Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani na Iran zafikia makubaliano ya kumaliza vita

Pakistan ambaye amekuwa msuluhishi wa mgogoro baina ya nchi hizi imesema mkataba rasmi utasainiwa Ijumaa kumaliza vita vilivyodumu kwa karibu miezi minne.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Jeneral Mstaafu wa Nigeria aliyetekwa afariki dunia

    Jenerali mstaafu wa jeshi la Nigeria ambaye alitekwa nyara na watu wenye silaha kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo amefariki dunia mikononi mwa watekaji wake, jeshi limesema.

    Meja Jenerali Rabe Abubakar, ambaye alikuwa msemaji wa jeshi kati ya 2015 na 2017, alitekwa nyara akiwa na mkewe walipokuwa wakisafiri katika jimbo la Katsina mwezi uliopita.

    Hakuna kundi ambalo limetangaza kuhuhusika na utekaji nyara huo.

    Kutekwa nyara na kifo cha Abubakar kunaangazia changamoto za kiusalama zinaziendela kuyakabili maeneo ya kaskazini-magharibi mwa Nigeria, ambapo magenge ya wahalifu wanaofahamika kama "majambazi" mara kwa mara huwateka watu kwa lengo la kupata fidia, kuiba mifugo na kuwashambulia wanavijiji.

    Kamishena wa Usalama na Masuala ya Ndani ya Jimbo hilo, Nasiru Mu'azu, alielezea kusikitishwa kwake msiba huo licha ya kile alichokiita "juhudi za pamoja" za serikali ya jimbo na vyombo mbalimbali vya usalama kusaidia kuachiwa kwa jenerali huyo.

    "Jenerali mstaafu Abubakar alifariki kutokana na matatizo ya kisukari na shinikizo la damu," aliwaambia waandishi wa habari wakati akitoa rambirambi zake.

    Wakati huo huo, familia ya marehemu imezitaka mamlaka kuimarisha juhudi za kumuokoa mkewe ambaye bado yuko mikononi mwa watekaji nyara hao.

    Soma zaidi:

  2. Meli ya mafuta yapita Hormuz baada ya makubaliano ya kumaliza vita kutangazwa

    BBC Verify imekuwa ikichunguza data ya ufuatiliaji wa meli ambayo inaonekana kuonyesha kwamba meli moja ya mafuta imevuka Mlango-Bahari wa Hormuz kufuatia tangazo la Rais Donald Trump la kufikiwa kwa makubaliano kati ya Marekani na Iran.

    Kulingana tovuti ya MarineTraffic, meli ya mafuta yenye bendera ya Malta Disha iliondoka kwenye bandari ya Ras Laffan nchini Qatar tarehe 13 Juni ikiwa na mizigo.

    Meli nyingine, yenye bendera ya Panama ya MDL Kamran, iliondoka Bandar Imam Khomeini nchini Iran tarehe 11 Juni na kuvuka lango hilo la bahari hapo jana.

    Vifuatiliaji vya eneo ilipo meli hiyo vilizimwa wakati ikipita kwenye njia hiyo lakini vilianza tena kufanya kazi baada ya kupita eneo hilo.

    Meli hiyo inaelekea bandari ya Shinas nchini Oman.

    Katsina ni mojawapo ya majimbo yaliyoathiriwa zaidi na ukosefu wa usalama.

    Maelezo zaidi:

  3. Helikopta zagongana Brazil; Mwanamuziki wa Marekani afariki dunia

    Helikopta mbili zimegongana nchini Brazil na kusababisha kifo cha mwanamuziki mashuhuri wa Marekani Oliver Tree miongoni mwa watu sita.

    Moja ya helikopta imeanguka kwenye maegesho ya muuzaji wa magari na kusababisha karibu magari 20 kuwaka moto.

    Picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Brazil zinaonyesha moja ya helikopta ikidondoka kutoka angani, huku miali ya moto na moshi mzito ukipanda kutoka eneo la ajali.

    Mwanamuziki aliyeaga dunia mwenye umri wa miaka 32 alikuwa kwenye ziara ya ulimwengu wakati ajali hiyo ilipotokea huko Rio de Janeiro siku ya Jumapili.

    Mamlaka zinasema uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo unaendelea.

    Idara ya Kijeshi ya Zimamoto ya Jimbo la Rio de Janeiro ilisema iliitwa kwenye eneo la ajali karibu 09:00 saa za eneo (12:00 GMT).

    Mtengenezaji maudhui kutoka Argentina Gaspar Prim Diaz - anayejulikana kama Gaspi - pia anaaminika kuwa katika mojawapo ya helikopta hizo, kulingana na chombo cha habari cha Associated Press.

    Oliver Tree Nickell alizaliwa huko Santa Cruz, California mnamo mwaka 1993 na alipata umaarufu kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2016 baada ya kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

    Soma zaidi:

  4. Mwana wa mfalme wa Norway apatikana na hatia ya makosa mawili ya ubakaji

    Marius Borg Høiby, mtoto wa miaka 29 wa Malkia Mette-Marit wa Norway, amepatikana na hatia ya makosa mawili ya ubakaji na kuhukumiwa kifungo cha miaka minne jela.

    Majaji watatu katika Mahakama ya Wilaya ya Oslo walimsamehe makosa mengine mawili ya ubakaji, lakini wakamkuta na hatia ya makosa mengine mengi ambayo alikuwa ameshtakiwa.

    Høiby hakuwepo mahakamani wakati wa uamuzi huo, lakini alijiunga na kikao hicho kwa njia ya video.

    Waendesha mashtaka walikuwa wametaka Høiby apewe kifungo cha miaka saba na miezi saba jela hata hivyo, mawakili wake wa utetezi walikuwa wametaka kifungo kiwe chini ya miezi 18 na wanaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

    Mama yake Marius Borg Høiby aliolewa katika familia ya kifalme alipokuwa na umri wa miaka minne, na ingawa alikulia katika familia hiyo, yeye mwenyewe si miongoni mwa familia ya kifalme.

    Mette-Marit ni mgonjwa sana na hivi karibuni ameorodheshwa kwenye orodha ya watu wanaohitaji kupandikizwa mapafu.

    Mawakili wa mwanawe wameomba aachiliwe huru kutoka gerezani mara kwa mara ili aweze kuwa na muda na mama yake kutokana na afya yake inayozorota.

    Baada ya hukumu hiyo, wakili wa utetezi wa Høiby, Petar Sekulic, aliiomba mahakama tena imwachilie huru.

  5. Mashambulizi ya Urusi yaua watu tisa nchini Ukraine

    Watu tisa wauawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika wimbi la mashambulizi ya Urusi dhidi ya Ukraine ambapo jengo kubwa la kidini huko Kyiv lilishika moto, ripoti zinasema.

    Watu wanne waliuawa katika mashambulizi dhidi ya Kyiv, huku wafanyakazi watano wa uokoaji wakifariki wakati wakijaribu kuzima moto uliosababishwa na shambulio la Urusi katika mji wa Kharkiv kaskazini-mashariki, maafisa wa Ukraine walisema.

    Kanisa Kubwa la Dormition la Karne ya 11 liliharibiwa vibaya katika kile Waziri Mkuu wa Ukraine Yulia Svyrydenko alichokiita "shambulio la kikatili kwa watu wetu na urithi wetu".

    Wakati huo huo, shambulio la ndege zisizo na rubani za Ukraine katika mji wa Tula, kusini mwa Moscow, liliua watu watatu na kuwajeruhi wengine watatu, akiwemo mtoto wa mwaka mmoja, maafisa walisema.

    Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora yalichoma moto majengo na magari na kuwaacha zaidi ya watu 140,000 katika mji mkuu wa Ukraine bila umeme, Meya wa Kyiv Vitali Klitschko alisema. Sehemu kubwa ya Ukraine ilikuwa imepewa onyo la mashambulizi ya anga siku ya Jumatatu.

    Mashambulizi ya Kyiv ambayo yalilenga majengo kadhaa ya makazi, yalisababisha takriban watu 23 kujeruhiwa huku wengine watano wakijeruhiwa huko Kharkiv.

    Soma zaidi:

  6. Aomba msamaha kwa ubaguzi wa rangi dhidi ya Korea katika mechi ya Kombe la Dunia

    Mwanamume mmoja wa Mexico aliyenaswa kwenye video akionyesha ishara ya ubaguzi wa rangi wakati wa mechi ya Kombe la Dunia kati ya Korea Kusini na Jamhuri ya Czech ameomba msamaha baada ya video hiyo kusababisha ghadhabu mtandaoni.

    Mtengenezaji wa maudhui kutoka Korea Kusini alichapisha video yake ya mechi hiyo Ijumaa iliyopita ambapo Ulises Fernando Bernal Miramontes, aliyeketi nyuma yake, alionekana akionyesha ishara ya ubaguzi kwa kutumia macho huku akicheka. Tukio hilo linaonekana kama la kukosa heshima kwa Waasia Mashariki.

    Video hiyo ilizua hasira nyingi mtandaoni, huku Wamexico wengi wakionyesha kuchukizwa na kitendo chake.

    Baadaye Bernal aliomba msamaha na ripoti zinasema ameondolewa katika wadhifa wake kama rais wa chama cha uhandisi cha Mexico.

    Mechi hiyo, iliyofanyika katika jiji la Guadalajara la Mexico Alhamisi usiku, Korea Kusini walisawazisha na baadaye kuishinda Jamhuri ya Czech 2-1.

    Soma zaidi:

  7. Tunisia hoi yachapwa 5–1 na Sweden

    Tunisia wamepata kipigo cha mabao 5–1 kutoka kwa Sweden katika mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Dunia 2026, ulioshuhudia makosa mengi ya kiulinzi yakigharimu timu hiyo ya Afrika.

    Sweden walitangulia mapema katika dakika ya saba kupitia Yasin Ayari, aliyenufaika na makosa ya beki wa Tunisia baada ya kipa Mouhibb Shamach kupiga mpira uliorudishwa vibaya. Ayari alipiga shuti kali lililoingia wavuni na kuwapa utangulizi Sweden.

    Baada ya bao hilo la mapema, Sweden waliendelea kutawala mchezo huo na kuongeza mabao mengine kupitia Viktor Gyökeres, Alexander Isak na Mattias Svanberg.

    Tunisia walipata bao lao pekee kupitia Rekik, lakini hawakuweza kurudi mchezoni kutokana na makosa ya mara kwa mara ya safu yao ya ulinzi yaliyozidi kuwapa nafasi Sweden kuendelea kushambulia.

    Matokeo hayo yanaiweka Sweden katika michuano hiyo, huku Tunisia wakiwasononesha Waafrika.

    Soma zaidi:

  8. Manusura wa Ebola aruhusiwa kuondoka hospitali DR Congo

    Manusura katika kituo cha matibabu cha Mongbwalu nchini DR Congo, ameruhusiwa kuondoka hospitalini na kujumuika na familia yake.

    Wahudumu wa afya wakiwa na sare maalum ya kujikiga na ugonjwa wa Ebola, walipiga foleni na manusura huyo akaonekana akiwa anatoka kwenye chumba kimoja kilicho na ulinzi mkali huku wakiwa wanashangilia na kuimba.

    Ndiye mgonjwa wa hivi punde kupona virusi hivyo na wa pili katika wilaya nzima ya Mongbwalu kupona tangu mlipuko wa Ebola kuanza.

    “Nina furaha sana, unajuwa ugonjwa wa Ebola sio mchezo,” alisema Daniel.

    "Sikufikiria kuwa nitarudi tena nyumbani kwa sababau hali yangu ilikuwa mbaya na wagonjwa wengi niliokuwa nao wamefariki au bado wanaendelea kupata matibabu hospitalini huku hali zao zikiwa mbaya," Daniel ameongeza.

    Katika eneo ambalo Ugonjwa wa Ebola umesababisha maafa makubwa, kupona kwake kunachukuliwa kuwa muujiza na ushindi mkubwa katika harakati za kutokomeza ugonjwa wa Ebola.

    Mlipuku huu ambao ndio wa kumi na saba katika nchi wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambao ulitangazwa kuwa janga la kitaifa mwezi wa tatu mwaka huu, baado unaendelea kusambaa nchini humo na katika nchi Jirani kama vile Uganda.

    Ugonjwa huu unaojulikana kama Bundibugyo, ni aina ambayo hado sasa haina chanjo.

    Mamia ya watu wameambukizwa na mamia ya wengine wamepoteza maisha yao hasa katika mikoa ya Ituri, miji ya Bunia, Mongbwalu na Rwampara.

    Wahudumu wa afya pekee ndio wanaoruhusiwa kufika maeneo haya tena wenye mavazi maalum ya kujikinga na Ebola.

    Soma zaidi:

  9. Rais Zelensky ajadili mazungumzo ya amani na Trump

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema siku ya Jumapili kwamba amezungumza na Rais wa Marekani Donald Trump na kujadili juhudi za kufikia mwisho wa vita vya zaidi ya miaka minne , kabla ya mkutano wa G7 nchini Ufaransa wiki hii.

    Zelensky, akiandika kwenye Telegram, alisema alikuwa amemtakia Trump siku njema ya kuzaliwa ya 80 na akamshukuru kwa msaada uliotolewa na Washington katika kipindi chote cha mzozo.

    "Nilimtakia Rais Trump mafanikio mema, kwanza kabisa katika juhudi zake za kukomesha vita vya Urusi dhidi ya Ukraine," Zelensky alisema.

    Akizungumza baadaye katika hotuba yake kwa njia ya video iliyotolewa usiku, Zelensky alisema yeye na Trump wamekubaliana kukutana wakati wa mikutano huko Evian-les-Bains.

    Alisema ni muhimu kuhakikisha Marekani inaunga mkono juhudi za Ukraine za kupata amani, pamoja na washirika wa Ukraine wa Ulaya.

    "Hili ndilo jambo muhimu zaidi tunalotaka sote, na ni muhimu kwamba jamii ya Marekani iunge mkono kikamilifu hamu yetu ya Waukraine, hamu ya kupata amani," alisema.

    Mazungumzo yanayosimamiwa na Marekani yanayolenga kukomesha vita yamekwama huku Washington ikiendelea kutoa kipaumbele kwa mzozo nchini Iran.

    Hata hivyo, Zelensky amesema katika wiki za hivi karibuni mabadiliko ya kasi katika vitani kwa upande wa Ukraine yamefungua fursa ya kufikia makubaliano ya amani.

    Soma zaidi:

  10. Wapiga mbizi 11 na rubani wafariki katika ajali ya ndege Marekani

    Wapiga mbizi kumi na mmoja na rubani mmoja wamefariki katika ajali ya ndege jimbo la Missouri nchini Marekani, maafisa wamesema.

    Ndege hiyo, ambayo ilikodishwa na kampuni ya wapiga mbizi, ilipaa karibu 11:20 saa za eneo siku ya Jumapili, kulingana na msemaji wa Usimamizi wa Dharura wa Kaunti ya Bates.

    Baada ya kushindwa kupata kasi ya mwinuko, ilipinda upande wa kushoto na kuanguka umbali wa yadi 200 kutoka uwanja wa ndege wa Butler Memorial, msemaji huyo aliiambia BBC. Watu wote 12 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walikufa, alisema.

    "Tunachukulia hilo ... kama majeruhi ya wengi," Mkuu wa Polisi Kaunti ya Bates Chad Anderson alisema wakati wa mkutano wa wanahabari mchana.

    Aliongeza kuwa ndege hiyo haikuwa ya kibiashara, badala yake ni "ndege ya ndani ambayo ilipaa kutoka uwanja wetu wa ndani."

    Utawala wa Usafiri wa Anga (FAA) ulisema ndege hiyo ilikuwa ya Pasifiki ya Aerospace P750 na ilianguka wakati ikipaa kwenye uwanja huo.

    "Huduma za usafiri wa anga hazikuwa zinatolewa wakati huo," FAA ilisema. Msemaji alieleza kuwa ndege hiyo haikuhitajika kuwa katika mawasiliano kutokana na aina ya anga iliyokuwa ikipaa.

    Vyombo vya habari vya eneo hilo viliripoti kwamba watoa huduma wa kwanza walikagua eneo hilo ili kuona kama kuna wapiga mbizi waliofanikiwa kuruka kutoka kwenye ndege kabla ya ajali hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Ivory coast ushindi wa kwanza Afrika, Ujerumani yaisambaratisha Curaçao 7-1

    Ivory Coast imeanza vyema kampeni yao ya Kombe la Dunia 2026 kutoka kundi E kwa ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Ecuador, ushindi wa kwanza kwa timu za Afrika katika mashindano ya mwaka huu.

    Bao pekee la mchezo lilifungwa dakika ya 90 na nyota wa Manchester United, Amad Diallo, akiipa Ivory Coast ushindi muhimu katika mechi yao ya kwanza ya kundi.

    Ecuador walikuwa na nafasi kadhaa nzuri za kufunga, ikiwa ni pamoja mara mbili mipira yao ikigonga mlingoti katika kipindi cha kwanza, lakini walishindwa kutumia nafasi hizo.

    Wakati huo huo, Ujerumani waliibuka na ushindi mnono wa 7–1 dhidi ya Curaçao katika mechi yao ya ufunguzi, katika mchezo mwingine wa kundi E.

    Curaçao, ambao wanacheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza, walipata bao la kushtukiza kupitia Livano Comenencia, ambaye shuti lake lilimgonga kipa Manuel Neuer na kuingia wavuni.

    Hata hivyo, Ujerumani walijibu haraka na kuendeleza ubabe wao kupitia mabao ya Nico Schlotterbeck, Kai Havertz (2), Jamal Musiala, Nathaniel Brown na Deniz Undav

    Japan na Uholanzi zenyewe zimeenda sare ya 2-2 katika mchezo wa kundi F.

    Pia unaweza kusoma:

  12. Bei za mafuta zashuka duniani baada ya makubaliano ya Marekani na Iran

    Bei za mafuta zilishuka katika masoko ya Asia baada ya Pakistan, ambayo imekuwa ikisaidia mazungumzo ya kumaliza vita kati ya Marekani na Iran, kutangaza kuwa makubaliano yamefikiwa.

    Rais wa Marekani Donald Trump alisema makubaliano hayo yatawezesha kufunguliwa tena kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.

    Mafuta ya Brent, ambayo ni kipimo kikuu cha bei za mafuta duniani, yalishuka kwa asilimia 3.8 na kufikia dola 84.02 kwa pipa. Mafuta yanayouzwa Marekani yalishuka kwa asilimia 4.1 na kufikia dola 81.40 kwa pipa.

    Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alisema hafla rasmi ya kusaini makubaliano hayo itafanyika Ijumaa, tarehe 19 Juni, nchini Uswisi.

    Baadaye, Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa "mafuta yataanza kutiririka."

    Mlango wa Hormuz ulikuwa umefungwa kwa kiasi kikubwa tangu muda mfupi baada ya Marekani na Israel kuanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran tarehe 28 Februari.

    Iran ilikuwa imetishia kushambulia meli zinazotumia njia hiyo muhimu ya bahari, ambayo kwa kawaida hupitisha karibu asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) duniani.

    Masoko ya nishati duniani yamekuwa yakibadilika sana katika miezi ya hivi karibuni, huku bei za mafuta zikipanda au kushuka kwa kasi kutokana na matukio mbalimbali yanayohusiana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Mafuta ya Brent, ambayo yalikuwa yanauzwa kwa takribani dola 70 kwa pipa kabla ya vita kuanza, yalipanda hadi karibu dola 120 kwa pipa wakati wa vita.

  13. Marekani na Iran zafikia makubaliano ya kumaliza vita

    Marekani na Iran zimetangaza kufikia makubaliano ya awali ya kumaliza vita kati yao, kumaliza miezi ya mvutano uliotikisa Mashariki ya Kati.

    Maafisa kutoka pande zote mbili walisema Jumapili kuwa wamekubaliana juu ya mfumo wa makubaliano ambao pia unajumuisha pia kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha sehemu kubwa ya mafuta ya dunia.

    Rais wa Marekani, Donald Trump, alitangaza mafanikio hayo kupitia mtandao wake wa Truth Social.

    "Makubaliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sasa yamekamilika," Trump aliandika.

    Tangazo hilo lilikuja muda mfupi baada ya Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, ambaye nchi yake imekuwa mpatanishi katika mazungumzo hayo, kusema makubaliano yalifikiwa mapema Jumatatu kwa saa za eneo hilo.

    Maelezo kamili ya makubaliano hayo hayajatangazwa mara moja. Sharif alisema kupitia mtandao wa X kwamba makubaliano hayo yanataka:

    "Kukomeshwa mara moja na kwa kudumu kwa operesheni zote za kijeshi katika maeneo yote ya mapigano, ikiwemo Lebanon."

    Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran nalo lilithibitisha kuwa shughuli zote za kijeshi katika maeneo yote ya mzozo, ikiwemo Lebanon, zitasitishwa kuanzia Jumatatu usiku.

    Trump alisema kuwa Mlango wa Bahari wa Strait of Hormuz, ambao ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani na ambao Iran imekuwa ikidhibiti kwa miezi kadhaa, utafunguliwa tena Ijumaa.

    Trump aliandika:

  14. Hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja