Kwa nini kuondoka kwa UAE kutoka OPEC ni muhimu?

Chanzo cha picha, Getty Images
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umetangaza kujiondoa kwa ghafla katika OPEC, jumuiya ya nchi zinazosafirisha mafuta ya petroli, hatua ambayo huenda ni muhimu na pia inaathari kubwa katika soko la nishati duniani.
UAE, ambayo ilikuwa mwanachama wa shirika hilo hata kabla ya kupata uhuru mwaka 1971, imekuwa miongoni mwa wazalishaji wakuu wa mafuta ndani ya OPEC na mara nyingi ikichukuliwa kama nchi yenye uwezo wa pili kwa uzalishaji baada ya Saudi Arabia.
Kwa miongo kadhaa, OPEC imekuwa na ushawishi mkubwa katika bei ya mafuta ghafi duniani kwa kudhibiti viwango vya uzalishaji na kuweka mgawo kwa wanachama wake, ikiwa na jukumu muhimu hasa katika migogoro ya mafuta ya miaka ya 1970 iliyobadilisha sera za nishati duniani.
Kwa maneno mengine, ilikuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuongeza uzalishaji kwa haraka baada ya Saudi Arabia, mwanachama ambaye angeweza kusaidia kupunguza shinikizo kwa bei kwa kuongeza uzalishaji.
Hata hivyo, uamuzi wa UAE unatokana na malalamiko ya muda mrefu kuhusu mgawo wa uzalishaji ulioweka kikomo cha kati ya mapipa milioni 3 hadi 3.5 kwa siku, hali iliyopunguza faida inayotokana na uwekezaji wake mkubwa katika sekta ya nishati.
Kwa kujiondoa OPEC, UAE sasa inapata nafasi ya kuzingatia kuongeza uzalishaji wake na kutumia kikamilifu uwezo wake wa kiuchumi katika soko la mafuta, ambapo inaweza kuongeza uzalishaji hadi takriban mapipa milioni tano kwa siku.
Hatua hiyo inakuja wakati wa mvutano unaoendelea katika eneo la Ghuba kufuatia vita vya Iran, hali ambayo tayari imeathiri uhusiano wa kidiplomasia na kiusalama katika ukanda huo, ikiwemo uhusiano kati ya UAE, Iran na Saudi Arabia.
Kwa OPEC, hili ni pigo kubwa wakati ambapo maswali mazito yameibuliwa kuhusu mshikamano wa muda mrefu wa shirika hilo.
Wachambuzi wanasema Saudi Arabia inaweza kujibu kwa kuongeza uzalishaji na kuingia katika ushindani wa bei ya mafuta, hatua ambayo inaweza kuleta shinikizo kwa uchumi wa nchi nyingine wanachama wa OPEC, hasa zile zenye uchumi dhaifu zaidi.
Hata hivyo, mwenendo wa soko la mafuta sasa utategemea sana namna Saudi Arabia na wazalishaji wengine wakuu watakavyojibu mabadiliko haya makubwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wanajadili mipango ya kujenga mabomba mapya ya mafuta kutoka maeneo ya uzalishaji ya Abu Dhabi, yatakayopita nje ya Mlango-Bahari wa Hormuz na kuelekeza mafuta hadi bandari ya Fujairah, ambayo haitumiki kwa kiwango kikubwa.
Bomba lililopo tayari linatumika kusafirisha mafuta, lakini linaelezwa kuwa litahitaji kupanuliwa ili kuendana na ongezeko la uzalishaji na kupunguza utegemezi wa njia za baharini katika Ghuba ya Uajemi, ambazo mara kwa mara hukumbwa na misukosuko ya kiusalama.
Hali ya sasa, ikiwa ni pamoja na mvutano na vizuizi vinavyoweza kutokea katika Mlango-Bahari wa Hormuz, inaifanya njia hii kuwa nyeti katika masoko ya mafuta, kwa kuwa huathiri moja kwa moja bei za mafuta, gesi, petroli, plastiki na hata bidhaa za chakula duniani.
Wakati bei ya mafuta duniani ikizunguka karibu dola 110 kwa pipa, wachambuzi wanaonya kwamba bei inaweza kushuka hadi karibu dola 50 katika kipindi kijacho, iwapo kutakuwa na utulivu katika Hormuz, hasa kuelekea muktadha wa kisiasa na uchaguzi nchini Marekani.
Uchambuzi unaonyesha kuwa OPEC leo haina ushawishi ule ule ilokuwa nao katika miaka ya 1970, ambapo ilidhibiti karibu asilimia 85 ya biashara ya mafuta duniani, ikilinganishwa na takriban asilimia 50 kwa sasa.
Wakati huo huo, mafuta yamepoteza sehemu ya nafasi yake kama mhimili mkuu wa uchumi wa dunia, huku vyanzo vingine vya nishati vikizidi kuchukua nafasi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ujumbe wa muda mrefu kutoka kwa Sheikh Yamani, aliyekuwa waziri wa mafuta wa Saudi Arabia na kiongozi mkuu katika OPEC, aliniambia, "Enzi ya Mawe haikuisha kwa sababu ulimwengu uliishiwa na mawe; Enzi ya Mafuta haitaisha kwa sababu ulimwengu unaishiwa na mafuta." , akisema kwamba historia ya nishati haitamalizwa na upungufu wa mafuta, bali na mabadiliko ya teknolojia na vyanzo mbadala vya nishati.
Kujiondoa OPEC kuna maana gani?
Uamuzi wa UAE unaweza pia kuonekana kama ishara ya dunia inayopunguza utegemezi wa mafuta, hasa katika kipindi ambacho uwekezaji katika nishati mbadala na umeme umeongezeka, hususan nchini China ambako magari na mifumo ya usafiri wa umeme imepunguza mahitaji ya mafuta kwa kiwango kikubwa.
Baadhi ya makadirio yanaonyesha kuwa mabadiliko hayo yamepunguza mahitaji ya mafuta nchini China kwa takriban mapipa milioni moja kwa siku, hali inayoweza kuathiri mwelekeo wa soko la kimataifa kwa muda mrefu.
Katika mazingira hayo, mataifa yenye akiba kubwa ya mafuta, ikiwemo UAE, yanaonekana kuongeza juhudi za kuyauza haraka zaidi kabla ya mahitaji kushuka zaidi katika siku zijazo.
Mengi sasa yatategemea hatima ya mivutano ya kisiasa katika Ghuba ya Uajemi na jinsi masoko ya nishati yatakavyojirekebisha.
UAE ina nguvu kubwa za kifedha na uchumi wa aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na huduma za kifedha na utalii.
Kujiondoa kwa UAE kutoka kwa OPEC kunaweza kuleta athari kubwa na sasa kutaweka shinikizo kubwa kwa Saudi Arabia.
Wakati meli za mafuta kwa mara nyingine tena zinapopitia mlango wa bahari, au ikiwa UAE itaongeza juhudi zake za kujenga mabomba mapya, mafuta ya nchi hiyo yataingia sokoni zaidi kuliko hapo awali, bila kuzuiliwa na ahadi za OPEC.
Hatua ya UAE, ikiwa na au bila kujiondoa OPEC, inaweza kuonekana kuwa ya muda mfupi kwa sasa, lakini wachambuzi wanaonya kuwa inaweza kuwa na athari kubwa kwa mfumo wa soko la mafuta duniani katika miaka ijayo.














