Hapa ndipo tunatamatisha matangazo yetu ya moja kwa moja. Kwaheri.
Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Trump aitaka Iran kufanya maamuzi haraka, vinginevyo aongeze muda wa kizuizi cha kijeshi
Trump amesema Iran“yapaswa kujirekebisha haraka” na kutia saini mkataba wa makubaliano, akisisitiza kuwa Iran haipaswi kuwa na silaha za nyuklia.
Muhtasari
- Mtoto wa Robert Mugabe kufukuzwa Afrika Kusini
- Shambulio la Israel la aina ya "double-tap" lasababisha vifo vya wahudumu watatu wa afya nchini Lebanon
- Iran inapaswa kufanya maamuzi ya haraka, aonya Trump
- Bei ya mafuta yapanda hadi dola 115 kufuatia ripoti za Marekani kuendeleza kizuizi cha kijeshi nchini Iran
- Wanaume wawili wakiyahudi wajeruhiwa kwa kudungwa kisu mjini London
- Ufaransa yawataka raia wake kuondoka nchini Mali
- Mwanaume abeba mwili wa dada yake hadi benki ili kutoa pesa kutoka kwenye akaunti yake.
- Kenya yapokea swala aina ya Mountain Bongo kutoka Jamhuri ya Czech
- Kim Jong Un awasifia wanajeshi 'waliojilipua' kuepuka kukamatwa na Ukraine
- Marekani yasema inaendelea vizuri katika vita dhidi ya Iran
- Israel yasema haina nia ya kutwaa ardhi Lebanon
- Comey ashtakiwa kwa kumtishia maisha Trump mtandaoni
- Wahamiaji watakiwa kufunga biashara zao Afrika Kusini
- PSG yailaza Bayern katika nusu fainali ya mabao tisa
- Mfalme Charles asisitiza umuhimu wa ushirikiano na Marekani katika 'ulimwengu wenye ushindani'
- Marekani yawekea vikwazo mashirika 35 na watu binafsi wanaohusishwa na 'mfumo wa benki uliofichwa' wa Iran
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi & Beldeen Waliaula
Mtoto wa Robert Mugabe kufukuzwa Afrika Kusini
Mtoto wa kiongozi wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe, ametakiwa kuondoka Afrika Kusini mara moja, mahakama moja mjini Johannesburg imetoa agizo hilo.
Bellarmine Mugabe alikiri kosa la kumyooshea mtu bunduki na kuwa nchini Afrika Kusini kinyume cha sheria.
Hii ni baada ya kukamatwa kufuatia tukio la kupigwa risasi mwanaume mwenye umri wa miaka 23 nyumbani kwake.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 28 pia ametakiwa kulipa faini ya dola 36,000.
Mwenzake katika kesi hiyo, Tobias Matonhodze, ambaye alikiri kosa la jaribio la mauaji, uhamiaji haramu, kumiliki risasi bila kibali na kujaribu kuzuia haki kutendeka, amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela.
Wote wawili walikamatwa tarehe 19 mwezi Februari baada ya polisi kuitwa nyumbani kwa Mugabe baada mtu mmoja, anayeaminika kuwa mlinzi wa lango, kukimbizwa hospitalini akiwa katika hali mahututi baada ya kupigwa risasi.
Pia unaweza kusoma:
Shambulio la Israel la aina ya “double-tap” lasababisha vifo vya wahudumu watatu wa afya nchini Lebanon
Mashambulizi mawili ya angani yaliyotekelezwa na Israel katika jengo moja kusini mwa Lebanon yamesababisha vifo vya watu watano, wakiwemo wahudumu watatu wa kutoa matibabu ya dharura.
Waziri mkuu wa Lebanon ametaja mashambulizi hayo kuwa “uhalifu wa kivita.”
Wizara ya Afya ya Lebanon imesema kuwa watu hao watatu waliokuwa wakitoa huduma za dharura, wanatoka katika jeshi la ulinzi wa raia, na walifika eneo hilo kuwasaidia waliojeruhiwa na shambulio lililotokea hapo jana, katika mji wa Majdal Zoun.
Watatu hao walikwama chini ya vifusi na baadaye kuripotiwa kufariki katika shambulio jingine lililolenga eneo hilo
Israel haijatoa maelezo yoyote kuhusu kuwalenga wahudumu hao wa afya na kutumia mbinu ya kijeshi maarufu “double tap” ambayo shambulio la kwanza hufanyika na kufuatiwa na jingine kuwalenga raia na timu ya uokoaji.
Inadaiwa Israel imekuwa ikitumia mbinu hii nchini Lebanon na eneo la Gaza.
Mashirika ya kutetea haki za kibinadamu yanasema kuwa mashambulizi ya makusudi dhidi ya wahudumu wa afya yana hesabiwa kama uhalifu wa kivita.
Pia unaweza kusoma:
Iran inapaswa kufanya maamuzi ya haraka, aonya Trump
Rais wa Marekani Donald Trump, kupitia mtandao wa Truth Social, amewaambia viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa “wafanye uamuzi wa busara kwa haraka”
Rais huyo alichapisha kuwa “Iran haiwezi kurekebisha hali kwa sasa. Wairani hata hawajui jinsi ya kutia saini makubaliano yasiyo jumuisha silaha za nyuklia.”
Rais huyo wa Marekani ameonya kwamba Iran“inapaswa kuanza kufikiria kwa haraka” au aongeze muda wa kizuizi cha kijeshi katika bandari za Iran.
Trump pia alichapisha picha yake akiwa amebeba bunduki, iliyo andamana na maelezo "sitakuwa mwema tena."
Pia unaweza kusoma:
Bei ya mafuta yapanda hadi dola 115 kufuatia ripoti za Marekani kuendeleza kizuizi cha kijeshi nchini Iran
Bei ya mafuta imepanda kufuatia ripoti kuwa Marekani inajiandaa “kuzuia kwa muda mrefu” bandari za Iran.
Mafuta aina ya Brent yalipanda hadi takriban dola 115 kwa pipa moja hii leo, kutoka dola 110 Jumanne jioni.
Hii inafuatia ripoti iliyochapishwa na jarida la Wall Street Journal iliyosema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump amewaagiza wasaidizi wake kuandaa mpango wa kuongeza muda wa zuio la kijeshi linaloendelea katika bandari za Iran, ili kudhoofisha uchumi wa taifa hilo.
Iran imesema itaendelea kuvuruga safari za meli zinazopitia Mlango bahari wa Hormuz ili kujibu kizuizi cha kijeshi cha Marekani.
Bei ya mafuta imekuwa ikipanda na kushuka tangu kuanza kwa vita, huku mlango bahari wa Hormuz ukisalia umefungwa kwa wiki kadhaa tangu kuanza kwa vita eneo hilo.
Pia unaweza kusoma:
Wanaume wawili wakiyahudi wajeruhiwa kwa kudungwa kisu mjini London
Wanaume wawili wamedungwa kisu katika barabara ya Golders Green kaskazini mwa mji wa London, huku mwanaume mmoja aliyebeba kisu akionekana akikimbia katika barabara hiyo akijaribu kuwadunga kisu watu wa asilia ya kiyahudi eneo hilo.
Shirika la usalama wa wayahudi la Shomrim, lilisema waliingilia kati na kumkamata mshukiwa, ambaye alisalimishwa kwa polisi.
Wanaume hao wawili waliodungwa kisu, kwa sasa wanapokea matibabu.
Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema tukio hilo ni la ‘kushangaza sana’
Starmer alisema kuwa uchunguzi wa kisa hicho umeanzishwa na taifa lake linakabiliana na visa kama hivyo.
Pia unaweza kusoma:
Ufaransa yawataka raia wake kuondoka nchini Mali
Ufaransa imewataka raia wake walioko nchini Mali, kuondoka haraka iwezekanavyo, baada ya mashambulizi yaliyoshuhudiwa kati makundi yaliyojihami na makundi yenye itikadi kali.
Kupitia ilani iliyotolewa hii leo, raia wa Ufaransa wamekatazwa kutosafairi katika taifa lolote magharibi mwa Afrika na kusema hali kwa sasa “si salama.”
Siku ya Jumamosi milio ya risasi ilisikia nchini kote ikiwemo mji mkuu wa Bamako, huku Waziri wa Ulinzi wa taifa hilo akiuawa, huku makundi mengine yakichukua udhibiti wa mji wa Kidal kaskazini mwa taifa hilo.
Mkuu wa jeshi la Mali, jenerali Assimi Goita amesema hali ya usalama nchini humo kwa sasa imedhibitiwa.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa imesema “ raia wa Ufaransa wanatakiwa wafanye mipango ya haraka ya kutoka Mali kwa kutumia ndege za abiria ambazo bado zinahudumu nchini humo”
Ufaransa pia imewaonya raia wake kutosafiri kuelekea Mali.
Pia unaweza kusoma:
Mwanaume abeba mwili wa dada yake hadi benki ili kutoa pesa kutoka kwenye akaunti yake.
Siku ya Jumanne, tarehe 28 mwezi Aprili, wafanyakazi na wateja katika benki moja wilayani Kendujhar, jimbo la Odisha nchini India, walipatwa na mshangao, baada ya mwanaume mwenye umri wa miaka 52, alipofika kwenye benki hiyo akiwa amebeba maiti ya dada yake begani.
Mwanaume huyo,kwa jina Jeetu Munda, alikuwa anata kutoa rupia 19,300 au dola 205 kutoka kwa akaunti ya dada yake.
Dadake alikuwa amefariki miezi miwili iliyopita.
Miezi michache kabla ya kifo chake, dadake alikuwa ameuza ndama wake mmoja na kuweka rupia 19,300 katika benki ya eneo hilo.
Jeetu Munda alisema kuwa “Nilijaribu mara kadhaa kumshawishi meneja wa benki kuwa dada yangu amefariki na ninahitaji kutoa fedha kutoka kwenye akaunti yake, lakini meneja alikataa kunisikiliza na kusisitiza nilete uthibitisho wa kifo chake. Ndipo nikaleta mwili wa dada yangu kama uthibitisho.”
Kulingana na Jeetu, aliwasili mapema katika eneo la kuchomea miili lililoko umbali wa kilomita tatu kutoka kijijini kwake, ambako alikusanya mabaki ya dada yake, akayaweka kwenye mfuko, kisha akayabeba hadi eneo iliopo benki hiyo.
Wafanyikazi wa benki waliwaita maafisa wa polisi ambao walimshawishi Jeetu kuwa matakwa yake yatashughulikiwa na kumsihi arudishe mwili wa dadake makaburini.
Kulingana na meneja wa benki hiyo ndungu wengine wawili walikuwa wamefika kwenye benki hiyo wakitaka kutoa fedha hizo, na wakatakiwa kutoa uthibitisho kuwa wana haki ya kupokea pesa za dada yao.
Tarehe 28 mwezi Aprili kiasi cha rupia 19,410 kiliwekwa kwenye akuanti ya Jeetu na warithi wengine wawili.
Pia unaweza kusoma:
Kenya yapokea swala aina ya Mountain Bongo kutoka Jamhuri ya Czech
Swala wa nne aina ya Mountain Bongo, wamerejeshwa nchini Kenya kutoka hifadhi moja ya wanyama nchini Czech
Swala hao wakiume waliwasili jana usiku, na kupokelewa na Waziri wa utalii pamoja na viongozi wengine, na zimepelekwa katika hifadhi binafsi nchini humo.
Shirika la kuhifadhi wanyamapori nchini Kenya, KWS, imesema kurejea kwa wanyama hao ni historia, na hatua nzuri ya kurejesha wanyama hao katika misitu ya Kenya.
Idadi ya wanyama hao imepungua kutoka 500 miaka ya 1970 hadi chini ya 100 ambao wanapatikana porini au hifadhi za wanyama nchini Kenya.
Shirika la KWS pamoja na washirika wengine wamekuwa wakifanya juhudi za kuzalisha wanyama hao na kuwaachilia waishi porini kwa lengo la kuongeza idadi yao.
Kenya inalenga kuongeza idadi ya mountain bongo hadi kufikia 700 ifikapo mwaka 2050, kupitia mpango wa kitaifa wa uokoaji unaoongozwa na KWS.
Pia unaweza kusoma:
Uganda yawakamata zaidi ya raia 200 wa kigeni katika oparesheni ya uhamiaji haramu
Mamlaka nchini Uganda zimewakamata raia 231 wa kigeni katika oparesheni inayoendelea dhidi ya uhamiaji haramu, maafisa wamesema.
Katika oparesheni nyingine iliyofanyika katika kitongoji cha hali ya juu cha mji mkuu, raia 169 wa kigeni walikamatwa na Idara ya kudhibiti Uhamiaji baada ya kupatikana wakiishi ndani ya jengo bila nyaraka halali za uhamiaji.
Waliokamatwa ni raia kutoka Pakistan, Bangladesh, Ethiopia, India, Ghana, Myanmar, Sri Lanka, Malaysia na Cambodia.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Simon Peter Mundeyi, amesema oparesheni hizo ni sehemu ya juhudi za serikali za kusimamia sheria za uhamiaji na kuvunja mitandao inayoshukiwa kujihusisha na uhalifu wa mtandaoni.
Wizara hiyo imesema baadhi ya waliokamatwa waliingizwa nchini kwa ahadi za uongo za ajira, huku wengine wakidaiwa kuhusika na shughuli za ulaghai wa mtandaoni.
Katika tukio jingine, maafisa wa uhamiaji katika mji wa Adjumani kaskazini mwa Uganda waliwakamata raia 69 wa Nigeria wanaodaiwa kufanya kazi bila vibali halali na kushiriki shughuli zisizoidhinishwa, ikiwemo kuendesha taasisi ya kidini.
“Watu hawa mara nyingi huingia nchini wakijitambulisha kama wahubiri wa injili, lakini baadaye hugundulika kujihusisha na shughuli zisizo halali,” alisema Mundeyi.
Wachunguzi wanasema mfululizo huo wa ukamataji unaonyesha kuongezeka kwa mitandao ya uhalifu wa mtandaoni inayohusisha raia wa kigeni nchini Uganda.
Mwaka 2020, mamlaka ziliwakamata raia 36 wa China katika operesheni kubwa ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni, ambapo zilipatikana simu 3,500, kadi za simu 1,700 pamoja na kompyuta mpakato, modemu na seva.
Maafisa wamesema waliokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria kabla ya kurejeshwa katika nchi zao za asili.
Soma zaidi:
Kim Jong Un awasifia wanajeshi 'waliojilipua' kuepuka kukamatwa na Ukraine
Rais wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amewapongeza wanajeshi wa wa nchi hiyo waliojitoa uhai kwa kujilipua wakati wakiipigania Urusi dhidi ya Ukraine, na kuthibitisha sera inayoshukiwa kwa muda mrefu kwenye uwanja wa vita.
Katika hotuba yake wiki hii, kiongozi huyo wa Korea Kaskazini alisema wale ambao "waliamua kujilipua bila kusita, walijitoa mhanga, ili kulinda heshima kubwa" ya nchi yetu ni "mashujaa".
Korea Kusini inakadiria kuwa takribani raia 15,000 wa Korea Kaskazini wametumwa kuisaidia Urusi kurejesha sehemu za magharibi mwa Kursk, na zaidi ya 6,000 wameuawa kufikia sasa.
Pyongyang na Moscow hazijathibitisha idadi hiyo ya vifo.
Mashirika ya kijasusi na walioasi wamesema wanajeshi hao walikuwa chini ya amri ya Pyongyang kujiua badala ya kuchukuliwa mateka na Ukraine.
"Walijitolea bila kutarajia fidia, wala kutarajia malipo... Hii [ndiyo] ufafanuzi wa uaminifu wa jeshi letu," Kim alisema mjini Pyongyang siku ya Jumatatu alipokuwa akizindua sanamu ya kumbukumbu ya wanajeshi waliofariki, vyombo vya habari vya serikali KCNA viliripoti.
Waziri wa Ulinzi wa Urusi Andrey Belousov na spika wa bunge la Urusi Vyacheslav Volodin ni miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo.
Huko Korea Kaskazini, wanajeshi wanafundishwa kuwa kukamatwa vitani ni kitendo cha uhaini.
Mapema mwaka huu, shirika la utangazaji la Korea Kusini MBC lilirusha hewani kipindi kilichowaangazia wafungwa wawili wa kivita wa Korea Kaskazini nchini Ukraine, mmoja wao alisema kwamba anajuta kwa nini hakujitoa uhai.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yasema inaendelea vizuri katika vita dhidi ya Iran
Rais wa Marekani Donald Trump amezungumzia kwa kifupi mgogoro wa Mashariki ya Kati, akisema Marekani “inaendelea vizuri sana” katika vita vyake dhidi ya Iran.
“Tayari tumemshinda adui huyo kijeshi,” alisema Donald Trump.
“Hatutawahi kumruhusu adui huyo, Mfalme Charles wa Tatu anakubaliana nami, hata zaidi yangu, hatutawahi kuwaruhusu kupata silaha za nyuklia.”
Rais huyo ameongeza kuwa Marekani na Uingereza daima zitasimama pamoja, “zikipinga na kushinda nguvu za ukomunisti, ufashisti na utawala wa kimabavu.”
Soma zaidi:
Israel yasema haina nia ya kutwaa ardhi Lebanon
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Sa’ar amesema nchi yake haina nia ya kutwaa maeneo ya Lebanon, wakati vikosi vya Israel vikiendelea na operesheni kusini mwa nchi hiyo dhidi ya kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran, licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.
“Israel haina matarajio ya kujitanua kimamlaka au kutwaa maeneo ya Lebanon,” Sa’ar alisema katika mkutano wa pamoja na mwenzake wa Serbia, Marko Đurić.
“Uwepo wetu katika maeneo ya mpakani kaskazini una lengo moja tu: kuwalinda raia wetu.”
Soma zaidi:
Comey ashtakiwa kwa kumtishia maisha Trump mtandaoni
Aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la kijasusi la Marekani, James Comey, ameshtakiwa kwa kumtishia maisha Rais wa Marekani Donald Trump, shitaka rasmi linalotokana na picha aliyowahi kushiriki kwa muda mfupi kwenye mitandao ya kijamii
Picha hiyo iliyochapishwa kwenye mtandao wa Instagram mwaka jana ilionyesha magamba ya baharini yaliyopangwa kuunda namba “86 47”. ni istilahi ya mtaani inayomaanisha “kuondoa” au “kuondoa kabisa”.
Comey amesisitiza kuwa hakujua maana ya namba hizo kwenye picha, lakini Trump na maafisa wengine wa utawala wamesema chapisho hilo lilikuwa tishio dhidi ya rais wa 47.
Akijibu mashtaka hayo Jumanne, Comey alisema: “Bado sina hatia, bado siogopi, na bado nina imani na mahakama huru ya shirikisho.”
Katika mkutano na waandishi wa habari kutangaza shitaka hilo, Mkurugenzi wa FBI Kash Patel alisema kuwa kama aliyekuwa mkuu wa taasisi hiyo, Comey “alijua vizuri athari na matokeo ya kufanya chapisho kama hilo.”
Comey alifutwa kazi na Trump katika muhula wake wa kwanza baada ya kuanzisha uchunguzi kuhusu uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi wa urais wa Marekani wa 2016.
Tangu wakati huo, Trump amekuwa akitaka mara kwa mara mashtaka kufunguliwa dhidi yake — na mashtaka ya Jumanne ni jaribio la pili la utawala wake kufanya hivyo.
Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, Comey anakabiliwa na mashtaka ya kutoa vitishio dhidi ya rais na kusambaza tishio katika biashara ya kati ya majimbo. Kila shitaka lina adhabu ya hadi miaka 10 jela.
Maafisa wa kijasusi wa Secret Service walimhoji Comey mwezi Mei mwaka jana kuhusu picha hiyo ya magamba ya baharini.
Comey alifuta chapisho hilo la Instagram, akisema katika maelezo yaliyofuata kuwa “alidhani [magamba ya baharini] yalikuwa ujumbe wa kisiasa.”
Trump, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akimkosoa Comey, alisema kuhusu chapisho hilo kwamba “hata mtoto anajua lilimaanisha nini.”
Baadhi ya wataalamu wa sheria wamesema shitaka hilo linaonekana dhaifu na limeibua maswali mapya kuhusu juhudi za Wizara ya Sheria kuwalenga wale wanaochukuliwa kuwa wapinzani wa kisiasa wa Trump.
Chapisho la Comey kwenye mitandao ya kijamii linaweza kutazamwa na mahakama kama uhuru wa kujieleza unaolindwa na Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani, wataalamu walisema.
Hii ni mara ya pili kwa wizara ya sheria kumfungulia Comey mashtaka.
Comey alishtakiwa na baraza la majaji wakuu wa shirikisho mwishoni mwa Septemba kwa madai kwamba alidanganya bungee la Congress wakati akitoa ushahidi wake Septemba 2020 na kuzuia mchakato wa bunge.
Mashtaka hayo yalikuja siku chache baada ya Trump kumtaka mkuu wa vyombo vya sheria nchini kuchunguza kwa nguvu zaidi wapinzani wake wa kisiasa, akiwemo Comey.
Comey alikana mashtaka hayo wakati wa kufikishwa kwake mahakamani kwa muda mfupi Oktoba kabla ya kesi hiyo kufutwa mwezi Novemba.
Jaji Cameron Currie alitupilia mbali shtaka dhidi ya Comey kutokana na uteuzi “usio halali” wa mwendesha mashtaka Lindsey Halligan.
Hata hivyo, jaji huyo aliacha wazi uwezekano kwa serikali kujaribu tena.
Mapema Jumanne, jaji mwingine aliamua kwamba aliyekuwa mwendesha mashtaka wa shirikisho Maurene Comey — ambaye ni binti wa James Comey — anaweza kuendelea na kesi yake ya kupinga kufutwa kazi kwake na utawala wa Trump.
Wahamiaji watakiwa kufunga biashara zao Afrika Kusini
Wahamiaji wa Kiafrika katika mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, wameshauriwa "kuchukua tahadhari" wakati wa maandamano ya kupinga uhamiaji haramu, huku kukiwa na hofu ya mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni.
Ghana imewashauri raia wake kufunga biashara na "kudhibiti shughuli zao za umma, huku mkuu wa Muungano wa Nigeria nchini Afrika Kusini akiwaomba wanachama wake kusali nyumbani.
Maandamano mengine yanatarajiwa kufanyika leo Jumatano mjini Johannesburg.
Hisia za kupinga wahamiaji zimepata fedha za kisiasa katika miaka ya hivi karibuni huku baadhi ya wageni wakiamini kuwa wanachukua kazi na kunufaika kutokana na huduma za umma.
Lakini rais alisema raia hawapaswi kuruhusu wasiwasi wao "kuzaa chuki na chuki dhidi ya Waafrika wenzetu".
Akilaani mashambulizi ya hivi majuzi dhidi ya wageni, Rais Cyril Ramaphosa alitumia hotuba yake ya Siku ya Uhuru siku ya Jumatatu - kuadhimisha uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo mwaka 1994 - pia kuikumbusha nchi yake deni lao kwa mataifa mengine barani humo katika kuunga mkono mapambano yao dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi.
Siku ya Jumanne, mamia ya watu walijitokeza katika mitaa ya Pretoria kushiriki maandamano yaliyoandaliwa kupinga uhamiaji kuelekea Majengo ya Muungano, makao rasmi ya serikali.
Wengine walivalia fulana zenye maandishi, huku wengine wakiimba na kuonyesha mabango yaliyotengenezwa kwa mikono.
Mwandamanaji mmoja aliiambia BBC kwamba anapinga "mmiminiko wa wahamiaji haramu" suala ambalo anasema wanasiasa wameshindwa kulitatua.
Soma pia:
PSG yailaza Bayern katika nusu fainali ya mabao tisa
Timu ya Paris St-Germain kutoka Ufaransa iliibuka kidedea kwa mabao 5 kwa 4 dhidi ya Bayern Munich kwenye Uwanja wa Parc des Princes na kuchukua uongozi mwembaba katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Mabao matano yalifungwa katika kipindi cha kwanza chenye mbwembwe baada ya kipindi cha mapumziko wakati watetezi wa kombe hilo PSG walipoanza kujinasua, na kufungua uongozi wa mabao matatu kwa moja.
Lakini Bayern, ambao tayari wametawazwa mabingwa wa Bundesliga na kushinikiza kunyakuaMakombe matatu msimu huu, walipunguza nakisi hadi moja na kuanzisha mechi nzuri ya mkondo wa pili huko Munich.
Kama timu mbili zilizofunga mabao mengi katika shindano hili mwaka huu, ilifaa tu umati huo uliochangamka kuonyeshwa mchezo wa kuvutia wa kuvutia wenyea vipaji vya kushambulia katika pambano la hali ya juu.
Wakiwa nyuma kwa mkwaju wa penalti wa Harry Kane baada ya Luis Diaz kumchezea rafu William Pacho, PSG walionyesha tishio lao la kuchukua uongozi.
Khvicha Kvaratskhelia aliuchukua mpira upande wa mkono wa kushoto na kuukata kwenye mguu wake wa kulia na kushambulia kwa ustadi mkubwa kwenye ya goli kabla ya mpira wa kichwa wa Joao Neves kuwapa uongozi.
Lakini dakika ya ustadi wa kibinafsi kutoka kwa Michael Olise, kuwapita wachezaji kabla ya kumfunga kipa Matvey Safonov, uliwarudisha wageni kwenye viwango sawa.
Ilidhaniwa kuwa kipindi cha kwanza kingekuwa sare wakati wa mapumziko lakini PSG walipata penalti ya kutatanisha katika dakika ya tano ya dakika za lala salama wakati Alphonso Davies alipochukuliwa kuwa aliumiliki mpira kwenye eneo la hatari.
Mwamuzi Sandro Scharer alikwenda kutazama marejeleo ya kisa hicho katika kisanduku cha VAR kandokando ya uwanja kabla ya kuwazawadia mkwaju wa penalti, mpira ukitoka kwenye mguu wa Davies na kwenye mkono wake kabla ya Ousmane Dembele kutia wavuni mkwaju huo.
Bayern walirejea kutoka mapumziko wakiwa wamedhamiria angalau kurejesha usawa lakini wakati fulani walibabaika huku Wafaransa wakichukua udhibiti wa mpira.
Soma zaidi:
Mfalme Charles asisitiza umuhimu wa ushirikiano na Marekani katika 'ulimwengu wenye ushindani'
Mfalme Charles wa Tatu amezitaka Marekani na Uingereza kufufua upya ushirikiano wao wa muda mrefu wa kuvuka Atlantiki, katika hotuba iliyotolewa kwenye karamu ya kitaifa katika Ikulu ya White House iliyoandaliwa na Rais Donald Trump huku kukiwa na mvutano kuhusu Iran na Ukraine.
Akizungumza pamoja na Rais Trump kwa mara ya kwanza wakati wa ziara yake ya kitaifa ya siku nne, Mfalme Charles aliepuka kutaja moja kwa moja uhusiano mbaya kati ya kiongozi huyo wa Marekani na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.
Lakini kama ilivyokuwa katika hotuba yake nadra kwa Bunge la Marekani , Mfalme huyo alisisitiza ushirikiano ambao London na Washington “zimesimama pamoja katika nyakati bora na mbaya zaidi.”
Mfalme Charles aliihimiza Marekani kusimama imara pamoja na washirika wake wa Magharibi katika hotuba iliyopokelewa kwa uchangamfu.
Wakati familia ya kifalme ilipowasili kwa chakula cha jioni, Trump pia alisifu “hotuba nzuri” na kusema alikuwa “na wivu sana” - ingawa Mfalme Charles aligusia mada nyeti kuanzia mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa kuweka mipaka kwa mamlaka ya rais hadi umuhimu wa muungano wa kujihami wa NATO na ulinzi wa Ukraine.
Akihutubia wabunge wakati wa maadhimisho ya miaka 250 tangu uhuru wa Marekani, Mfalme Charles alisisitiza kwamba “azma isiyoyumba” inahitajika ili kuhakikisha “amani ya haki na ya kudumu” nchini Ukraine, ambayo imekuwa ikipambana na uvamizi kamili wa Urusi tangu mwaka 2022.
Soma zaidi:
Marekani yawekea vikwazo mashirika 35 na watu binafsi wanaohusishwa na 'mfumo wa benki uliofichwa' wa Iran
Marekani inasema imeyawekea vikwazo mashirika 35 na watu binafsi wanaohusishwa na Iran wanaohusika na "mfumo wa benki uliofichwa wa Iran."
Ofisi ya Idara ya Hazina ya Marekani ya Udhibiti wa Mali za Kigeni inasema watu waliowekewa vikwazo walihusika katika kuwezesha "uhamisho wa mabilioni ya dola" na "wanahusishwa na ukwepaji wa vikwazo na uungaji mkono wa Iran kwa ugaidi."
Marekani inasema, "Mitandao hii inaruhusu vikosi vya kijeshi vya Iran, pamoja na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kufikia mfumo wa fedha wa kimataifa."
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mtandao ulioidhinishwa "ulipokea pesa kwa mauzo haramu ya mafuta," "ulinunua sehemu maalum za makombora na mifumo mingine ya silaha," na "kuhamisha pesa kwa makundi ya wakala wa Iran" katika eneo hilo.
Pia unaweza kusoma:
Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.