Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump akanusha 'kuihonga' Iran dola milioni 300

Kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema madai hayo yanatokana na upotoshaji unaoenezwa na wapinzani wake wa kisiasa, akisisitiza kuwa Marekani haijafanya malipo yoyote ya aina hiyo kwa Iran.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma & Ambia Hirsi

  1. Mahakama nchini Canada kusikiliza kesi ya Thomas Partey kunyimwa viza

    Mahakama nchini Canada inatarajiwa kusikiliza kesi iliyowasilishwa na serikali ya Ghana ikiomba kutathminiwa upya kwa hatua ya mchezaji wake Thomas Partey kunyimwa viza. S

    erikali inaomba Partey kuruhusiwa kuingia Canada kwa muda mfupi ili kushiriki katika mchezo wa ufunguzi wa timu ya taifa ya Ghana dhidi ya Panama siku ya Jumatano.

    Pia wanaomba mahakama kuiagiza mamlaka ya uhamiaji ya Canada kumruhusu Partey kuwasilisha ombi jipya la viza.

    Kunyimwa viza kwa Partey kunahusishwa na kesi za uhalifu dhidi yake nchini Uingereza, ambapo anakabiliwa na mashtaka ya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia.

    Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal, ambaye sasa anachezea Villarreal ya Uhispania, amekanusha mashitaka yote na anatarajiwa kusomewa mashitaka mwaka ujao nchini Uingereza.

    Serikali ya Ghana katika taarifa yake siku ya Jumamosi ilielezea uamuzi wa Canada wa kumnyima Thomas Partey viza kuwa ‘‘uonevu na usio wa haki’’, ikisema ulitokana na madai ambayo hayajajaribiwa mahakamani.

    Katika taarifa kwa BBC, Mamlaka ya Uhamiaji, Wakimbizi na Uraia wa Canada ilisema: ‘’Canada inazingatia sheria zake kikamilifa, kuandaa Kombe la Dunia hakujabadilishi sheria zake uhamiaji. Kila mtu anayetaka kuzuru Canada anafanyiwa tathmini ya kibinafsi, kwa mujibu wa sheria.’

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, amesema kuwa nchi hiyo pia inatumia njia za kidiplomasia kumtafutia Thomas Partey viza ya Canada.

    Partey amekuwa mchezaji muhimu katika timu ya taifa ya soka ya Ghana, Black Stars na kukosekana kwake uwanjani kutakuwa na thari.

    Wachambuzi wanaamini kwamba anaweza kukosa michezo mingi ikiwa Ghana itafuzu zaidi ya hatua ya makundi katika michuano hiyo.

    Soma zaidi:

  2. Jeshi la Nigeria lamuokoa mjane wa jenerali mstaafu aliyefariki baada kutekwa

    Jeshi la Nigeria linasema kuwa limemuokoa mjane wa jenerali mstaafu ambayealifariki mwishoni mwa juma alipokuwa akishikiliwa na watekaji nyara.

    Meja Jenerali Rabe Abubakar na mkewe Amina walitekwa katika jimbo la kaskazini-magharibi la Katsina mwishoni mwa mwezi uliopita.

    Jeshi lilisema watekaji nyara hao walimpiga risasi Bi Abubakar wakati wa operesheni ya uokoajii kabla ya kutoroka.

    Taarifa zaidi zinasema Bi Abubakar anapokea matibabu katika hospitali ya kijeshi.

    Mmoja wa mabinti wa wanandoa hao, Bilkisu, alithibitisha uokoaji huo kwenye mtandao wa WhatsApp, akisema: "Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake. Mama yetu ameokolewa na Jeshi la Nigeria. "Tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie uponaji wa haraka, afya njema na utulivu wa kiakili kwa yote aliyopitia."

    Kifo cha Meja Jenerali Abubakar akiwa kizuizini kinasadikiwa kutokana na matatizo ya kiafya.

    Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatatu, jeshi lilisema kuwa misheni ya kumwokoa mkewe "ilifuatia juhudi kubwa za utafutaji na uokoaji".

    Soma zaidi:

  3. Binti aliyeolewa ana haki sawa za urithi na kijana wa kiume - Mahakama ya Juu Kenya

    Mahakama ya Juu nchini Kenya imeamua kwamba mabinti wana haki sawa za kurithi mali ya mzazi kama vile wana wa kiume, bila kujali kama wameoa au la.

    Uamuzi huo ulitokana na mzozo wa urithi ambapo baadhi ya wanafamilia walibishana kwamba mabinti walioolewa wanapaswa kupokea sehemu ndogo au kutopokea kabisa sehemu yoyote ya mali ya urithi.

    Hata hivyo, mahakama ilitupilia mbali hoja hii, ikithibitisha kuwa ndoa haiathiri haki ya binti kurithi.

    "Mashamba mengi nchini Kenya yanamilikiwa, yanaendelezwa, na kudhibitiwa kulingana na dhana kwamba mabinti 'tayari wamefaidika kwingineko' kupitia ndoa," Mahakama ilisema.

    Mahakama iliongeza kwamba ahadi zisizo rasmi au za kusemwa kwa mdomo tu za ugawaji wa ardhi kwa watoto wa kiume hazifungamani kisheria ikiwa hakuna stakabadhi sahihi za kisheria zilizokamilika wakati mzazi anaaga dunia.

    Muhimu zaidi, mahakama ilithibitisha tena kwamba chini ya Kifungu cha 38 cha Sheria ya Urithi, kikisomwa pamoja na Katiba, binti na kijana wa kiume wana haki sawa.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Trump huenda akaachia nakala ya awali ya makubaliano kabla ya Ijumaa - JD Vance

    Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema kuwa Rais wa Marekani Donald Trump anaweza kuachia hadharani hati ya awali ya makubaliano ya kumaliza vita na Iran kabla ya Ijumaa.

    Kauli ya Vance imekuja baada ya Trump kudai kuwa makubaliano hayo tayari yameshatiwa saini kwa njia ya kielektroniki.

    Vance alieleza kuwa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Marekani na Iran ni waraka wa jumla sana, wenye urefu wa takribani ukurasa mmoja na nusu.

    Wakati huo huo, maafisa waandamizi wa Marekani wamesema kuwa baadhi ya maelezo ya makubaliano hayo tayari yanajitokeza, wakibainisha kuwa makubaliano rasmi yanatarajiwa kutiwa saini Ijumaa, na Mlango wa Bahari wa Hormuz kufunguliwa tena siku hiyo hiyo.

    Hatua hiyo inajiri wakati Trump akiwa katika mkutano wa G7 nchini Ufaransa, ambapo kikao maalum kuhusu Iran kinatarajiwa kufanyika Jumanne. Viongozi wa Misri, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu pia wanatarajiwa kushiriki.

    Akizungumza akiwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Trump alisema: “Nimefurahi kutangaza kwamba makubaliano yameshatiwa saini, kila kitu kimekamilika,” akirejelea makubaliano ya awali na Iran.

    Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, makubaliano hayo yalitiwa saini kwa njia ya kielektroniki na Trump, Vance na kiongozi wa bunge la Iran Mohammad Baqer Qalibaf.

    Maafisa hao wamesema mazungumzo ya kiufundi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yanatarajiwa kuanza wiki hii, huku suala la kuondolewa kwa vikwazo na kurejeshwa kwa mali likitegemea utekelezaji wa Iran wa masharti ya makubaliano hayo.

    Ingawa Trump awali alisema maelezo kamili ya makubaliano yatawekwa hadharani baada ya sherehe ya Ijumaa, Vance amesema katika mahojiano na Fox News kuwa huenda rais huyo akaamua kuyatoa mapema zaidi.

    Vance pia aliieleza CNN kuwa waraka huo wa makubaliano ni wa jumla sana, na maelezo mengi yatafanyiwa kazi katika mazungumzo yajayo.

    Kwa mujibu wa Vance, aya ya kwanza ya waraka huo inaweka wazi kuwa Iran itajizatiti kwa amani na utulivu wa kikanda, ikiwa ni pamoja na kusitisha uungaji mkono wa kifedha kwa kile alichokiita “mashirika ya kigaidi”.

    Ameongeza kuwa jambo la msingi zaidi ni kwamba Iran itatoa ahadi inayoweza kuthibitishwa kuwa haitatengeneza silaha za nyuklia.

    Soma zaidi:

  5. Wakaguzi wa nyuklia kuruhusiwa kurejea Iran chini ya makubaliano mapya: JD Vance

    Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema kuwa wakaguzi wa nyuklia wataruhusiwa kuingia tena Iran chini ya makubaliano yaliyofikiwa kati ya Washington na Tehran.

    Akizungumza katika mahojiano na shirika la habari la Marekani NBC, Vance aliulizwa iwapo wakaguzi wa nyuklia watapewa ruhusa ya kurejea Iran chini ya makubaliano hayo.

    Akijibu, alisema: “Ndiyo, bila shaka. Moja ya vipengele muhimu vya makubaliano ni kwamba Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) na Marekani watasaidia Iran kuondoa akiba yake ya urani iliyoboreshwa. Hilo limeandikwa wazi kabisa katika waraka wa makubaliano.”

    Vance pia aliulizwa kama makubaliano hayo yanajumuisha kipengele kinachoruhusu Iran kutoza ada kwa meli zinazopita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz, lakini kuruhusu ada ya huduma.

    Akijibu, alisema kuwa katika makubaliano ya awali pande hizo zitajadili makubaliano ya mwisho kwa kipindi cha siku 60, na katika kipindi hicho kupita katika Mlango wa Hormuz kutakuwa huru bila tozo yoyote.

    Makamu huyo wa Rais wa Marekani aliongeza kuwa baadhi ya makundi ndani ya Iran yanaweza kujaribu kupotosha au kuzidisha faida zinazopatikana Tehran kupitia makubaliano hayo.

    “Ni lazima tuelewe kuwa katika makubaliano ya aina hii mambo kama hayo hutokea. Hata hivyo, ukweli ni kwamba hakutakuwa na tozo yoyote na Mlango wa Hormuz utaendelea kuwa wazi.”

    Soma zaidi:

  6. Trump akanusha madai ya malipo ya dola milioni 300 kwa Iran

    Rais wa Marekani Donald Trump amekanusha taarifa zinazodai kuwa Washington imelipa Iran kiasi cha dola milioni 300, akizitaja kama “habari za uongo”.

    Kupitia ujumbe aliouchapisha katika mtandao wake wa Truth Social, Trump amesema madai hayo yanatokana na upotoshaji unaoenezwa na wapinzani wake wa kisiasa, akisisitiza kuwa Marekani haijafanya malipo yoyote ya aina hiyo kwa Iran.

    “Iran imekubali kutowahi kuwa na silaha za nyuklia! Pia, taarifa kwamba Marekani inalipa Iran dola milioni 300 ni habari za uongo zilizoenezwa na chama cha Democrats.”

    Tuhuma hizo zimeibua mjadala mpana katika anga za siasa za kimataifa, zikichochea mvutano unaoendelea kati ya Washington na Tehran, licha ya juhudi za hivi karibuni za kufikia makubaliano ya kupunguza uhasama kati ya mataifa hayo mawili.

    Soma zaidi:

  7. Makubaliano ya Marekani na Iran yasababisha hasira miongoni mwa Waisrael

    Waisraeli kutoka nyanja zote za kisiasa wameonyesha hasira siku ya Jumatatu kutokana na habari za makubaliano ya kusitisha vita kati ya Marekani na Iran, wakiita hatua hiyo kuwa janga kwa Israeli na kuelekeza hasira zao kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

    Kiongozi huyo wa Israel alisema katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu kwamba "kwa makubaliano au bila makubaliano," antaendelea kupigana ili kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia, jambo ambalo Tehran imesisitiza kwa muda mrefu kwamba haijaribu kufanya hivyo, ikisema mpango wake wa nyuklia ni kwa madhumuni ya raia.

    "Mradi mimi ni Waziri Mkuu wa Israeli, haitatokea," Netanyahu alisema, akisisitiza kwamba makubaliano hayo yalifikiwa na Marekani, wala sio Israeli, na kwamba hakukubali ombi la Iran la kujiondoa kwa Israeli kutoka Lebanon kuwe sehemu ya makubaliano hayo.

    "Iran ilitaka tuondoke huko, lakini hilo halikutokea. Unajua ni kwa nini halikutokea, miongoni mwa sababu zingine? Kwa sababu nilisimama kidete," alisema.

    Lakini maafisa wengine wa serikali ya Israeli, wapinzani, wanasiasa na wachambuzi walikuwa wepesi kukosoa makubaliano ya awali, wakiashiria aina ya kura ya maoni isiyo rasmi kuhusu muda wa waziri mkuu huyo kabla ya uchaguzi.

    Soma zaidi:

  8. Mtoto wa Rais Jenerali Muhoozi ajisifia kwa kumkamata mpinzani Uganda

    Mkuu wa majeshi ya Ulinzi nchini Uganda Jenerali Muhoozi siku ya Jumatatu alijisifu kwa kupanga kumsababishia "maumivu na uchungu" mwanasiasa wa upinzani ambaye amemkamata, aliyekuwa akijiandaa kuwasilisha pingamizi la kisheria dhidi yake.

    Muhoozi Kainerugaba, mwana wa Rais aliyetawala kwa muda mrefu Yoweri Museveni, alichapisha picha kwenye mtandao wa X ya Erias Lukwago, mwanasiasa wa upinzani na wakili anayeshikiliwa na jeshi.

    "Ninajivunia maumivu na uchungu WOTE nitakaoupata kwa LUKWAGO MHALIFU!" Kainerugaba alichapisha ujumbe huo kwa wafuasi wake milioni 1.3 kwenye mtandao wa X.

    "Anaendelea kusema 'Samahani, samahani'. Haitamsaidia kwa sasa," aliandika kando ya picha ya Lukwago, akiwa amevaa fulana nyeupe.

    Picha nyingine inaonyesha mwanamume aliyevaa nguo kama hiyo, kwenye mandhari kama hayo hayo, uso wake ukiwa umefunikwa kwa kitambaa na mikono ikiwa imeunganishwa kana kwamba anaomba dua.

    Katika chapisho la awali kwenye mtandao wa X, Kainerugaba alisema "alimkamata mjinga na kumpeleka kwenye chumba cha chini ya ardhi", lakini hakumtaja Lukwago.

    Aliandika katika chapisho lingine: "aliniita?? Unathubutuje kutamka maneno hayo", akiongeza: "mpumbavu huyu atajifunza kutokana na makosa yake".

    Soma zaidi:

  9. Kombe la Dunia 2026: Saudi Arabia walazimishwa sare na Uruguay

    Saudi Arabia wamelazimishwa sare ya 1-1 na Uruguay waliosawazisha dakika ya 80 baada ya Saudia kuongoza dakika ya 41 ya mchezo huo uliopigwa usiku wa manane.

    Mapema usiku wawakilishi wa Afrika Misri walitoshana nguvu na Ubelgiji kwa sare ya goli 1-1.

    Misri waliongoza katika dakika ya 20 kupitia kwa Emam Ashour aliyeachia mkwaju mkali baada ya pasi safi ya Mohamed Salah.

    Ubelgiji walisawazisha dakika ya 66 baada ya mlinzi wa kulia wa Misri Mohamed Hany kujifunga katika harakati za kuokoa.

    Mapema zaidi, Cape Verde waliiwakilisha Afrika na kushangaza dunia baada ya kuonesha mbinu za hali ya juu za ulinzi na kutoka sare ya bila kufungana na Hispania ambao ni mabingwa wa dunia wa mwaka 2010 na mabingwa wa sasa wa Ulaya huku mlinda lango wa Cape Verde, Vozinha mwenye umri wa miaka 40 akijizolea sifa kemkem kwa umahiri wake.

    Alibubujikwa na machozi baada ya kipenga cha mwisho.

    Pia unaweza kusoma:

  10. Kombe ya Dunia 2026: Iran na New Zealand zatoshana nguvu

    Mchuano kati ya Iran na New Zealand umekamilika kwa sare ya mabao 2-2.

    New zealand walikuwa wa kwanza kugusa nyavu dakika ya 7 kupitia kwa Elijah Just.

    Iran wakasawazisha dakika ya 32 kupitia kwa Ramin Rezaeian.

    New Zealand wakaongoza tena dakika ya 54 kwa bao la Elijah Just tena, kisha Iran wakasawazisha tena dakika ya 64 kupitia kwa Mhammad Mohebi.

    Sasa kuna ugumu wa kundi G kwani timu zote nne Iran New Zealand, Misri na Ubelgiji zote zina alama moja.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Watu wanane wafariki baada ya ndege aina ya B-52 kuanguka Marekani

    Watu wanane, wakiwemo wafanyakazi wawili wa Boeing, wameuawa baada ya ndege aina ya B-52 ya Jeshi la Anga la Marekani kuanguka mara tu baada ya kupaa kutoka Kituo cha Jeshi la Anga cha Edwards kusini mwa California.

    Tukio hilo lilitokea saa 11:20 kwa saa za eneo (19:20 GMT) siku ya Jumatatu wakati ndege hiyo ilikuwa katika misheni ya kawaida ya majaribio. Ajali hiyo ilisababisha moshi mkubwa mweusi angani ambao ungeweza kuonekana umbali wa maili nyingi.

    "Leo, Kituo cha Jeshi la Anga cha Edwards kilipata ajali mbaya, na tumewapoteza Wamarekani wanane mashuhuri," Kanali James Hayes alisema, akiwaelezea kama "kikosi mchanganyiko cha wanajeshi, wafanyakazi na wakandarasi wa serikali".

    Awali, Kambi hiyo ilisema kwamba dalili za awali zinaonyesha kuwa ajali hiyo "haingeweza kunusurika".

    Ndugu wa karibu wa wafanyakazi wanaarifiwa na watatajwa baada ya saa 24, Hayes alisema katika mkutano wa alasiri.

    Kituo hicho kimesitisha shughuli zake kwa muda.

    Alisema ndege aina ya B-52 ilikuwa yenye muundo wa kisasa wa rada na ilianguka mara tu baada ya kupaa na kuwaka moto.

    Baada ya kupitia video za awali, tukio hilo lilionekana kutokea "ajali isiyoweza kukingika," Hayes alisema.

    Pia unaweza kusoma:

    Soma zaidi:

  12. Marekani na Iran zatia saini makubaliano ya kusitisha vita

    Marekani na Iran zimetia saini makubaliano ya awali ya kusitisha vita vya Ghuba, katika juhudi za kumaliza mzozo uliotikisa eneo hilo na kuathiri soko la nishati duniani.

    Rais wa Marekani Donald Trump usiku wa kuamkia Jumanne kwa saa za Afrika Mashariki alisema kuwa makubaliano hayo tayari yamesainiwa, ingawa maelezo yake kamili bado hayajawekwa wazi na pande zote mbili zimesema mazungumzo zaidi yanahitajika kabla ya kufikiwa kwa mkataba wa kudumu wa amani.

    Makubaliano hayo yanatarajiwa kuongeza siku 60 zaidi za usitishaji vita uliotangazwa mwezi Aprili na pia kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao Iran imekuwa ikiuzuia tangu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Februari.

    Masuala nyeti, ikiwemo mustakabali wa mpango wa nyuklia wa Iran, yanatarajiwa kujadiliwa katika hatua inayofuata ya mazungumzo.

    "Makubaliano yamesainiwa kikamilifu," alisema Trump baada ya kuwasili nchini Ufaransa kuhudhuria mkutano wa viongozi wa mataifa tajiri duniani wa G7.

    Pamoja na kusema yametiwa saini Trump akaongeza Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance anatarajiwa kuhudhuria hafla rasmi ya utiaji saini wa makubaliano hayo mjini Geneva, Uswisi, siku ya Ijumaa.

    Habari za makubaliano hayo zilisababisha bei za mafuta duniani kushuka hadi kiwango cha chini zaidi tangu Machi 10, baada ya matarajio ya kufunguliwa tena kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayopitisha karibu asilimia 20 ya biashara ya mafuta duniani.

    Mkataba huo unachukuliwa kuwa hatua kubwa zaidi hadi sasa katika juhudi za kumaliza mzozo ambao umeua watu wasiopungua 7,000, wengi wao nchini Iran na Lebanon, huku pia ukiitikisa sekta ya nishati duniani.

    Soma zaidi:

  13. Hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja