukua wiki kadhaa kupatikana.

Fisher alisisitiza kwamba ingawa aina ya Candida auris iliyogunduliwa nchini Kenya, ambayo ni sugu kwa dawa zote za kuua fangasi, huenda ikawa kesi ya pili kuwahi kurekodiwa rasmi duniani, hilo halimaanishi kuwa ni tukio la pili kutokea.

"Wasiwasi wangu si kuzuka kwa mlipuko mkubwa wa ghafla, bali kuenea kimya kimya kwa fangasi huyu katika jamii au hospitali kwa muda mrefu," alisema.

Aliongeza:

"Kwa kila mgonjwa mmoja anayepata maambukizi makubwa yanayoonekana wazi, kuna wengine kadhaa ambao fangasi huyu hukaa katika miili yao bila kusababisha dalili zozote. Hivyo basi, unaweza usione dalili za mlipuko isipokuwa kama unaufuatilia na kuutafuta kwa makusudi."

Kauli hiyo inaashiria kwamba Candida auris huenda ikawa inaenea kimya kimya katika baadhi ya maeneo bila kugunduliwa, hasa katika mazingira ambayo uwezo wa kufanya uchunguzi wa maabara ni mdogo. Hali hiyo inawafanya wataalamu wa afya kuonya kuwa ufuatiliaji wa karibu na uwekezaji katika vipimo vya utambuzi ni muhimu ili kuzuia kuenea kwa fangasi huyu hatari.