Nilisema
hivi: mabadiliko yanahitaji muda, na kama kweli kulikuwa na utayari wa kufanya
mageuzi, basi uchaguzi ungeweza kuahirishwa ili kutoa nafasi ya kuyatekeleza.
Hata hivyo, CCM ilikataa kabisa wazo hilo.
Matokeo
yake, watu waliuawa. Kwa mujibu wa Tume ya Jaji Chande, watu 518 walipoteza
maisha, huku hatima ya wengine ikiwa haijulikani. Ninaamini kuwa kama uchaguzi
ungeahirishwa, maafa hayo yangeweza kuepukika.
Baadaye
nikaelezwa kuwa nilisema "nitakinukisha" na kwamba nilihamasisha
maandamano. Lakini maneno hayo yalinyofolewa ‘nje ya muktadha’.
Katika
mazungumzo yale, sikuzungumzia tutaifanyaje serikali hii. Hayo hayakuwa sehemu
ya ajenda yangu.
Leo
ninaambiwa nilikuwa na nia ya kuitishia serikali. Ilitoka wapi? Mliambiwa na
nani?
Nia yangu
ilikuwa kuwaelewesha watia nia wa chama changu kuhusu matatizo ya mfumo wetu wa
uchaguzi ili waweze kuelewa na kuunga mkono msimamo wa CHADEMA wa "No
Reforms, No Election".
Haikuwa
kuitishia serikali, kwa sababu hilo halikuwa lengo wala ajenda yangu.
Sikuhamasisha
watu kufanya fujo. Mimi ni mwanasheria, na hakuna sheria yenye masuala ya
"kukinukisha."
Kusudi letu
lilikuwa kuwaelimisha na kuwahamasisha Watanzania nchi nzima.
Tutakapokutana
kesho kutwa, nataka niwapitishe kwenye ushahidi uliowasilishwa mbele yenu muone
kama unajitosheleza kunyonga mtu.
Kwa kuwa
muda umeisha, naomba niishie hapa kwa leo. Tukutane tena Jumatano.
Lissu: Kwa
hiyo mfumo wa kampeni wa uchaguzi umekaa katika namna inayoipendelea CCM. Kuna
fujo sana. Mimi nimefanyiwa fujo, nimepigwa na mabomu ya polisi Tarime,
Serengeti, nimesimamishiwa kampeni kwa siku kumi.
Mfumo mzima
wa kampeni unaumiza upinzani.
Majaji,
nilizungumza na watia nia kuhusu maadili ya uchaguzi. Utafikiri wanapenda
maadili ya uchaguzi, lakini ni silaha nyingine ya kuchangia uonevu.
Wanaosimamishiwa kampeni ni wapinzani halisi.
Wale ambao
si upinzani wa kweli hawana shida nao.
Nilizungumza
juu ya masuala ya media na election. Majaji, vyombo vya habari vya nchi, vya
serikali na visivyo vya serikali, vyote vinakuwa CCM wakati wa uchaguzi.
Mwaka 2020,
ripoti ya utazamaji wa ndani wa uchaguzi ya Research for Independent Democracy
Tanzania, iliyoandikwa na Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
iliandika kitu muhimu sana, kwamba vyombo vya habari vyote wakati wa uchaguzi
ni CCM.
BBC
walilipishwa faini ya zaidi ya milioni kumi kwa kufanya interview na mimi na
TCRA. Jambo TV yenyewe imefungiwa mara nyingi sana na TCRA.
Masuala
yanayohusu siku ya uchaguzi, hilo somo nimelizungumza kwenye mihadhara mingi na
matatizo yake. Mnabadilishiwa matokeo, ukishinda kishambashamba
wanakubadilishia matokeo, ukipinga unakutana na FFU.
Hayo ndiyo
matatizo ya wagombea wa udiwani na urais niliyoyazungumza nao pale.
Nilizungumza nao kuhusu what happens baada ya uchaguzi.
Kimsingi, nilichowaambia ni kwamba mahakamani haiwezekani kwa sababu hizo
taratibu za kutengua matokeo ya uchaguzi, kwa sababu the law is designed in
such a way, ina-defend CCM.
Licha ya kuwa matatizo ya uchaguzi ni makubwa na kila mtu
anafahamu.
Nikawaambia hii ndiyo reform tunayoipigania, hii ndiyo
tunayoitaka, na hii ndiyo ya kuwahamasisha Watanzania waidai.
Lissu: Mgombea wa upinzani hashindani na wapinzani pekee
Lissu: Mama amepata asilimia 98 ya kura,
lakini swali langu ni: kura hizo zilipatikana kutoka kwa wapiga kura gani, na
kwa utaratibu gani?
Haya ni
baadhi ya masuala ambayo yamekuwa yakizungumzwa kwa muda mrefu katika ripoti
mbalimbali za waangalizi na wasimamizi wa uchaguzi.
Pia
tulizungumza na watia nia kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea na namna baadhi
yao walivyoenguliwa katika chaguzi tofauti.
Nilieleza
jinsi sheria na mamlaka za uchaguzi zinavyotumika kuwaengua wagombea wa
upinzani.
Katika
historia ya uchaguzi nchini, sijawahi kuona wagombea wa CCM wakienguliwa kwa
kiwango kinachoonekana kwa wagombea wa upinzani. Hilo ndilo lilikuwa moja ya
maeneo ya mjadala wetu kuhusu mfumo wa uchaguzi.
Nilizungumza
pia kuhusu mazingira ya kampeni za uchaguzi.
Waheshimiwa
Majaji, kwa uzoefu wetu wa kushiriki uchaguzi, mgombea wa upinzani hukutana na
changamoto nyingi wakati wa kampeni.
Mara nyingi
hulazimika kushughulika na vikwazo vinavyotokana na mamlaka mbalimbali za
serikali katika maeneo anayosafiri kufanya kampeni.
Nilieleza
kuwa, kwa mtazamo wangu, mgombea wa upinzani hukabiliana na mfumo mpana
unaojumuisha wasimamizi wa uchaguzi, vyombo vya dola na maafisa mbalimbali wa
serikali.
Changamoto
hizo, kwa mujibu wa maelezo yangu, zinaweza kuathiri usawa wa ushindani wa
kisiasa wakati wa uchaguzi.
Aidha,
nilisema kuwa mgombea wa upinzani anaposhiriki uchaguzi hukutana na ushindani
ambao hauhusishi wagombea wengine pekee, bali pia mifumo ya usimamizi wa
uchaguzi iliyopo.
Lissu: Shahidi wa mashtaka ndiye aliyechapisha video
Lissu: George Bagyemu ndiye aliyeniambia
makosa niliyokuwa nashtakiwa nayo.
Kuhusu
suala la uchapishaji, kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani, shahidi
pekee aliyekuwepo mkutanoni, aliyeyaona na kuyasikia maneno yangu moja kwa moja
ni PW17.
Mashahidi
wengine wote hawakuwepo katika mkutano huo.
PW17 ndiye
aliyeieleza mahakama kuwa alirekodi mkutano huo, akaifanyia uhariri na baadaye
akaichapisha katika mitandao ya kijamii kupitia video zilizorekodiwa kwa
kamera.
Kuhusu
uchapishaji wenyewe, PW17 alisema wazi kuwa yeye ndiye aliyefanya hatua zote za
uchapishaji. Kwa maneno mengine, he did everything, si mimi.
Alipoulizwa
nani aliyemualika, alisema aliwasiliana na Mkurugenzi wa Jambo TV, John Maro,
ambaye naye alielekezwa na afisa wa CHADEMA, Brenda Rupia.
Maelezo
hayo yote yalikuwa mikononi mwa vyombo vya uchunguzi tangu tarehe 8 Aprili.
Walikuwa
wanajua nani aliandaa mkutano na nani alichapisha maudhui yake. Hata hivyo,
wananituhumu kuandaa mkutano ambao uliandaliwa na Naibu Katibu Mkuu wa chama,
na pia wananituhumu kuchapisha maneno ambayo, kwa mujibu wa ushahidi wa shahidi
wao wenyewe, yalichapishwa na mtu mwingine.
Mwishowe
wakafungua kesi dhidi yangu, na leo nimekaa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Sasa,
nilizungumza nini katika mkutano huo?
Majaji,
katika saa hizo takribani tatu, nilizungumza na watia nia kuhusu mfumo wa
uchaguzi nchini.
Niliwaeleza
changamoto zilizopo katika Katiba ya nchi, sheria za uchaguzi na namna mfumo wa
usimamizi wa uchaguzi ulivyojengwa.
Pia
nilizungumzia muundo wa Tume ya Uchaguzi na hoja mbalimbali zinazotolewa kuhusu
uhuru wake.
Kwa mfano,
niliwatajia aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Augustino Ramadhani,
na mjadala uliowahi kuwepo kuhusu ushiriki wake katika siasa.
Aidha,
nilitoa mfano wa mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi kati ya Tanzania Bara na
Zanzibar.
Niliwaeleza
kuwa Dar es Salaam ndiyo mkoa wenye idadi kubwa ya wakazi nchini, lakini
Zanzibar ina uwakilishi mkubwa wa majimbo ukilinganisha na idadi yake ya watu.
Hoja yangu
ilikuwa kwamba mfumo wa ugawaji wa majimbo haujazingatia idadi ya watu pekee,
bali pia vigezo vingine vya kijiografia na kiutawala ambavyo vimekuwepo tangu
zamani.
Lissu: Nilivamiwa na kukamatwa nikiwa nahitimisha mkutano Songea
Chanzo cha picha, CHADEMA
Lissu: Tarehe 4 Aprili 2025, mimi na John
Heche tulianza ziara ya kusini kwa kuanzia mkoani Lindi. Akiwa huko, Askofu wa
Jimbo la Lindi alitupa nafasi ya kukutana naye na tukamueleza msimamo wetu
kuhusu ajenda ya "No Reforms, No Election." Baada ya
mazungumzo hayo alinipa rozari, ambayo bado ninaivaa hadi leo.
Baadaye
tulielekea mkoani Ruvuma. Tarehe 9 Aprili, majira ya saa kumi na mbili jioni,
nilikuwa nikihitimisha mkutano wangu wa hadhara pale Songea, ghafla polisi
walivamia mkutano huo.
Mimi na
viongozi wenzangu tulipigwa na kukamatwa, kisha nikapelekwa katika Kituo cha
Polisi Songea.
Baadaye
nilipelekwa katika ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma (RPC), Michael
Chiriwa. Wakati huo nilikuwa na njaa sana, hivyo nikaomba dada yangu aruhusiwe
kuniletea chakula. Baada ya kuwasiliana naye, alifika na chakula na nikala
nikiwa ofisini kwa RPC.
RPC Chiriwa
aliniambia kwamba ningesafirishwa kwenda Dar es Salaam usiku huo huo kwa
maagizo yaliyotoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi.
Usiku huo
nilipakiwa kwenye gari la polisi na kuanza safari ya kuelekea Dar es Salaam.
Mmoja wa maafisa aliyekuwa kwenye msafara huo alijitambulisha kwangu kama RCO
Makunja.
Tulisafiri
usiku kucha hadi Dar es Salaam, ambapo nilifikishwa mahabusu katika Gereza la
Shimoni.
Lissu: Tulizungumza hadharani, Hatukuwa na mpango wa uhaini
Chanzo cha picha, Getty Images
Lissu: Nilialikwa Chuo Kikuu cha Makerere
nchini Uganda mwezi Machi 2025 kutoa mhadhara kuhusu urithi wa Mwalimu Julius
Nyerere na nafasi yake katika Afrika Mashariki.
Katika
mhadhara huo nilizungumzia mchango wa Nyerere pamoja na changamoto za mfumo wa
uchaguzi ambazo Tanzania inaendelea kukabiliana nazo.
Baadaye
nilialikwa Luanda, Angola. Niliporejea Tanzania baada ya takribani wiki moja,
tulipanga kuanza ziara ya kitaifa kueleza msimamo wa "No Reforms, No
Election".
Ziara hiyo
ilianza tarehe 22 Machi na kuhitimishwa tarehe 31 Machi 2025, ikihusisha
mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali nchini. Tulizungumza hadharani
bila kuficha jambo lolote.
Hatukuwa na
mpango wa kufanya uhaini. Kila tulichokuwa tukifanya kilikuwa wazi kwa umma.
Nilihitimisha
ziara hiyo Iringa tarehe 31 Machi. Nikiwa huko, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA,
Amani Golugwa, alinifikishia taarifa kwamba chama kilikuwa kimeandaa kikao cha
watia nia kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.
Lengo
lilikuwa kujadili namna ya kuwapa maelekezo watia nia hao kuhusu msimamo wa
chama wa "No Reforms, No Election".
Tukakubaliana
kuwa tukirejea Dar es Salaam tarehe 3 Aprili, tungezungumza nao na kuwaeleza
msimamo rasmi wa chama.
Mimi na
John Heche tulimaliza ziara tarehe 31 Machi na kurejea Dar es Salaam tarehe 1
Aprili.
Tarehe 3
Aprili 2025 ndipo kikao hicho kilifanyika, ambacho baadaye kikawa sehemu ya
msingi wa kesi hii.
Katika
kikao hicho, mimi ndiye nilikuwa mzungumzaji mkuu kwa sababu jukumu la
Mwenyekiti wa chama ni kuelezea na kutetea misimamo ya chama.
Kikao hicho
kiliandaliwa na Sekretarieti ya chama chini ya Katibu Mkuu, si Mwenyekiti wa
chama.
Mimi
niliarifiwa tu kuwa kutakuwa na kikao hicho kupitia Naibu Katibu Mkuu. Kwa
hiyo, madai kwamba Mwenyekiti wa Taifa ndiye aliyeandaa mkutano huo yanaonesha
kutoeleweka kwa mfumo wa uendeshaji wa chama.
Majaji,
ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi 17 unaonesha kuwa mkutano huo
ulikuwa mrefu.
Mimi mwenyewe sikumbuki nilizungumza kwa muda gani. Hata video inayodaiwa kurushwa na
Jambo TV sijawahi kuitazama hadi leo.
Hata
mngeniuliza nilizungumza kwa muda gani, nisingeweza kusema kwa uhakika.
Ninachoweza kusema ni kwamba nilizungumza kwa muda mrefu sana.
Katika
ushahidi wangu, nitaeleza kwa muhtasari yale niliyoyasema ili mahakama iamue
yenyewe kama yalikuwa ya uhaini au la.
Mimi ni
mzungumzaji wa muda mrefu, jambo ambalo naamini wengi wameliona. Watu
waliouliza maswali walijibiwa, na ndiyo maana mkutano huo ulidumu kwa muda
mrefu.
Inawezekana
ulikuwa wa saa nne au tano, kwa sababu ulikuwa mrefu sana.
Kama
shahidi PW17 alivyosema, ni kweli Jambo TV walikuwepo. Tulikuwa tumefanya kazi
nao kwa muda mrefu, na pia kulikuwa na vyombo vingine vya habari.
Lissu: CHADEMA ilihamasisha ‘No Reforms, No Election’ Nchi Nzima
Chanzo cha picha, URT/Globa
Baada ya
hapo, tulianza kuandaa mkakati wa kutekeleza sera ya "No Reforms, No
Election". Tulifanya kikao Bagamoyo na kukubaliana kutumia njia
zinazotambuliwa kisheria, ikiwemo mikutano ya hadhara, kampeni za uhamasishaji,
maandamano ya amani na hatua nyingine za kidemokrasia.
Tulikubaliana
kuwa tungehamasisha wananchi kutumia haki zao za kikatiba kwa njia za amani.
Hatukupanga kutumia vurugu wala kuharibu mali za mtu yeyote.
Aidha,
tuliona ni muhimu kuzungumza na makundi mbalimbali ya Watanzania. Tulianza kwa
taasisi za kidini na kukutana na viongozi wa Kiislamu kutoka Shura ya Maimamu
na taasisi nyingine za Kiislamu.
Pia
tuliomba kukutana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) pamoja na
Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), ingawa hatukufanikiwa kufanya mikutano hiyo.
Tulikutana
pia na Jukwaa la Wahariri Tanzania pamoja na viongozi wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS) ili kuwaeleza msimamo wetu.
Kwa kuwa
Tanzania ina marafiki na washirika katika ukanda huu, tuliamua pia kuonana na
baadhi ya viongozi wa kikanda. Mimi, John Heche na Godbless Lema tulisafiri
kwenda Nairobi na kukutana na Raila Odinga.
Vilevile
tulikutana na baadhi ya wazee wa taifa, akiwemo Jaji mstaafu Joseph Warioba, na
kuzungumza naye kuhusu hoja ya "No Reforms, No Election".
Kwa ujumla,
tulifanya kila tulichoweza kuhakikisha kuwa msimamo wetu unaeleweka kwa umma
kwa njia ya wazi na ya amani.
Lissu: 'No Reforms, No Election' haikuwa kauli yangu pekee
Chanzo cha picha, AFP
Lissu: Mwezi Desemba 2024 ndipo kauli ya "No
Reforms, No Election" ilipoibuka rasmi ndani ya CHADEMA.
Tulijiuliza
tufanye nini katika mazingira hayo, na tukakubaliana kwenda kuzungumza na
Watanzania kuhusu msimamo wetu ili marafiki na wapinzani wetu wote wauelewe.
Tarehe 10
Desemba 2024, msimamo huo ulitangazwa rasmi chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa
CHADEMA wakati huo, Freeman Mbowe.
"No
Reforms, No Election" si kauli ya Lissu, bali ilikuwa msimamo wa
Mwenyekiti wa CHADEMA wakati huo, Freeman Mbowe.
Katika
vikao vya chama tulijadili namna ya kutekeleza msimamo huo. Wakati huo tulikuwa
tunakaribia uchaguzi mkuu wa chama uliopangwa kufanyika Januari 2025, hivyo
tukakubaliana kuumaliza kwanza kabla ya kuendelea na hatua nyingine.
Majaji,
tarehe 20 Januari 2025 tulifanya kikao cha Baraza Kuu la CHADEMA, ambalo
kimsingi ni chombo kikuu cha maamuzi ya chama.
Kamati Kuu
iliwasilisha mapendekezo ya kuifanya sera ya "No Reforms, No
Election" kuwa msimamo rasmi wa chama. Baraza Kuu lilikubali
mapendekezo hayo na kuyapeleka kwenye Mkutano Mkuu wa chama uliokuwa ufanyike
siku iliyofuata, tarehe 21 Januari 2025.
Tarehe 21
Januari 2025, Mkutano Mkuu ulijadili na kupitisha rasmi sera ya "No
Reforms, No Election". Wakati huo Freeman Mbowe alikuwa Mwenyekiti wa
chama, nami nilikuwa Makamu Mwenyekiti.
Katika
mkutano huo pia tulifanya uchaguzi wa viongozi wa chama kwa uwazi, huku
waangalizi mbalimbali wakialikwa kufuatilia mchakato huo. Baadaye nilichaguliwa
kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA.
Kufuatia
uchaguzi huo, nilimteua John Mnyika kuendelea kuwa Katibu Mkuu wa chama pamoja
na viongozi wengine katika nafasi mbalimbali.
Lissu: Baada ya kushambuliwa kwa risasi
wakati wa utawala wa Rais John Magufuli, nilikwenda uhamishoni. Nilinusurika
kuuawa na hatimaye nikakimbilia katika Ubalozi wa Ujerumani.
Tarehe 17 Februari 2022, Rais Samia Suluhu Hassan alipokuwa
katika ziara barani Ulaya kwa mkutano uliowakutanisha viongozi wa Umoja wa
Ulaya (EU) na Umoja wa Afrika (AU), nilipokea ujumbe kupitia watu wangu kwamba
alikuwa anataka kuonana nami.
Wakati huo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alikuwa
gerezani kwa takribani miezi sita au saba akikabiliwa na kesi ya ugaidi.
Nilipopata
ujumbe huo, nilishauriana na viongozi wenzangu. Tuliona ilikuwa ni hatua nzuri,
hivyo nikaenda kukutana naye. Aliniambia alikuwa na nia ya kuyamaliza matatizo
yaliyokuwa yamejitokeza wakati wa utawala uliopita.
Nikamwambia
aanze kwa kumwachilia Mwenyekiti wetu, Freeman Mbowe, ndipo mazungumzo mengine
yaweze kuendelea. Pia nikasema tunahitaji kuzungumzia Katiba Mpya na Tume Huru
ya Uchaguzi. Alijibu kuwa alikuwa tayari kufanya mazungumzo hayo.
Aidha,
nilimweleza kuwa mimi, Godbless Lema na wengine tulikuwa tumekimbia nchi
kutokana na hofu ya usalama wetu, hivyo tulihitaji uhakikisho kwamba ilikuwa
salama kurejea nyumbani. Baadaye, alitangaza bungeni kuwa Watanzania waliokuwa
uhamishoni warejee nchini. Mbowe naye aliachiwa huru, jambo lililotupa faraja
ya kurudi nyumbani.
Tuliporejea,
tulipendekeza kuwa watu wote waliokuwa wamefunguliwa kesi ambazo tuliamini
zilikuwa na misingi ya kisiasa wafutiwe mashtaka, na baadhi ya kesi hizo
zilifutwa.
Baadaye
yakaanza mazungumzo kati ya CHADEMA na CCM. Tulipeleka mapendekezo mbalimbali
kuhusu Katiba Mpya, muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi na ratiba ya utekelezaji wa
mageuzi hayo.
Kwa upande
wetu, tulitaka mchakato wa Katiba Mpya ukamilike kabla ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2025. Hata hivyo, tulianza kuona hakuna hatua za kutosha zilizokuwa
zinachukuliwa. Mara nyingi tuliwasilisha mapendekezo kwa maandishi lakini
majibu yalitolewa kwa njia ya mazungumzo badala ya maandishi rasmi.
Takribani
mwaka mmoja ulipita bila majibu rasmi ya maandishi kuhusu mapendekezo yetu.
Mwaka 2025,
tuliendelea kusisitiza kuwa majibu yatolewe kwa maandishi ili kuwe na uwazi
kuhusu mambo yaliyokubaliwa na yaliyokataliwa.
Tarehe 21
Mei 2025, tulipokea majibu ya maandishi yaliyokataa mapendekezo yetu yote.
Baada ya
hapo, tulikaa na kujiuliza maana ya maridhiano ikiwa hakuna makubaliano
yanayotekelezwa zaidi ya vikao vya mazungumzo. Tukafikia hitimisho kwamba ni
lazima kurejea kwa wananchi.
Tarehe 31
Mei 2025, tuliamua kama chama kuanzisha kampeni ya kuhamasisha madai ya Katiba
Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi. Tulizunguka nchi nzima kuzungumza na wananchi
kuhusu masuala hayo.
Kadiri joto
la kisiasa lilivyoongezeka, ndivyo madai ya kukamatwa kwa wanachama na viongozi
wa upinzani pamoja na kesi mbalimbali yalivyoendelea kujitokeza.
Hali hiyo iliendelea hadi uchaguzi wa serikali za mitaa na
vijiji wa Novemba 2024.
Ndani ya chama kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu kushiriki
au kutoshiriki uchaguzi huo kutokana na kutokuwepo kwa mageuzi yaliyokuwa
yanadaiwa. Hatimaye, CHADEMA iliamua kushiriki.
Lissu alidai kuwa uchaguzi huo ulisimamiwa na mfumo wa
utawala wa serikali kupitia TAMISEMI, huku watendaji mbalimbali wa uchaguzi
wakiwa ni wateule wa mamlaka ya serikali.
Pia alidai kuwa wagombea wengi wa upinzani walienguliwa
katika maeneo mbalimbali ya nchi, hali ambayo, kwa mujibu wake, iliathiri
ushindani wa kisiasa katika uchaguzi huo.
Lissu alidai kuwa wagombea wengi wa upinzani walienguliwa
katika maeneo mbalimbali ya nchi, hali ambayo, kwa mujibu wake, iliathiri
ushindani wa kisiasa katika uchaguzi huo.
Alisema waliopinga matokeo hayo walikumbana na nguvu za dola
katika maeneo mbalimbali, akidai kuwa watu kadhaa waliuawa Tarime.
Baada ya uchaguzi huo wa Novemba 28, wiki iliyofuata, tarehe
3 Desemba, Kamati Kuu ya CHADEMA ilikutana kujadili hatua za kuchukua kufuatia
yaliyotokea katika uchaguzi na mazingira ya kisiasa yaliyokuwepo nchini.
Lissu: Masuala ya uchaguzi si ya kuyachukulia kwa wepesi
Lissu: Majaji, masuala ya uchaguzi, Katiba
na uendeshaji wa nchi yasipowekwa sawa yanaweza kusababisha maafa.
Leo, mtu
anayezungumzia masuala hayo hawezi kuonekana kama chawa. Kabla ya Oktoba mwaka
jana, mtu aliyesema hivyo mara nyingi alionekana kwa mtazamo huo.
Sisi ni
Jamhuri ya Muungano, lakini wengi wetu hatufundishwi historia yake kwa kina.
Watu wengi hufahamu tu majina ya Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani
Karume bila kuelewa mazingira yaliyopelekea kuundwa kwa Muungano.
Inaitwa
Jamhuri ya Muungano kwa sababu Zanzibar ilipitia Mapinduzi ya mwaka 1964,
yaliyotanguliwa na migogoro mikubwa ya kisiasa na uchaguzi. Ushahidi wangu ni
Ripoti ya Tume ya Jaji Francis Nyalali ya mwaka 1991.
Tume hiyo
ilieleza kuwa, baada ya wananchi wa Zanzibar kuchoshwa na hali ya kisiasa ya
wakati huo, kulitokea mapinduzi yaliyoambatana na umwagaji wa damu. Kwa hiyo,
historia ya Jamhuri hii inaonesha madhara yanayoweza kutokea pale malalamiko ya
kisiasa na uchaguzi yanapopuuzwa.
Tangu
kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, tumekuwa tukishuhudia
malalamiko kuhusu uchaguzi na madai ya kutotendewa haki katika ushindani wa
kisiasa.
Ripoti za
Tume ya Nyalali, Tume ya Jaji Othman Chande pamoja na ripoti mbalimbali za
waangalizi wa uchaguzi zimeendelea kubainisha changamoto hizo kwa miaka mingi.
Madai ya
Katiba Mpya, usawa wa vyama vya siasa na kuimarishwa kwa demokrasia yamekuwa
yakijitokeza mara kwa mara katika mijadala ya kisiasa nchini.
Katika
ushahidi wangu nitaonesha jinsi tulivyojaribu, mwaka 2025, kuhimiza mabadiliko
kwa njia za amani ili kuepusha migogoro, lakini hatukusikilizwa.
Waheshimiwa
Majaji, masuala ya uchaguzi si ya kuyachukulia kwa wepesi. Mfumo wetu wa
uchaguzi una changamoto ambazo zimekuwa zikijulikana kwa miaka mingi.
Changamoto hizo zimeandikwa katika ripoti za ndani na za kimataifa, na mara
nyingi zimeambatana na onyo kwamba zisipotatuliwa zinaweza kuendelea kuleta
migogoro.
Nimesikia Mbowe yuko kwenye uzinduzi wa bwawa, wakati Mwenyekiti wake yuko Ukonga - Lissu
Chanzo cha picha, CHADEMA
Mwaka 2005, Rais Benjamin Mkapa aliondoka madarakani
na nafasi yake kuchukuliwa na Jakaya Kikwete. Miaka yake ya kwanza madarakani
ilikuwa ya vuguvugu la mageuzi ya kisiasa, Lissu amesema.
Ameendelea kusema kuwa mwaka 2010, uchaguzi ulifanyika chini ya mfumo huohuo
wa uchaguzi, na kulizuka malalamiko makubwa, hususan Zanzibar. Kelele za kudai
mabadiliko zikawa nyingi.
Alipochaguliwa kwa muhula wa pili, Kikwete alisema
kulikuwa na haja ya kupata Katiba mpya ili kushughulikia changamoto hizo.
Mwaka 2014, wakati mchakato wa Katiba Mpya ukiwa
kwenye hatua za mwisho chini ya Rasimu ya Jaji Joseph Warioba, CCM ilipinga
baadhi ya mapendekezo yake. Baadaye, Kikwete alisema masuala hayo yangejadiliwa
baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Mwaka 2015, chini ya mfumo huohuo wa uchaguzi, John
Magufuli alichaguliwa kuwa Rais akiwa na Samia Suluhu Hassan kama Makamu wa
Rais.
Majaji, nilisahau kutaja kwamba mwaka 2020 nilirudi
kutoka uhamishoni ili kushiriki uchaguzi dhidi ya Magufuli kama mgombea urais
wa CHADEMA.
Kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, baada ya matokeo
kutangazwa, Tume ya Uchaguzi huchapisha matokeo ya majimbo katika Gazeti la
Serikali. Ukiangalia chaguzi zilizopita kabla ya mwaka 2020, utaratibu huo
ulikuwa ukifuatwa.
Hata hivyo, mwaka 2020 matokeo ya urais
hayakuchapishwa. Sina uhakika kuhusu uchaguzi uliofuata kwa sababu nilikuwa
gerezani, lakini ninaamini kulikuwa na mambo mengi yasiyo ya kawaida.
Majaji, ukisoma taarifa za waangalizi wa uchaguzi wa
kimataifa pamoja na zile za Umoja wa Afrika, utaona walieleza kuwepo kwa dosari
mbalimbali katika uchaguzi huo.
Ripoti ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 2020 iliwasilishwa
kwa Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2021. Kwa mujibu wa Lissu, mijadala kuhusu
umuhimu wa mageuzi ya kisiasa na kikatiba iliendelea kujitokeza baada ya
uchaguzi huo.
Baadaye, CHADEMA ilianzisha kampeni ya kudai Katiba
Mpya. Katika kipindi hicho, Mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe, alikamatwa na
kukabiliwa na kesi ya ugaidi iliyodumu kwa miezi kadhaa kabla ya kuhitimishwa.
"Jana nimesikia Mbowe yuko kwenye uzinduzi wa
Bwawa la Mwalimu Nyerere, wakati mimi niko hapa Ukonga," alisema Lissu.
CCM imekuwa ikikataa mabadiliko ya katiba na tume huru ya uchaguzi - Lissu
Lissu: Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985 ilifanya wasimamizi wa uchaguzi watoke kwenye mfumo wa serikali za mitaa. Wote ni wateule wa Rais na wanafanya kazi kwa niaba ya Rais. Kwa hiyo, hoja yangu ni kwamba mfumo mzima wa uchaguzi unaonekana kuwa chini ya ushawishi wa CCM.
Haya yote yapo yameelezwa kwenye pendekezo la katiba ya Warioba ambayo ilifanya utafiti kwenye mfumo mzima wa uchaguzi. Matokeo ya mfumo huu yalianza kujitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa 1995.
Sasa mbali na uchaguzi, kelele za mamabdiliko zilikuwa kubwa sana na nimewambia nimefafanya utafiti wa masuala haya kwa miaka mine.
Na moja ya mapendekezo ya kuboresha yalikuwa ni kwamba yafanyike mabadiliko ya kikatiba na kuwe na tume huru ili yaliyojitokeza 1995 yasijirudie tena. Kwasbabu haya masuala ya CCM yanaweza kuleta uvunjifu wa amani.
Serikali ya rais Mkapa na CCM ikakataa. Mwaka 1998
Mkapa akaunda tume ya kuchunguza ya Jaji Kisanga na ikapendekeza kuwe na mabadiliko, Mkapa akakataa na CCM.
Mwaka 2002 maafa yakajirudia tena na wengine wakakimbilia Msumbiji na maeneo mengine.
Mkapa akaunda tume nyingine na kumuweka mtu wake amabaye mwaka 2005 uchaguzi akataka kugombea urais na wakamwambia 'ebo wewe si upo kwenye tume?'
Mfumo mzima wa uchaguzi umetengenezwa na CCM - Lissu
Chanzo cha picha, X
Lissu: Tumekuwa
tukifanya uchaguzi mkuu tangu mwaka 1957. Uchaguzi wa pili ulifanyika Agosti
1960 na ndio uliozaa Bunge la Uhuru. Tangu miaka ya 1960, Tanzania imekuwa
ikifanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano bila kukosa.
Majaji,
kabla ya mwaka 1995, kati ya mwaka 1965 na 1995, nchi ilifanya chaguzi chini ya
mfumo wa chama kimoja. Kuna vijana wengi hapa ambao huenda hawaelewi maana ya
mfumo huo. Kulikuwa na mgombea mmoja na sanduku moja la kura; wananchi walipiga
kura kwa mgombea huyo pekee.
Baada ya
marekebisho ya mwaka 1992 yaliyoruhusu mfumo wa vyama vingi, Tanzania iliingia
katika enzi mpya ya ushindani wa kisiasa. Wakati huo, Rais Ali Hassan Mwinyi
aliunda tume iliyopendekeza kuwepo kwa Katiba mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.
Hata hivyo,
Katiba iliyopo sasa ilitungwa katika mazingira ya mfumo wa chama kimoja. Kwa
mujibu wa Lissu, mapendekezo yaliyohusu Katiba mpya, Tume Huru ya Uchaguzi na
wagombea binafsi yalikataliwa na serikali ya wakati huo pamoja na chama tawala.
Amesema
marehemu Rais Mwinyi aliwahi kuandika katika kumbukumbu zake kwamba walikataa
pendekezo la Tume Huru ya Uchaguzi na wagombea binafsi kwa lengo la kuokoa
chama, hatua ambayo ilizua mvutano mkubwa kati yake na Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere.
Lissu
amedai kuwa marekebisho ya Katiba ya mwaka 1992 yaliifanya Tume ya Uchaguzi
kuwa karibu zaidi na chama tawala kuliko ilivyokuwa hapo awali. Amesema wajumbe
wa tume pamoja na wawakilishi wake waliendelea kuwa wateule wa Rais, ambaye pia
ni Mwenyekiti wa CCM.
Aidha,
amesema sheria za uchaguzi zimewaweka wasimamizi wa uchaguzi kutoka ngazi za
serikali za mitaa na majimbo kuwa watendaji wanaotokana na mfumo wa uteuzi wa
Rais.
"Kwa
hiyo, mfumo mzima wa uchaguzi ni wa CCM," alidai Lissu.
Lissu ahoji muktadha wa kauli zinazounda shtaka la uhaini
Majaji, kwa mtazamo wangu, kesi hii inahusu uchaguzi.
Hati ya mashtaka iliyopo mahakamani inanishtumu kuwa nilikuwa na nia ya
kuhamasisha watu kuitishia serikali kwa kuwachochea kuvuruga uchaguzi.
Maneno ninayodaiwa kuyasema yanahusu uchaguzi.
Mashahidi wote 17 wa upande wa mashtaka wametoa ushahidi wao kwa kurejea kauli
zangu zinazodaiwa kutolewa kuhusu uchaguzi.
Nyaraka za ushahidi kuanzia B1 hadi D16 pia
zinahusu uchaguzi. Hakuna nyaraka hata moja ambayo haizungumzii suala la
uchaguzi.
Kwa hiyo, Majaji, katika sehemu hii ya ushahidi wangu,
naomba nizungumzie uchaguzi.
Mashahidi PW1, PW2, PW3, na kwa kiwango fulani PW16
na PW17, waliieleza mahakama kwamba kauli ninayodaiwa kuitoa na
iliyochapishwa kupitia Jambo TV kwenye YouTube ilikuwa sehemu ya video
yenye urefu wa takribani saa tatu.
PW16 na PW17 walisema video hiyo ilikuwa na urefu wa
takribani saa mbili na zaidi. Hata hivyo, kwa ujumla wao wote walikubaliana
kwamba video hiyo ilikuwa ndefu.
Kauli zinazodaiwa kuunda msingi wa shtaka la uhaini
hazifikii hata dakika moja. Swali langu ni kuwa, katika muda wote uliobaki wa
takribani saa tatu, nilizungumza nini?
Katika sehemu hii ya ushahidi wangu, nataka kueleza
mantiki na muktadha wa kauli nilizozungumza katika kipindi hicho mwaka jana.
Upande wa Serikali:
"Sasa ushahidi unaotolewa unatoka nje ya mawanda ya kesi, kwa sababu
shahidi analeta masuala yasiyohusiana moja kwa moja na shauri hili. Hii si
sehemu sahihi ya kuyajadili.
Haya masuala ya watu kufa anaweza kuyazungumzia,
lakini yanahusiana vipi na kesi iliyopo mbele ya mahakama? Kwa hiyo, naomba
majaji, kama inawezekana, wamuelekeze shahidi asitutoe nje ya reli. Hivyo
ndivyo sheria inavyotaka."
Lissu:
"Majaji, msingi wa utetezi wangu ni kwamba baadhi ya kesi hizi
zimetengenezwa, na hiyo ni sehemu ya tabia ya polisi na waendesha mashtaka.
Kesi yangu ni uthibitisho kwamba mamlaka yanaweza
kutumika vibaya. Sizungumzi mambo haya ili mahakama inionee huruma, bali
kuonyesha kwamba kuna tatizo ambalo linahusiana na ushahidi wangu.
Kusema kwamba tunaweza kutumia wiki mbili kunanitia
wasiwasi, kwa sababu wao wamekuwa na mwaka mmoja na miezi kadhaa kuwasilisha
upande wao. Leo ninapotaka kutumia muda kujitetea, wanaeleza kuwa napoteza
muda. Sipotezi muda, najitetea. Wana wasiwasi gani?"
Hii ni mara yangu ya nne kukamatwa chini ya Samia, Lissu amesema
Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA
Kuhusu kesi hii, nilikamatwa tarehe 9 Aprili 2025 na
kufikishwa mahakamani siku iliyofuata. Hii ni mara yangu ya nne kukamatwa chini
ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na polisi wake.
Safari hii nimefunguliwa kesi ya uhaini. Kufikia sasa,
tayari nimekaa gerezani kwa miezi 16 na ninaelekea kutimiza mwezi wa 17, sawa
na zaidi ya mwaka mmoja na miezi minne.
Majaji, hiki ni kipindi kirefu zaidi kuwahi kukaa
gerezani katika maisha yangu. Pia ni kipindi kirefu zaidi kwa kiongozi wa
CHADEMA kushikiliwa gerezani.
Aidha, hii ndiyo kesi kubwa zaidi kuwahi kufunguliwa
dhidi ya kiongozi wa upinzani tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini
takriban miaka 35 iliyopita. Hakuna kiongozi mwingine aliyewahi kufunguliwa
kesi ya aina hii.
Haya yote yamenitokea mimi binafsi. Ninaamini hakuna
kiongozi mwingine wa ngazi ya juu wa CHADEMA aliyepitia mateso na changamoto
nyingi kama nilizopitia.
Nina bahati kwamba, licha ya kujeruhiwa na kubaki na
ulemavu wa kutembea kwa kuchechemea, bado niko hai. Wapo wengi tuliowahi
kufanya kazi pamoja katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ambao wengine
wameuawa na wengine hadi leo hawajulikani walipo.
Kama chama, tumepitia nyakati ngumu sana. Tumebeba
maumivu makubwa na tumekumbwa na mateso mengi. Mimi binafsi nimefunguliwa kesi
mbalimbali ambazo naamini ni za uongo, zikihusisha polisi na mawakili wa
serikali.
Kesi hii si ya polisi pekee, bali inahusisha pia
waendesha mashtaka wa serikali. Katika miaka miwili au mitatu iliyopita,
tumezika viongozi wengi wa chama.
Tumepitia maumivu makubwa sana, na mimi binafsi
nimeumizwa sana.
Lissu: Mwaka 2024 ulikuwa mgumu kwa viongozi wa CHADEMA
Chanzo cha picha, bbc
Mwezi uliofuata September 7 mkesha wake Mkurugenzi wa Hamasa CHADEMA makao makuu, Ally Kibao akatekwa kwenye busi akiwa anakwenda Tanga, akiwa Tegeta alishushwa kwa nguvu.
Ukiangalia unaona kabisa ni police kulingana na magari yao, ni polisi ambao ni usalama wa taifa. Kesho yake mzee Kibao akaokotwa akiwa ameuawa maeneo ya ufukweni Ununio, inaelekea aliteswa vibaya sana.
Majaji wakati marehemu Kibao anatekwa nyara na kuuawa kulikuwa na matukio mengi ya viongozi wa CHADEMA kutekwa na kuawa kilikuwa kipindi kigumu sana 2024.
Katika kupinga hayo yote chama kilisema kitaandamana tarehe 23 September. Ilipotika asubuhi nikavamiwa na jeshi la polisi mapema asubuhi nyumabani kwangu nikakamatwa. Nikawekwa kituo cha polisi Mbweni.
Nikakaa Mbweni mpaka usiku, kisha wakanirudisha nyumbani kwangu hawakunifungulia mashtaka.
Majaji, nakumbuka nilisema nilikamatwa Karatu ili nisiende kuonana na wananchi wa Ngorongoro hiyo ilikuwa Machi 2023. Nilienda kuwekwa kituo cha polisi cha Wilaya ya Monduli waheshimiwa majaji, ili tu kuniharibia mipango yangu
Siku niliyoshambuliwa, walinzi wote hawakuwepo na
mageti yalikuwa wazi. Nikiwa kwenye eneo la maegesho ya magari, nilipigwa
risasi 16, hali iliyosababisha kufanyiwa operesheni 26. Hadi leo, bado nina
risasi moja mwilini, karibu na uti wa mgongo.
Hakuna mtu aliyekamatwa wala kutuhumiwa kuhusika na
tukio hilo. Aidha, sijawahi kuitwa na polisi kueleza kilichotokea siku hiyo.
Sidhani hata kama polisi walifungua jalada la uchunguzi (RB).
Majaji, sikufa. Mungu si Athumani. Sikufa. Badala
yake, Magufuli alifariki dunia. Baada ya kifo chake, kesi sita zilizokuwa
zimefunguliwa dhidi yangu katika Mahakama ya Kisutu zilifutwa mwezi Septemba
2021.
Baadaye, Rais Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani
na kuja na agenda ya 4R.
Katika kutekeleza agenda hiyo, tarehe 12 Agosti 2024
niliitwa, kwa nafasi yangu ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, kushiriki pamoja na
Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) katika maadhimisho ya Siku ya Vijana
Duniani.
Jeshi la Polisi lilipiga marufuku maadhimisho ya
CHADEMA, lakini ya CCM yaliendelea kufanyika. Nikasema Jeshi la Polisi halina
mamlaka ya kuzuia shughuli hizo na kwamba jukumu lake ni kulinda raia.
Tarehe 12 Agosti 2024 nilisafiri kwa ndege kwenda
Mbeya. Nilipowasili, ilikuwa tayari jioni, ndipo nikaelekea katika ofisi za
chama ngazi ya kanda.
Majaji, siku hiyo nilivamiwa na polisi wakiongozwa na
Mkuu wa Operesheni, Awadh Juma. Mimi na viongozi wenzangu tulipigwa na baadaye
kukamatwa. Baadaye nilipelekwa mkoani Songwe na kuwekwa mahabusu huko.
Siku iliyofuata mchana, nilisafirishwa kwa gari
kurudishwa Dar es Salaam.
Nilipofikishwa Dar es Salaam, nilikabidhiwa kwa polisi
wa Kituo Kikuu cha Polisi (Central) na askari kutoka Songwe na Mbeya.
Nilipowauliza kosa langu ni lipi, waliniambia walikuwa wakinipeleka nyumbani.
Sikufunguliwa mashtaka yoyote. Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kukamatwa
chini ya utawala wa Rais Samia.
Tarehe 29
Julai, nilikamatwa kwa kosa la kumuita Rais Magufuli "dikteta
uchwara", siku tatu baada ya kuachiliwa. Nikasafirishwa usiku na kulazwa
Kituo cha Polisi Chamwino, ambako kulikuwa na mbu wengi. Baadaye nikaletwa Dar
es Salaam na kushtakiwa kwa uchochezi.
Septemba
mwaka huo, nilikamatwa tena na kuletwa Dar es Salaam. Kufikia mwisho wa mwaka
2016, nilikuwa nimekamatwa mara nne na polisi wa Magufuli, huku kesi zote
zikisikilizwa katika Mahakama ya Kisutu.
Kesi ya nne
ilifunguliwa mwezi Desemba mwaka huo huo.
Majaji,
mwaka 2017 nilikamatwa tena Dodoma mwezi Februari. Mwezi Aprili kulikuwa na
uchaguzi wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Wanachama
walinitaka nigombee. Siku tatu au nne kabla ya uchaguzi, nilikamatwa na
kupelekwa Segerea, ambako nilikaa kwa siku nne.
Siku ya
Ijumaa nikapelekwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Hakimu alisema kesi
hiyo ilikuwa na dhamana na akaniruhusu kwenda kugombea urais wa TLS.
Baada ya
uchaguzi wa TLS, nilikamatwa tena mara mbili, mwezi Juni na Agosti. Katika moja
ya matukio hayo, nilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupimwa mkojo kwa
tuhuma za uchochezi, ingawa hadi leo sijui jambo hilo lilihusiana na nini.
Lissu: Polisi walitaka kuvunja chumba cha maiti na kuchukua miili
Chanzo cha picha, mtandao
Mwaka 2005,
Jakaya Kikwete aliingia madarakani.
Mwezi Julai
2011, polisi walifanya mauaji katika Mgodi wa North Mara, Nyamongo. Wananchi wa
Nyamongo walinipigia simu wakiniomba niende kuwasaidia kwa sababu polisi
walikuwa wanawalazimisha kuzika miili ya waliouawa. Nikasafiri kwenda huko na
kudai uchunguzi ufanyike kuhusu mauaji hayo.
Nilipofika
Tarime, nilipata taarifa kuwa polisi walitaka kuvunja milango ya chumba cha
kuhifadhia maiti ili wachukue miili. Tulikesha nje ya chumba hicho, na ndipo
nilipopigwa sana na kujeruhiwa vibaya.
Baada ya
hapo, nilipewa kesi yangu ya pili ya jinai, ambayo nayo ushahidi wake ulikuwa
wa mashaka.
Mwaka
uliofuata, 2012, polisi waliua wananchi kadhaa wakati wa maandamano mjini
Arusha. Sheria za nchi hii zinaruhusu maandamano, lakini watu waliuawa.
Tukaenda kusisitiza haki itendeke, ndipo mimi na wabunge wenzangu, akiwemo Dk.
Slaa, tukakamatwa.
Baadaye,
Rais John Pombe Magufuli aliingia madarakani, na kisha Samia Suluhu Hassan.
Mwaka 2015,
wakati wa uchaguzi mkuu Zanzibar, Seif Sharif Hamad alitangazwa kuwa ameshinda,
lakini matokeo yakafutwa.
Ilipotangazwa
kuwa uchaguzi wa marudio ungefanyika mwaka 2016, waandishi wa habari
waliniuliza maoni yangu. Nikasema kuwa walikuwa wanataka kuleta maafa. Tarehe
26 Juni 2016, nilikamatwa kwa mashtaka ya uchochezi na kupelekwa mahakamani,
lakini mashahidi hawakuletwa tena.
Hata baada
ya kupigwa risasi, mashahidi hawakuwahi kuletwa mahakamani.