Marekani imemwekea vikwazo vikubwa Rais wa zamani wa Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Joseph Kabila, ikimtuhumu kuyaunga mkono makundi ya waasi ya M23 na AFC.
Washington inadai Kabila alitoa msaada wa kifedha kwa AFC, alihamasisha wanajeshi kuasi kutoka jeshi la Congo, na hata alijaribu mashambulizi ya kuvuka mipaka dhidi ya vikosi vya serikali.
Maafisa wanasema lengo la Kabila lilikuwa kuyumbisha serikali iliyopo madarakani na kumuweka mgombea wa upinzani ili kurejesha ushawishi wa kisiasa.
Chini ya uamuzi wa Wizara ya Fedha, mali zote za Kabila nchini Marekani zimezuiwa.
Raia na kampuni za Marekani zimepigwa marufuku kufanya biashara naye, na taasisi yoyote anayodhibiti kwa asilimia 50 au zaidi pia imewekewa vikwazo.
Benki na washirika wa kigeni wameonywa dhidi ya kushirikiana naye kwa njia isiyo ya moja kwa moja, huku ukiukaji ukibeba adhabu kali za makosa ya kiraia au jinai.
Vikwazo hivyo vimekusudiwa si tu kuadhibu bali pia kulazimisha mabadiliko ya tabia, vikionesha utayari wa Washington kulenga viongozi wa zamani wanaotuhumiwa kuchochea migogoro.BBC ilitafuta maoni kutoka jopo la mawasiliano la Kabila lakini bado haijapata majibu.
Septemba, 2025, Mahakama ya Kijeshi mjini Kinshasa ilimhukumu kifo bila kuwepo mahakamani kwa kosa la uhaini, uhalifu wa kivita na kushirikiana na M23, aliporejea nchini kutoka uhamishoni mapema mwaka huo.
Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent alisema hatua hizo zinaimarisha makubaliano ya amani na Ustawi ya Washington, zilizosainiwa Disemba, 2025 kati ya DRC na Rwanda.
Aliongeza kuwa Rais Donald Trump ameweka wazi kwamba wale wanaosambaza machafuko watawajibishwa.
Vikwazo hivyo vinafuatia hatua za awali za Marekani dhidi ya jeshi la Rwanda Machi, 2026, iliyotuhumiwa kuunga mkono kutekwa kwa miji ya Goma na Bukavu na kundi la M23.
Kigali imekanusha madai hayo, ikisisitiza kuwa hatua zake zilikuwa za kujilinda.
Kabila, ambaye alitawala DRC kuanzia mwaka 2001 hadi alipoondoka madarakani 2019, alisimamia makabidhiano ya kwanza ya madaraka kwa amani tangu uhuru wa nchi hiyo mwaka 1960.