Mahakama yakataa kuwaita Samia, Majaliwa na Mpango kutoa ushahidi

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Mahakama imekataa ombi la kuwaita Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, pamoja na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu.

Mahakama imeeleza kuwa si sahihi kuwaita mashahidi hao kwa madhumuni ya kuthibitisha iwapo walitishika au hawakutishika kutokana na kauli zinazolalamikiwa katika shauri hilo.

"Kuhusu mashahidi wengine, mtakumbuka kwamba tarehe 21 Agosti Mahakama hii ilitoa uamuzi mdogo kwamba mshtakiwa ana kesi ya kujibu na ikamweleza kuwa ana haki ya kuleta mashahidi wake," Mahakama imesema.

Katika orodha ya mashahidi aliowataja, walikuwemo:

  • Samia Suluhu Hassan
  • Dk. Philip Mpango
  • Kassim Majaliwa
  • Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP)
  • Jenerali John Jacob Mkunda, Mkuu wa Majeshi
  • Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa
  • Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai
  • Wengine ni John Mnyika, Amani Golugwa, John Heche na Brenda.

"Baada ya kuwasilisha orodha hiyo, mshtakiwa aliiomba Mahakama itoe wito kwa mashahidi hao ili waweze kufika kutoa Ushahidi," Mahakama iliendelea kusema.

Upande wa mashtaka uliweka pingamizi chini ya Kifungu cha 218(1) na Kifungu cha 304 vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Upande wa mashtaka uliwasilisha hoja sita za kupinga mashahidi hao.

Hoja ya kwanza ilikuwa kwamba wakati shauri likiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mashahidi hao hawakuwa wametajwa, hivyo hawakustahili kuitwa baadaye. Walieleza kuwa ingawa mshtakiwa aliwataja mashahidi hao shauri lilipofika Mahakama Kuu, hakuwataja katika hatua za awali.

Aidha, Wakili wa Serikali alidai kwamba ushahidi wa baadhi ya mashahidi hao, hususan Samia Suluhu Hassan na Dk. Philip Mpango, haukuwa na uhusiano wa moja kwa moja na masuala yanayobishaniwa kwenye kesi hiyo.

Alieleza pia kuwa baadhi ya mashahidi waliopendekezwa ni watumishi wa umma, na kwamba kuwaita kulionekana kuwa ni juhudi za kuwauliza maswali ya dodoso kuhusu ushahidi uliokwisha kutolewa, hususan iwapo walitishika au hawakutishika kutokana na kauli zinazodaiwa kutolewa na mshtakiwa.

Hoja nyingine ya mashtaka ilitokana na Kifungu cha 9 cha Sheria ya Kinga ya Rais, ambacho kinaeleza kwamba Rais si shahidi anayelazimika kuitwa kutoa ushahidi mahakamani.

Baada ya kusikiliza hoja za mashtaka, mshtakiwa alijibu kwa kuomba Mahakama itoe wito kwa mashahidi wote aliowataja, akisema ni haki yake ya kikatiba kuita mashahidi anaowaona kuwa muhimu katika utetezi wake.

Alieleza kwamba Mahakama hii ilishapokea orodha ya mashahidi hao wakati shauri likiendelea, licha ya kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikuwa imekataa ombi hilo. Aidha, alisema kuwa ingawa baadhi yao ni maafisa wa Serikali, bado wanawajibika kutoa ushahidi endapo wataitwa na Mahakama.

Mshtakiwa alisisitiza kuwa hakuna sheria inayowazuia viongozi hao kupewa wito wa Mahakama. Aliongeza kuwa ushahidi wao una umuhimu mkubwa kwa sababu shtaka linalomkabili linahusu kutishia Serikali, na kwamba Rais akiwa Mkuu wa Nchi anahusika moja kwa moja na suala hilo.

Pia alidai kuwa mashahidi hao wangeisaidia Mahakama kufahamu vizuri iwapo tukio linalodaiwa lilitokea na mazingira yake.

Kuhusu hoja ya kwamba baadhi ya mashahidi walikuwa wamewakilishwa tayari kupitia mashahidi wengine walioitwa na upande wa mashtaka, mshtakiwa alisema sheria haisemi kwamba jambo hilo linamzuia kuwaita mashahidi hao.

Upande wa mashtaka ulipopewa nafasi ya kujibu hoja za mshtakiwa, ulisisitiza msimamo wake wa awali.

Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, Mahakama ilijielekeza kwenye suala la msingi la kuamua iwapo pingamizi hilo lina mashiko au la.

Mahakama imebaini kwamba katika mwenendo wa shauri lililokuwa Mahakama ya Kisutu, ni kweli mshtakiwa hakuwataja mashahidi hao na pia Mahakama hiyo haikuwa imewaorodhesha.

Kwa hiyo, Mahakama imeona kwamba hatua zilizofanyika baadaye haziwezi kurekebisha makosa au mapungufu yaliyotokea katika hatua za awali za shauri. Kwa msingi huo, Mahakama imekubaliana na hoja hiyo ya Jamhuri.

Hata hivyo, Mahakama imeeleza kuwa katika kuamua kama mashahidi hao waitwe au la, jambo la msingi ni kuangalia iwapo ushahidi wao una umuhimu (relevance) katika shauri lililopo.

Mahakama imebainisha kwamba jukumu la kuthibitisha mashitaka ni la upande wa Jamhuri na si la upande wa utetezi. Aidha, mashauri ya jinai huanzishwa na upande wa mashtaka.

Mahakama imeendelea kusema kuwa hati ya mashitaka inaeleza kwamba mshtakiwa anatuhumiwa kuwa na nia fulani ya kutenda kosa, na si kwamba aliwatisha watu fulani moja kwa moja.

Kwa hiyo, suala la iwapo watu hao walitishika au hawakutishika si hoja ya msingi katika kuthibitisha mashtaka yaliyopo mbele ya Mahakama.

Kutokana na sababu hiyo, Mahakama imeona kuwa si sahihi kutoa wito kwa mashahidi hao ili waje kujibu swali la iwapo walitishika au hawakutishika.

Mahakama yakubali IGP, DCI na Mkuu wa Majeshi kutoa ushahidi Kesi ya Lissu

Kuhusu ombi la kumuita Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa kutoa ushahidi, Mahakama imeirejea kesi ya Khatibu Gandhi ambayo ilitumiwa na mshtakiwa katika hoja zake. Mahakama imebainisha kuwa katika shauri hilo shahidi husika alikuwa shahidi wa upande wa mashtaka na si wa upande wa utetezi kama ilivyo katika kesi ya sasa.

Baada ya kufanya uchambuzi huo, Mahakama imebaki na mashahidi watatu ambao haikuwa imewatolea uamuzi wa moja kwa moja, ambao ni:

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai

Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP)

Mkuu wa Majeshi, Jenerali John Jacob Mkunda.

Mahakama imeona kuwa mashahidi hao wana umuhimu katika shauri hili na ushahidi wao unaweza kusaidia katika kuibainishia Mahakama baadhi ya masuala yanayohusika katika kesi hiyo.

Kwa msingi huo, Mahakama imeamuru mashahidi hao watatu wapewe wito na waitwe kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi.