Rare Earth: Je, madini haya yataleta maajabu Tanzania?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Tanzania inatarajia kukuza uchumi wake baada ya kugundulika kuwa na utajiri wa madini muhimu ya Rare Earth Elements (REEs) katika kijiji cha Mkiu, Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, aina ya Neodymium (Nd) na Praseodymium (Pr).

Bila shaka inaeleweka kuwa Tanzania ina utajiri wa madini mengi. Uchimbaji madini hutoa zaidi ya 50% ya jumla ya mauzo ya nje ya nchi, ambayo sehemu kubwa hutokana na dhahabu. Tanzania ina akiba ya dhahabu ya wakia milioni 10.

Lakini leo hatuzungumzii dhahabu, almasi wala Tanzanite. Tunazungumzia madini muhimu ya Rare Earth Elements, ambayo yanaundwa na kundi la kemikali 17 zenye sifa za kipekee, na ni muhimu katika teknolojia mbalimbali za kisasa.

Rare Earth hutumika kwenye nini?

Kinachofanya madini haya kuwa ya kipekee ni sifa yake ya kuwa na sumaku, ambayo ni muhimu katika teknolojia za kila siku na nishati ya kijani.

John Mavrogenes, profesa wa jiolojia ya kiuchumi katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia, anasema, “madini haya yanaweza kutoa nishati katika uzalishaji wa umeme wa upepo, gari lako la umeme, na lifti ya ghorofa na friji.”

Ni muhimu katika utengenezaji wa mikrochip, ambazo hutumika katika kila sekta kuanzia ulinzi hadi huduma za afya. Pia hutumika katika utengenezaji wa magari ya umeme, mitambo ya kuzalisha umeme wa upepo, simu za kisasa, vifaa vya kielektroniki pamoja na teknolojia nyingine zinazotegemea nishati ya kijani.

Katika maeneo ya Ulinzi, hutumika katika mifumo ya rada, makombora ya kisasa, na miwani ya kuonea gizani. Na katika matibabu, hutumika kwenye mashine za uchunguzi wa afya na upasuaji.

Ingawa madini haya yanapatikana katika nchi nyingi, ugumu wake unatokana na kuwa membamba na huchanganyika na madini mengine. Hilo hufanya kazi ya kugundua na kuyachimba kuwa ngumu. Na mchakato wake wa kusafisha ni mgumu vilevile.

Wazalishaji Wakuu

Kwa sasa China inatawala sehemu kubwa ya mnyororo wa usambazaji wa madini haya adimu duniani, ikidhibiti sehemu kubwa ya uchimbaji na kusafisha na kisha utengenezaji wa vifaa vyenye uwezo wa hali ya juu. Makampuni ya China yamezidi kupanua uwepo wao kote Afrika huku mahitaji ya kimataifa ya madini haya yakiendelea kuongezeka.

China inadhibiti karibu 70% ya uzalishaji wa madini haya duniani na ina akiba kubwa zaidi duniani. Marekani mzalishaji wa pili kwa ukubwa, huchangia takriban 13% ya uzalishaji wa kimataifa hasa kupitia mgodi wa Mountain Pass huko California.

Australia mzalishaji wa tatu kwa ukubwa duniani, huzalisha zaidi ya 7% ya ugavi wa dunia kutoka katika migodi ya mlima Weld. Nayo Myanmar inachangia takriban 5% ya uzalishaji wa duniani.

Uwepo wa madini hayo ardhini sio jambo pekee linaloathiri uchimbaji wake, pia kuna changamoto ya jinsi ya kuyafikia na kuyasafisha. Nchi nyingi hazina uwezo wa kusafisha madini hayo muhimu. Ni China ndiyo inayotawala usafishaji.

China ina uwezo mkubwa hata katika usafishaji wa madini mengine muhimu ambayo hayako katika kundi la madini ya REEs.

Chukua mfano huu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilizalisha 70% ya kobalti duniani mwaka 2021, lakini 90% ya ilienda China kusafishwa, kulingana na shirika la utafiti la Taasisi ya Faraday.

Zaidi ya 75% ya uchimbaji wa lithiamu duniani mwaka 2021 ulifanyika Australia na Chile, lakini 72% ya usafishaji hufanyika nchini China, kulingana na Jukwaa la Uchumi Duniani.

Kwa baadhi ya madini adimu, China hufanya zaidi ya 95% ya usafishaji.

Afrika ina nafasi gani?

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Utafiti wa Rasilimali la Marekani (USGS) zinaonyesha kuwa Tanzania, Afrika Kusini, na Nigeria zinashikilia hifadhi kubwa zaidi barani ya Afrika ya madini hayo. Na kueleza kuwa nchi hizo ziko katika mstari wa mbele wa mbio mpya ya dunia juu ya madini adimu.

Tanzania inaongoza Afrika, ikiwa na tani 890,000 za hifadhi iliyothibitishwa. Huu ni mojawapo ya miradi mikubwa duniani ambao bado haujaanza kuchimbwa, huku inatarajiwa kuanza uzalishaji mwaka 2027.

Afrika Kusini ina tani 790,000–860,000, huku miradi kadhaa ikitarajiwa kuanza uzalishaji mwaka 2029. Nigeria ina tani 127,200 za hifadhi, huku ikiwa na maeneo makubwa ambayo hayajagunduliwa.

Miradi mingine mbali na Tanzania na Afrika Kusini, ni huko Malawi na Angola ambako uchimbaji unatarajiwa kuanza 2026. Madini hayo yakielezwa kuwa yapo katika nchi nyingine kumi la mbili za Afrika.

Changamoto ya Afrika ni kubadilisha hifadhi zake kuwa uzalishaji, usafishaji na uuzaji wa kimkakati huku migodi mipya ikitarajiwa kuanza kufanya kazi duniani kati ya 2026 na 2029.

Kutokana na maendeleo ya akili mnemba AI na mahitaji makubwa ya nishati safi duniani, yatafanya mahitaji ya madini haya kuongezeka. Swali, Je, Tanzania itafanikiwa kuingia katika soko la dunia na nchi hiyo kunufaika kiuchumi?