Mazungumzo ya mkataba na Real Madrid na nia ya Arsenal - hatima ya Vinicius Jr ni ipi?

.

Chanzo cha picha, GETTY

Maelezo ya picha, Vinicius Jr alijiunga na Real Madrid akiwa kijana mwaka wa 2018.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Huenda hakuna jambo la kuvutia zaidi katika masuala ya usajili kwa sasa kuliko hatima ya Vinicius Jr.

Bila shaka, mshambuliaji huyo wa Real Madrid ni mmoja wa wanasoka wenye hadhi ya juu zaidi duniani.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil alijiunga na Real akiwa na umri wa miaka 18 mnamo mwaka 2018, akishinda mataji 14 na kufunga mabao 128 katika mechi 375 akiichezea klabu hiyo kubwa ya Uhispania.

Inashangaza kufikiria kuwa wamemruhusu kuingia katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake lakini ndiyo hali halisi ilivyo sasa.

Katika hali ya kawaida, kulingana na wadau wa sekta hiyo, thamani ya soko ya Vinicius ingezidi pauni milioni 200.

Uwanjani, kiasi hicho cha pesa kingekupatia winga wa kushoto wa kiwango cha dunia ambaye pia ana uwezo mkubwa wa kucheza katikati, pamoja na mchezaji ambaye akiwa na umri wa miaka 26, anafikia kilele cha kiwango chake cha soka.

Nje ya uwanja, ungekuwa ukimsajili mtu maarufu duniani ambaye thamani yake ya kibiashara ingekuwa na faida kubwa ya kifedha.

Arsenal wanataka vipaji vilivyothibitika – na Vinicius anafaa

.

Chanzo cha picha, GETTY

Maelezo ya picha, Vinicius Jr ameshinda Ligi ya Mabingwa mara mbili akiwa na Real, mara ya hivi karibuni ikiwa msimu wa 2023-24.

Real Madrid wamejaribu kuhuisha mkataba wa mshambuliaji wao na kuanza mazungumzo zaidi naye siku ya Jumatatu - lakini, hadi sasa, bila mafanikio.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Uwezekano wa yeye kupatikana sokoni umevutia hisia za Arsenal, ambao ni miongoni mwa klabu zilizojadili ndani kwa ndani uwezekano wa kutumia fursa ya kutofautiana kwao kimkataba. Timu za Saudi Arabia nazo zinafuatilia kwa karibu hali yake.

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, anataka kusajili mchezaji mwenye uwezo uliothibitishwa - na Vinicius anakidhi vigezo hivyo.

Vyanzo vya karibu na Arsenal vinasisitiza kuwa yeye ni mmoja tu wa chaguzi kadhaa ambazo klabu inazichunguza katika harakati za kutafuta mshambuliaji wa upande wa kushoto, baada ya kukosa saini ya Morgan Rogers iliyochukuliwa na Chelsea.

Hata hivyo, BBC Sport inaelewa kuwa Arteta amevutiwa sana na wazo la kumsajili Vinicius kiasi kwamba ndani ya klabu anachukuliwa kuwa mlengwa namba moja.

Kama Arsenal ilivyobaini kupitia sakata la Rogers, hakuna uhakika kwamba klabu zitafanikiwa kuwapata wachezaji wanaowapa kipaumbele.

Kwa hakika, Arsenal wanatambua uhalisia wa nafasi yao ya kumpata Vinicius Jr. Wanajua kuwa ni jambo gumu sana kufanikiwa.

Vivyo hivyo, kuna mtazamo miongoni mwa watu wa karibu na Vinicius Jr kwamba hatua yoyote ya kwenda Arsenal ingekuwa ngumu.

Kwa wachezaji wengi wa Amerika Kusini, kuichezea Real Madrid au Barcelona ni ndoto ya maisha yao yote. Kuondoka katika mji mkuu wa Uhispania - hata kwenda kwenye klabu yenye hadhi kubwa kama Arsenal - kungeonekana, katika hali nzuri zaidi, kama hatua ya kubaki palepale (bila maendeleo makubwa).

Kwa vile Real inachukuliwa kuwa klabu kubwa zaidi duniani, kuna hisia kwamba kuondoka Bernabeu kungeweza pia kuathiri hadhi ya kibiashara ya mchezaji huyo.

Je, Vinicius yuko tayari kuondoka Real?

.

Chanzo cha picha, GETTY

Maelezo ya picha, Mkataba wa Vinicius Mdogo wa Real Madrid utaendelea hadi 2027

Hali ya uhamisho wa bure inamaanisha kuwa Vinicius anaweza kuongeza mapato yake maradufu mwaka ujao.

Kwa kuwa fursa hiyo sasa inawezekana, ni wazi kuwa mshambuliaji huyo karibu ataomba nyongeza kubwa ya mshahara iwapo atahama msimu huu wa joto.

Kulazimika kutenga kiasi cha angalau pauni milioni 130 pamoja na mishahara itakuwa changamoto kubwa kwa klabu yoyote, hata iwe tajiri kiasi gani, katika kipindi hiki cha kanuni za udhibiti wa fedha.

Hata hivyo, Arsenal wamefanya tathmini ya gharama hizo na wanaamini wana uwezo wa kifedha kufanikisha usajili wa Vinicius. Inafahamika kuwa hatua hiyo ya kumsajili inaungwa mkono na watu wengi ndani ya klabu.

Hapo awali, Arsenal imewahi kuwapa wachezaji mikataba minono ya haki za picha (image rights). Hili litakuwa kipengele muhimu katika makubaliano yoyote ya kumleta Vinicius kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.

Washauri wa winga huyo kutoka wakala wa Roc Nation bila shaka wanafahamu vyema mambo haya.

Ukweli kwamba Roc Nation pia inamwakilisha mshambuliaji wa Arsenal, Gabriel Martinelli ambaye nafasi yake ingepungua sana iwapo Vinicius angejiunga na timu hiyo unaongeza kipengele cha kuvutia katika sakata hili.

Inafahamika kuwa Martinelli, ambaye amesalia na hadi miaka miwili katika mkataba wake, anafurahia maisha Arsenal na atafikiria kuondoka tu iwapo atapata fursa inayomfaa.

Kwa hakika, nguvu ya maamuzi iko mikononi mwa Vinicius zaidi.

Bila shaka, Arsenal ni moja ya klabu zenye mvuto mkubwa zaidi katika soka la Ulaya. Watakuwa miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, baada ya kupoteza kwa mikwaju ya penalti katika fainali ya msimu uliopita. Pia, wana hali nzuri sana ya kifedha.

Lakini kuhamia kaskazini mwa London kungemlazimu Vinicius kuachana na aina ya nguvu ya maamuzi ambayo wachezaji wengi, hata wale wa kiwango chake, hawana.

Labda jambo muhimu zaidi ni kwamba hatua hiyo ingemaanisha kuacha kuwa mchezaji wa Real Madrid.

Je, yuko tayari kufanya hivyo? Tutapata jibu hivi karibuni.