Nini siri ya mwanga mwekundu katika kuboresha ngozi?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

"Huu ni mwanga mwekundu, unarekebisha seli ya Ngozi yako na hauchomi" Dkt. Cal Shields anaelezea.

"Inachukua muda wa dakika 15 tu"anasema alipokuwa akifunga kifuniko cha kifaa cha tiba ya mwanga mwekundu na kuondoka kwenye chumba cha matibabu kilichoko eneo la Thriyv huko Manchester, Uingereza.

Miezi ya hivi karibuni, sekta ya urembo imeanza kutumia tiba ya mwanga mwekundu kwa wingi. Iwe unataka kuonekana kijana zaidi, kuishi muda mrefu zaidi, kuwa na furaha zaidi, au kupona haraka zaidi, tiba ya mwanga mwekundu inasemakana kusaidia.

Lakini tiba ya mwanga mwekundu ni nini hasa, na je, rangi hizi za mwanga mwekundu zinachangia vipi kuimarisha afya yetu?

Tiba ya mwanga mwekundu hufanya kazi mwilini kwa kutumia mawimbi ya mwanga.

Mwanga mwekundu tunaouona kwa macho ya kawaida una urefu wa mawimbi kati ya nanomita 630–660, ambapo nanomita ni kipimo kidogo sana sawa na milioni moja ya milimita

Kadiri urefu wa wimbi la mwanga unavyoongezeka, ndivyo unavyopenya ndani zaidi ya mwili. Mwanga wa urefu mfupi wa wimbi huathiri tabaka la juu kabisa la ngozi, wakati mwanga wa urefu mrefu zaidi huweza kufika kwenye tabaka la misuli na inaaminika kusaidia katika mchakato wa urekebishaji na urejeshaji wa tishu.

Chembechembe hizi ndogo za mwanga mwekundu zinaweza kusaidia kuongeza kasi ya uzalishaji wa nishati ndani ya seli, hivyo kuruhusu seli zilizozeeka au zilizoharibika kurekebishwa na kuzalishwa upya, kulingana na urefu wa wimbi na nguvu ya mwanga huo.

Huko Thrive mjini Manchester, Kate McLellan, mmoja wa wateja wa Dkt. Shields, alikuwa ametoka tu kwenye kitanda chake cha kupokea tiba ya mwanga mwekundu. Amekuwa akipokea tiba ya mwanga mwekundu kwa miaka miwili baada ya kuvunjika shingo akifanya mazoezi.

"Nilipitia tiba ya mwili kwa ajili ya jeraha langu," McLellan alisema, "lakini pia nilikuwa nikifanya tiba ya mwanga mwekundu."

Mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 32 anaamini kwamba ilimsaidia tishu za misuli yake kupona haraka zaidi.

McLellan ni shabiki mkubwa wa teknolojia hii, hata anamiliki barakoa ya uso ya LED. Watengenezaji wanadai kuwa kutumia mwanga mwekundu kunaweza kuchochea uzalishaji wa kolajeni na kupunguza mikunjo ya ngozi.

Baadhi ya vifaa hivi pia hutumia mwanga wa bluu, ambao una urefu mfupi wa wimbi, na tafiti fulani zinaonyesha kuwa unaweza kusaidia katika matatizo ya chunusi.

"Ninahisi ngozi yangu inaonekana bora zaidi," McLellan alisema. "Ngozi yangu ilikuwa imeharibika sana kutokana na jua, lakini sasa naweza kuona wazi maboresho yake."

Lakini je, vifaa vya tiba ya mwanga mwekundu vilivyopo sokoni vina ufanisi kiasi gani?

"Kutumia vifaa vya bei nafuu vya tiba ya mwanga mwekundu vinavyopatikana mtandaoni ili kuangaza mwanga kwenye mwili mara nyingi hakutoi matokeo yanayotarajiwa," anasema Profesa Glenn Jeffery, mtaalamu wa sayansi ya neva katika Chuo Kikuu cha University College London.

Licha ya kuwepo kwa dalili chanya kwamba tiba ya mwanga mwekundu inaweza kusaidia katika maeneo mbalimbali, kuanzia kurejesha afya ya ngozi hadi kupunguza maumivu ya misuli, Dk. Sophie Weatherhead wa British Dermatological Society anaonya dhidi ya kutumia njia hii bila tahadhari.

"Tuna tafiti kadhaa za utafiti, lakini nyingi ni ndogo kwa ukubwa na hutumia mchanganyiko wa aina tofauti za tiba ya mwanga pamoja na viwango tofauti sana vya nguvu ya mwanga."

Mbinu tofauti za tiba ya mwanga mwekundu

Barakoa za uso za mwanga mwekundu

Vifaa hivi mara nyingi hutumia mwanga mwekundu unaoonekana kwa macho ya kawaida.

Dk. Sophie Weatherhead wa British Dermatological Society anasema unene wa ngozi huathiri uwezo wa mwanga mwekundu kupenya ndani ya ngozi. Anasema inaweza kufanya kazi kwa kiwango fulani kwenye uso kwa sababu ngozi ya eneo hilo ni nyembamba kuliko sehemu nyingine za mwili.

Lakini alisisitiza kuwa pia inategemea kama kifaa kina nguvu ya kutosha.

"Mwanga mwekundu unapaswa kufika kwenye kilele cha ngozi," alieleza.

Pia inategemea chanzo cha mwanga huo, na anasema vifaa vya matumizi ya nyumbani vinaweza visiwe na ufanisi kama vifaa vya kiwango cha matibabu.

Kitanda cha tiba ya mwanga mwekundu

Vifaa hivi pia hutumia mwanga mwekundu unaoonekana kwa macho, lakini huzingatia zaidi mionzi ya karibu ya infrared yenye urefu mrefu wa wimbi.

Profesa Jeffery wa UCL anasema utafiti wake uligundua kuwa mwanga wa karibu wa infrared unaweza kupenya mwilini, hivyo unaweza kufikia tabaka za kina za tishu.

Hata hivyo, alitilia shaka ufanisi wa vitanda vilivyopo sokoni, akisema havichanganyi urefu wa mawimbi muhimu unaohitajika kuchochea uzalishaji wa nishati ya seli ipasavyo.

Aliongeza kuwa ni vigumu kukadiria ni kiasi gani cha mwanga mwekundu kinahitajika kwa ngozi ya kila mtu, kwa kuwa mahitaji hutofautiana kutoka mtu hadi mtu.

Profesa Zubair Ahmed, mtaalamu wa sayansi ya neva kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, anakubaliana kwa kiasi fulani, lakini anasema ikiwa kitanda cha tiba kina urefu sahihi wa wimbi na nguvu ya mwanga inayofaa, kinaweza kusaidia katika kurejesha ngozi, kupunguza uvimbe, na kusaidia urejeshaji wa misuli.

Sauna ya infrared

Sauna za tiba ya mwanga mwekundu hutumia urefu wa mawimbi ya mwanga ulio mkubwa zaidi kuliko ule unaopatikana kwenye vitanda vya tiba au barakoa za uso. Badala ya kulenga chanzo cha nishati ya seli, yaani mitochondria, faida yake kuu hutokana na joto.

Profesa Chris Minson, mtaalamu wa fiziolojia kutoka Chuo Kikuu cha Oregon, anaeleza kuwa molekuli ndani ya seli zinazojibu msongo wa joto hubadilishwa kuwa nishati, jambo ambalo linaweza kuwa na manufaa mbalimbali, kama kupunguza uvimbe na "kusafisha protini zilizoharibika," hali inayosaidia seli kujirekebisha.

Utafiti unaonyesha pia kuwa joto linaweza kusaidia kuimarisha mfumo wa moyo na mishipa ya damu, kupunguza ukakamavu wa viungo, na kuboresha usingizi.

Kwa Eloise Alexia, mwalimu wa yoga na Pilates katika kituo cha ustawi London, mwanga wa infrared katika studio yake una sifa fulani ambazo joto la kawaida haliwezi kutoa.

"Wanafunzi wangu wanaupenda sana," Alexia alisema. "Mwanga wa infrared hupiga maeneo sahihi, ukiwapa joto miili yao badala ya kupasha hewa inayowazunguka, na huwasaidia kupata joto haraka zaidi."

"Hawachoki haraka kama wanavyofanya wanapokabiliwa na joto la kawaida."

Ingawa tiba ya mwanga mwekundu kwa ujumla inachukuliwa kuwa salama, watu wenye hali fulani za ngozi, magonjwa inayoathiri misuli ya mwili na watu wenye unyeti wa mwanga (photosensitivity), au wanaopitia matibabu ya saratani wanashauriwa kwanza kushauriana na daktari kabla ya kupata matibabu haya

Wataalamu pia wanashauri kuepuka kutumia kupita kiasi tiba hii ya mwanga na kufuata maelekezo ya watengeneza vifaa hivyo.