Kombe la Dunia halitakuwa kama ulivyozoea, kuna sheria 7 mpya

Manchester City goalkeeper Gianluigi Donnarumma sitting on the floor during their Premier League game against Leeds United in November

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Meneja wa Leeds United, Daniel Farke alimlalamikia mlinda mlango wa Manchester City, Gianluigi Donnarumma kwa kudanganya ameumia kwenye mechi ya ligi kuu
    • Author, Dale Johnson
    • Nafasi, BBC Spor
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kombe la Dunia la mwaka 2026 linatarajiwa kuleta mabadiliko kadhaa katika sheria za mchezo (Laws of the Game) zitakazobadilisha namna soka linavyochezwa na kusimamiwa. Mabadiliko hayo yanalenga kupunguza upotevu wa muda, kuongeza haki katika maamuzi ya waamuzi na kudhibiti mbinu ambazo zimekuwa zikitumika kuvuruga kasi ya mchezo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi wa FIFA, Pierluigi Collina, amesema baadhi ya mabadiliko hayo tayari yameidhinishwa, huku mengine yakitarajiwa kutumika rasmi wakati wa mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani. Lengo kuu ni kuhakikisha mchezo unakuwa wa kasi zaidi na wenye uwazi, huku matokeo yakiamuliwa zaidi na uwezo wa timu uwanjani.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na malalamiko kuhusu mbinu za kupoteza muda na "mapumziko ya kimkakati" wakati wa mechi, ambapo baadhi ya wachezaji hujifanya kuumia ili kutoa nafasi kwa makocha kutoa maelekezo. FIFA sasa inachukua hatua kali kuhakikisha tabia hizo zinadhibitiwa.

Mabadiliko haya yanatarajiwa kuifanya Kombe la Dunia la 2026 kuwa moja ya michuano yenye sheria zilizobadilishwa zaidi katika historia ya soka la kisasa, huku waamuzi wakipewa mamlaka zaidi ya kusimamia mchezo kwa haki na kwa kasi.

Si vyema wachezaji wote kutoka uwanjani

Moja ya mabadiliko muhimu ni kuzuia kile kinachoitwa "mapumziko ya kimkakati ya kipa". Hii ni hali ambapo kipa hujilaza chini akidai kuumia, huku wachezaji wengine wakitoka uwanjani kuelekea benchi la ufundi kwa ajili ya maelekezo ya kocha.

FIFA imeamua kuwa iwapo kipa ataumia na mchezo kusimamishwa, wachezaji wa timu zote hawataruhusiwa kwenda kwenye benchi la ufundi. Badala yake, watabaki sehemu walipo au kukusanyika katikati ya uwanja wakisubiri mchezo kuendelea.

Hatua hii inalenga kuondoa matumizi ya majeraha kama njia ya kupata muda wa kupanga mikakati na kuhakikisha mchezo haukatizwi kwa sababu zisizo za lazima.

Collina amesema ni jambo lisilo la kawaida kuona kipa, mwamuzi na wahudumu wa afya pekee uwanjani huku wachezaji wengine wote wakiwa pembeni, na kwamba mabadiliko haya yatafanya mchezo kuwa wa haki zaidi.

Collina: Bao linalotokana na faulo kabla ya mpira kuchezwa si la haki

Uruguaylı Federico Valverde ve Jose Maria Gimenez, Wembley Stadyumu'nda İngiltere'nin ilk golünden sonra hakem Sven Jablonski'ye kızdı.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kwa mujibu wa sheria mpya, VAR ingeweza kulikataa bao la England dhidi ya Uruguay, ambalo zilitokea rabsha kabla ya kufungwa

Mabadiliko mengine makubwa yanahusu matumizi ya teknolojia ya usaidizi wa Video (VAR) katika mipira ya adhabu na kona. Hapo awali, matukio ya faulo yaliyotokea kabla ya mpira kuchezwa rasmi hayakuweza kuchunguzwa na VAR, jambo lililozua malalamiko katika baadhi ya mechi.

Collina amesema baadhi ya mabao yamekuwa yakipatikana katika mazingira yasiyo ya haki, hasa pale ambapo washambuliaji wanapofanya makosa au vizuizi kabla ya mpira kupigwa lakini mchezo unaendelea kama kawaida.

Kwa sasa, IFAB imekubali mabadiliko yanayoruhusu VAR kuchunguza makosa yanayotokea kabla ya mpira kuchezwa, ikiwa tukio hilo linaathiri moja kwa moja matokeo ya mchezo kama bao, penalti au adhabu ya kinidhamu.

Hii ina maana kuwa iwapo itabainika kulikuwa na faulo kabla ya kona au mpira wa adhabu kupigwa, mwamuzi anaweza kuamuru mpira urudiwe tena.

Hizi ndizo sheria saba mpya za Kombe la Dunia

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Miongoni mwa mabadiliko makubwa yatakayotumika katika Kombe la Dunia la 2026 ni sheria ya kuhesabu sekunde tano kwa mipira ya kurushwa. Ikiwa mchezaji atachelewesha kwa makusudi kuurudisha mpira mchezoni baada ya muda huo kuisha, mwamuzi anaweza kuipa timu pinzani haki ya kurusha mpira huo.

Sheria kama hiyo itatumika pia kwenye mipira ya golikiki (Sekunde tano kwa mpira wa golikiki). Endapo timu itajaribu kupoteza muda kwa kuchelewesha kuanza tena mchezo, mwamuzi anaweza kuipa timu pinzani kona kama adhabu. Lengo ni kupunguza tabia ya kupoteza muda hasa katika dakika za mwisho za mechi.

Mabadiliko mengine yanahusu mabadiliko ya wachezaji. Mchezaji anayefanyiwa mabadiliko (sub), atakuwa na sekunde 10 tu kufika nje kupitia njia ya karibu zaidi. Akichelewesha zaidi ya muda huo, mchezaji mbadala hataruhusiwa kuingia mara moja na timu italazimika kucheza ikiwa pungufu kwa muda dakika moja.

Kwa upande wa matibabu ya majeruhi, mchezaji anayepatiwa huduma ya kitabibu atalazimika kubaki nje ya uwanja kwa sekunde 60 kabla ya kuruhusiwa kurejea kucheza, isipokuwa katika mazingira maalumu kama majeraha ya kipa au pale ambapo mpinzani amepewa kadi ya njano au nyekundu.

Kufunika mdomo huku ukizungumza: Aidha, mchezaji atakayefunika mdomo wake kwa mkono, jezi au njia nyingine wakati wa kuzungumza au kubishana na mpinzani anaweza kuadhibiwa kwa kadi nyekundu, hatua inayolenga kuongeza uwazi na kuzuia tabia zinazoweza kuficha mawasiliano ya wachezaji, hasa matusi na ubaguzi wa rangi.

VAR pia imepewa mamlaka mapya. Waamuzi wa video sasa wataweza kuchunguza kama kona au mpira wa adhabu umetolewa kwa usahihi kabla ya mchezo kuendelea, na pia wataweza kupitia uamuzi wa kadi ya pili ya njano uliosababisha mchezaji kutolewa uwanjani. Hata hivyo, kadi za njano za kawaida hazitaangaliwa na VAR.

FIFA inasema mabadiliko haya yote yanalenga kufanya Kombe la Dunia la 2026 kuwa la haki zaidi, la kasi zaidi na lenye kupunguza malalamiko kuhusu maamuzi ya waamuzi, huku likihakikisha soka linabaki kuwa mchezo wa ushindani na burudani duniani.