Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Amnesty: Mwaka mmoja baadaye, hakuna aliyewajibishwa kwa mauaji ya waandamanaji Tanzania

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema mamlaka nchini Tanzania zimeshindwa kuwawajibisha waliohusika na vifo vya mamia ya watu waliouawa na vyombo vya usalama wakati wa kukandamiza maandamano yaliyofuata uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Beldeen Waliaula

  1. Mgombea urais wa Brazil Flavio Bolsonaro awasili Marekani

    Flávio Bolsonaro amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Biashara wa Opa-locka, Miami,Florida, siku moja baada ya mamlaka nchini Brazil kufuta pasipoti yake.

    Mwanasiasa huyo amewasili nchini Marekani baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika siku ya Jumapili nchini Brazil, ambapo alishindwa na Rais Luiz Inácio Lula da Silva.

    Hapo jana , afisa mwandamizi wa Marekani alithibitisha kuwa Wizara ya Mambo ya Kigeni ya nchi hiyo ingewapatia Bolsonaro na familia yake viza na kuwaruhusu kuingia nchini humo iwapo wangeziomba.

    Soma pia:

  2. Real Madrid yaiomba China msamaha baada ya matamshi ya Mbappe

    Klabu ya soka ya Real Madrid imeomba radhi, baada ya mshambuliaji wake kutoka Ufaransa, Kylian Mbappe, kuzua ghadhabu baada ya kumtaja kiongozi wa zamani wa China, Mao Zedong, kuwa dikteta.

    Ombi la msamaha alilolitoa Mbappe pamoja na ule wa ligi kuu ya soka ya Uhispania, LaLiga, hazikuweza kutuliza hasira za watu nchini China.

    Hali hiyo imemfanya rais wa LaLiga, Javier Tebas, kuunda kikosi maalumu cha kushughulikia mgogoro huo na kukutana na balozi wa China, Yao Jing.

    Katika taarifa yake, Real Madrid imesema,"Klabu ya Real Madrid inawaomba radhi raia wa China kwa kero lililosababishwa na matamshi ya hivi karibuni ya mchezaji wetu Kylian Mbappe."

    "Klabu yetu inaiheshimu China, historia yake, utamaduni wake na wananchi wake, pamoja na mamilioni ya mashabiki wa China wanaoipenda na kuikubali Real Madrid," taarifa hiyo ilisema.

    Kituo cha habari kinachomilikiwa na serikali ya China, Migu, hakitapeperusha mechi ya LaLiga kati ya Real Madrid na Racing Santander itakayochezwa siku ya Jumapili.

    Wakati huohuo, kampuni kadhaa za China zimesitisha ushirikiano wao na Mbappe.

    Soma pia:

  3. Tanzania yaadhimisha ugunduzi wa gesi asilia baada ya muongo mmoja

    Tanzania imetangaza ugunduzi mkubwa wa gesi asilia katika eneo la Mnazi Bay, kusini mwa nchi hiyo, ikiwa ni mara ya kwanza kupata ugunduzi wa aina hiyo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

    Waziri wa Nishati, Juma Homera, alihudhuria hafla ya uzinduzi wa gesi hiyo katika kisima cha Kasa-1X ST2.

    Kisima hicho kinamilikiwa kwa pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), linalomilikiwa na serikali, pamoja na kampuni ya mafuta ya Ufaransa ya Maurel & Prom.

    Homera alisema kuwa ugunduzi huo, unaokadiriwa kuwa na futi bilioni 6.3, ni hatua muhimu katika maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi ambayo bado inakuwa nchini humo.

    Kisima hicho kipya kinatarajiwa kuanza uzalishaji mapema mwezi ujao, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa gesi asilia kwa matumizi ya ndani ya nchi.

    Soma pia:

  4. Zaidi ya 80% ya kura zahesabiwa, Netanyahu bado anaongoza

    Zaidi ya asilimia 80 ya kura katika uchaguzi wa Israel zimehesabiwa, huku matokeo ya awali yakimuweka Benjamin Netanyahu mbele ya wapinzani wake. Hata hivyo, hakuna muungano wowote uliopata idadi ya viti vinavyohitajika kuunda serikali ya wengi.

    Kwa mujibu wa Tume Kuu ya Uchaguzi ya Israel, muungano wa Netanyahu unaongoza ukiwa na viti 54, licha ya kupoteza baadhi ya viti kadri hesabu inavyoendelea.

    Upande wa mpinzani wake, Gadi Eisenkot, umeimarika na kufikia viti 47, wakati vyama vya Arab List vimeongeza uwakilishi wao hadi viti 19.

    Ili kuunda serikali katika Bunge la Israel (Knesset), muungano wowote unahitaji angalau viti 61. Hali hiyo inaashiria kuwa mazungumzo ya kutafuta washirika wa kisiasa yataendelea kuwa muhimu kabla ya serikali mpya kuundwa.

    Soma Pia:

  5. Ajali ya treni yaua watu 64 Uhispania

    Treni mbili zimegongana nchini Uhispania na kusababisha vifo vya watu takriban 64, ingawa kuna hofu kuwa idadi halisi ya waliofariki inaweza kuwa kubwa zaidi.

    Ajali hiyo imetokea karibu na mji wa Urda, takriban kilomita 140 kusini mwa Madrid.

    Huduma za dharura ziko katika eneo la tukio kuwasaidia waliojeruhiwa na kuwatafuta manusura.

    Ajali hiyo ilitokea wakati treni ya mwendo kasi iliyokuwa ikisafiri kutoka Madrid kuelekea kusini mwa nchi hiyo ilipogongana na treni nyingine ambayo ilikuwa imesimama. Mgongano huo ulisababisha angalau mabehewa mawili kutumbukia chini ya mteremko.

    Wazima moto, wahudumu wa afya na maafisa wengine wa uokoaji wako katika eneo la tukio, huku helikopta tatu pia zikitumika katika shughuli za uokoaji.

    Kulingana na taarifa, serikali inaamini kuwa hitilafu za kibinadamu zinazohusiana na mfumo wa kutoa ishara za reli huenda ndizo zilizosababisha ajali hiyo.

    Kampuni ya kitaifa ya reli ya Renfe limetoa nambari maalumu ya simu kwa ajili ya ndugu wa watu waliokuwa ndani ya treni hizo kupata taarifa.

    Bunge la Uhispania limehairisha shughuli zake zote zilizopangwa kufanyika sikuya leo.

    Waziri Mkuu Pedro Sánchez aliandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba amesikitishwa na habari hizo, na kutoa pole pamoja na kuahidi mshikamano na msaada kwa waliojeruhiwa na familia zao.

    Mwezi Januari, ajali iliyohusisha treni mbili katika njia hiyo hiyo ilisababisha vifo vya watu 46.

  6. Kesi ya mwanajeshi wa Uingereza anayedaiwa kumuua Mkenya yaahirishwa hadi 2027

    Familia ya mwanamke kutoka Kenya anayedaiwa kuuawa na mwanajeshi wa Uingereza miaka 14 iliyopita, imeelezea kutoridhishwa kwao, baada ya kesi ya kurejeshwa kwa mshukiwa nchini Kenya kuahirishwa hadi mwezi Mei 2027.

    Ndugu wa Agnes Wanjiru, ambaye mwili wake ulipatikana ndani ya tenki la maji taka karibu na kambi ya mafunzo ya jeshi la Uingereza nchini Kenya mwaka wa 2012, wamesema kucheleweshwa kwa kesi hiyo ‘hakukubaliki kabisa’. Pia wameishutumu mamlaka kwa kushindwa kuwapa taarifa kuhusu kesi hiyo inavyoendelea.

    Kikao cha kusikiliza kesi ya Robert James Purkiss, aliyekuwa mwanajeshi wa Uingereza anayeshukiwa kumuua Wanjiru, mwenye umri wa miaka 21 na mama wa mtoto mmoja, ilikuwa imeratibiwa kufanyika mwezi ujao. Hata hivyo, familia hiyo imesema kikao hicho sasa kimeahirishwa hadi Mei 2027.

    Purkiss alikamatwa nchini Uingereza mwezi Novemba mwaka uliopita na anapinga hatua ya kurejeshwa nchini Kenya kukabiliana na kesi ya mauaji na pia amekanusha tuhuma hizo.

    Mpwa wa Wanjiru, Esther Njoki, aliiambia BBC kuwa familia ilipata taarifa kuhusu kuahirishwa kwa kesi hiyo kupitia ubalozi wa Uingereza na kwamba haikuwa imepokea maelezo rasmi kuhusu sababu za uamuzi huo.

    "Tumekuwa wavumilivu na kuvumilia hali ya kutokuwa na uhakika kwa miaka mingi, lakini sasa uvumilivu wetu unatumika vibaya," alisema katika taarifa.

    "Agnes anastahili haki. Binti yake Stacy anastahili kupata majibu kuhusu kilichotokea. Na sisi kama familia, tunastahili heshima na kupewa taarifa kuhusu mwenendo wa kesi zinazogusa maisha yetu kwa kiasi kikubwa."

    Familia hiyo imesema ilikuwa tayari imechangisha fedha na kufanya mipango ya kusafiri hadi Uingereza kuhudhuria kikao hicho, ambacho kilitarajiwa kufanyika baada ya wiki tatu.

    Wanjiru alitoweka mwezi Machi mwaka wa 2012.

    Mwili wake ulipatikana karibu miezi mitatu baadaye ndani ya tenki la maji taka katika hoteli moja alikokuwa ameenda kukutana na mwanajeshi wa Uingereza. Alikuwa na majeraha ya kuchomwa kisu kifuani na tumboni, na aliacha mtoto wa kike aliyekuwa na umri wa miezi mitano.

  7. Amnesty: Mwaka mmoja baadaye, hakuna aliyewajibishwa kwa mauaji ya waandamanaji Tanzania

    Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeishutumu serikali ya Tanzania kwa kushindwa kuwawajibisha waliohusika na vifo vya waandamanaji wakati wa ukandamizaji wa maandamano yaliyofuata uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

    Katika taarifa ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu ghasia hizo za Oktoba 29, Amnesty imesema mamia ya watu waliuawa na maelfu kujeruhiwa, lakini hakuna afisa aliyefunguliwa uchunguzi wa jinai, kushtakiwa au kuadhibiwa kwa matumizi ya nguvu kupita kiasi.

    Hata hivyo, serikali imekanusha kuwalenga raia wasio na hatia, ikiwalaumu watu na makundi ndani na nje ya nchi kwa kuchochea vurugu. Rais Samia Suluhu Hassan ameunda tume mbili za uchunguzi. Tume ya kwanza iliwasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026, ikibaini kuwa watu wasiopungua 518 waliuawa na maelfu kujeruhiwa. Tume ya pili, iliyoanzishwa Agosti 7, imepewa miezi mitano kuchunguza waliohusika na kubaini wanaopaswa kuwajibishwa.

    Amnesty imesema ripoti ya tume ya kwanza bado haijawekwa wazi kwa umma, jambo linaloendeleza usiri na utamaduni wa kutowawajibisha waliohusika na ukiukaji wa haki za binadamu.

    Mkurugenzi wa Amnesty International kwa Afrika Mashariki na Kusini, Tigere Chagutah, amesema mamlaka zinazidi kutumia sheria za kupambana na ugaidi kuwanyamazisha wakosoaji na kuwatia hofu wananchi.

    Madai ya utekaji na mateso

    Amnesty imesema imeandika visa vya watu waliotekwa na watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa usalama, kuzuiliwa bila mawasiliano na familia au mawakili, na wengine kutofahamika waliko.

    Miongoni mwao ni Ibrahim Myovella, kiongozi wa vijana wa CHADEMA, aliyepotea pamoja na marafiki zake wawili Aprili 18, 2026, baada ya kuripoti katika kituo cha polisi cha Iringa Kati kwa masharti ya dhamana. Mamlaka zimekanusha kuwashikilia.

    Amnesty pia imesema watu 130 walikamatwa Julai 2026 kwa madai ya kupanga mikutano na kuchochea vitendo vya uhalifu. Angalau 64 walishtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi. Shirika hilo limetaja pia madai ya wanafunzi na wanachama wa CHADEMA kupigwa na kunyimwa fursa ya kuonana na mawakili.

    Limetaka mamlaka kusitisha matumizi ya sheria za ugaidi kukandamiza uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani, na kuondoa mashtaka dhidi ya wanaozuiliwa kinyume cha sheria.

    Uhuru wa vyombo vya habari

    Amnesty imesema mamlaka zimezuia upatikanaji wa majukwaa ya mitandao ya kijamii, yakiwemo X na Clubhouse, huku marufuku ya mikutano ya kisiasa na mikusanyiko ya watu wengi ikitangazwa Juni 26, 2026.

    Pia imetaja kusimamishwa kwa leseni ya matangazo ya mtandaoni ya Jambo Online TV kwa siku 90 mwezi Aprili na agizo la Jaji Mkuu la Februari lililowazuia mawakili kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu kesi zilizo mahakamani.

    Chagutah ameitaka serikali kurejesha leseni ya Mwanahalisi, kuruhusu majukwaa yaliyopigwa marufuku na kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi bila vitisho.

    Amnesty imesema serikali haikujibu ombi lake la kutoa maoni kuhusu madai hayo.

    Soma Pia:

  8. Trump adai kumpigia upatu Netanyahu kulibadili mwelekeo wa uchaguzi

    Rais wa Marekani Donald Trump anadai kuwa uungwaji mkono wake ulimsaidia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kugeuza kushindwa vibaya katika uchaguzi na kuwa uwezekano wa matokeo yasiyo na mshindi wa wazi au ushindi.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, Trump alisema mabadiliko hayo yalitokea baada ya yeye kumuunga mkono Netanyahu.

    “Yote haya yalitokea baada ya Rais Trump kutoa uungwaji mkono wake, ambaye anataka tu mema kwa Mashariki ya Kati, Israel na Marekani!” aliandika Trump.

    Haya yanajiri, baada ya matokeo ya awali ya uchaguzi wa Israel kuonyesha hakuna mshindi wa wazi.

  9. Trump adai udanganyifu wa kura ni mkubwa Marekani, lakini ushahidi unaonyesha ni nadra

    Rais Donald Trump ametoa zawadi ya dola milioni moja kwa yeyote atakayetoa taarifa kuhusu udanganyifu wa uchaguzi nchini Marekani, itakayowezesha wahusika kutiwa hatiani.

    Kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula wa urais unaotarajiwa kufanyika Novemba 3, Trump amekuwa akitilia shaka usalama wa uchaguzi, akidai kuwa kuna udanganyifu mkubwa katika upigaji kura kwa njia ya posta na madai ya raia wasio Wamarekani kushiriki kupiga kura.

    Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kuwa visa vya udanganyifu wa aina hiyo ni nadra sana.

    BBC Verify imechunguza ushahidi uliopo pamoja na mapendekezo ya Trump ya kubadilisha mfumo wa upigaji kura.

    Kwa miaka kadhaa, Trump amekuwa akidai bila kutoa ushahidi wa kutosha kwamba upigaji kura kwa njia ya posta unasababisha udanganyifu mkubwa. Hata hivyo, amewahimiza pia Warepublican kutumia njia hiyo kupiga kura katika uchaguzi wa katikati ya muhula, na amewahi kusema kuwa yeye mwenyewe alipiga kura kwa njia ya posta.

    Rais huyo ameshindwa kufanikisha juhudi zake za kuishawishi Bunge la Marekani kupitisha sheria ambayo ingeruhusu upigaji kura kwa njia ya posta kwa watu wenye ulemavu, wagonjwa, wanajeshi walioko kazini au watu wanaosafiri pekee.

    Utafiti uliochunguza chaguzi kadhaa nchini Marekani unaonyesha kuwa udanganyifu katika upigaji kura kwa njia ya posta umetokea kwa kiwango kidogo sana.

    Taasisi ya utafiti wa sera ya Brookings ilichunguza chaguzi za mwaka 2016, 2018, 2020 na 2022 na kubaini wastani wa visa vinne hivi vya udanganyifu kwa kila kura milioni 10 zilizopigwa kwa njia ya posta.

    Ikulu ya Marekani imetaja kisa cha jimbo la New Jersey, ambako hitilafu ya mfumo wa idara ya leseni za udereva ilisababisha takribani watu 6,600 wasio raia wa Marekani kusajiliwa kupiga kura kati ya Juni 2023 na Juni 2024. Maafisa wa jimbo hilo wamesema kuwa chini ya watu 400 kati yao walipiga kura, na majina yao yote yameondolewa kwenye mfumo.

    Wizara ya Sheria ya Marekani pia iliitaka California kutohesabu kura 20,000 zilizopigwa kwa njia ya posta kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula, ikidai kuwa huenda wapiga kura hao walikuwa watu wasio raia waliokuwa wamesajiliwa. Hata hivyo, mahakama ya rufaa ilikataa ombi hilo.

    Kati ya watu wanaohusishwa na kura hizo, Wizara ya Sheria imetangaza mashtaka dhidi ya watu 28 wa kigeni, ikidai kuwa walijisajili kinyume cha sheria ili kupiga kura.

    Soma pia:

  10. Tshisekedi amshutumu Kabila kwa kugeuka dhidi ya wananchi aliowaongoza

    “Sie­lewi jinsi mtu aliyewahi kuongoza nchi yenye mamilioni ya wananchi anavyoweza kutawaliwa na hasira, kushindwa kujizuia, kuchukua silaha na kuzitumia dhidi ya watu aliowaongoza kwa miaka 18.”

    Hayo ni maneno ya Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, akimzungumzia mtangulizi wake, Joseph Kabila, ambaye hivi karibuni alitangaza kuongoza muungano mpya wa kisiasa na kijeshi ulioundwa mapema mwezi huu kwa lengo la kupambana na serikali ya Kinshasa, ukichukua nafasi ya AFC/M23.

    Akizungumza na wabunge wa chama chake tawala mwishoni mwa wiki iliyopita, Tshisekedi alisema hakushangazwa na uamuzi wa Kabila kuvunja ukimya wake, lakini akadai kuwa Rwanda inamtumia.

    Tangu kutangazwa rasmi kwa muungano huo mpya, hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa DRC kutoa kauli hadharani kuhusu kuundwa kwake au kuhusu Joseph Kabila.

    Serikali ya Rwanda haijatoa maoni kuhusu matamshi hayo ya Tshisekedi.

    BBC ilimtafuta Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, ili kupata maoni yake. Katika ujumbe mfupi wa maandishi, alijibu: “Hatujawahi kuwa tukijibu kila anachosema Tshisekedi kuhusu Rwanda.”

    Katika hotuba yake, Tshisekedi aliishutumu Rwanda na Rais wake, Paul Kagame, kwa kuhusika katika vita vinavyoendelea mashariki mwa DRC. Pia alidai kuwa Rwanda inamtumia Kabila katika juhudi zake za kuendeleza mzozo huo.

    Kwa mujibu wa Tshisekedi, kuundwa kwa vuguvugu la FRN ni njama ya Rwanda ya kuushawishi jumuiya ya kimataifa iamini kuwa mzozo huo ni suala la ndani la Wakongo, badala ya kutambua nafasi ya Rwanda katika mgogoro huo.

    Alisema hatua za kidiplomasia zilizochukuliwa na serikali yake zimeisaidia kuonyesha kuwa Rwanda inaikandamiza DRC, hali ambayo, kwa madai yake, imesababisha nchi hiyo kukabiliwa na vikwazo.

    Tshisekedi alisema:

    “Ndiyo maana ilimwomba mfanyakazi wake aliyekuwa gerezani atoke nje na kuchukua jukumu la uhalifu huu, kwa sababu ilikuwa muhimu kuleta taswira kwamba hili ni suala la Wakongo wenyewe.”

    “Kwa hiyo, ilimbidi atoke mafichoni na kuchukua mambo mikononi mwake, ili kuonyesha kuwa huu ni mzozo kati ya Wakongo wenyewe. Namshukuru Mungu, hakuna asiyejua ukweli huo.”

    Alisema kilichomvutia zaidi ni namna wananchi walivyoungana kupinga hatua hizo.

    “Kilichonivutia zaidi ni kuona wananchi wetu, wanasiasa na raia wa kawaida, wakiungana kulaani vitendo hivi.”

    Tshisekedi anaamini kuwa Kabila amewasaliti wananchi na nchi aliyowahi kuiongoza. Kwa maoni yake, hatua hiyo inaonyesha kuwa katika miaka 18 aliyokuwa madarakani, Kabila hakuwahi kuonyesha mapenzi ya dhati kwa nchi na wananchi wake.

    Aliongeza:

    “Kwa sababu ikiwa unaipenda nchi yako na wananchi wake, huwezi kufanya mambo kama haya. Nilitoa mfano wa maisha yangu mwenyewe, kwa kuwa nami nimepitia hali kama hizo. Tulipopambana na makundi mbalimbali yenye silaha yaliyokuwepo nchini humu, hatukuwahi kufikiria kuchukua silaha ili kupigania nchi yetu.”

    Tarehe 12 Oktoba, kuundwa kwa FRN kulitangazwa rasmi chini ya uongozi wa Joseph Kabila. Muungano huo ulisema unalenga kuunganisha kile unachokiita “vikosi vya upinzani” ili kukomesha utawala unaodai kuwa wa kidikteta na kuweka mwelekeo mpya wa kisiasa nchini humo.

    Kabla ya Tshisekedi kutoa kauli yake kuhusu Kabila na FRN, serikali yake haikuwa imetangaza hadharani msimamo wake kuhusu muungano huo. Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wanaoshirikiana na serikali walikuwa wameikosoa hatua ya Kabila kuongoza kundi hilo lililochukua nafasi ya AFC/M23.

    Ubelgiji, iliyokuwa mtawala wa kikoloni wa DRC, pia imekosoa kuundwa kwa muungano huo.

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Maxime Prévot, alisema ni “jambo la kusikitisha sana” kuona kiongozi wa zamani wa nchi aliyewahi kukabiliwa na madhara ya makundi yenye silaha akiamua kuongoza muungano wa kisiasa na kijeshi unaolenga kutwaa madaraka kwa kutumia nguvu.

    Soma Zaidi:

  11. Likud ya Netanyahu yaongoza kwa asilimia 25 ya kura zilizohesabiwa

    Tume Kuu ya Uchaguzi ya Israel imesema zaidi ya kura milioni 1.6 zimehesabiwa katika uchaguzi wa bunge nchini humo.

    Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizosasishwa saa 4:47 asubuhi kwa saa za nchini Israel, chama cha Likud kinachoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kinaongoza kwa kupata asilimia 24.22 ya kura zilizohesabiwa.

    Chama cha Yashar kinachoongozwa na Gadi Eisenkot kinafuata, kikiwa na asilimia 41.15 ya kura, huku Muungano wa Pamoja (Joint List), unaojumuisha Waarabu na Wayahudi, ukiwa nafasi ya tatu kwa asilimia 28.8.

    Chama cha Yisrael Beitenu kinachoongozwa na Naftali Bennett kinafuata kwa asilimia 22.8 ya kura.

  12. Abiria wa meli ya kifahari ya kitalii wamekwama nchini Kambodia kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta

    Abiria wa meli ya kifahari iliyokuwa ikizunguka dunia wamekwama nchini Cambodia baada ya kampuni inayoendesha meli hiyo kusitisha safari kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta.

    Kampuni ya Marekani inayomiliki meli ya Villa Vie Odyssey imesema inashirikiana na abiria kupanga namna ya kushuka melini na kupata makazi ya muda.

    Haijafahamika idadi kamili ya abiria waliokuwa melini, lakini meli hiyo yenye urefu wa karibu mita 200 ina uwezo wa kubeba hadi abiria 650. Ilianza safari yake kutoka Belfast, Ireland Kaskazini, mwezi Oktoba 2024, ikiwa na mpango wa kuzunguka dunia.

    Bei ya mafuta imepanda kwa kiasi kikubwa tangu kuanza kwa vita vya Iran mapema mwaka huu. Kampuni hiyo imesema gharama ya mafuta kwa kila chumba cha abiria kwa mwezi katika baadhi ya maeneo ya Asia imeongezeka kutoka dola 1,800 hadi dola 8,000.

    Kampuni hiyo imesema ilichukua hatua za kupunguza matumizi ya mafuta, zikiwemo kupunguza kasi ya meli na kuongeza muda wa kusimama bandarini. Hata hivyo, hatua hizo hazikutosha kukabiliana na ongezeko kubwa la gharama.

    Kampuni hiyo imesema haiwezekani kuwabebesha abiria gharama zote za ongezeko hilo.

    Imeongeza kuwa itatumia siku 60 zijazo kurekebisha shughuli zake na kutafuta mtaji zaidi, ingawa hakuna uhakika wa matokeo ya mchakato huo.

    Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni hiyo, safari hiyo ilipangwa kudumu miaka mitatu na nusu na kutembelea karibu nchi 150.

    Meli hiyo ilikuwa imezunguka dunia kwa zaidi ya siku 750 ilipotangaza kusitisha safari yake Jumanne, na kuwaacha abiria nchini Cambodia.

    Shirika la habari la Bloomberg, likimnukuu mwanzilishi wa kampuni hiyo, limeripoti kuwa takribani abiria 200 walikuwa melini walipoambiwa washuke nchini Cambodia.

    Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni hiyo, meli ya Villa Vie Odyssey ina baa na mikahawa kadhaa, eneo la kuogelea na uwanja wa mchezo wa pickleball.

  13. Cameroon yasitisha shughuli za chama cha upinzani baada ya ghasia za uchaguzi

    Waziri wa Utawala wa Maeneo nchini Cameroon amesitisha kwa miezi mitatu shughuli za chama cha kiongozi wa upinzani Issa Tchiroma Bakary, akikituhumu kwa utovu wa nidhamu kabla, wakati na baada ya uchaguzi wa urais uliokuwa na utata mwaka jana.

    Katika agizo lililotolewa leo, Waziri Paul Atanga Nji amekituhumu chama cha Cameroon National Salvation Front (CNSF) kwa kuchochea uasi na ghasia, kutishia uadilifu wa eneo la nchi, umoja wa kitaifa na mamlaka ya kujitawala, pamoja na kuvuruga amani na usalama wa umma.

    “Shughuli zote za chama cha kisiasa kinachojulikana kama Cameroon National Salvation Front (CNSF) zimepigwa marufuku na zitaendelea kuwa marufuku katika eneo lote la nchi katika kipindi cha kusimamishwa kwake,” amesema Nji.

    Uamuzi huo umefikiwa kabla ya uchaguzi muhimu wa serikali za mitaa na bunge unaotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa mwaka ujao. Hatua hiyo imeibua dhana kwamba huenda lengo ni kukizuia chama cha Tchiroma kushiriki katika chaguzi hizo mbili.

    Hata hivyo, kiongozi huyo wa upinzani, ambaye kwa sasa anaishi uhamishoni nchini Gambia, alikuwa amesema awali kuwa chama chake hakitashiriki uchaguzi huo. Alisema mazingira yanayohitajika kwa uchaguzi wa kidemokrasia, uwazi na amani hayajatimizwa.

    Katika taarifa iliyotolewa mwezi Februari, chama hicho kilisema kushiriki katika mchakato huo kungekuwa sawa na kuhalalisha utawala ambao, kwa mtazamo wake, ulishindwa kwenye uchaguzi, na kuunga mkono uchaguzi ambao matokeo yake tayari yameamuliwa.

    BBC imewasiliana na msemaji wa Tchiroma Bakary kutaka maoni yake kuhusu kusimamishwa kwa shughuli za chama hicho.

    Tchiroma alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 2025, lakini akajitangaza kuwa mshindi halali dhidi ya aliyekuwa bosi wake, Paul Biya. Alidai kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na ukiukaji mkubwa wa taratibu na kutoa wito wa maandamano ili kutetea kile alichokiita ushindi wake.

    Katika baadhi ya miji nchini humo, maandamano yaligeuka kuwa ghasia zilizosababisha uharibifu wa majengo ya umma na miundombinu mingine.

    Tume ya Haki za Binadamu ya Cameroon ilisema watu 14 waliuawa katika mapigano kati ya vikosi vya usalama na waandamanaji waliopinga kile walichokitaja kuwa udanganyifu wa uchaguzi. Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu, zaidi ya watu 1,200 walikamatwa na kuwekwa kizuizini.

    Mapema mwezi huu, mahakama katika mji mkuu wa Yaoundé iliwahukumu zaidi ya watu 60 waliokamatwa kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi. Baadhi yao walifungwa jela kwa kati ya miezi sita na 15.

    Soma Pia:

  14. Tetesi za soka Jumatano: Liverpool yamfukuzia beki wa Stuttgart Jeltsch

    Liverpool, Barcelona na Real Madrid ni miongoni mwa klabu kubwa za Ulaya zinazomfuatilia beki wa kati wa Stuttgart, Finn Jeltsch, mwenye umri wa miaka 20 na raia wa Ujerumani.

    Chelsea imeelekeza nguvu zake katika kumsajili kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, mwenye umri wa miaka 23, baada ya uhamisho wake kushindikana dirisha lililopita. Liverpool pia imemjumuisha mchezaji huyo wa England katika orodha ya wanaowindwa.

    Chelsea, Manchester City, Arsenal, Tottenham na Newcastle zimekuwa zikituma maskauti kumfuatilia mshambuliaji wa Club Brugge, Nicolo Tresoldi, ambaye amewahi kuiwakilisha Ujerumani katika ngazi za vijana. Hata hivyo, Club Brugge haiko tayari kumuuza mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 katika dirisha la Januari.

    Manchester United ilipanga kumtimua kocha Michael Carrick wiki hii, lakini imeshindwa kukubaliana kuhusu atakayechukua nafasi yake.

    United italazimika kulipa Newcastle takribani pauni milioni 3 kama fidia iwapo itaamua kumteua Eddie Howe kuwa mrithi wa Carrick.

    Brighton haina wasiwasi wa kumpoteza kiungo wa Paraguay, Diego Gomez, mwenye umri wa miaka 23, licha ya kuvutiwa naye kwa AC Milan na Atletico Madrid.

    Kocha Pierre Sage anaendelea kukabiliwa na shinikizo kubwa, na anaweza kutimuliwa iwapo Crystal Palace itafungwa na Tottenham Jumamosi.

    Liverpool itafuatilia uwezekano wa kumsajili winga wa Valencia, David Otorbi, mwezi Januari iwapo klabu hiyo ya La Liga itaongeza kipengele cha kuvunja mkataba wake kutoka pauni milioni 30 hadi milioni 50. Otorbi ana umri wa miaka 19 na ni raia wa Hispania.

    Juventus imemweka mshambuliaji wa Monaco, Folarin Balogun, kuwa kipaumbele chake katika dirisha la usajili la Januari. Mshambuliaji huyo wa Marekani mwenye umri wa miaka 25 aliwahi kukaribia kujiunga na Everton siku ya mwisho ya dirisha la usajili, lakini uhamisho huo ukakwama.

    Soma pia:

  15. Flávio Bolsonaro afika Marekani baada ya Brazil kufuta hati zake za usafiri

    Mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi wa urais wa Brazil, Flávio Bolsonaro, amewasili Marekani saa chache baada ya mamlaka za Brazil kufuta hati zake za kusafiria, vyanzo vimeiambia BBC.

    Bolsonaro, mwanasiasa wa mrengo wa kulia, aliondoka Brazil baada ya Mahakama ya Juu kuamuru akabidhi hati zake za kusafiria, wakati uchunguzi kuhusu madai ya utakatishaji fedha ukiendelea. Hata hivyo, hajafunguliwa mashtaka na amekanusha madai hayo.

    Hati zake zilifutwa Jumanne baada ya kushindwa kuzikabidhi kwa mamlaka ndani ya muda uliowekwa, hatua iliyozua uvumi kuhusu uwezekano wa kuondoka nchini humo.

    Vyanzo vilivyozungumza na BBC Brasil na BBC Mundo vimesema Flávio alikutana na mdogo wake, Eduardo, katika jimbo la Florida, Marekani. Hata hivyo, haijulikani njia aliyotumia kusafiri kutoka Brazil hadi Marekani.

    Hakuna kati ya ndugu hao aliyeweza kupatikana moja kwa moja ili kutoa maoni yake.

    Kuwasili kwake kunaripotiwa saa chache baada ya afisa mwandamizi wa Marekani kuthibitisha kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo itatoa visa kwa Bolsonaro na familia yake na kuwaruhusu kuingia Marekani.

    BBC imewasiliana na Ikulu ya Marekani, Wizara ya Mambo ya Nje na balozi za nchi hizo mbili kupata maelezo zaidi.

    Siku ya Jumatatu, Mahakama ya Juu ya Brazil iliamuru Bolsonaro akabidhi hati zake za kusafiria kwa polisi ndani ya saa 24, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa madai ya utakatishaji fedha.

    Bolsonaro pia alikuwa akichunguzwa kuhusu madai ya ufisadi katika ufadhili wa filamu inayomhusu baba yake, rais wa zamani Jair Bolsonaro. Jair alitiwa hatiani kwa kupanga njama ya mapinduzi na kwa sasa yuko chini ya kifungo cha nyumbani.

    Uchunguzi mwingine unahusu madai ya uhusiano wake na wakili wa Brazil anayetuhumiwa kutakatisha zaidi ya dola bilioni moja kupitia mpango wa ulaghai.

    Flávio amekanusha kufanya biashara na wakili huyo na kueleza kuwa kunyang’anywa hati zake za kusafiria ni jaribio la kumtisha.

    Bado haijulikani ni nani aliyesafiri naye kwenda Marekani, au iwapo anakusudia kubaki nchini humo na kuishi huko.

    Soma Pia:

  16. Matokeo ya awali ya uchaguzi Israel hayaonyeshi mshindi wa wazi

    Matokeo ya awali ya kura za maoni zilizofanywa baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura nchini Israel yanaashiria kuwa hakuna mshindi wa wazi katika uchaguzi mkuu unaotajwa kuwa muhimu kwa mustakabali wa nchi hiyo.

    Waziri Mkuu wa zamani Benjamin Netanyahu wala aliyekuwa mkuu wa jeshi, Gadi Eisenkot, hawaonekani kuwa na uhakika wa kupata viti vya kutosha kuunda serikali kwa wingi wa wabunge.

    Taarifa za vituo viwili vya utangazaji nchini Israel zinaonyesha kuwa chama cha Yashar cha Eisenkot na vyama vingine vitatu vya upinzani vinavyounda muungano wa kisiasa unaoitwa Change Bloc vinatarajiwa kupata viti 51 kati ya 120 katika bunge la Israel, Knesset. Idadi hiyo ni sawa na inayotarajiwa kupatikana na chama cha Likud cha Netanyahu pamoja na washirika wake wa mrengo mkali wa kulia na vyama vya Wayahudi wa Kiorthodoksi kali.

    Hata hivyo, kura ya maoni ya kituo kingine cha utangazaji inampa Netanyahu uongozi wa viti vitatu.

    Mwelekeo wa kuundwa kwa serikali unaweza kutegemea kwa kiasi kikubwa nafasi ya vyama viwili vya Waarabu, ambavyo vinatarajiwa kupata jumla ya viti 18 au 19, idadi ambayo ingekuwa rekodi.

    Ushiriki wa wapiga kura Jumanne ulikuwa mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa miongo kadhaa.

    Tume Kuu ya Uchaguzi imesema kuwa idadi ya wapiga kura waliojitokeza ilikuwa asilimia 77.7 wakati vituo vilipofungwa saa nne usiku kwa saa za Israel. Huo ndio ulikuwa kiwango cha juu zaidi kufikia muda huo tangu mwaka 1999.

    Matokeo rasmi yanatarajiwa kuanza kutangazwa usiku kucha. Hata hivyo, kura takribani 600,000 zilizopigwa na wapiga kura wasiokuwepo katika maeneo yao, wengi wao wakiwa wanajeshi, hazitakuwa zimehesabiwa kikamilifu hadi Alhamisi. Kura hizo zinakadiriwa kuwa takribani asilimia 10 ya kura zote.

    Baada ya matokeo ya mwisho kuthibitishwa na rais wa Israel kufanya mashauriano na makundi yote ya kisiasa, atamwalika kiongozi wa chama anayeona ana nafasi kubwa zaidi ya kufanikiwa kuunda muungano wa serikali.

    Mchakato huo unaweza kuchukua wiki kadhaa. Iwapo juhudi za kuunda serikali zitashindikana, uchaguzi mwingine utalazimika kufanyika.

    Eisenkot amesema wameandika historia na kuahidi kuhakikisha kuwa uamuzi wa wananchi unatafsiriwa katika kuundwa kwa serikali ya Kizayuni ambayo itakuwa imara na yenye manufaa kwa raia wote wa Israel.

    Hata hivyo, katika makao makuu ya chama cha Likud cha Netanyahu mjini Jerusalem, hakukuwa na dalili za kukubali kushindwa.

    Kura za maoni zinaonyesha kuwa Likud bado inaweza kuwa chama chenye viti vingi zaidi bungeni.

    Soma Pia:

  17. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 28/10/2026.