Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Trump aionya Iran kuhusu mashambulizi ya Wahouthi

Trump ameonya kuwa "iwapo mashambulizi kama hayo yatatokea tena, Marekani itaiwajibisha Iran kwa sababu Wahouthi ni vibaraka na washirika wa Iran.

Muhtasari

Moja kwa moja

Lizzy Masinga & Asha Juma

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu ya leo. Kwaheri.

  2. Watu watatu wafungwa maisha kwa utekaji wa wanafunzi Nigeria

    Watu watatu wamehukumiwa kifungo cha maisha jela na mahakama ya Nigeria baada ya kukiri makosa yanayohusiana na utekaji nyara wa wanafunzi na walimu kadhaa katika shule ya jimbo la Oyo, kusini-magharibi mwa nchi hiyo.

    Hukumu hiyo imetolewa siku chache baada ya mamlaka za Nigeria kutangaza kuokolewa kwa wanafunzi 44 na wafanyakazi wa shule ambao walitekwa nyara wakati wa mashambulizi yaliyoratibiwa dhidi ya shule tatu katika wilaya ya Oriire. Walimu wawili walifariki dunia wakiwa wameshikiliwa mateka.

    Mahakama Kuu ya Abuja iliwatia hatiani Abdulrazak Umar, anayejulikana pia kama Abu Khalifa au Abu Khalid, pamoja na Yunusa Musa na Shamsu Adamu Sani, baada ya kukiri baadhi ya mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yao na serikali ya shirikisho la Nigeria.

    Wanaume hao watatu walikabiliwa na mashtaka yanayohusiana na ugaidi, utekaji nyara, kuficha taarifa muhimu, uchochezi, na uchimbaji madini haramu.

    Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, washtakiwa hao walikiri kuwa walificha taarifa kuhusu watu waliohusika na shambulio la shule hiyo.

    Waendesha mashtaka pia walisema kwamba watuhumiwa hao walikiri kuwa wanachama wa kundi ambalo serikali ya Nigeria imelielezea kuwa mshirika wa kundi la wapiganaji wa Kiislamu la Boko Haram.

    Nigeria imeendelea kushuhudia ongezeko la matukio ya utekaji nyara wa makundi ya watu, hasa katika shule, jamii na maeneo ya ibada, hali ambayo imefanya usalama kuwa moja ya masuala makuu ya kisiasa kuelekea uchaguzi wa mwaka 2027.

    Serikali ya Nigeria imesema inaongeza juhudi za kukabiliana na uasi wa makundi yenye silaha pamoja na vikundi vya uhalifu, lakini mashambulizi yanayoendelea yamezua maswali kuhusu iwapo hatua za sasa za usalama zinatosha kuhakikisha ulinzi wa raia.

    Soma Zaidi:

  3. Saudi Arabia lazima ijiunge na mkataba wa Abraham Accord - Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa kuidhinishwa kwa mkataba unaopendekezwa wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia kati ya Marekani na Saudi Arabia kutategemea iwapo Saudi Arabia itajiunga na Makubaliano ya Abraham Accord.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa Truth Social, Trump amesema mkataba huo unahusu ushirikiano wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia kupitia Wizara ya Nishati ya Marekani na Saudi Arabia, akisisitiza kuwa hautahusisha urutubishaji wa nyenzo za nyuklia na kwa matumizi yasiyo ya kijeshi pekee.

    Alielezea kuwa makubaliano hayo yanafanana na yale ambayo tayari Iran, Falme za Kiarabu (UAE) na mataifa mengine yametia Saini.

    Rais huyo alisema mkataba huo utaidhinishwa, lakini kwa sharti kwamba Saudi Arabia ijiunge na Makubaliano ya Abraham Accord, ambayo aliutaja kuwa wa "heshima kubwa na wenye mafanikio."

    Trump pia alisisitiza kwa mara nyingine kwamba Marekani haipingi matumizi ya nyuklia kwa shughuli za kiraia, mradi shughuli hizo zisihusishe urutubishaji wa nyenzo za nyuklia kwa matumizi ya kijeshi.

    Soma pia:

  4. Uingereza yakanusha madai ya kusitisha mafunzo yote ya kijeshi nchini Kenya

    Uingereza imekanusha taarifa ya kuwa imesitisha shughuli zote za mafunzo ya kijeshi nchini Kenya, ikisema madai hayo si ya kweli.

    Uingereza imetoa ufafanuzi huo kufuatia ripoti za vyombo vya habari vya Kenya zilizodai kuwa Kikosi cha Mafunzo cha Jeshi la Uingereza nchini Kenya (BATUK) kimesitisha shughuli zake baada ya serikali ya Kenya kuchelewa kutoa leseni inayohitajika kwa mafunzo hayo kufanyika.

    Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ameiambia BBC kwamba "BATUK haijafungwa."

    Aliongeza kuwa kilichositishwa ni zoezi moja tu la mafunzo lililokuwa limepangwa kufanyika baadaye mwaka huu.

    "Tunasikitika kwamba leseni muhimu zilizohitajika kuruhusu mafunzo hayo kufanyika katika kambi ya Laikipia baadaye mwaka huu hatujazipokea. Kutokana na hilo, mafunzo yaliyokuwa yameratibiwa sasa yatafanyika katika eneo jingine nje ya Kenya."

    BATUK, yenye makao yake karibu na Kituo cha Anga cha Laikipia, huendesha mara kwa mara mafunzo ya pamoja ya kijeshi na Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).

    Mwezi Disemba mwaka uliopita, uchunguzi wa bunge la Kenya uliwashutumu wanajeshi wa Uingereza wanaofanya mafunzo eneo la Laikipia kwa unyanyasaji wa kingono na uharibifu wa mazingira.

    Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilijibu na kusema kuwa inasikitika kuhusu masuala yaliyoibuliwa na kuahidi kuchunguza madai yoyote yaliyo na ushahidi.

    Soma pia:

  5. Aliyekuwa gavana wa Migori nchini Kenya, Okoth Obado, apatikana na hatia ya mauaji

    Aliyekuwa gavana wa kaunti ya Migori iliyoko magharibi mwa Kenya, Zachary Okoth Obado, na washitakiwa wenzake wamepatikana na hatia ya kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu, Sharon Otieno, kulingana na mahakama moja nchini Kenya.

    Katika hukumu iliyotangazwa kupitia televisheni, Mahakama Kuu ya Milimani jijini Nairobi ilimpata Obado, aliyekuwa msaidizi wake binafsi Michael Oyamo na aliyekuwa karani wa kaunti ya Migori, Caspal Obiero na hatia ya mauaji ya Sharon Otieno.

    "Upande wa mashtaka umethibitisha makosa yanayowakabili mshtakiwa wa kwanza, wa pili na wa tatu. Ninawapata kila mmoja na hatia ya kosa la mauaji. Kila mmoja wao amehukumiwa kwa kosa hilo," Jaji Cecilia Githua alisema.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kenya, jaji alisema Obado "alikuwa na motisha ya kutaka Sharon auawe na ndiye aliyepanga njama za kumuua."

    Obado na washitakiwa wenzake wataendelea kuzuiliwa rumande.

    "Tumefurahishwa na hukumu hii. Tunaamini kwamba hatimaye haki imetendeka kwa Sharon," alisema wakili wa familia ya Sharon.

    Sharon Otieno, mwenye umri wa miaka 26, alidaiwa kutekwa nyara na kuuawa mwaka wa 2018. Mwili wake ulipatikana kwenye kichaka karibu na mji mdogo wa Oyugis, magharibi mwa Kenya.

    Ripoti ya uchunguzi wa maiti wakati huo ilionyesha kuwa huenda alibakwa na kudungwa kisu mara nane shingoni, tumboni na mgongoni. Pia alipoteza mtoto wake ambaye alikuwa hajazaliwa wakati wa tukio hilo.

    Barrack Oduor, ambaye wakati huo alikuwa mwandishi wa habari wa Nation Media Group, alitekwa pamoja na Sharon lakini alifanikiwa kujiokoa baada ya kuruka kutoka kwenye gari lililokuwa likienda kwa kasi, ingawa alipata majeraha.

    Kesi hii, ilikuwa miongoni mwa kesi zilizovutia umakini mkubwa wa watu nchini Kenya. Hukumu hiyo imehitimisha kesi iliyodumu kwa zaidi ya miaka saba.

  6. Trump aionya Iran kuhusu mashambulizi ya Wahouthi

    Rais wa Marekani Donald Trump, ameonya kwamba iwapo waasi wa Houthi nchini Yemen wataendelea kushambulia meli, Marekani itailaumu Iran kwa mashambulizi hayo na huenda ikachukua hatua kali za kijeshi dhidi ya Tehran.

    Katika taarifa aliyochapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema kuwa mwaka mmoja uliopita Marekani ilichukua hatua kali za kijeshi dhidi ya Wahouthi baada ya kundi hilo kulenga meli za kibiashara na kuvuruga biashara ya kimataifa.

    Hata hivyo, Trump alidai kuwa Wahouthi wameanza tena mashambulizi na kwamba usiku uliopita walifyatua risasi dhidi ya ndege mbili za Saudi Arabia.

    Trump ameonya kuwa "iwapo mashambulizi kama hayo yatatokea tena, Marekani itaiwajibisha Iran kwa sababu Wahouthi ni vibaraka na washirika wa Iran.

    Rais huyo amesema kuwa ikiwa hali itaendelea kama ilivyo sasa huenda Wahouthi na Iran wakachukuliwa hatua kali za kijeshi.

    Soma pia:

  7. Oman inajaribu kuzuia kuongezeka kwa mgogoro wa Bahari ya Shamu

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman imesema kuwa nchi hiyo inaratibu juhudi na Saudi Arabia, pande mbalimbali za Yemen, na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen ili kurejesha mchakato wa kisiasa unaolenga kuleta usalama na utulivu katika eneo hilo.

    Taarifa iliyotolewa na Oman ilisisitiza umuhimu wa kuepuka kuongezeka kwa mvutano na vitisho vinavyoweza kuzidisha hali katika Bahari ya Shamu na kuhatarisha uhuru wa usafiri wa baharini.

    Katika ujumbe tofauti kwenye mtandao wa X, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Albusaidi, alisema amejadili masuala muhimu ya kikanda, ikiwa ni pamoja na Mlango wa Hormuz na Yemen, na mwenzake wa Pakistan. Pakistan imekuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran.

    Saudi Arabia ilitumia miaka mingi kupambana na Wahouthi lakini ilishindwa kuwaondoa kutoka mji mkuu wa Yemen, Sanaa, pamoja na maeneo makubwa wanayoyadhibiti. Sehemu nyingine za Yemen ziko chini ya serikali inayotambuliwa kimataifa.

    Makubaliano yasiyo rasmi ya kusitisha mapigano kati ya Houthi na Saudi Arabia yalianza kutekelezwa mwaka 2022 na kwa kiasi kikubwa yameheshimiwa tangu wakati huo. Hata hivyo, hali ilianza kubadilika baada ya Wahouthi kurusha makombora kuelekea Saudi Arabia tarehe 13 Julai, wakidai kuwa majeshi ya Riyadh yalishambulia uwanja wa ndege wa Sanaa.

    Mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya meli za mafuta za Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu yaliyofanyika Alhamisi sasa yanatishia kuongeza zaidi hali ya sintofahamu na kuyumbisha utulivu wa eneo hilo.

    Oman ni nchi yenye umuhimu mkubwa wa kimkakati kutokana na Rasi ya Musandam ambayo inaingia katika Mlango wa Hormuz, mkabala na pwani ya Iran.

    Oman ina mipaka ya nchi kavu na Yemen, ambako waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran wana makazi yao, pamoja na Saudi Arabia, adui mkubwa wa Houthis.

    Pia unaweza kusoma:

  8. Lavrov aionya Marekani kuhusu kupeleka silaha Ukraine

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi imesema kwamba Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, aliiambia Washington iachane na hatua ya kuendelea kupeleka silaha nchini Ukraine wakati wa mkutano na mwenzake wa Marekani, Marco Rubio, mjini Manila Alhamisi, akitaja hatua hiyo kuwa "isiyokubalika."

    Wizara hiyo ilisema katika taarifa kwamba Bw. Lavrov alimwambia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani: "Kuendelea kutoa silaha kwa Kyiv hakukubaliki."

    Katika mkutano huo, uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN), Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi pia alikosoa kile alichokiita "sera za kuyumbisha utulivu za nchi za Ulaya," akisema kuwa nchi hizo zinaendelea kutafuta njia za kuisababishia Urusi "kushindwa kimkakati."

    Huu ni mkutano wa kwanza rasmi kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Urusi na Marekani tangu mnamo mwezi Septemba mwaka jana. Mkutano huo ulifanyika wakati ambapo Marekani imehamisha shinikizo lake kutoka upatanishi wa vita vya Ukraine na kuelekeza zaidi juhudi zake katika kushughulikia mgogoro wa vita vya Mashariki ya Kati.

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza katika taarifa fupi kwamba Bw. Rubio na Sergey Lavrov walijadili "uhusiano kati ya Marekani na Urusi pamoja na umuhimu wa kumaliza vita vya Urusi na Ukraine."

    Kwa mujibu wa taarifa ya Moscow, Bw. Lavrov alisisitiza tena kwamba Urusi iko tayari kufikia "suluhisho la kisiasa na kidiplomasia la mzozo huu."

    Mawaziri hao wawili wakuu wa mambo ya nje wako nchini Ufilipino kuhudhuria mkutano wa ASEAN. Pia wanatarajiwa kujadili vita vya Mashariki ya Kati, mgogoro ambao Urusi imezituhumu na kulaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya mshirika wake, Iran.

    Soma Zaidi:

  9. Marekani yasaini makubaliano muhimu ya nyuklia na Saudi Arabia

    Marekani na Saudi Arabia zimesaini makubaliano muhimu ambayo yataruhusu ufalme wa Ghuba kuunda mpango wa nyuklia wa kiraia.

    Mkataba huo unaelezwa kuwa ni "makubaliano ya ushirikiano wa amani katika masuala ya nyuklia" ambayo yatatoa "fursa kubwa kwa kampuni za Marekani kushiriki katika mpango wa nishati ya nyuklia wa Saudi Arabia," kulingana na Idara ya Nishati ya Marekani.

    Mkataba huo haujawekwa wazi kwa umma, lakini vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kwamba unaweza kuiruhusu Saudi Arabia kurutubisha madini ya urani katika siku zijazo. Urani hiyo inaweza kutumika kama mafuta ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme, lakini pia inaweza kutumika kutengeneza mabomu ya nyuklia.

    Wataalamu wanasema hatua hiyo itakuwa ya kwanza kwa Marekani na inaweza kuongeza hatari ya kuenea kwa silaha za nyuklia katika eneo ambalo tayari lina changamoto za ukosefu wa utulivu.

    Idara ya Nishati ya Marekani ilisema kwamba "makubaliano ya pande mbili ya hatua za ulinzi na usalama" yalisainiwa pamoja na mkataba huo wa ushirikiano.

    Soma Zaidi:

  10. Axios: Marekani yatumia ndege ya kivita ya B-1 dhidi ya Iran

    Tovuti ya Axios iliripoti, ikinukuu maafisa wa Marekani, kwamba jeshi la Marekani lilitumia ndege ya kivita ya masafa marefu aina ya B-1 siku ya Jumanne (Julai 21) katika shambulio dhidi ya "maeneo ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) nchini Iran."

    Kulingana na ripoti hiyo, hii ni mara ya kwanza tangu kuanza tena kwa uhasama na Iran siku kumi na mbili zilizopita ambapo jeshi la Marekani limetumia aina hii ya ndege ya kivita katika operesheni zake.

    Axios ilisema ndege hiyo ya B-1 ilianza safari yake ya kijeshi kutoka "kituo cha jeshi la anga nchini Uingereza" na mienendo yake ilionekana kwenye tovuti zinazofuatilia safari za ndege mtandaoni.

    Ripoti hiyo inaeleza kuwa "matumizi ya ndege za B-1, ambazo zina uwezo wa kubeba mabomu 24 yenye uzito wa zaidi ya kilo 900 au makombora mengi ya aina ya 'cruise', yanaashiria kuongezeka kwa kiasi kikubwa na kupanuka kwa wigo wa kampeni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran."

    Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) haikutaja matumizi ya ndege hiyo ya B-1 katika taarifa yake ya Jumanne kuhusu mashambulizi yaliyofanyika siku hiyo.

    Taarifa ya CENTCOM ilisema kuwa vikosi na vifaa vya kamandi hiyo "vililenga vituo vya operesheni za kijeshi vya Iran, uwezo wa majini, hanga za ndege, vituo vya matengenezo ya ndege zisizo na rubani (droni), na miundombinu ya usafirishaji wa vifaa vya kijeshi ili kudhoofisha zaidi uwezo wa Iran kutishia usafirishaji wa meli za kibiashara katika Mlango-bahari wa Hormuz."

  11. Jeshi la Kuwait: Tunakabiliana na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Iran

    Jeshi la Kuwait lilitangaza Alhamisi asubuhi kuwa linakabiliana na mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani kutoka Iran.

    Mashambulizi hayo, ambayo yaliripotiwa sambamba na mashambulizi ya anga ya Marekani kusini mwa Iran, yalifafanuliwa na mashirika ya habari yenye uhusiano na vyanzo vya kijeshi vya Iran kama "mashambulizi ya ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi ya Marekani huko Ali al-Salem."

    Shirika la Habari la Fars pia liliripoti kusikika kwa mlipuko katika bandari ya Aqaba nchini Jordan, lakini vyanzo vingine havikutaja mashambulizi ya aina hiyo.

  12. Kenya yapokea vifaa vya matibabu kutoka India kuimarisha mapambano dhidi ya Ebola

    Kenya imepokea shehena ya kwanza ya tani 4.5 za vifaa vya matibabu kutoka kwa serikali ya India ili kuimarisha uwezo wa nchi hiyo wa kujiandaa na kukabiliana na uwezekano wa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, The Star imeripoti.

    Shehena hiyo ilikabidhiwa rasmi na Kamishna Mkuu wa India nchini Kenya kwa Waziri wa Afya, Aden Duale, katika hafla iliyofanyika siku ya Jumatano.

    Msaada huo ni sehemu ya jitihada pana za India kusaidia nchi za Afrika kuimarisha uwezo wa kuzuia na kukabiliana na milipuko ya Ebola.

    Vifaa vya matibabu vilivyotolewa vinajumuisha vifaa vya kujikinga binafsi (PPE), vifaa vya kusafirisha sampuli za vipimo, vipima joto vya infrared, kinga za uso, viatu vizito za kujikinga, pamoja na vifaa vingine vya kuzuia na kudhibiti maambukizi.

    Shehena ya pili ya msaada wa matibabu inatarajiwa kuwasili Kenya ndani ya siku chache zijazo.

    Wakati wa hafla ya makabidhiano, maafisa walisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kuimarisha mifumo ya afya na kuboresha maandalizi ya kukabiliana na dharura zinazotokana na vitisho vya magonjwa ya kuambukiza.

    Msaada huo unakuja wakati Kenya ikiendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa, maandalizi, na hatua za haraka za kukabiliana na dharura ili kujikinga dhidi ya hatari ya kuenea kwa Ebola kuvuka mipaka na magonjwa mengine mapya ya kuambukiza.

    Unaweza kusoma;

  13. Meya wa New York: Sina mamlaka ya kumkamata Netanyahu

    Meya wa Jiji la New York, Zohran Mamdani, ambaye awali aliahidi kumkamata Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu iwapo angetembelea jiji hilo, sasa amesema hana mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

    Katika video aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Mamdani alisema badala yake anatoa wito kwa serikali ya Marekani kuchukua hatua kuhusu hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) dhidi ya Netanyahu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita.

    Kisheria, iwapo Netanyahu angeingia katika nchi mwanachama wa ICC, angeweza kukamatwa na kukabidhiwa mahakamani. Hata hivyo, Marekani si mwanachama wa ICC, hivyo haiwajibiki kutekeleza hati hiyo.

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Netanyahu hatakamatwa kwa namna yoyote akiwa nchini Marekani.

    Trump alisema Netanyahu anaendelea kupambana na Iran, ambayo aliituhumu kwa kuhusika na mauaji ya waandamanaji na wanajeshi wa Marekani.

    Kauli hiyo ya Trump ilijibu mahojiano ambayo Mamdani alifanya na gazeti la The New York Times, ambapo alisema alikuwa akifanya mazungumzo na vyombo vya sheria kuhusu uwezekano wa kutekeleza hati ya ICC.

    Hata hivyo, siku iliyofuata Mamdani alisema timu yake ya wanasheria imepitia njia zote zinazowezekana kisheria na kubaini kuwa ofisi ya meya haina mamlaka huru ya kutekeleza hati hiyo.

    Aliongeza kuwa mamlaka hayo yako mikononi mwa serikali ya shirikisho la Marekani, na akaisihi Marekani ijiunge na ICC na kutekeleza hati hiyo ya kukamatwa.

  14. Meli za mafuta zageuza njia ghafla baada ya tishio la Wahouthi dhidi ya usafirishaji wa baharini

    Takribani meli saba za kusafirisha mafuta zimegeuza njia karibu na pwani ya Yemen baada ya kundi la Wahouthi, linalohusishwa na Iran, kutangaza "zuio la baharini" dhidi ya Saudi Arabia siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa taarifa za ufuatiliaji wa meli.

    Meli zote zilikuwa zikielekea au zikitoka katika bandari za Saudi Arabia, lakini zilibadili ghafla mwelekeo baada ya tangazo hilo.

    Takriban asilimia 15 ya biashara ya baharini duniani hupitia Bahari ya Shamu, ambayo inaunganisha Bahari ya Mediterania na Ghuba ya Aden kupitia njia mbili muhimu: Mfereji wa Suez nchini Misri na Mlango wa Bab al-Mandab kati ya Yemen na Pembe ya Afrika.

    Bahari ya Shamu imekuwa njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta ya Saudi Arabia tangu vita kati ya Marekani, Israel na Iran visababishe kuzorota kwa usafiri kupitia Mlango wa Hormuz, hali iliyopunguza kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa mafuta na gesi kutoka Ghuba ya Uajemi.

    Mchambuzi Rosemary Kelanic wa taasisi ya Defense Priorities nchini Marekani amesema njia ya Bahari ya Shamu imekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza shinikizo kwenye masoko ya dunia, na ikiwa Wahouthi watazuia zaidi biashara ya baharini, bei za mafuta zinaweza kupanda.

    Kwa mujibu wa kampuni ya ujasusi wa masuala ya baharini ya Kpler, siku moja kabla ya Wahouthi kutangaza zuio hilo, meli 20 ziliingia Bahari ya Shamu na meli 22 zilitoka kupitia Mlango wa Bab al-Mandab.

    Kelanic ameambia BBC Verify kuwa iwapo Wahouthi wataendelea kushambulia meli katika Bahari ya Shamu au Ghuba ya Aden, hali hiyo itaathiri usafiri wa kimataifa kwa ujumla, si meli zinazoelekea Saudi Arabia pekee.

    Wakati huo huo, kikosi cha majini cha Umoja wa Ulaya kilitoa ushauri siku ya Jumatano kikizitaka meli za kibiashara zinazohusishwa na maslahi ya Israel, Marekani au Saudi Arabia kuepuka kupita Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden hadi kiwango cha tishio kitakapopungua.

    Unaweza kusoma;

  15. Marekani inachunguza uwezekano wa msaada wa Urusi kwa Iran kulenga vituo vya CIA

    Reuters iliripoti katika ripoti ya kipekee, ikinukuu vyanzo vyenye taarifa, kwamba Marekani inachunguza kama Urusi ilihusika katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Iran dhidi ya vituo vya Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) katika nchi za Ghuba ya Uajemi.

    Kulingana na vyanzo hivi, uchunguzi wa Marekani bado unaendelea na maafisa wa Marekani wanatathmini ushahidi na taarifa zilizopo kuhusu uwezekano wa Urusi kuhusika katika mashambulizi haya.

    Maelezo rasmi ya vituo vinavyolengwa na CIA katika eneo hilo hayajatolewa. Ikulu ya White House na Pentagon hazijatoa habari yoyote kuhusu kulengwa kwa nafasi zao katika eneo hilo au majeruhi au hasara za kijeshi katika miezi minne iliyopita, na hata zimeagiza satelaiti za kibinafsi kudhibiti na kutochapisha picha za angani.

    Nchi katika eneo hilo pia zimezuia na kudhibiti vikali ufikiaji huru wa vyombo vya habari na hata uwasilishaji wa ripoti za umma kutoka maeneo yaliyolengwa, na zimezuia uvujaji wa habari kwa adhabu kali - katika baadhi ya matukio hata tishio la adhabu ya kifo.

  16. Wahouthi wadai kuhusika na shambulio dhidi ya meli za mafuta baada ya Marekani kufanya mashambulizi zaidi dhidi ya Iran.

    Kundi la Houthi nchini Yemen linasema limezishambulia meli mbili za mafuta za Saudi Arabia katika Bahari ya Shamu, muda mfupi baada ya Marekani kufanya mashambulizi dhidi ya Iran kwa usiku wa 12 mfululizo.

    Vyombo vya habari vya serikali ya Iran viliripoti kuwa watu wawili waliuawa katika mashambulizi ya Marekani siku ya Jumatano, na kwamba meli moja ya mafuta ilishika moto kufuatia mlipuko katika njia yenye mabomu ya majini kwenye Lango la Hormuz.

    Kabla ya mfululizo huo wa hivi karibuni wa mashambulizi, Rais wa Marekani Donald Trump alikuwa ametishia kuharibu daraja au kituo cha kuzalisha umeme cha Iran iwapo nchi hiyo ingeshambulia meli katika lango hilo, na pia "kushughulikia" kundi la Houthi iwapo lingezuia usafiri katika Bahari ya Shamu.

    Iwapo itathibitishwa, shambulio hilo la Houthi litakuwa la kwanza tangu kundi hilo linaloungwa mkono na Iran litangaze "vikwazo vya usafiri wa baharini" dhidi ya Saudi Arabia. Kundi la Houthi lilitaja meli hizo kuwa ni *Encelia* na *Layla*, ingawa hakuna uthibitisho rasmi kuhusu kuhusika kwao au shambulio dhidi ya meli ya *Layla*.

    Msemaji wa kijeshi wa kundi hilo, Yahya Saree, alisema walizilenga meli hizo kwa kutumia ndege zisizo na rubani (drones) na makombora kwa madai ya kukiuka zuio lao la usafiri wa majini. Saree aliongeza kuwa kundi la Houthi limeahidi kuendeleza operesheni zake za majini na kuendelea "kutekeleza mkakati wa 'kuzingirwa kwa '" (kulipiza kisasi kwa hatua kama hiyo).

    Shirika la Uingereza la Operesheni za Biashara ya Baharini (UKMTO) liliripoti kuwa "kitu kisichojulikana kilichorushwa" kiligonga meli ya mafuta ya Saudi Arabia umbali wa takriban kilomita 130 kutoka Al Shuqaiq nchini Saudi Arabia saa 20:00 kwa saa za GMT. Shirika hilo lilisema shambulio hilo lilisababisha moto lakini hakukuwa na majeruhi au vifo.

  17. Hujambo na karibu katika taarifa zetu za moja kwa moja