Wagonjwa watano wapona Ebola DRC

Chanzo cha picha, Reuters
Mamlaka za afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zina sababu ya kusherehekea baada ya wagonjwa watano waliokuwa wameambukizwa virusi vya Ebola kupona na kuruhusiwa kutoka hospitalini.
Mlipuko wa sasa wa Ebola unashukiwa kusababisha vifo vya karibu watu 250. Hata hivyo, watu wanaoambukizwa wanaweza kupona, na maafisa wa afya wanasisitiza kwamba yeyote anayeshuku ameambukizwa anapaswa kutafuta matibabu haraka.
Siku ya Jumapili, hafla maalum ilifanyika kwa ajili ya wauguzi wanne waliopona na kuruhusiwa kutoka hospitali moja mjini Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, ambalo ndilo kitovu cha mlipuko huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, aliwaambia wauguzi hao wakati wa ziara yake mjini Bunia:
“Ninyi ni ushahidi hai kwamba mlipuko huu unaweza kudhibitiwa na kusimamishwa.”
Mmoja wa wauguzi hao, Etienne Ezo, aliliambia shirika la habari la Reuters kuhusu hali aliyopitia:
“Tulikuwa tumekata tamaa kabisa kwa sababu tulijua kwamba wakati fulani tungekufa. Hiyo ndiyo ilikuwa hali halisi. Ninawaambia, kama hujawahi kuwekwa kwenye karantini, huwezi kujua jinsi ilivyo ngumu.”
Mtu wa kwanza kupona katika mlipuko huu, ambaye alikuwa mfanyakazi wa maabara, aliruhusiwa kutoka hospitalini wiki iliyopita.
Wahudumu wa afya wako mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya kuenea kwa Ebola, na mara nyingi ndio walio katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa virusi hivyo.
Unaweza kusoma;








